Kumhani Aliyefiwa Baada Ya Siku Tatu
SWALI:
Asalam alaykum,
Mie naomba kuelimishwa kuhusu suali hili, ikiwa mtu amefiliwa nikapata habari ktk siku ya nne au sikupata kuenda kumuhani wala mazikoni jee nikienda siku ya nne baada ya msiba hii haifai? Au kumpigia simu kwa nia ya kumuhani pengine nipo mbali naye pia ni makosa?
Maana nimeambiwa na mtu kuwa mwisho siku tatu tu ikifika ya nne kama hukuenda nisiende tena, kwa hiyo nilikuwa nataka ufafanuzi zaidi kutoka kwenu wenye elimu inshAllaah. jazakAllaahul kheir
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Inapendeza kuwapa pole (taazia) wafiwa wakiwa wanaume au wanawake na
Tamko la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lilikuwa: “Lillahi maa Akhadha walahu maa A‘twaa wa kullu shay’in ‘indahu biajalin musammaa faltaswbir wal tahtasib – Kwa hakika ni cha Allaah Alichokichukua, na ni Chake Alichokitoa, na kila kitu Kwake kina muda maalumu… basi subiri na taka malipo kwa Allaah” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na pia: “A‘dhwama Llahu ajraka wa ahsana ‘azaa’aka wa ghafara limayyitika – Ayafanye mengi malipo yako, na Akufanye kuzuri kuhaniwa kwako na Amsamehe maiti wako” (Tazama Minhaajul Muslim na Hiswnul Muslim).
Ama kuhusu kutoa pole kwa muda wa siku tatu za kwanza baada ya kufariki, yamelezwa hayo katika kitabu cha Minhaajul Muslim cha Shaykh Abubakar Jaabir al-Jazaairiy ingawa hajatoa dalili. Lakini Shaykh ameendelea kusema kuwa atakapokuwa mmoja wa watoa pole hayupo au yuko mbali si vibaya pole ikichelewa kwani kuhusu kutoa pole Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa fadhila zake kwa kusema: “Mwenye kumtaazi nduguye Muumini kwa msiba, Allaah Atamvisha mtu huyo kipambo kijani cha utukufu Siku ya Qiyaama” (Ibn Maajah).
Na kwa kuwa hakuna dalili ya kukatazwa baada ya siku ya tatu tunakwenda na kanuni ambayo tunaipata kwenye maneno ya Allaah: “Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo” (2: 286).
Na Allaah Anajua zaidi