Kitabu Cha Du'aa Kiitwacho 'Ad-Du'aa Al-Mustajaab' Kimejaa Uzushi Mkubwa
Kitabu Cha Du'aa Kiitwacho 'Ad-Du'aa Al-Mustajaab' Kimejaa Uzushi Mkubwa
SWALI:
Kuna kitabu kinaitwa Duaa Mustajab, ni kitabu maarufu cha duaa na kimeenea katika maduka ya vitabu na watu wanakitumia sana je ni kitabu sahihi kwa duaa?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kitabu hicho kilishazungumziwa na Wanachuoni wakubwa wa Ahlus Sunnah wal-Jamaa’ah na kubainisha kutofaa kwake.
Hizi hapa chini Fataawa za Wanachuoni hao:
Kamati ya Kudumu ya Utoaji Fatwa na Tafiti za Kielimu ya Saudia (Al-Lajnatu Ad-Daaimah) chini ya Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) wamesema:
"Kitabu "Ad-Du'aa Al-Mustajaab" si cha kutegemewa kwa sababu kimekusanya idadi kubwa ya Ahaadiyth dhaifu na za kutungwa.
[Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah, mj. 2, uk.449]
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:
"Ni kitabu ambacho hakiwezi kutegemewa na mtunzi wa kitabu hicho si Mwanachuoni. Hivyo, tumetoa tanbihi kwa muda mrefu na tumeeleza kuwa hicho kitabu si cha kutegemewa. Wasomaji wanapaswa kutanabahishwa kwamba hakitegemewi kwa sababu kimekusanya Hadiyth dhaifu na za kutungwa.
[Fataawa Ibn Baaz, mj. 26, uk. 354-355]
Shaykh Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) amesema:
"Kuna kitabu ambacho kimeenezwa sana kwa watu leo hii, na kinapatikana katika maduka ya vitabu, kinaitwa "Ad-Du’aa Al-Mustajaab" cha Muhammad ‘Abdul-Jawwaad. Ni kitabu chenye ngano kilichokusanya du’aa za kuzushwa za Kisufi na Adhkaar ambazo zimenukuliwa bila dalili zozote kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Jina la kitabu chenyewe lina maelezo ya ujasiri kwa Allaah Aliyetakasika, mtunzi kakiita kitabu "Ad-Du’aa Al-Mustajaab (Du’aa Zenye Kujibiwa)", je, ni nani kamjulisha huyo mtunzi kuwa du’aa hizo zinajibiwa? Ushahidi gani anao kwa hilo, zaidi tu ya kutaka kuwavutia watu ‘awwaam (wa kawaida wasio na elimu) na kuwahadaa kwa kitabu cha uzushi.
Nawashauri wasomaji (watafute na kuvitumia) vitabu vya du’aa na adhkaar vya kuaminika vilivyoandikwa na Wanachuoni weledi wenye kuaminika wa Ahlus-Sunnah:
1. Al-Waabil Asw-Swayyib cha Imaam Ibn Al-Qayyim
2. Al-Kalim Atw-Twayyib cha Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah
3. Al-Adhkaar cha Imaam An-Nawawiy
Vitabu hivi, havina ndani yake adhkaar za uzushi; zimekusanya adhkaar zilizopokelewa kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
Vinatosheleza na vinakidhi haja na hakuna haja ya vitabu vya masimulizi ya ngano vilivyoandikwa na wafanya mzaha, na himidi zote ni za Allaah.
[Majmuw’ Fataawa Fadhwiylat Ash-Shaykh Swaalih bin Fawzaan, mj. 2, uk. 697]
Na Allaah Anajua Zaidi