023-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL BAARIU

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

الْبَارِءُ

AL-BAARIU

 

 

 

 

Al-Baariu:  Mwanzishi viumbe bila kasoro.

 

Mwanzishi viumbe bila kasoro.

 

Al-Baariu: Muumbaji viumbe kwa maumbile yanayonasibiana na mazingira ya maisha yao.

 

Jina hili tukufu limetajwa mara mbili katika Qur-aan:

 

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ  

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile. [Al-Hashr: 24]

 

فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ

basi tubuni kwa Muumbaji wenu; [Al-Baqarah: 54]  

 

 

1-Al-Baariu: Mwanzishi, Mvumbuzi, Mwenye kuendelea. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٢٢﴾

22. Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Al-Hadiyd: 22]

 

 

2-Al-Baariu: Ametenganisha baadhi ya viumbe kwa baadhi yake, yaani amevipambanua kutoka aina moja kwenda aina nyingine, na kila kiumbe alikipa sura yake, inayonasibiana na malengo ya kuumbwa kwake, yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaumba kitu kutoka kisichokuwa chochote, na kila kimoja anakipa sifa yake ya kipekee tofauti na viumbe vingine.

 

 

3-Yeye Al-Baariu Ameumba maumbile yaliyoepukana na tofauti na kuchukiza, na kudhalilika, vimejipambanua vyote na kujikosha na hivyo, Anasema (‘Azza wa Jalla):

 

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾

Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka, hutaona katika uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho je, unaona mpasuko wowote ule?  [Al-Mulk: 3]

 

 

4-Yeye Al-Baariu Amemuumba mwana Aadam kutokana na udongo, na katika lugha ya Kiarabu, Al-Bariyyu ni udongo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾

55. Kutokana nayo (ardhi) Tumekuumbeni, na humo Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine.  [Twaahaa: 55]

 

 

5-Yeye Al-Baariu Aliyeumba maji na udongo na moto na hewa si kutoka katika kitu, kisha baada ya hapo Akaumba maumbo mbali mbali.

 

[Marejeo ya maana zilizotangulia katika: Al-Minhaaj (1/192), Al-Asmaau cha Ar-Raaziy (216), Tafsiyr Asmaai Allaah (27) Asmaau cha Al-Bayhaqiy (40) na An-Nahjul Asmaa cha Muhammad Al-Hamuwd 117]

 

 

6-Yeye Al-Baariu: Ambaye Anamtakasa aliyedhulumiwa na alichodhulumiwa, kama vile Alivyomtakasa Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾

Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliomuudhi Muwsaa, lakini Allaah Akamtoa tuhumani kutokana na yale waliyoyasema. Na alikuwa mbele ya Allaah mwenye kuheshimika. [Al-Ahzaab: 69]

 

 

7-Yeye Al-Baariu Ametakasika na  upungufu wowote ule na aibu yoyote ya dhati Yake, sifa na matendo yake, na kufananishwa na chochote, kushirikishwa, usuhuba kuwa na watoto na kila anachonasibishwa nacho na makafiri.

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Baariu:

 

1-Tafakari Uumubaji wa Al-Baariu. Na kutafakari uumbaji na utukufu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni miongoni mwa ‘ibaadah adhimu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa. Tafakari kwa kutazama mbinguni; jua, mwezi, nyota ndege na tafakari viumbe vinginevyo visivyoonekana; Malaika, majini n.k. Tazama ardhini, milima, miti, wana Aadam, wanyama, wadudu n.k. Tazama na tafakari vya baharini; kila aina ya samaki. Tazama kila mahali utakuta uumbaji ambao hakuna awezaye kuumba kama Yeye (‘Azza wa Jalla), hivyo usije kumshirikisha na yeyote yule. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

Huu ni uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye. Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana. [Luqmaan: 11]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ ﴿١٧﴾

Je, hawamtazami ngamia namna walivyoumbwa?

 

وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ ﴿١٨﴾

Na mbingu vipi zilivyonyanyuliwa?

 

وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ ﴿١٩﴾

Na majabali vipi yamekongomewa imara kabisa.

 

وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ ﴿٢٠﴾

Na ardhi vipi ilivyotandazwa?  [Al-Ghaashiyah: 17-20]

 

 

2-Mtii Al-Baariu Ambaye Amekuumba wala usimtii yeyote mwengine katika maasia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

لا طاعةَ لِمخلُوقٍ في معصيةِ الخالِقِ

((Hakuna kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba)) [Swahiyh Al-Jaami’ (7520)

 

 

3-Unapomuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), rudi kutubia Kwake kama vile Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) alivyowaamrisha wana wa Israaiyl:

 

 وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِنَّكُمْ ظَلَمْتُمْ أَنفُسَكُم بِاتِّخَاذِكُمُ الْعِجْلَ فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ عِندَ بَارِئِكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۚ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿٥٤﴾

Na pindi Muwsaa alipowaambia kaumu yake: “Enyi kaumu yangu! Hakika nyinyi mmedhulumu nafsi zenu kwa kuabudu kwenu ndama, basi tubuni kwa Muumbaji wenu;  na ziueni nafsi zenu, hivyo ni bora kwenu mbele ya Muumbaji wenu.” Akapokea tawbah yenu; hakika Yeye Ndiye Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah: 54]

 

 

04-Muombe du’aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kukiri kwamba Yeye ni Muumbaji wako; Du’aa inayoitwa Sayyid Al-Istighfaar ambayo ni du’aa bora kabisa kuliko nyinginezo katika kuomba maghfirah:

 

اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ.

Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘abduka wa anaa ‘alaa ‘ah-dika wawa’-dika mastatwa’-tu, a’uwdhu bika min sharri maa swana’-tu, abuw-u Laka bini’-matika ‘alayya wa abuw-u bidhanbiy, faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh dhunuwba illaa Anta

 

Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie kwani hakuna wa kughufuria madhambi ila Wewe.  [Al-Bukhaariy (7/150) [2306]]

 

 

Share