007-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Nabiy Amejitibu Na Akaamuru Dawa Kwa Maswahaba Zake Na Familia Yake
Swahiyh Twibbin-Nabawiy
007-Nabiy Amejitibu Mwenyewe Na Akaamuru Dawa
Kwa Maswahaba Zake Na Familia Yake
Ilikuwa katika mwongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kujiaguwa. Kadhalika aliwaamuru watu wake na Maswahaba wake waliopatwa na maradhi wajitibie. Haikuwa katika mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake kutumia kinachoitwa أقرباذين (Aqrabaadhiyn – mchanganyiko wa madawa kadhaa ya kemikali); bali mara nyingi dawa zao zilikuwa ni aina moja kwa kila ugonjwa, mara nyingine huongezea nguvu kwa dawa nyingine au kupoza ukali wa dawa. Tiba hii sana ndio tiba ya mataifa mbalimbali, Waarabu, Waturuki, na watu wote wanaosihi majangwani, mataifa yaliyokazana na tiba ya michanganyo ni Warumi, Wagiriki, lakini mataifa ya Asia kama Wahindi sana walijitibu kwa dawa moja moja.
Matabibu wamekubaliana kwamba pale ambapo yamkinika kutumia chakula kama tiba, isitumike dawa badala yake. Na iwezekanapo kutia dawa moja tu, basi ni bora zaidi kuliko mchanganyiko wa aina nyingi.
Wakasema na kila shida inayowezekana kuondoshwa kwa chakula na kinga, watu wasijaribu kuiondosha kwa dawa. Haifai kwa tabibu kubobea kunywesha watu madawa bila kiasi.[1] Kwa sababu dawa huharibu mwili kama haijakuta ugonjwa humo mwilini, vile vile inadhuru mwili ikiwa ugonjwa upo, lakini hauafikiani na dawa ile, au hata dawa ikikutana na ugonjwa lakini imezidi kiwango kuliko ugonjwa huo au kuliko nguvu ya mwili kustahamilia dawa ile, au namna ilivyotumika hiyo dawa, yote hii huvuruga hali ya afya.
Wataalamu wanaofanya majaribio sana, tiba yao ni katika dawa moja moja. Kundi hili ni kati ya makundi matatu ya kitabibu.
Hakika ya hayo, ni kuwa tiba ni kutokana na jinsi ya vyakula vilivyo; taifa la watu ambao hula mno vyakula vya aina moja moja, huwa na maradhi machache sana. Basi na tiba yake ni kwa dawa za aina moja moja. Ama watu wa mijini ambao ada yao ni kula vyakula vingi mbali mbali kwenye mlo mmoja tu hawa wanahitajia tiba mchanganyiko. Basi watu hawa huhitaji tiba kwa dawa zilizochanganywa pamoja kwa aina mbali mbali. Sababu ni kuwa maradhi yao zaidi huwa mchanganyiko huwa zinawafaa sana. Maradhi ya watu wa mashambani na majangwani huwa ni aina moja moja, hao hutosha kuwatibu kwa dawa zilizo moja-moja, hii ni hoja kulingana na taaluma ya tiba.
Sisi tunasema, “Kuna jambo lingine hapa, nali ni: Tiba ya Nabiy hailingani na tiba za matabibu wengine, na kama ilivyo tiba ya wataalamu wa tiba wanavyowazidi matabibu wasio mabingwa wa taaluma ya tiba. Hili wamekiri wataalamu mabingwa wa tiba, kati yao husema: “Tiba ni kiyasi (malinganisho ya pande mbili).” Na wapo wasemao: “Tiba ni majaribio.” Na wapo wasemao: “Tiba ni mawazo ya ki-ihamu, njozi, na dhana zenye kusibu.” Na wapo wasemao: “Elimu ya tiba kiasi kikubwa imechukuliwa kutoka kwa wanyama.” Kama tunavyoshuhudia wanyama mfano wa paka wanapokula vitu vyenye sumu, hukimbilia kwenye taa na kuramba mafuta kuweza kujitibia. Nyoka pia wanapotokea ardhini, macho yao yana kifuniko hawaoni vizuri. Basi nyoka hao huja katika majani ya الرازيانج )Ar-Raaziyaanij)[2] basi hupitisha macho yao kwenye dawa hiyo. Na kama mazowea ya ndege kuonekana wakijitibia kwa maji ya bahari baada ya kutatizika afya zao n.k. Mfano ya hayo yaliyotajwa katika msingi ya tiba.
Majani Ya Ar-Raaziyanij Shimaar (Bizari tamu)
Hakika tiba zitokazo katika Wahyi ziko juu kuliko tiba za matabibu, kama zilivyo elimu za Manabii kuwa ziko juu kuliko elimu za watu wengine. Bali unapata dawa ambazo hutibu magonjwa kutoka katika maelekezo ya Kinabii; dawa ambazo hawakuzigundua matabibu wakubwa. Elimu zao zote na maarifa yao yote, majaribio na vipimo vyao hawavikugundua. Miongoni mwao ni madawa ya nyoyo na kiroho, nguvu ya moyo, kutawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kumuelekea na kujitupa, na kunyenyekea mbele Yake, kutoa swadaqah, kuomba du’aa, kuomba maghfirah na kutubia, kuwafanyia ihsaan watu na viumbe kwa ujumla, kuwapa msaada waliohemewa, kutatua matatizo ya wenye shida. Dawa hizi zimejaribiwa na mataifa mbali mbali ya watu kwa dini mbali mbali na kuona matokeo makubwa kwenye kuponesha kwa namna ambayo matabibu wakubwa elimu zao zilikuwa hazijafikia huko.
Sisi pia tumefanya majaribio ya tiba nyingi kama hizi. Tumeziona zikitenda yasiyotendwa na tiba za kimaada, bali hizo huwa katika kiwango cha chini mbele ya tiba hizi za kimoyo, kiroho na kadhalika. Na haya yanakwenda na hekima ya Ki-Ilaah (Allaah) bila kutoka nje ya hapo, ila ifahamike kuwa sababu ziko aina kwa aina, pale moyo unapokuwa umeungana na Rabb wa walimwengu, Muumba wa maradhi na dawa Anayemiliki maumbile yote, na kuyaweka chini ya udhibiti Wake.
Moyo wa namna hii utakuwa na tiba tofauti na moyo ulio mbali na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni jambo linalojulikana kuwa nyoyo zikipata nguvu, nafsi na tabia ikapata nguvu pia huweza kusaidiana kuondoa maradhi na kuyashinda.
Kwa mwenye kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) huwezi kukana haya, kwamba, kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni katika tiba kubwa, kuna nguvu ya kuweza kuondosha maumivu jumla.
Hayakanushi haya ile asiyejua na aliye mbali na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hakika ya ki mwana Aadam. Na tutaeleza In Shaa Allaah kwa nini Suwrah Al-Faatihah iliposomwa iliweza kuponyesha maradhi ya kung’atwa, aliyefanyiwa Ruqya kwa kisomo hicho akasimama kana kwamba hakuwa na shida.
Hizi ni aina mbili katika tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa uwezo wa Allaah (Ta’aalaa) tutazungumzia kadri ya uwezo wetu, na upeo wa ujuzi wetu kiasi, lakini tutatoa hayo kwa kutegemea fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Mwenye ushindi, mpaji.
[1] Kama pana maradhi ya aina fulani; yapasa kutumia dawa fulani bila kuzidisha kipimo; kwani kila dawa ni silaha yenye ncha mbili, kwa upande mmoja humsaidia mgonjwa; kiwango kikizidi na muda wa kutumia kuwa mrefu; huenda ikapelekea katika maradhi na kuathiri kiungo kilichokuwa kizima. Kuna baadhi ya magonjwa ambayo tiba yake ni mapumziko kwa muda maalum na utaratibu maalum wa mlo.
[2] Neno la kifursi nalo ni Ansiyuwn ni mti wenye mauwa madogo na matunda yake ni mbegu zenye harufu nzuri hutumiliwa katika matibabu mbali mbali. Na katika nchi za Shaam na Miswr zinajulikana kama ‘shimaar’ au ‘shamuwr’. Na katika nchi za Magharibi zinaitwa ‘bisbaas’. Taz Mu’jim Al-A’shaab wan-Nabaat Atwibiyyah (Uk. 208) (Mti huu Afrika Mashariki huitwa: ima aynisuni (au bizari shimari au bizari tamu). Kiingereza ni: Fennel Seeds.