012-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Tiba Kwa Dawa Za Ki-Twabi’iyyah (Ki-Asilia): Tiba Ya Homa
Swahiyh Twibbin-Nabawiy
Sehemu Ya Kwanza
Tiba Kwa Dawa Za Ki-Twabi’iyyah (Asilia, Natural)
012-Tiba Ya Homa[1]
Imethibiti katika Asw-Swahiyhayn:
عَنْ ابْنِ عُمَرَ أَنّ النّبِيّ صَلّى اللّهُ عَلَيْهِ وَسَلّمَ قَالَ: ((إنّمَا الْحُمّى أَوْ شِدّةُ الْحُمّى مِنْ فَيْحِ جَهَنّمَ فَأَبْرِدُوهَا بِالْمَاءِ))
Kutoka kwa Ibn Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika homa, au ukali wa homa unatokana na joto la Jahannam, ipozeni kwa maji.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy (5723) na Muslim (2209)]
Hadiyth hii imewapa mushkeli matabibu wengi wasiojua, wakaona inapingana na dawa ya homa na tiba yake. Sisi tunabainisha kwa uwezo wa Allaah na nguvu Zake - iliyo na fiqhi yake, basi tunasema: Maelezo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ya aina mbili. Kwa watu wote ardhini, na mahsusi kwa baadhi yao.
Ya kwanza, ni kama maelezo yake kwa ujumla na ya pili, ni kama pale aliposema:
لاَ تَسْتَقْبِلُوا الْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ وَلاَ بِبَوْلٍ وَلاَ تَسْتَدْبِرُوهَا وَلَكِنْ شَرِّقُوا أَوْ غَرِّبُوا
“Msielekee qibla kwa haja kubwa au ndogo, wala msikipe mgongo, lakini elekeeni Mashariki au Magharibi.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy (144) na Muslim (264) kutoka katika Hadiyth ya Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu).
Maelezo haya hayawahusu watu wa Mashariki wala Magharibi, wala Iraq, lakini ni kwa watu wa mji wa Madiynah na walio katika uelekea wake, kama Shaam na miji kama hiyo[2] kadhalika aliposema:
مَا بَيْنَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ قِبْلَةٌ
“Eneo kati ya Mashariki na Magharibi ndio qibla.” [At-Tirmidhiy (344), Ibn Abiy Shaybah katika Al-Muswannaf (2363), na wengineo ni Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) marfuw’an kwake]
Hii likijulikana basi, maelezo yake katika Hadiyth hii yanawaelekea watu wa Hijaaz peke yao, na wanaowafuatia, kwani ilikuwa homa zao nyingi ni zile aina ya homa za kila siku zinazojitokeza zinazotokana na joto la jua. Homa ya namna hii inatosha maji baridi kunywa na kuoga. Homa ni joto la ajabu linafukuta kutoka moyoni na huko hutawanyika kupitia roho na damu kwenye mishipa ya mwili kusambaa mwili mzima, na hufukuta fukuto linalodhuru utendaji kazi wa mwili wa kawaida[3]. Nayo homa inagawika sehemu mbili.
i) Ya kupita: Ambayo huzuka kutokana na malengelenge au kushughulika, au kupatwa na joto la jua.
ii) Ya kimaradhi: Na hii haiwi isipokuwa katika kiungo cha awali kutokea hapo huchemsha mwili mzima. Ikiwa chanzo chake ni kuhusiana na roho, nafsi; basi huitwa: Homa ya Siku; kwani mara nyingi huondoka ndani ya siku moja na ukomo wake ni siku tatu.
Ikiwa chanzo chake ni kuhusiana na michanganyiko; huitwa: Homa ya kuambukiza (kama bakteria, virusi), nayo ina aina nne: Umanjano, weusi, balghami na kidamu.
Ikiwa chanzo chake ni kuhusiana na viungo vigumu ya asili huitwa ni homa ya دق kushindika (kugandamiza, kushinikiza; homa kuu) Chini ya aina hizi kuna vigawanyo vingi.
Mwili waweza kufaidika sana kwa kupata homa kuliko kufaidika kwa dawa. Na mara nyingi hii huwa katika homa ya siku moja. Na homa ya kuambukiza, ni sababu ya kuivisha vitu vigumu bila ya joto hilo visingeweza kuiva, pia ni sababu ya kufunguka kwa tundu ambazo dawa bila ya hivyo isingeweza kufika dawa zenye kufungua.
Ugonjwa wa Ramad (kuvimba macho). Wa muda mfupi au wa zamani, aina zake nyingi hupona kwa haraka ya ajabu na husaidia kutokana na Al-Faalij (Hemiplegia) na Al-Laqwah (ugonjwa hufikia usoni na kupindisha shavu) na kufura, na maradhi mengi yanayozuka yanayotokana na ziada nzito.
Baadhi ya matabibu bora wameniambia kuwa magonjwa mengi, baadhi yake huwa tunapata taarifa yake kupitia homa. Homa inaashiria kuja kwa maradhi mengine mwilini kama mgonjwa anapobashiri kupata nafuu. Basi homa kwake huwa na faida zaidi kuliko kunywa dawa kwa kiasi kikubwa tu.
Homa huiva kwa michanganyo na maada mbovu inayodhuru mwili inapoisha inasadifu dawa, hali tayari iko kwa ajili ya kutoka kwani imeiva hapo ikaitoa na kuwa ndio sababu ya kupona[4].
Iikijulikana hili, basi inajuzu kuwa muradi wa Hadiyth ni zile homa za mpito; kwani homa hizi mtu hupona kwa kuzama kwenye maji baridi. Na kunywa maji baridi yenye barafu. Mwenye homa hii hahitaji tiba nyengine. Hiyo ni hali ya ujoto tu iliyoambatana kwenye roho. Hivyo yatosha kuiondosha kwa maji baridi. Haihitaji kutoa maada, au kungojea kuiva. Pia inajuzu kuwa kusudio ni homa aina zote.
Bingwa wa matabibu Galenus[5] amekiri kuwa maji baridi yanafaa kutibu homa. Amesema katika makala ya kumi kutoka katika kitabu cha ‘Mbinu za Tiba’. “Kama mtu ni kijana, mwenye mwili mzuri, nyakati za joto kali, akiwa katika homa kali sana, na hana uvimbe, malengelenge tumboni, akatoa maji baridi au akaogelea, ingemsaidia kutibu homa hiyo”. Akasema: “Nasi tunaamrisha kufanya hivyo mfululizo bila kuacha.”.
Amesema Ar-Raaziy[6] katika kitabu chake kikubwa[7]: “Ikiwa kuna nguvu kubwa na homa ni kali, na kuiva kuko waziwazi na hakuna vidonda tumboni, malenge malenge, uvimbe, maji baridi yanafaa kwa kunywa, mgonjwa akiwa na mwili mzuri, na kipindi cha joto, na amezowea kutumia maji baridi kutoka nje na aambiwe kutumia.”[8]. Kauli yake kuwa: “Homa ni kutokana na joto la moto wa Jehannamu” ni ukali wa miali yake na kuenea kwake, na mifano kama hiyo. Aliposema, “Ukali wa joto ni kutokana na joto la Jahannam.” [Al-Bukhaariy (533, 534) kutoka katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah na Ibn Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kuna sura mbili.
Kwanza, ni mfano tu unatokana na moto wa Jahannam, waja wapate kushuhudia kuwepo kwake, wapate mazingatio, kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekadiria kudhihiri kwake kutokana na sababu zake, kama starehe, furaha, ladha ni katika neema za Jannah, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amevidhihirisha hapa duniani. Waja wapate kufaidika ni dalili kwao na imekadiriwa kutokea kwake kwa sababu zake.
Pili: Muradi wake ni kushabihisha akafananisha, ukali wa homa na moto wake na joto la Jahannam. Na kufananisha joto na homa kuwazindua watu wapate kuzingatia.
Hii nikuzindua nafsi za watu watambue ukali wa adhabu ya moto, kwamba joto hili kali limefananishwa na joto ya fukuto la miali ya moto wa Jahannam. Ni ile joto linalopatikana kwa kukaribia tu kabla hata ya kuingia motoni. Aliposema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) “Ipoozeni” imepokewa kwa namna mbili: kwa hamza mkato na kuipa fat-hah kitenzi chenye herufi nne. Kutokana na kama atakifanya kuwa baridi kitu, mfano: atakichemsha na kukifanya cha moto.
Ya Pili: Kutumia hamzah ya kuungia, yenye dhwammah “Hamzah Al-Waswli” kutokana na kitu kimekuwa baridi kwa kufanywa baridi. Na hii ndio lugha fasaha zaidi na yenye kutumiwa zaidi, na kitenzi chenye herufi nne “Ar-Rubaa’iy” ni lugha mbaya kwao.
Amesema: Al-Hamaasiy:
***
Nimeelekea yaliko maji ya jamii ya watu kutafuta burudisho
kupoza moyo uwakao kwa mapenzi…
Nipate baridi ya nje ya mwili,
ni yupi atakayesaidia mbele ya moto uwakao ndani ya mwili.[9]
***
Kauli yake: kwa maji hapo kuna kauli mbili:
Mojawapo ni kuwa kila maji, na hii ndio kauli sahihi.
Na ya pili ni: Maji ya zamzam. Watu wanaoshika kauli hii wanatoa hoja kwa Hadiyth iliyopokelewa na Imaam Al-Bukhaariy katika Swahiyh Al-Bukhaariy (3261 kutoka kwa Abuu Jamrah Naswr bin ‘Imraan Adhw-Dhwuba’iy amesema: “Nilikaa na Ibn ‘Abbaas Makkah, nikashikwa na homa akasema: Ipoze ipate kukuondoka hiyo homa kwa maji ya zamzam kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Homa inatokana na fukuto la Jahannam, ipozeni kwa maji.” Au amesema: “Kwa maji ya Zamzam.”
Ametia shaka mpokezi huyu kama angesema bila shaka yoyote kwa kauli ya kukata shauri moja kwa moja, basi hiyo ingekuwa ni amri mahsusi kwa watu wa Makkah kutumia maji ya zamzam. Kwa sababu ni rahisi kwao kuyapata, na watu wengine watumie maji waliyokuwa nayo kwenye mazingira yao.
Wale wanaosema ni maji ya aina yote wamehitilafiana kuhusu muradi ni kutoa swadaqah ya maji, au kuyatumia maji? Katika kauli mbili. Na iliyo sahihi, yaani kuyatumia. Nadhani waliopeleka kwenye maana ya swadaqah ya maji ni kwa sababu ameona mushkeli wa kuyatumia maji baridi katika homa, wala hakufahamu kusudio lake pamoja na kuwa ni zuri sana. Nayo ni kwamba malipo hulingana na jinsi kazi ilivyo. Kama maji baridi yanavyozima moto unaowaka kutokana na kiu, kwa hivyo pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atazima homa inayowaka kwa huyo mgonjwa kama malipo yaliyo muwafaka kabisa na hali yake. Yaani moto huzimwa kwa kutumia maji. Lakini uelewa huu unatokana na kuzingatia fiqh iliyomo kwenye Hadiyth na ishara yake, ama muradi hapo ni kuwa maji yatumike.
Imepokewa kutoka kwa Anas amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
إذَا حُمَّ أَحَدُكُمْ فَلْيُرَشَّ عَلَيْهِ الْمَاءُ الْبَارِدُ ثَلاثَ لَيالٍ مِنَ السَّحَرِ
“Mmoja Wenu akiugua homa, basi na arashiziwe maji baridi siku tatu kutokea usiku wa manane.” [Imepokewa na Abuu Ya’-laa katika Musnad (379), Al-Hakam (4/200) na (401). Nimesema: Isnaad yake ni Swahiyh, imesahihishwa na Al-Hakam na Adh-Dhahabiy (Rahimahuma-Allaah) kwa sharti la Muslim, na imewafikiwa na Shaykh wetu Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika Asw-Swahiyhaa (1301).
Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
لاَ تَسُبَّهَا فإنها تَنْفِى الذُّنُوبَ، كما تَنْفِى النَّارُ خَبَثَ الْحَدِيدِ
“Homa ni joto katika joto la Jahannam, basi liepusheni nanyi kwa maji baridi.” [Imepokewa na Ibn Maajah (3475). Nimesema: Isnaad yake ni Swahiy, na watu wake ni thiqah; kama alivyosema Al-Buwswariy (Rahimahu Allaah) katika Zawaid na kusahihishwa na Shaykh wetu Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah)]
Na pia:
عَنْ جَابِرُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَى أُمِّ السَّائِبِ أَوْ أُمِّ الْمُسَيَّبِ فَقَالَ: ((مَا لَكِ يَا أُمَّ السَّائِبِ)) أَوْ ((يَا أُمَّ الْمُسَيَّبِ تُزَفْزِفِينَ؟)) قَالَتْ: "الْحُمَّى لاَ بَارَكَ اللَّهُ فِيهَا" فَقَالَ: ((لاَ تَسُبِّي الْحُمَّى فَإِنَّهَا تُذْهِبُ خَطَايَا بَنِي آدَمَ كَمَا يُذْهِبُ الْكِيرُ خَبَثَ الْحَدِيدِ)) مسلم
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwa Ummu As-Saaib akasema: “Je, una nini ee Ummus-Saaib?” Akasema: Homa Allaah Asiibariki [ilaaniwe] Akasema: “Usiitukane homa kwani inaondosha dhambi za mwana Aadam kama tanuri la muhunzi linavyoodosha uchafu wa chuma.” [Muslim (2575)]
Kwa kuwa homa hufuatiwa na himaya ya vyakula vibaya, na kula vyakula na madawa yenye manufaa, na kufanya hivyo kuna faida katika kusafisha mwili, na kutowesha uchafu na ziada yake, kadhalika kuusafisha na maada mbaya, homa hufanya kile kinachofanywa na moto kwenye chuma kuondosha uchafu wake. Na kusafisha asili yake ya chuma: ndio maana ikafanana sana homa na moto wa kwenye tanuri la kuua vyuma ambao husafisha maada asili ya chuma kiasi hiki ndicho kinachojulikana na matabibu.
Ama homa kusafisha moyo hata ukasafika kutokana na taka zake jambo hili analijua matabibu wa nyoyo. Wanalikuta liko sawa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyowaelezea, lakini maradhi ya moyo ikiwa yamefikia kiwango cha kukatisha tamaa kupona katika tiba hii haifai.
Basi kwa maana hiyo, homa ina faida kwa mwili na moyo. Ikiwa homa ina nafasi hii basi kuilaani ni dhulma na ni uadui. Mara moja nilikumbuka, nikiwa naugua homa, kauli ya mshairi anayeitukana homa:
***
Amenitembelea anayekumbusha dhambi na ameaga.
Aangamie kabisa mgeni huyo ajaye na aagaye.
Ameniuliza wakati akiniaga,
Unataka nini?
Nikamjibu usirudi tena hapa!
***
Nikasema: Aangamie yeye; ameitukana kile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekikataza kutukana kama angetaka angesema:
***
Anayefikirisha madhambi amenitembelea,
karibu mgeni ajaye na aagaye.
Ameuliza wakati akiniaga,
Wataka nini? Nikamwambia usiondoke.
***
Angesema hivyo, ilikuwa bora kwake, hapo homa, ikaniondoka haraka.
[1] Hali zote za homa ikipanda hutibiwa kwa njia ya maji katika hali mbili: a) Kutokea nje kwa njia ya مكمدات (bendeji au taula, au kitambaa kinachowekwa juu ya sehemu iliyojeruhiwa) iliyokuwa ni baridi au yenye barafu, kwa ajili ya kushusha joto. b) Mwenye homa kunywa maji mengi, hili linasaidia viungo vya mwili na zaidi figo kufanya kazi zake sawasawa.
[2] Al-Baghwiy amesema: katika Sharh As-Sunnah (1/359) na kauli yake: “Elekeeni Mashariki au Magharibi” ni maelezo kwa watu wa Madiynah, na wale ambao Qiblah chao ni muelekeo huo. Ama wale ambao Qiblah chao ni muelekeo wa Mashariki ama Magharibi basi hawa wataelekee Kusini ama Kaskazini.”
[3] Imaam Ibn Muflih (Rahimahu Allaah) amesema: katika Al-Aadab Ash-Shar’iyyah’ (3/100): Wamesema baadhi ya matabibu: “Hili ni bora kuliko tiba ya ugonjwa huu ikiwa imetokea Hijaaz, na huo ni mji wenye joto jingi na kavu, na joto kali ni dhaifu katika wakazi wake wa ndani, na kuwamwagia maji katika wakati ule uliotajwa (nao ni siku iliyo wazi kabisa) inapasa kukusanya joto kubwa lililosambaa lililotapakaa mwilini unaobebaa nguvu yote, na hivyo kuwa na nguvu yenye kusukuma na hukusanyika katika maeneo tofauti ya kiwiliwili kwenda ndani yake ambapo ndipo penye maradhi yale, na itadhihiri baki ya nguvu yake katika kuondosha maradhi yaliyotajwa, na hivyo kuyasukumu kwa idhinii ya Allaah (Ta’aalaa).
[4] Kwa hakika baadhi ya maradhi ya zama hizi, mfano maradhi ya Romatizim (rheumatism) ambayo mishipa huwa inavimba, inamfanya mtu asiweze harakati yoyote, au maradhi ya Zuhri yaliyozidi katika ubongo hali huwa nzuri kwa kupanda joto la kiwiliwili; yaani katika hali mbali mbali za homa; na hiyo ni miongoni mwa mlolongo wa njia za matibabu katika hali hizi: Homa ya viwanda; yaani: Kutengeneza hali ya homa ya mgonjwa kwa sindano ya mada maalum.
[5] Tabibu wa kigiriki mwenye vumbuzi nyingi katika upasuaji. Ni miongoni mwa rejea nyingi za Waarabu, alifariki mwaka (201).
[6] Jina lake ni Abu Bakr Muhammad bin Zakariyyah, alizaliwa katika mji wa Ar-Ray, na akanasibishwa nao na akapewa jina la Galinus Al-‘Arab, kwa umaarufu wake.
[7]Jina la kitabu chenyewe ni ‘Al-Haawiy fiy Swinaa’ah Atw-Twibb’ yenye mijeledi thelathini.
[8] Nimesema: Vivyo hivyo tiba ya zama hizi maji hunufaisha katika kutibu homa. Dr. Mahmuwd An-Nusaimiy amesema katika: ‘Atw-Twibb An-Nabawiy wal-‘Ilm Al-Hadiyth’ (3/211): “Kwa hakika dawa anuwai zenye kutibu homa mbali mbali hazikuwa zinafahamika kabla ya karne ya tisa, na ya kuwa kushuka kwa joto maarufu katika tiba ya zama hizi, ambayo yalivumbuliwa mapema kama vile kwinini na asprini, hazikusambaa ulimwenguni kabla ya karne hiyo, na hivyo utumiaji wa dawa kwa kupunguza joto ni la mwanzo.
[9] Miongoni mwa mashairi ya ‘Urwah bin Adhiynah; kama ilivyo kwenye ‘Ash-Sha’r wash-Shu’araa’ (uk 580) na ‘Wafiyaat Al-A’yaan’ (2/394).