Kauli Za Salaf Kuthibitisha Adhabu Ya Kaburi

Kauli Za Salaf Kuthibitisha Adhabu Ya Kaburi

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

1.   Sufyan bin 'Uyaynah (Rahimahu Allaah) Amesema:

"Sunnah ni kumi. Yeyote mwenye kuzikubali amekamilisha Sunnah na mwenye kukataa chochote katika hizo ameiwacha Sunnah; kukubali Qadar (makadirio ya Allaah), kuwatambua Abuu Bakr na 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa), mto ulioko Pepo, Ash-Shafaa'ah, Miyzaan, Swiraatw, Iymaan, Iymaan ni maneno na matendo, Qur-aan ni maneno ya Allaah, adhabu ndani ya kaburi, kufufuliwa siku ya hesabu na kutokubali yakuwa Muislamu yeyote bila ya shaka atakuwa Peponi au motoni" [(15) Sharh Uswuwl I'tiqaad Ahlis-Sunnah wal Jamaa'ah (namba 312)]

 

 

 

2.   Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Bila shaka Al-Qadar (kudura za Allaah): yote ya kheri na shari ni kutoka kwake Allaah Mwenye Uwezo na Nguvu. Bila shaka adhabu ya kaburi ni jambo la kweli, kuulizwa kwa wale walioko makaburini ni kweli, kufufuliwa ni kweli, kufanyiwa hesabu ni kweli, Pepo na moto ni kweli. Jambo lolote linalohusiana ndani ya Sunnah na kutajwa na ‘Ulamaa na wafuasi wao kote katika ardhi za Waislamu ni kweli." [Manaaqib Ash-Shafi'iy (1/415) cha Al-Bayhaqiy]

 

 

 

3.   Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Kutoka katika Sunnah ambayo mtu yeyote akiiacha au kutoikubali na kutokua na iymaan nayo basi hatokua katika sisi watu wake! (Kisha akataja) iymaan katika adhabu ya kaburi ni jambo la kweli. Mja ataulizwa maswali kuhusu Dini yake na Rabb wake. Munkar na Nakiyr na Pepo na Moto vilevile ni mambo ya kweli. [Risaalat As-Sunnah, uk. 72 cha Imaam Ahmad]

 

 

 

4.   Abu Dawuwd (d.275H) (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Sura: Maswali ndani ya kaburi na adhabu ndani ya kaburi." [Kitaabus-Sunnah, uk. 900, sehemu ya Sunan Abiy Daawuwd]

 

 

 

5.   Ibn Qutaybah (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Ahlul-Hadiyth wameungana juu ya ukweli ya kwamba chochote Rabb Akikadiriacho kiwe, basi huwa, na chochote Akikadiriacho kisiwe, basi  hakiwi; ya kwamba Yeye ni Muumbaji wa uzuri na uovu; ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah, haikuumbwa, ya kwamba Allaah Ataonekana siku ya malipo, kuwafadhilisha Abuu Bakr na 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa), kuwa na iymaan ya adhabu ya kaburi. Hawakhitalifiani katika mambo haya. Yeyote mwenye kupinga mambo haya basi wao humkataa, humchukia na kumtangaza mtu kama huyo kuwa ni mzushi na hujiweka mbali nae."  [Ta-wiyl Mukhtalifil-Hadiyth, uk. 18)]

 

 

 

6.   Imaam Atw-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Huu ni ufafanuzi wa ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah juu ya njia ya ‘Ulamaa wa Dini hii; Abuu Haniyfah An-Nu'maan bin Thaabit Al-Kuwfiy, Abuu Yuwsuf Ya’quwb bin Ibraahiym Al-Answaariy na Abuu Abdillaah Muhammad bin Al-Hasan Ash-Shaybaaniy (Rahimahumu Allaah) na Awaridhie wote, na iymaan yao juu ya misingi ya Dini na 'Aqiydah yao juu ya Allaah…Mpaka akafikia aliposema: Walisema tuna iymaan na Malaika wa mauti ambaye kazi yake ni kutoa roho za watu wote ulimwenguni; na katika adhabu ya kaburi kwa wale wanaostahili. [Aqiydatu Atw-Twahaawiyyah (79-80)]

 

 

 

7.   Abul-Hassan Al-Ash'ariy (Rahimahu Allaah) Amesema:

"Mu'tazilah walikataa adhabu ndani ya kaburi. Imepokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa njia nyingi na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Hakuna kitu kilichopokewa kutoka kwa hata mmoja wao kuhusu kupinga au kukataa jambo hili (adhabu ya kaburi), kufikia kiwango ambapo kumepatikana ijmaa' (makubaliano) kutoka kwa Maswahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)" [Al-Ibaanah 'An Uswuwl Ad-Diyaanah, uk. 201)]

 

 

Pia akaendelea kusema: “Kumepatikana makubaliano ya kwamba adhabu ya kaburi ni jambo la kweli, na kwamba watu watatahiniwa na kuulizwa maswali ndani ya makaburi yao. Kwa hivyo, Allaah Atuthibitishe sisi na kile akipendacho."  [Risaalah ilaa Ahlith-Thaghr, uk. 279 cha Abul-Hasan Al-Ash'ariy].

 

 

 

8.   Imaam Al-Aajuriy (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Sura: taswdiyq (kuthibitisha) na kuamini adhabu ya kaburi "ambapo ameleta Ahaadiyth zilizopokewa na Al-Bukhaariy na Muslim na amemalizia sura kwa kusema: "Wale watu wanaokataa Ahaadiyth hizi, hapana usalama kwao isipokua wako kwenye upotofu ulio mbali na wamo katika hasara kubwa."  [Ash-Shariy’ah, uk. 358-364 cha Al-Aajurriy]

 

 

 

9.   Ibn Abiy Haatim (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

“Njia tuliyochagua ni kumfuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba, Taabi'iyn na wale wote waliowafuata wao kwa wema, yakiandamana na kujiepusha na mambo ya uzushi, kushikamana na njia ya Ahlul-Athar (wapokezi wa riwaayah) kama vile Abuu 'Abdillaah Ahmad bin Hanbal, Is-haaq bin Ibraahiym, Abuu 'Ubayd Al-Qaasim bin Salaam na Ash-Shaafi'iy, kushikamana na Kitabu (Qur-aan) Sunnah na njia za Maimaam wenye kufuata riwaayah za Salaf, kuchukua yaliochukuliwa na Ahlus-Sunnah katika miji tofauti mpaka aliposema: "Iymaan yaongezeka na yapungua na tuna iymaan katika adhabu ya kaburi." [Ahlus-Sunnah wal I'tiqaadid-Diyn (namba 14)]

 

 

 

10.   Imaam Al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) Amesema:

"Iymaan katika adhabu ya kaburi na Munkar na Nakiyr." [Sharhus-Sunnah (namba 18)]

 

 

 

11.   Al-Ismaa’iliy (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Tambua na tanabahi - Allaah Aturehemu pamoja na wewe – ya kwamba njia ya Ahlul-Hadiyth, Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa'ah ni kukubali kidhati Iymaan kuhusu Allaah, Malaika Wake, Manabii Wake na kukubali chochote kilichoandikwa ndani ya Kitabu cha Allaah Ta’alaa - na mambo sahihi yalioyopokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka akasema; "Adhabu ndani ya kaburi ni jambo la kweli." [I'tiqaad Aimmatil-Hadiyth (namba 22)]

 

 

 

12.   Al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

Katika Sura: Yale yaliotajwa katika Sunnah kuhusu ‘Aqiydah ya moyo kutokana na mambo ya waajib katika Dini. Miongoni mwa hayo ni: Iymaan ndani ya moyo na kutamka kwa ulimi ya kwamba Allaah Peke  Yake Ndiye Muabudiwa wa haki, na mwengine yeyote asiyekua Allaah hana haki ya kuabudiwa." Kisha akaendelea mpaka alipofikia kusema: "Na adhabu ndani ya kaburi ni jambo la kweli na Waumini watatahiniwa ndani ya makaburi yao." [Imepokewa na Ibn Al-Qayyim katika Ijtimmaa Al-Juyuuwshil-Islaamiyyah (uk152)]

 

 

 

13.   Ibn Abiy Aamniyn (Rahimahu Allaah) Amesema:
 

"Ahlus-Sunnah wana Iymaan kuhusu adhabu ya kaburi, Allaah Atukinge nayo sote." [Uswuwl As-Sunnah (swali namba 7)]

 

 

 

14.   Imaam Al-Laalikaaiy (Rahimahu Allaah) Amesema:

"Sura: Riwaayah kuhusu yaliyopokewa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na ukweli ya kwamba wakati Waislamu wakiteremshwa ndani ya makaburi yao, wataulizwa na Munkar na Nakiyr, na kwamba adhabu ndani ya kaburi ni kweli na kuiamini ni waajib." [Sharh Uswuwl I'tiqaad Ahlis-Sunnah Wal-Jamaa'ah (6/1127) cha al-Laalikaaiy]

 

 

 

15.   Imaam Al-Bayhaqiy (Rahimahu Allaah) Amesema.

"Sura: Iymaan katika adhabu ya kaburi." [Al-I'tiqaad, uk. 107 cha Al-Bayhaqiy]

 

 

Share