094-Aayah Na Mafunzo: Kila Moja Atafika Siku Ya Qiyaamah Pekee Akiwa Uchi Kama Alivyozaliwa Na Akiacha Kila Kitu Nyuma Yake
Aayah Na Mafunzo
Al-An’aam 94
094-Kila Moja Atafika Siku Ya Qiyaamah Pekee Akiwa Uchi Kama Alivyozaliwa
Na Akiacha Kila Kitu Nyuma Yake
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَقَدْ جِئْتُمُونَا فُرَادَىٰ كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَتَرَكْتُم مَّا خَوَّلْنَاكُمْ وَرَاءَ ظُهُورِكُمْ ۖ وَمَا نَرَىٰ مَعَكُمْ شُفَعَاءَكُمُ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ أَنَّهُمْ فِيكُمْ شُرَكَاءُ ۚ لَقَد تَّقَطَّعَ بَيْنَكُمْ وَضَلَّ عَنكُم مَّا كُنتُمْ تَزْعُمُونَ ﴿٩٤﴾
Na kwa yakini mmetujia mmoja mmoja kama Tulivyokuumbeni mara ya kwanza, na mmeyaacha nyuma yenu yote Tuliyokuruzukuni. Na Hatuwaoni pamoja nanyi waombezi wenu ambao mlidai kwamba wao ni washirika wenu. Kwa yakini yamekatika (mahusiano) baina yenu na yamekupoteeni mliyokuwa mkidai. [Al-An'aam: 94]
Mafunzo:
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلا)) قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ، النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ قَالَ: ((يَا عَائِشَةُ! الأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يُهِمَّهُم ذلِكَ)) وَفِي رِواية: ((ألأَمْرُ أَهَمُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Watu watafufuliwa Siku ya Qiyaamah ilhali hawana viatu, wako uchi, ni mazunga [hawakutahiriwa])). Nikamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Wanaume na wanawake wote watatazamana? Akasema: ((Ee ‘Aaishah! Hali itakuwa ngumu mno hata hawatoweza kushughulika na jambo hilo!))
Katika riwaayah nyingine imesema: ((Hali itakuwa ngumu mno kiasi kwamba hawatoweza kutazamana)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Bin Aadam husema: “Mali yangu, mali yangu! Lakini mali gani uliyonayo isipokuwa uliyokwishaila ukaimaliza, au uliyoivaa ikachakaa, au uliyoitolea swadaqah ikatangulia (kuwa akiba yako ya Aakhirah). Ama nyingineyo utoandoka duniani na kuwaachia watu.” [Muslim].