09-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Twahaarah: Mlango Wa Tayammum (Kujitwaharisha Kwa Mchanga)
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتابُ الطَّهارَة
Kitabu Cha Twahaarah
بَابُ اَلتَّيَمُّمِ
09-Mlango Wa Tayammum (Kujitwaharisha Kwa Mchanga)
107.
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا; أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {أُعْطِيتُ خَمْسًا لَمْ يُعْطَهُنَّ أَحَدٌ قَبْلِي: نُصِرْتُ بِالرُّعْبِ مَسِيرَةَ شَهْرٍ، وَجُعِلَتْ لِي اَلْأَرْضُ مَسْجِدًا وَطَهُورًا، فَأَيُّمَا رَجُلٍ أَدْرَكَتْهُ اَلصَّلَاةُ فَلْيُصَلِّ} وَذَكَرَ اَلْحَدِيثَ
وَفِي حَدِيثِ حُذَيْفَةَ عِنْدَ مُسْلِمٍ: {وَجُعِلَتْ تُرْبَتُهَا لَنَا طَهُورًا، إِذَا لَمْ نَجِدِ اَلْمَاءَ}
وَعَنْ عَلِيٍّ رضى الله عنه عِنْدَ أَحْمَدَ: {وَجُعِلَ اَلتُّرَابُ لِي طَهُورًا}
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Nimepewa mambo matano hakupewa yeyote kabla yangu: Nimenusuriwa na (kutiwa) kizaazaa (nyoyoni mwa maadui) kwa mwendo wa mwezi. Na nimefanyiwa ardhi kuwa sehemu ya kufanyia ‘ibaadah na kujitwaharishia[1], basi mtu mtu yeyote katika ummah wangu akifikiwa na Swalaah, aswali.”[2]
Katika Hadiyth ya Khudhayfah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) iliyoandikwa na Muslim inaeleza:
“Mchanga[3] wake (au udongo) umefanywa kitoharisho changu ikiwa hatukupata maji.”
Na Hadiyth ya ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) iliyoandikwa na Ahmad inasema: “Ardhi (mchanga) wake umefanywa kitoharisho kwa ajili yangu.”
108.
وَعَنْ عَمَّارِ بْنِ يَاسِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {بَعَثَنِي اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فِي حَاجَةٍ، فَأَجْنَبْتُ، فَلَمْ أَجِدِ اَلْمَاءَ، فَتَمَرَّغْتُ فِي اَلصَّعِيدِ كَمَا تَمَرَّغُ اَلدَّابَّةُ، ثُمَّ أَتَيْتُ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم فَذَكَرْتُ ذَلِكَ لَهُ، فَقَالَ: "إِنَّمَا كَانَ يَكْفِيكَ أَنْ تَقُولَ بِيَدَيْكَ هَكَذَا" ثُمَّ ضَرَبَ بِيَدَيْهِ اَلْأَرْضَ ضَرْبَةً وَاحِدَةً، ثُمَّ مَسَحَ اَلشِّمَالَ عَلَى اَلْيَمِينِ، وَظَاهِرَ كَفَّيْهِ وَوَجْهَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
وَفِي رِوَايَةٍ لِلْبُخَارِيِّ: وَضَرَبَ بِكَفَّيْهِ اَلْأَرْضَ، وَنَفَخَ فِيهِمَا، ثُمَّ مَسَحَ بِهِمَا وَجْهَهُ وَكَفَّيْهِ
Kutoka kwa ‘Ammaar bin Yaasir[4] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alinituma katika haja fulani, kisha nikapata janaba na sikupata maji, nilijiviringisha kwenye mchanga kama mnyama, nikarejea kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) nikamtajia tukio hilo. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaniambia: “Inakutosha kufanya hivi kwa mikono.” Akapiga mikono yake mara moja juu ya mchanga, na akaupangusa mkono wa kushoto juu ya kiganja cha mkono wake wa kulia mbele na nyuma na uso wake.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi ni la Muslim]
Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy: “Na (Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)) akapiga viganja vyake viwili ardhini[5], halafu akavipuliza, akapangusa navyo usoni na viganja vyake.”
109.
وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {التَّيَمُّمُ ضَرْبَتَانِ ضَرْبَةٌ لِلْوَجْهِ، وَضَرْبَةٌ لِلْيَدَيْنِ إِلَى اَلْمِرْفَقَيْنِ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَصَحَّحَ اَلْأَئِمَّةُ وَقْفَهُ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Tayammum (kujitwaharisha kwa mchanga), ni mapigo mawili, pigo moja kwa ajili ya uso jingine kwa ajili ya mikono hadi kwenye viwiko viwili[6].”” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy, na akaisahihisha Imaam kama Mawquwf]
110.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {اَلصَّعِيدُ وُضُوءُ اَلْمُسْلِمِ، وَإِنْ لَمْ يَجِدِ اَلْمَاءَ عَشْرَ سِنِينَ، فَإِذَا وَجَدَ اَلْمَاءَ فَلْيَتَّقِ اَللَّهَ، وَلْيُمِسَّهُ بَشَرَتَهُ} رَوَاهُ اَلْبَزَّارُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ اَلْقَطَّانِ، و لَكِنْ صَوَّبَ اَلدَّارَقُطْنِيُّ إِرْسَالَهُ
وَلِلتِّرْمِذِيِّ: عَنْ أَبِي ذَرٍّ نَحْوُهُ، وَصَحَّحَهُ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mchanga ni wudhuu wa Muislamu hata kama hatapata maji kwa miaka kumi[7], akiyapata amche Allaah na ayagusishe ngozi yake.” [Imetolewa na Al-Bazzaar, na akaisahihisha Ibn Al-Qatwaan. Lakini aliidhinisha Ad-Daaruqutwniy kama Mursal]
Na katika Riwaayah ya At-Tirmidhiy amepokea Hadiyth inayofanana na hiyo kutoka kwa Abuu Dharr[8], ambayo aliisahihisha.
111.
وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: {خَرَجَ رَجُلَانِ فِي سَفَرٍ، فَحَضَرَتْ اَلصَّلَاةَ وَلَيْسَ مَعَهُمَا مَاءٌ فَتَيَمَّمَا صَعِيدًا طَيِّبًا، فَصَلَّيَا، ثُمَّ وَجَدَا اَلْمَاءَ فِي اَلْوَقْتِ. فَأَعَادَ أَحَدُهُمَا اَلصَّلَاةَ وَالْوُضُوءَ، وَلَمْ يُعِدِ اَلْآخَرُ، ثُمَّ أَتَيَا رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَذَكَرَا ذَلِكَ لَهُ، فَقَالَ لِلَّذِي لَمْ يُعِدْ: "أَصَبْتَ اَلسُّنَّةَ وَأَجْزَأَتْكَ صَلَاتُكَ" وَقَالَ لِلْآخَرِ: "لَكَ اَلْأَجْرُ مَرَّتَيْنِ"} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، و النَّسَائِيُّ
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al Khudriy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Watu wawili walikwenda safarini, Swalaah ikawadia, hawakuwa na maji. Walitayammam kwa mchanga safi na wakaswali. Baadaye wakapata maji wakati wa Swalaah. Mmoja wao akarudia Swalaah na kutawadha, mwenzie hakurudia. Walipofika kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) wakamueleza hilo, akamgeukia yule ambaye hakurudia akamwambia kuwa: “Umefuata Sunnah, na Swalaah yako ya kwanza imekutosheleza[9].” Akamwambia yule aliyerudia kutawadha na kuswali akamwambia: “Wewe una malipo mara mbili[10].”” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]
112.
وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا فِي قَوْلِهِ عَزَّ وَجَلَّ ﴿وَإِنْ كُنْتُمْ مَرْضَى أَوْ عَلَى سَفَرٍ﴾ قَالَ: "إِذَا كَانَتْ بِالرَّجُلِ اَلْجِرَاحَةُ فِي سَبِيلِ اَللَّهِ وَالْقُرُوحُ، فَيُجْنِبُ، فَيَخَافُ أَنْ يَمُوتَ إِنْ اِغْتَسَلَ: تَيَمَّمَ" . رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ مَوْقُوفًا، وَرَفَعَهُ اَلْبَزَّارُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَالْحَاكِم
Kutoka kwa Ibn “Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuhusu kauli yake Allaah (عَزَّ وَجَلَّ): “...Na mkiwa wagonjwa[11] au mko safarini…” [Al-Maaidah (5: 6)] kuwa: “Ikiwa mtu ana jeraha aloumia akiwa katika (jihaad) njia ya Allaah, kisha akapata janaba, na akaogopa kuwa atakufa endapo ataoga, basi atayammam.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy katika Hadiyth Mawquwf, na Al-Bazzaar katika Hadiyth Marfuw’aa, na wakaisahihisha Ibn Khuzaymah na Al Haakim]
113.
وَعَنْ عَلِيٍّ رضى الله عنه قَالَ: {اِنْكَسَرَتْ إِحْدَى زَنْدَيَّ فَسَأَلَتْ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَأَمَرَنِي أَنْ أَمْسَحَ عَلَى اَلْجَبَائِرِ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَه بِسَنَدٍ وَاهٍ جِدًّا
Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mkono wangu mmoja ulivunjika, nikamuuliza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) nifanyeje, akaniamrisha nipanguse juu ya bendeji[12].” [Imetolewa na Ibn Maajah kwa Isnaad dhaifu sana]
114.
وَعَنْ جَابِرٍ بْنُ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا فِي اَلرَّجُلِ اَلَّذِي شُجَّ، فَاغْتَسَلَ فَمَاتَ :{"إِنَّمَا كَانَ يَكْفِيهِ أَنْ يَتَيَمَّمَ، وَيَعْصِبَ عَلَى جُرْحِهِ خِرْقَةً، ثُمَّ يَمْسَحَ عَلَيْهَا وَيَغْسِلَ سَائِرَ جَسَدِهِ"} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ بِسَنَدٍ فِيهِ ضَعْفٌ، وَفِيهِ اِخْتِلَافٌ عَلَى رُوَاتِهِ
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuhusu mtu aliyejeruhiwa kichwani akaoga na akafariki, kwamba Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ilikuwa inamtosha kutayammam, kisha afunge bendeji na apanguse maji juu yake, kisha aoshe sehemu nyingine za mwili wake.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, Isnaad yake ni dhaifu, na kuna kutofautiana wasimulizi wake]
115.
وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {مِنْ اَلسُّنَّةِ أَنْ لَا يُصَلِّيَ اَلرَّجُلُ بِالتَّيَمُّمِ إِلَّا صَلَاةً وَاحِدَةً، ثُمَّ يَتَيَمَّمُ لِلصَّلَاةِ اَلْأُخْرَى} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ جِدًّا
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Ni Sunnah mtu kutokuswali zaidi ya Swalaah moja[13] kwa Tayammum moja, kisha atayammam kwa ajili ya Swalaah nyingine.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy kwa Isnaad dhaifu sana[14]]
[1] Maana yake ni kwamba, kama maji hakuna, mtu asipoteze nusu ya wakati wa Swalaah kwa kutafuta maji.
[2] Vitu vingine hivi vitatu ni: (a) Ngawira amefanyiwa ziwe Halaal, (b) Shufaa siku ya Qiyaamah, (c) Unabii kwa ulimwengu wote.
[3] Mchanga au udongo na vitu vyote vingine vitokanavyo na udongo vinahesabika kuwa sawa, na Tayammam kwayo inaruhusiwa. Lakini siyo metali kama antimoni, arseniki, n.k. ambavyo havimo katika fungu la udongo.
[4] ‘Ammaar alipewa jina la utani la Abul-Yaqzaan, na alikuwa miongoni mwa Swahaba waandamizi wa mwanzo, aliteswa kule Makkah kwa ajili ya Iymaan yake. Alishiriki katika Hijrah zote mbili, na katika vita vya Badr na vita vyote muhimu. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuambia kuwa: “Ee ‘Ammaar, kundi la wapotofu litakuua wewe.” Hiyo ilitokea Siffiyn mnamo mwaka wa 36 A.H wakati akiwa na ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ), aliuawa na askari wa Mu’aawiya akiwa na umri wa miaka 73.
[5] Hadiyth hii inaongelea kuhusu Tayammam (kujitwaharisha kwa udongo). 'Ulamaa wa Fiqh wanasema kuwa pigo moja tu linatosha kwa uso na mikono yote miwili. Wengine wanasema kuwa mapigo mawili ni lazima, moja kwa uso na jingine kwa mikono, kama inavyotajwa katika Hadiyth hii inayofuata. Lakini Hadiyth zote zinazotaja mapigo mawili ni dhaifu.
[6] ‘Ulamaa wa Hadiyth wameihesabu Hadiyth hii kuwa ni dhaifu na milolongo yake yote ni dhaifu.
[7] Inamaanisha kwamba, wakati wa dharura, mchanga (udongo) ni badala kamili ya maji, na unakidhi shughuli zote za utwahirishaji, uwe ni kutawadha, au kuoga. Kwa kila Tayammam moja, matendo mengi ya faradhi yanaweza kufanywa, iwapo hakuna mazingira yanayoubatilisha.
[8] Jina la Abuu Dharr lilikuwa ni Jundub bin Junaadah, naye alikuwa miongoni mwa Swahaba maarufu na ni mtu aliyejinyima anasa za kimwili. Alisilimu mapema sana kule Makkah, kisha akaenda kwa watu wake. Alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) Al-Madiynah, na baadaye akalowea na akafia Rabdha mnamo mwaka wa 32 A.H.
[9] Inamaanisha kwamba, ikiwa mtu amekwisha kuswali Swalaah moja kwa kutumia Tayammam, basi hakuna haja ya kurudia kuswali, hata kama maji yamepatikana baadaye tena kabla wakati wa Swalaah ile haujapita.
[10] Haikuwa lazima kurudia kuiswali Swalaah ile, kama Swalaah ile iliswaliwa kwa wudhuu wa kutayammam. Huyo mtu wa pili alipata malipo maradufu siyo kwa sababu kaswali mara mbili Swalaah moja, bali kwa sababu ya kufanya uamuzi kuhusu tatizo lililowakabili, hata kama uamuzi ule haukuwa sahihi, lakini kuna malipo zaidi kwa uamuzi usiyo sahihi. Sababu ya pili ya kupata malipo mara mbili, inawezekana ni kwamba aliswali mara mbili, mara moja kwa wudhuu wa Tayammam na mara ya pili kwa wudhuu wa maji.
[11] Inamaanisha kuwa ukiwa unataka kuswali lakini kuna kizuizi katika kutawadha au kuoga, Tayammam huwa ni lazima. Hapa ugonjwa ni ugonjwa kweli, siyo vipele au vijipu tu. (Kulingana na Maalik, Hanafi na moja katika maneno ya Imaam Shaafi’). Wengine kama (Ahmad na moja katika maneno ya Imaam shaafi’) kuwa Tayammam hairuhusiwi isipokuwa kwa mgonjwa anayehofia kuwa maji yatamsababishia kifo. Daawuwd anaona kuwa Tayammam inaruhusiwa kwa mgonjwa yoyote bila kujali kama anadhurika na maji au la.
[12] Neno la Kiarabu ni اَلْجَبَائِرِ ambalo hutumika kwa vile vipande vya mbao vinavyowekwa kuuzunguka mkono au mguu uliovunjika ili kuufanya ukae umenyooka saa zote.
[13] Kwa kuwa kutawadha kwa kutayammam ni badala ya kutawadha kwa maji, hufanya kazi namna ile ile. Swalaah nyingi zinaweza kuswaliwa kwa kutawadha kwa maji mara moja tu. Halikadhalika, Swalaah nyingi zinaweza kuswaliwa kwa kutayamamu mara moja tu. Watu wengine baada ya kutayamamu kwa kujamiiana au kwa kuota na kutoa manii husita kuingia Msikitini au kusoma Qur-aan. Hii ni kutia shaka kuovu na ni ushawishi wa shaytwaan tu, na wala usiujali. Hadiyth hii ya Hasan bin ‘Ammaar ni dhaifu katika mlolongo wa wapokezi. Kuna Hadiyth mbili zingine kuhusu kadhia hii hii na zote ni dhaifu.