02-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Adhaan

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ اَلْأَذَانِ

02-Mlango Wa Adhaan[1]

 

 

 

 

 

142.

عَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ زَيْدِ بْنِ عَبْدِ رَبِّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {طَافَ بِي وَأَنَا نَائِمٌ رَجُلٌ فَقَالَ: تَقُولُ: "اَللَّهُ أَكْبَرَ اَللَّهِ أَكْبَرُ،  فَذَكَرَ اَلْآذَانَ  بِتَرْبِيع اَلتَّكْبِيرِ بِغَيْرِ تَرْجِيعٍ،  وَالْإِقَامَةَ فُرَادَى،  إِلَّا قَدْ قَامَتِ اَلصَّلَاةُ  قَالَ: فَلَمَّا أَصْبَحْتُ أَتَيْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   فَقَالَ: "إِنَّهَا لَرُؤْيَا حَقٍّ..."}  اَلْحَدِيثَ. أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ،  وَأَبُو دَاوُدَ،  وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ،  وَابْنُ خُزَيْمَةَ 

وَزَادَ أَحْمَدُ فِي آخِرِهِ قِصَّةَ قَوْلِ بِلَالٍ فِي آذَانِ اَلْفَجْرِ: {اَلصَّلَاةُ خَيْرٌ مِنَ اَلنَّوْمِ}  

وَلِابْنِ خُزَيْمَةَ: عَنْ أَنَسٍ قَالَ: {مِنْ اَلسُّنَّةِ إِذَا قَالَ اَلْمُؤَذِّنُ فِي اَلْفَجْرِ: حَيٌّ عَلَى اَلْفَلَاحِ،  قَالَ: اَلصَّلَاةُ خَيْرٌ مِنَ اَلنَّوْمِ}

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zayd bin ‘Abdi-Rabbih[2] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Mtu mmoja alinitembelea wakati nimelala[3], akaniambia: Sema:

اَللَّهُ أَكْبَرَ اَللَّهِ أَكْبَرُ

“Allaahu Akbar, Allaahu Akbar” (Allaah ni Mkubwa zaidi, Allaah ni Mkubwa zaidi). Akataja Adhaan kwa tamko la

اَللَّهُ أَكْبَر

Allaahu Akbar”

mara nne bila Tarjiy’[4] na Iqaamah mara moja, isipokuwa

قَدْ قَامَتِ اَلصَّلَاةُ 

Qad Qaamati Swalaah”[5]

(Swalaah imekwishakimiwa), ‘Abdullaah akasema: Asubuhi yake nilikwenda kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) naye akasema: “Hiyo ni ndoto ya kweli.” [Hadiyth hii imetolewa na Ahmad na Abuu Daawuwd, na wakaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Khuzaymah]

 

Ahmad aliongeza mwishoni wa Hadiyth hiyo, Hadiyth ya msemo wa Bilaal[6] katika Adhaan ya Alfajiri:

 

اَلصَّلَاةُ خَيْرٌ مِنَ اَلنَّوْمِ

“Asw-Swalaatu khayrun minan-nawm (Swalaah ni bora kuliko usingizi).”

 

 

Ibn Khuzaymah alisimulia kuwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Ni Sunna Muadhini anaposema:

حَيٌّ عَلَى اَلْفَلَاحِ

Hayya ‘alal falaah” (Njooni kwenye kufaulu), aongeze:

 

اَلصَّلَاةُ خَيْرٌ مِنَ اَلنَّوْمِ

Asw-Swalaatu khayrun minan-nawm”

 (Swalaah ni bora kuliko usingizi).”

 

 

 

143.

 عَنْ أَبِي مَحْذُورَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم {عَلَّمَهُ اَلْآذَانَ،  فَذَكَرَ فِيهِ اَلتَّرْجِيعَ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ. وَلَكِنْ ذَكَرَ اَلتَّكْبِيرَ فِي أَوَّلِهِ مَرَّتَيْنِ فَقَطْ 

وَرَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ فَذَكَرُوهُ مُرَبَّعًا 

Kutoka kwa Abuu Mahdhuwrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimfundisha Adhaan, na yeye (msimuliaji) akataja Tarjiy’ ndani yake.” [Imetolewa na Muslim, lakini alitaja Takbiyra, mwanzo wake mara mbili tu[7]]

[Imetolewa na Al-Khamsah, lakini wamesema Takbiyra hutajwa mara nne]

 

 

 

144.

وَعَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {أُمِرَ بِلَالٌ أَنْ يَشْفَعَ اَلْآذَانَ،  وَيُوتِرَ اَلْإِقَامَةَ،  إِلَّا اَلْإِقَامَةَ،  يَعْنِي قَوْلَهُ: قَدْ قَامَتِ اَلصَّلَاةُ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ،  وَلَمْ يَذْكُرْ مُسْلِمٌ اَلِاسْتِثْنَاءَ  

وَلِلنَّسَائِيِّ: {أَمَرَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم   بِلَالاً}

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Bilaal aliamrishwa aitamke Adhaan kwa shufwa (mara mbili)[8], na Iqaamah kwa witri[9] isipokuwa “Qad Qaamati Swalaah” (yaani Swalaah imekwishakimiwa).” [Al-Bukhaariy, Muslim; lakini Muslim hakutaja huko kuvua]

 

 

Na An-Nasaaiy alipokea: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuamrisha Bilaal.”

 

 

 

145.

وَعَنْ أَبِي جُحَيْفَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {رَأَيْتُ بِلَالاً يُؤَذِّنُ وَأَتَتَبَّعُ فَاهُ،  هَاهُنَا وَهَاهُنَا،  وَإِصْبَعَاهُ فِي أُذُنَيْهِ}  رَوَاهُ أَحْمَدُ،  وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ 

وَلِابْنِ مَاجَهْ: وَجَعَلَ إِصْبَعَيْهِ فِي أُذُنَيْهِ 

وَلِأَبِي دَاوُدَ: {لَوَى عُنُقَهُ،  لَمَّا بَلَغَ "حَيَّ عَلَى اَلصَّلَاةِ " يَمِينًا وَشِمَالاً وَلَمْ يَسْتَدِرْ}

وَأَصْلِهِ فِي اَلصَّحِيحَيْنِ 

Kutoka kwa Abuu Juhayfah[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nimemuona Bilaal akiadhini, nami nilikuwa nikifuatisha kwa kumtazama mdomo wake akiugeuza upande huu (kuume), na upande ule (kushoto)[11], kaweka vidole vyake masikioni.” [Imetolewa na Ahmad na At-Tirmidhiy aliyeipa daraja la Swahiyh]

 

Na katika mapokezi ya Ibn Maajah: “Na aliweka vidole vyake viwili kwenye masikio yake.”

 

Na mapokezi ya Abuu Daawuwd: “Aligeuza shingo yake kuumeni na kushotoni alipofika:  “Hayya ‘alasw-Swalaah” (njoo katika Swalaah), na hakugeuza mwili wake.” Na chanzo chake ni katika Swahiyh mbili.

 

 

 

146.

وَعَنْ أَبِي مَحْذُورَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم   أَعْجَبَهُ صَوْتُهُ،  فَعَلَّمَهُ اَلْآذَانَ}  رَوَاهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ 

Kutoka kwa Abuu Mahdhuwrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipenda sauti yake[12] kwa hivyo akamfundisha Adhaan.” [Imetolewa na Ibn Khuzaymah]

 

 

 

147.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {صَلَّيْتُ مَعَ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم   اَلْعِيدَيْنِ،  غَيْرَ مَرَّةٍ وَلَا مَرَّتَيْنِ،  بِغَيْرِ أَذَانٍ وَلَا إِقَامَةٍ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

وَنَحْوُهُ فِي اَلْمُتَّفَقِ: عَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا،  وَغَيْرُهُ 

Kutoka kwa Jaabir bin Samurah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nimeswali na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ‘Iyd mbili, siyo mara moja au mara mbili tu[13], bila Adhaan wala Iqaamah.” [Imetolewa na Muslim]

 

Hadiyth kama hiyo imo katika Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) na wengineo.

 

 

 

148.

وَعَنْ أَبِي قَتَادَةٌ فِي اَلْحَدِيثِ اَلطَّوِيلِ،  {فِي نَوْمهُمْ عَنْ اَلصَّلَاةِ  ثُمَّ أَذَّنَ بِلَالٌ،  فَصَلَّى رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   كَمَا كَانَ يَصْنَعُ كُلَّ يَوْمٍ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

وَلَهُ عَنْ جَابِرٍ: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم   أَتَى اَلْمُزْدَلِفَةَ فَصَلَّى بِهَا اَلْمَغْرِبَ وَالْعِشَاءَ،  بِأَذَانٍ وَاحِدٍ وَإِقَامَتَيْنِ}

 وَلَهُ عَنْ اِبْنِ عُمَرَ: {جَمَعَ بَيْنَ اَلْمَغْرِبِ وَالْعِشَاءِ بِإِقَامَةٍ وَاحِدَةٍ}

زَادَ أَبُو دَاوُدَ: {لِكُلِّ صَلَاةٍ} 

وَفِي رِوَايَةِ لَهُ: {وَلَمْ يُنَادِ فِي وَاحِدَةٍ مِنْهُمَا}

Kutoka kwa Abuu Qataadah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) katika Hadiyth ndefu kuhusu: Maswahaba kulala kwao wakapitwa na Swalaah, kisha Bilaal akaadhini na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaswalisha kama alivyokuwa akifanya kila siku[14].” [Imetolewa na Muslim]

 

 Na Jaabir alihadithia: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipofika Muzdalifah[15] aliswali hapo Maghrib na ‘Ishaa kwa Adhaan moja na Iqaamah mbili.”

 

Alihadithia Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikusanya Swalaah ya Maghrib na ya ‘Ishaa kwa Iqaamah moja.”

 

Na Abuu Daawuwd akaongezea: “Kwa kila Swalaah[16].”

 

Na katika Riwaayah nyingine: “Adhaan haikuadhiniwa katika Swalaah yoyote kati ya hizo mbili.”

 

 

 

149.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ،  وَعَائِشَةَ قَالَا: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {إِنَّ بِلَالاً يُؤَذِّنُ بِلَيْلٍ،  فَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّى يُنَادِيَ اِبْنُ أُمِّ مَكْتُومٍ"،  وَكَانَ رَجُلاً أَعْمَى لَا يُنَادِي،  حَتَّى يُقَالَ لَهُ: أَصْبَحْتَ،  أَصْبَحْتَ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

وَفِي آخِرِهِ إِدْرَاجٌ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar na ‘Aaishah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) wamesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Bilaal huadhini usiku[17], kwa hivyo kuleni na kunyweni mpaka Ibn Ummi Maktuwm[18] aadhini.” Na Ibn Ummi Maktuwm alikuwa kipofu na kwa hivyo hakuadhini mpaka aambiwe: “Kumekucha, kumekucha.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na katika sehemu yake ya mwishoni mwake kuna Idraaj[19]

 

 

 

150.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ; {إِنَّ بِلَالاً أَذَّنَ قَبْلَ اَلْفَجْرِ،  فَأَمَرَهُ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم   أَنْ يَرْجِعَ،  فَيُنَادِيَ: "أَلَا إِنَّ اَلْعَبْدَ نَامَ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَضَعَّفَهُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Bilaal aliadhini kabla ya kupambazuka, na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamwambia arejee[20] na aadhini: Mja wa Allaah (Yaani Bilaal), amelala (na hiyo ndiyo sababu ya kosa lile).” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na ikapewa daraja la dhaifu]

 

 

 

151.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {إِذَا سَمِعْتُمْ اَلنِّدَاءَ،  فَقُولُوا مِثْلَ مَا يَقُولُ اَلْمُؤَذِّنُ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

وَلِلْبُخَارِيِّ: عَنْ مُعَاوِيَةَ 

 وَلِمُسْلِمٍ: {عَنْ عُمَرَ فِي فَضْلِ اَلْقَوْلِ كَمَا يَقُولُ اَلْمُؤَذِّنُ كَلِمَةً كَلِمَةً،  سِوَى اَلْحَيْعَلَتَيْنِ،  فَيَقُولُ: "لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ"}

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kwamba Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkisikia Adhaan semeni[21] kama anavyosema Muadhini.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na Al-Bukhaariy amepokea hivyo hivyo kutokana na uslimulizi wa Mu’aawiyah.

 

Na Muslim alipokea usimulizi wa ‘Umar kuhusu fadhila ya kusema kama anavyotamka Muadhini isipokuwa pale Muadhini anaposema: “Hayya ‘alasw-Swalaah” (Njoo katika Swalaah) na “Hayya ‘alal-falaah” (Njoo kwenye kufaulu) ambapo mtu hutakiwa aseme:  “Laa hawla wa laa quwwata illaa biLLaah” (Hakuna uwezo wala nguvu ila kwa msaada wa Allaah).”

 

 

 

152.

وَعَنْ عُثْمَانَ بْنِ أَبِي الْعَاصِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّهُ قَالَ : يَا رَسُولَ اَللَّهِ اِجْعَلْنِي إِمَامَ قَوْمِي . قَالَ : "أَنْتَ إِمَامُهُمْ،  وَاقْتَدِ بِأَضْعَفِهِمْ،  وَاِتَّخِذْ مُؤَذِّنًا لَا يَأْخُذُ عَلَى أَذَانِهِ أَجْرًا}  أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ،  وَحَسَّنَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ،  وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin Abiy Al-‘Aasw[22] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Ee Rasuli wa Allaah! Niteue niwe Imaam wa watu wangu. Akasema: “Wewe ni Imaam wao, zingatia wadhaifu wao zaidi[23], na uteue Muadhini asiyechukua ujira[24] kutokana na kuadhini.” [Imetolewa na Al-Khamsah, na aliipa daraja la Hasan At-Tirmidhiy, na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

153.

وَعَنْ مَالِكِ بْنِ الْحُوَيْرِثِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ لَنَا اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  {وَإِذَا حَضَرَتِ اَلصَّلَاةُ فَلْيُؤَذِّنْ لَكُمْ أَحَدُكُمْ . ..}  اَلْحَدِيثَ أَخْرَجَهُ اَلسَّبْعَةُ

Kutoka kwa Maalik bin Al-Huwayrith[25] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ametuambia: “Ukifika wakati wa Swalaah, mmoja wenu aadhini[26]….” [Imetolewa na Maimaam Saba]

 

 

 

154.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   قَالَ لِبِلَالٍ : {إِذَا أَذَّنْتَ فَتَرَسَّلْ ،  وَإِذَا أَقَمْتُ فَاحْدُرْ ،  وَاجْعَلْ بَيْنَ أَذَانِكَ وَإِقَامَتِكَ قَدْرَ مَا يَفْرُغُ اَلْآكِلُ مِنْ أَكْلِهِ}  اَلْحَدِيثَ . رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَضَعَّفَهُ .

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimwambia Bilaal: “Unapoadhini, tamka taratibu, na unapokimu kimu haraka, na acha muda baina ya Adhaan na Iqaamah kiasi cha mlaji amalize kula[27] kwake.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy, na akaidhoofisha]

 

 

 

155.

وَلَهُ : عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم   قَالَ : {لَا يُؤَذِّنُ إِلَّا مُتَوَضِّئٌ}  وَضَعَّفَهُ أَيْضًا 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Asiadhini isipokuwa mwenye wudhuu[28].” [Pia ameidhoofisha]

 

 

 

156.

وَلَهُ : عَنْ زِيَادِ بْنِ اَلْحَارِثِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {وَمَنْ أَذَّنَ فَهُوَ يُقِيمُ}  وَضَعَّفَهُ أَيْضًا

Tena At-Tirmidhiy amepokea kuwa Ziyaad bin Al-Haarith[29] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kuadhini ndiye mwenye kukimu[30].” [Pia ameidhoofisha]

 

 

 

157.

وَلِأَبِي دَاوُدَ: فِي حَدِيثِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ زَيْدٍ أَنَّهُ قَالَ : أَنَا رَأَيْتُهُ  يَعْنِي : اَلْأَذَانُ  وَأَنَا كُنْتُ أُرِيدُهُ . قَالَ : "فَأَقِمْ أَنْتَ " وَفِيهِ ضَعْفٌ أَيْضًا 

 Abuu Daawuwd amepokea kutokana na Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zayd kuwa amesema: “Niliiona (yaani Adhaan) ndotoni, nami nilikuwa naitaka (kuitumia), Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Kimu wewe (Swalaah).” [Hadiyth hii pia ni dhaifu]

 

 

 

158.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   {اَلْمُؤَذِّنُ أَمْلَكُ بِالْأَذَانِ ،  وَالْإِمَامُ أَمْلَكُ بِالْإِقَامَةِ}  رَوَاهُ اِبْنُ عَدِيٍّ وَضَعَّفَهُ

وَلِلْبَيْهَقِيِّ نَحْوُهُ : عَنْ عَلِيٍّ مِنْ قَوْلِهِ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Muadhini ana haki zaidi ya kuadhini na Imaam ana haki zaidi ya kukimu.” [Imetolewa na Ibn ‘Adiy na akaidhoofisha]

 

Na Al-Bayhaqiy mfano wake: kutoka kwa ‘Aliy kutoka katika kauli yake.

 

 

 

159.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {لَا يُرَدُّ اَلدُّعَاءُ بَيْنَ اَلْأَذَانِ وَالْإِقَامَةِ}  رَوَاهُ النَّسَائِيُّ ،  وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Dua baina ya Adhaan na Iqaamah haikataliwi.” [Imetolewa na An-Nasaaiy na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

160.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   قَالَ : {مَنْ قَالَ حِينَ يَسْمَعُ اَلنِّدَاءَ : اَللَّهُمَّ رَبَّ هَذِهِ اَلدَّعْوَةِ اَلتَّامَّةِ،  وَالصَّلَاةِ اَلْقَائِمَةِ،  آتِ مُحَمَّدًا اَلْوَسِيلَةَ وَالْفَضِيلَةَ،  وَابْعَثْهُ مَقَامًا مَحْمُودًا اَلَّذِي وَعَدْتَهُ، حَلَّتْ لَهُ شَفَاعَتِي يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ}  أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kusema anaposikia Adhaan:

 اَللَّهُمَّ رَبَّ هَذِهِ اَلدَّعْوَةِ اَلتَّامَّةِ،  وَالصَّلَاةِ اَلْقَائِمَةِ،  آتِ مُحَمَّدًا اَلْوَسِيلَةَ وَالْفَضِيلَةَ،  وَابْعَثْهُ مَقَامًا مَحْمُودًا اَلَّذِي وَعَدْتَهُ

Allaahumma Rabba haadhihid-dda’watit- ttaamah, wasw-Swaalaatil qaaimah, aati Muhammada  al-wasiylata wal fadhwiylah, wab-‘ath-hu maqaaman mahmuwdan alladhiy wa’adtah[31].

 

(Ee Allaah, Rabb wa mwito huu uliotimia, na Swalaah iliyosimama, mpe (Nabiy) Muhammad al-Wasiylah (cheo, daraja), na fadhila[32], na mfikishe daraja yenye kuhimidiwa, ambayo Umemuahidi).

 

Ash-Shafaa’ah (Uombezi) wangu umehalalika kwake Siku ya Qiyaamah.” [Imetolewa na Al-Arba’ah]

 

 

 

 

[1] Maneno yanayounda “Adhaan” yamepangiliwa Kiilaahi. Hayaruhusiwi kuongezwa, kupunguzwa wala kubadilishwa. Maneno hayo alipewa ‘Abdullaah bin Zayd Answaariy na ‘Umar bin Khattwaab na Malaika ndotoni, na yakathibitishwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), yakakwezwa kufikia hadhi ya Wahyi. Kuna dalili pia katika Qur-aan juu ya hili.

 

[2] ‘Abdullaah bin Zayd ni Answaar Mkhariji (wa Al-Madiynah). Alipewa jina la utani, Abuu Muhammad. Alishuhudia Al-‘Aqaba, Badr na Vita vingine muhimu. Alionyeshwa ndotoni namna ya kuita watu kuenda kuswali katika mwaka wa kwanza wa Hijrah, baada ya kujengwa kwa Msikiti wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Alifariki mwaka 32 A.H. akiwa na umri wa miaka 64.

 

[3] Waislaam walipoongezeka, tatizo la kuwaita watu waende kuswali likajitokeza. Mapendekezo mengi yalitolewa. Wengine wakapendekeza kupuliza kombe (gamba ya wanyama wa baharini) au pembe, na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema hiyo ilikuwa njia ya Mayahudi. Wengine wakapendekeza kuwasha moto, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema hiyo ilikuwa njia ya Majusi. Hawakufikia uamuzi wowote. Lakini usiku ule, ‘Abdullaah bin Zayd akamuota mtu amesimama na kombe mkononi mwake. ‘Abdullaah akamuuliza iwapo anaweza kumuuzia lile. Yule mtu akamuuliza ni kwa ajili gani? ‘Abdullaah akajibu kwa kuwaitia Waislaam kuja kuswali. Akamuuliza iwapo anataka amfunze njia nzuri kuliko hiyo; na akasoma maneno ya Adhaan. Asubuhi yake ‘Abdullaah akamuambia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), naye akasema ndoto ilikuwa ni ya kweli.

 

[4] تَرْجِيعٍ (Kurudia) Ni kutamka maneno ya Shahada mbili Yaani

 أشهد أن لا إله إلا الله وأشهد أن محمدا رسول الله

mara mbili kwa sauti ya chini, halafu utamke kwa sauti kubwa.

 

[5] Katika Iqaamah (mwito wa kuanza Swalaah), maneno yote ya Takbiyr (kumtukuza Allaah) lakini hapa ina maana ya Iqaamah hutamkwa mara moja isipokuwa maneno

 

 قد قامت الصلاة

 

(yaani Swalaah iko tayari kuanza) ambayo hutamkwa mara mbili.

 

[6] Bilaal bin Rabbaah, mtumwa aliyeachwa huru wa Banu Taym. Alisilimu mapema sana, na akateswa sana katika jihaad ya njia za Allaah (عز وجل). Alipigana katika Vita ya Badr na Vita vingine vikuu. Alikuwa muadhini wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na hakuadhini kwa ajili ya mtu yeyote mwingine isipokuwa mara moja aliporejea Madiynah kutoka Damascus alikolowea. Inasemekana hakuwahi kuimaliza Adhaan hiyo kwa sababu ya kelele za Swahaba waliokuwa wakilia waliposikia sauti ya Bilaal, kwa sababu ya mazowea na kumbukumbu. Bilaal alifia Shaam mnamo mwaka 17 au 18 au 20 A.H akiwa na umri wa miaka sitini hivi, na hakuacha watoto wowote.

 

[7] Mwanzo wa Adhaan, maneno haya

 اَللَّهُ أَكْبَرُ

Allaahu Akbar (Allaah ni Mkuu Zaidi kuliko wote)

hutakiwa yarudiwe mara nne. Kuyarudia mara mbili tu siyo sahihi kama walivyosimulia Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad)

 

[8] Adhaan iliyo na Tarji’ au hata isiwe na Tarji’ inaruhusiwa, na hali kadhalika Iqaamah nayo inaruhusiwa ikiwa mara moja au mara mbili. Lakini ni vizuri kuitangaza Adhaan pamoja na Tarji’ na kuitangaza Iqaamah bila marudio.

 

[9] Inamaanisha kwamba, maneno

 

 قد قامت الصلاة

(Yaani Swalaah iko tayari kuanza) yarudiwe mara mbili, na maneno mengine yatangazwe mara moja tu.

 

[10] Huyu Abuu Juhayfah ndiye Wahaab bin ‘Abdillaah As-Suwa’i Al-‘Aamir, ambaye alikuwa miongoni mwa Swahaba vijana. Alilowea Kufa. ‘Aliy alimfanya awe mkuu wa Baytul-Maal; na alishuhudia pamoja naye vita vyote. Alifia Kuwfah mnamo mwaka 74 A.H.

 

[11] Wakati anatamka maneno haya

 حَيَّ عَلَى اَلصَّلَاةِ

(njoo katika Swalaah) na

 حَيٌّ عَلَى اَلْفَلَاحِ

(njoo kwenye kufaulu),

kugeuza uso kuume na kisha kushoto ni Sunnah. Kugeuza mwili mzima hakuruhusiwi. Hadiyth zinazokataza kugeuka, zinamaanisha kugeuza mwili wote na siyo kugeuza uso tu.

 

 

[12] Inamaanisha kuwa awe anateuliwa Muadhini mwenye sauti nzuri.

 

[13] Hii ina maana kwamba, Swalaah za ‘Iyd zote mbili (ya Fitwr na ya Adhwhaa) huswaliwa bila Adhaan wala Iqaamah

 

[14] Ikiwa Swalaah ya Qadhwaa (Swalaah inayolipwa) inataka kuswaliwa kwa jamaa, basi ni Sunnah kutoa Adhaan kwa ajili yake. Siku moja Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na Swahaba zake walisafiri usiku sana. Waliposimama na wakataka kuenda kulala, walikuwa hawana hakika ya kuwahi kuamka Alfajiri iliyofuata ili kuiswali. Kwa hivyo wakamuomba Bilaal abakie macho, lakini naye akazidiwa na usingizi akalala. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa wa kwanza kuamka baada ya jua kuchomoza akawaamsha Swahaba. Walisogelea pembeni wakaswali baada ya kuadhini.

 

[15] Muzdalifah ni mahali kati ya Makkah na ‘Arafah. Usiku wa tarehe 9 kuamkia tarehe 10 ya mwezi wa Dhul-Hijjah, baada ya kurudi kutoka ‘Arafah, Mahujaji hubakia hapo. Swalaah za Maghribi na ‘Ishaa huswaliwa hapo kwa pamoja kwa Adhaan moja tu, bali hutolewa Iqaamah moja kwa kila Swalaah. Hii yamaanisha kuwa, kila panaposwaliwa Swalaah ya jamaa, lazima ikimiwe.

 

[16] Hadiyth hii inatofautiana na Hadiyth iliyosimuliwa na Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) ambapo imetajwa Adhaan moja na Iqaamah mbili.

 

[17]  Katika mwezi wa Ramadhwaan Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliteua Waadhini wawili, wa kwanza kuadhini ili kujulisha wakati wa kula daku, na Muadhini wa pili kuadhini ili kuwaita watu waende kuswali.

 

[18] Ibn Umm Maktuwm ndiye ‘Amr au ‘Abdullaah bin Qays Al-Qurayshiy Al-‘Aamir, yule mtu kipofu anayetajwa katika Suwrah ‘Abasa. Alisilimu zamani na akafanya Hijrah (kuhama). Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimteua yeye awe Mkuu wa Madiynah mara 13 akiwaswalisha watu. Alikufa shahidi kule Al-Qadisiya wakati akishika bendera siku ile.

 

[19] Neno إِدْرَاجٌ  Idraaj (kilichoongezwa) linamaanisha kwamba, maneno hayo: "Na alipokuwa kipofu." Hayakusemwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mwenyewe, bali msimulizi aliongeza maneno haya kwa utashi wake mwenyewe.

 

[20] Hii inamaanisha kuwa kama kumeadhiniwa kabla ya wakati, kuadhiniwe tena ukifika wakati wake sahihi.

 

[21] Ni amri kwamba, tunaposikia Adhaan, watu warudie yale maneno ya Adhaan kwa kujibu kila mara, kama mtu anao wudhuu au asiwe nao, awe msafi bila najsi au awe na najsi ya kijinsia; lakini wakati mtu anafanya tendo la ndoa au akiwa chooni, haifai kujibu.

 

[22] ‘Uthmaan bin Abiy Al-‘Aasw ndiye aliyepewa jina la utani la Abuu ‘Abdillaah. Alikuwa mdogo kuliko watu waliokuwa katika ujumbe wa Twaaif wa Banu Thaqif. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimteua awe mkuu wa Twaaif, na aliwazuia watu wake wasiasi, na kwa hivyo wabakie katika Uislaam. ‘Umar alimteua awe Gavana wa Bahrayn na Oman. Alifariki mnamo mwaka 51 A.H.

 

[23] Imaam (anayeswalisha) ni sharti awajali watu dhaifu na wazee kwa kutorefusha sana Swalaah, kiasi cha kuwafanya wafikirie kuacha jamaa.

 

[24] Inamaanisha kwamba, Muadhini sharti asiwe analipwa kwa kazi hiyo ya kuadhini. Lakini huku siyo kukataza, bali ni pendekezo linalopendeza.

 

[25] Maalik bin Al-Huwayrith alikuwa wa Banu Layth, na alipewa jina la utani la Abuu Salmaan. Alimzuru Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na akakaa naye kwa siku ishirini. Alilowea Basra na akafia huko mnamo mwaka wa 74 A.H.

 

[26] Inamaanisha kuwa, wakati wa safari pia, kuadhini na kukimu ni Sunnah.

 

[27] Mambo mengine yanajulikana kuhusu Hadiyth hii:

a) Adhaan sharti itolewe kwa sauti kubwa, pakiweko mapumziko kidogo kati ya maneno yake.

(b) Iqaamah itolewe haraka haraka.

(c) Sharti kuweko muda wa kutosha kati ya Adhaan na Swalaah, ili mtu aweze kuja kujiunga na jamaa baada ya kumaliza kula au baada ya kuenda na kutoka msalani na kutawadha. ‘Ulamaa wengine wamekisia wakati huo uwe sawa na muda wa Rakaa nne.

 

[28] Ni Sunnah kwa Muadhini kutoa Adhaan akiwa na wudhuu, lakini isipowezekana, Adhaan itolewe bila wudhuu. Hili ni pendekezo tu siyo lazima.

 

[29] Ziyaad bin Al-Haarith alikuwa Swahaba kutoka Yaman aliyekubaliana na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na akatoa Adhaan mbele yake. Inasemekana alilowea Basra.

 

[30] Ni Sunnah kwa mtu mmoja huyo huyo atoe Adhaan na Iqaamah; lakini akiruhusu, mtu mwingine anaweza kutoa Iqaamah.

 

[31] Du’aa kamili (اَلدَّعْوَةِ اَلتَّامَّةِ) maana yake ni ung’avu wa Umoja wa Allaah (عز وجل)  na Nuru ya Unabiy.

 

[32] Baki ya kumaanisha ‘uombezi na ukuu (wasiylah)’, hilo pia ni jina la mahali. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alisema kwamba, ni mtu mmoja tu miongoni mwa viumbe wa Allaah (عز وجل)   atakayefika kule, naye alitegemea, kwa Rahmah za Allaah (عز وجل), mtu huyo atakuwa yeye Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

 

 

Share