05-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Sisitizo La Khushuw’ (Unyenyekevu) Katika Swalaah
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلصَّلَاةِ
Kitabu Cha Swalaah
بَابُ اَلْحَثِّ عَلَى اَلْخُشُوعِ فِي اَلصَّلَاةِ
05-Mlango Sisitizo La Khushuw’[1] (Unyenyekevu) Katika Swalaah
188.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ يُصَلِّيَ اَلرَّجُلُ مُخْتَصِرًا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
وَمَعْنَاهُ: أَنْ يَجْعَلَ يَدَهُ عَلَى خَاصِرَتِهِ
وَفِي اَلْبُخَارِيِّ : عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا أَنَّ ذَلِكَ فِعْلُ اَلْيَهُودِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikataza mtu kuswali hali ya kuweka mikono kiunoni.[2]” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
Na maana yake ni: “Mtu kuweka mikono yake kwenye kiuno.”
Na katika Al-Bukhaariy kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا): “Kuwa ni kitendo cha Mayahudi katika Swalaah zao.”
189.
وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : {إِذَا قُدِّمَ اَلْعَشَاءُ فَابْدَءُوا بِهِ قَبْلَ أَنْ تُصَلُّوا اَلْمَغْرِبَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kikiwadia chakula cha jioni (na huku Swalaah imewadia) kianzeni kabla hamjaswali[3] Magharibi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
190.
وَعَنْ أَبِي ذَرٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {إِذَا قَامَ أَحَدُكُمْ فِي اَلصَّلَاةِ فَلَا يَمْسَحِ اَلْحَصَى، فَإِنَّ اَلرَّحْمَةَ تُوَاجِهُهُ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ بِإِسْنَادٍ صَحِيحٍ
وَزَادَ أَحْمَدُ : "وَاحِدَةً أَوْ دَعْ"
وَفِي "اَلصَّحِيحِ" عَنْ مُعَيْقِيبٍ نَحْوُهُ بِغَيْرِ تَعْلِيلٍ
Kutoka kwa Abuu Dharr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Anaposimama mmoja wenu katika Swalaah, asijipanguse vijiwe[4] kwani Rahmah inamuelekea yeye.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) kwa Isnaad swahiyh]
Na akaongezea Ahmad: “(Ondosha) mara moja tu, au acha.”
Na ndani ya Swahiyh (Al-Bukhaariy) kuna Hadiyth kama hiyo, kutoka kwa Mu’ayqib[5] bila kutajwa sababu.
191.
عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ : {سَأَلْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَنْ اَلِالْتِفَاتِ فِي اَلصَّلَاةِ ؟ فَقَالَ : "هُوَ اِخْتِلَاسٌ يَخْتَلِسُهُ اَلشَّيْطَانُ مِنْ صَلَاةِ اَلْعَبْدِ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
وَلِلتِّرْمِذِيِّ: عَنْ أَنَسٍ وَصَحَّحَهُ {إِيَّاكَ وَالِالْتِفَاتَ فِي اَلصَّلَاةِ، فَإِنَّهُ هَلَكَةٌ، فَإِنْ كَانَ فَلَا بُدَّ فَفِي اَلتَّطَوُّعِ}
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) juu ya kugeuka geuka ndani ya Swalaah naye akasema: Huko ni kunyakua ambako shaytwaan hunyakua kutoka katika Swalaah ya mja.” [Imetolew na Al-Bukhaariy]
Na katika At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas aliisahihisha ameandika: “Epuka kugeuka geuka ukiwa ndani ya Swalaah, kwani kutazama pembeni ni uharibifu, na ikiwa ni lazima[6] basi iwe katika Swalaah ya Sunnah.[7]”
192.
وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {إِذَا كَانَ أَحَدُكُمْ فِي اَلصَّلَاةِ فَإِنَّهُ يُنَاجِي رَبَّهُ، فَلَا يَبْزُقَنَّ بَيْنَ يَدَيْهِ وَلَا عَنْ يَمِينِهِ، وَلَكِنْ عَنْ شِمَالِهِ تَحْتَ قَدَمِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَفِي رِوَايَةٍ : {أَوْ تَحْتَ قَدَمِهِ}
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akiwa ndani ya Swalaah, anakuwa anamnong’oneza Allaah, kwa hivyo asiteme mate mbele yake[8], wala upande wa kuume, lakini kushotoni kwake na chini ya mguu wake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na katika Riwaayah nyingine: “Au chini ya mguu wake.”
193.
وَعَنْهُ قَالَ : {كَانَ قِرَامٌ لِعَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا سَتَرَتْ بِهِ جَانِبَ بَيْتِهَا فَقَالَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم أَمِيطِي عَنَّا قِرَامَكِ هَذَا، فَإِنَّهُ لَا تَزَالُ تَصَاوِيرُهُ تَعْرِضُ لِي فِي صَلَاتِي} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
وَاتَّفَقَا عَلَى حَدِيثِهَا فِي قِصَّةِ أَنْبِجَانِيَّةِ أَبِي جَهْمٍ ، وَفِيهِ : {فَإِنَّهَا أَلْهَتْنِي عَنْ صَلَاتِي}
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “’Aaishah alikuwa na Qiraam[9] aliyoitumia kusitiri upande mmoja wa nyumba yake, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamwambia: “Ondoa[10] pazia lako, kwani picha zake hazijaacha kunitokea katika Swalaah yangu.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
Al-Bukhaariy na Muslim pia waliafikiana Hadiyth iliyosimuliwa naye (‘Aaishah) amabayo inataja kisa cha Anbijaaniyyah[11] Abiy Jahm[12], ikieleza pia: “Hiyo[13] imenivurugia umakinifu[14] wa Swalaah yangu.”
194.
وَعَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَيَنْتَهِيَنَّ قَوْمٌ يَرْفَعُونَ أَبْصَارَهُمْ إِلَى اَلسَّمَاءِ فِي اَلصَّلَاةِ أَوْ لَا تَرْجِعَ إِلَيْهِمْ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
وَلَهُ : عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ : سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ : {لَا صَلَاةَ بِحَضْرَةِ طَعَامٍ ، وَلَا هُوَ يُدَافِعُهُ الْأَخْبَثَانِ}
Kutoka kwa Jaabir bin Samurah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu wanaoelekeza macho yao mbinguni wanapokuwa ndani ya Swalaah, waache, au sivyo kuona kwao hakutawarudia[15].” [Imetolewa na Muslim]
Pia (Muslim) amenukuu Hadiyth ya ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) kuwa amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema hakuna Swalaah wakati wa kuhudhuria chakula, wala mtu anapojizuia haja mbili (kubwa na ndogo)[16].”
195.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ : {اَلتَّثَاؤُبُ مِنْ اَلشَّيْطَانِ فَإِذَا تَثَاءَبَ أَحَدُكُمْ فَلْيَكْظِمْ مَا اِسْتَطَاعَ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
وَاَلتِّرْمِذِيُّ ، وَزَادَ : {فِي اَلصَّلَاةِ}
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kupiga miayo hutokana na shaytwaan[17], kwa hivyo mmoja wenu anapopiga miayo ajizuie kadiri anavyoweza.” [Imetolewa na Muslim]
Na katika At-Tirmidhiy ameongeza: “Ndani ya Swalaah[18].”
[1] Khushuw’ maana yake ni unyenyekevu, utulivu, ushwari, na kumakinia mwili mzima na akili yote kwa Allaah (سبحانه وتعالى).
[2] Kuweka mikono pembeni au kiunoni ni kitendo cha kujiona, wakati unyenyekevu na upole ndio unaotakiwa katika Swalaah. Nukta nyingine iliyofafanuliwa katika Hadiyth inayofuata ni kuwa hii inafanana na desturi ya Mayahudi, na kuwaiga wao imekatazwa.
[3] Ikiwa chakula kimeandaliwa, kula chakula hicho ni afadhali hata kama huna njaa. Falsafa ya kufanya hivi ni kwamba, mtu anatakiwa asimame mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) huku akiwa karidhika kikamilifu na akiwa juu ya mahitaji yoyote ya kidunia. Lakini hairuhusiwi kuenda kula wakati wa Swalaah ilhali hicho chakula hakijaandaliwa.
[4] Kuondosha changarawe kutoka mahala pa kusujudia kumekatazwa ikiwa vijiwe vyenyewe ni vidogo na havina madhara. Ama ikiwa vijiwe ni vikubwa na vinaleta adha na vinazuia umakinifu, basi hakuna dhara kuviondosha.
[5] Mu’ayqiyb bin Abiy Faatwimah Ad-Daws alisilimu zamani sana kule Makkah, na akahama Abyssinia wakati wa Hijrah ya pili. Alishuhudia Badr. Alikuwa akiihifadhi lakiri ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na baadaye Abuu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) na baadaye tena ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) walimfanya mkuu wa Baytul-Maal. Alikufa wakati wa Ukhalifa wa ‘Uthmaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).
[6] Iwapo ni lazima, waweza kugeuka katika Swalaah ya Sunnah (nafl) lakini siyo katika Swalaah ya fardhi. Kwa sababu kuna madhara kidogo zaidi kufanya kitendo hicho katika Swalaah ya Sunnah. Katika dharura muhimu sana, huruhusiwa, kama ilivyodhihirika katika ugonjwa wa mwisho wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipotoka nje ya nyumba yake ili akaswali Msikitini, Abuu Bakr Swiddiyq (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) aliyekuwa akiswalisha wakati huo alitaka arudi nyuma kumpisha Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aswalishe, lakini aliashiriwa na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) asirudi nyuma akaendelea kuswalisha, naye Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakumkosoa Abuu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).
[7] Hata katika Swalaah ya khiari, uso ukigeuka mbali na Qiblah, Swalaah inakatika.
[8] Sharti ikumbukwe kwamba mtu kamwe asiteme mate kuelekea Qiblah, au upande wa kuume, awe ndani ya Swalaah au nje ya Swalaah.
[9] Kipande cha nguo laini chenye nakhsi rangi.
[10] Inamaanisha kuwa kitu chochote kinachovuruga khushuw’ ni lazima kiondoshwe kutoka katika mahala pa kuswalia. Ikiwa hii haiwezekani, basi epuka mahala hapo na uende kwengine.
[11] Vazi la sufi lisilokuwa na nakshi wala picha au maandishi.
[12] Abuu Jahm ndiye Ibn Hudhayfah bin Ghaniym Al-‘Adawi. Jina lake ni ‘Aamir au ‘Ubayd. Alisilimu katika mwaka ule ilipotekwa Makkah. Alikuwa miongoni mwa Swahaba walioishi umri mrefu, kwani huyu alihudhuria ujenzi wa Ka’bah wa Maqurayshi kabla ya ujio wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na akashuhudia ujenzi wake upya wa ‘Abdullaah bin Az-Zubayr ambaye Abuu Jahm alifariki mwanzoni mwa Ukhalifa wake.
[13] Kipande cha nguo laini chenye nakshi na rangi.
[14] Inamaanisha kwamba Misikiti isipambwe kwa nakshi na urembo n.k. kwa kuwa vinazuwia umakinifu. Imaam Nawawi amenukuu maafikiano ya ‘Ulamaa wa Kiislamu kuwa katazo hili ni halisi.
[15] Imaam An-Nawawi ameripoti maafikiano ya ‘Ulamaa wa Kiislamu kwamba katazo hili ni halisi. Ibn Hazm anasema kuwa Swalaah inabatilika.
[16] Endapo mtu anahisi kutaka kuenda haja (choo), kukojoa au kutoa upepo, na akiwa anao muda wa kutosha, basi afanye hivyo kabla hajaanza kuswali, vinginevyo itakuwa karaha. Kwa mujibu wa wengine, hiyo haitahesabika kuwa ni Swalaah kabisa kwa sababu ya kutokuwepo umakinifu na unyenyekevu kwa Allaah (عز وجل). Iwapo muda ni mfupi sana na mtu ana haraka sana, basi aswali ile Swalaah kuliko kuchelewa.
[17] Kutoa mwayo ni matokeo ya kujaa tumbo ni uvivu. Shaytwaan hufurahi kumuona mwana Aadam yuko hivyo, kwa hivyo kupiga mwayo kunahesabika kuwa ni tabia ya kishaytwaan.
[18] Kuzuia mwayo ndani ya Swalaah au katika wakati wowote ni Sunnah