Fatwaair Za Mchicha
Fatwaair Za Mchicha
Vipimo Vya Unga Wa Fatwaair
Unga - 4 Magi (au vikombe vya chai)
Maziwa ya maji - 1 ½
Maziwa ya unga – vijiko vya kulia
Sukari - 3 Vijiko vya kulia
Mafuta - Robo Magi
Mtindi – Vijiko 3 vya kulia
Hamira - 1 kijiko kikubwa cha kulia
Baking powder – 1 kijiko cha chai
Chumvi - robo kijiko cha chai
Namna Ya Kutayarisha Mchanganyiko Wa Fatwaair
- Tia katika mashine vitu vyote isipokuwa unga upige vichanganyike vizuri.
- Tia unga kidogo kidogo huku unachanganya mpaka umalizike.
- Ukishachanganyika unga wote, utazame usiwe wenye kunata sana, ikiwa unanata sana ongezea kidogo unga.
- Utoe katika mashine na uweke katika bakuli ufunike kwa muda mpaka ufure.
- Utatumia mchanganyiko wa unga huu kwa aina yoyote ile upendayo ya kujazia vitu au kupikia mapishi kama ya Khalyat Nahl (Mzinga wa nyuki), aina ya vitobosho, fatwaair zozote na kadhaalika.
Vipimo Vya Mjazo Wa Mchicha
Mchicha – Kiasi cha kutokea vikombe 4 baada ya kukatwakatwa
Siagi (butter isiyo na chumvi) vijiko 3 vya kulia
Kitunguu – kilokatwakatwa – 1
Chumvi kaisi kidogo sana
Paprika (aina ya pilipili au bizari) – 1 kijiko cha chai
Sumac (aina ya ndimu nyekundu ya chengachenga) – 1 kijiko cha chai
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Mjazo Wa Mchicha
- Osha mchicha vizuri sana kisha uchuje maji kisha katakata (chopped)
- Weka siagi (butter) katika sufuria kisha kaanga vitunguu hadi vilainike na kuanza kugeuka rangi.
- Tia mchicha ukaange na kisha tia chumvi humo na paprika na sumac na kaanga kwa dakika 2 – 3 tu ichanganyike vizuri.
- Kata madonge ya unga kwa kutumia kikombe itokee viduara.
- Weka kiasi cha kijiko kimoja cha mchanganyiko wa mchicha katikati ya kiduara.
- Kunja na kubana ncha tatu cha duara kufunika mchanganyiko wa mchicha ufanye kama kufinya ili kukifunga mchicha uwe ndani.
- Panga katika treya iliyopakwa siagi.
- Rashia (Brush) kwa siagi au mafuta kisha choma (Bake) katika oven kwa moto wa baina ya 180°C na 200°C kwa muda wa dakika 15- 20 mpaka vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown).
- Epua vikiwa tayari.
Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)