03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Zakaah: Mlango Wa Swadaqah Za Khiari

 

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلزَّكَاةُ

Kitabu Cha Zakaah

 

 

بَابُ صَدَقَةِ اَلتَّطَوُّعِ

03-Mlango Wa Swadaqah Za Khiari

 

 

 

 

508.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمُ اَللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لَا ظِلَّ إِلَّا ظِلُّهُ.‏.‏.‏.} فَذَكَرَ اَلْحَدِيثَ وَفِيهِ: {وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لَا تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake tu, na akawataja miongoni mwao ni mtu anayetoa Swadaqah kwa siri hata mkono wake wa kushoto haujui mkono wake wa kuume umetoa nini.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

509.

وَعَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ رضى الله عنه قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يَقُولُ: {كُلُّ اِمْرِئٍ فِي ظِلِّ صَدَقَتِهِ حَتَّى يُفْصَلَ بَيْنَ اَلنَّاسِ} رَوَاهُ اِبْنُ حِبَّانَ وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema nilimsikia Rasuli wa  Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Kila mmoja atakuwa chini ya kivuli[1] cha Swadaqah yake hadi ihukumiwe baina ya watu.” [Imetolewa na Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

510.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ، عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {أَيُّمَا مُسْلِمٍ كَسَا  مُسْلِمًا ‏ ثَوْبًا عَلَى عُرْيٍ كَسَاهُ اَللَّهُ مِنْ خُضْرِ اَلْجَنَّةِ، وَأَيُّمَا مُسْلِمٍ أَطْعَمَ مُسْلِمًا عَلَى جُوعٍ أَطْعَمَهُ اَللَّهُ مِنْ ثِمَارِ اَلْجَنَّةِ، وَأَيُّمَا مُسْلِمٍ سَقَى مُسْلِمًا عَلَى ظَمَإٍ سَقَاهُ اَللَّهُ مِنْ اَلرَّحِيقِ اَلْمَخْتُومِ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَفِي إِسْنَادِهِ لِينٌ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Muislamu yeyote atakayemvisha Muislam aliye uchi, Allaah Atamvisha huyo nguo za kijani za Al-Jannah. Na Muislam yeyote atakayemlisha Muislam mwenye njaa, Allaah Atamlisha matunda ya Al-Jannah. Na Muislam yeyote atakayemnywesha Muislam mwenye kiu, Allaah Atamnywesha Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm (kinywaji kizuri cha mvinyo Al-Jannah).” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na kuna udhaifu katika mlolongo wa wapokezi]

 

 

 

511.

وَعَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ رضى الله عنه ‏ عَنِ اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {اَلْيَدُ اَلْعُلْيَا خَيْرٌ مِنَ اَلْيَدِ اَلسُّفْلَى، وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ، وَخَيْرُ اَلصَّدَقَةِ عَنْ ظَهْرِ غِنًى، وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اَللَّهُ، وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اَللَّهُ.} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa Hakiym bin Hizaam (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkono wajuu ni mbora kuliko wa chini, na anza kwa kuwapa Swadaqah wanaokutegemea.[2] Na Swadaqah bora ni inayotolewa kwa ajili ya kujitosha, na yeyote anayejizuia kuwaomba watu Swadaqah, Allaah Atamfanya aridhike, na kila anayeridhika na anachopewa na Allaah, basi Allaah Atamfanya awe anajitosheleza.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

512.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: {قِيلَ يَا رَسُولَ اَللَّهِ: أَيُّ اَلصَّدَقَةِ أَفْضَلُ؟ قَالَ: "جُهْدُ اَلْمُقِلِّ، وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ"} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَابْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliulizwa Swadaqah gani iliyokuwa bora zaidi? Akasema: “Ni juhudi ya mwenye mali kidogo sana anayoweza kutoa, na aanze na watu wanaomtegemea yeye.” [Imetolewa na Ahmad, na Abuu Daawuwd, na wakaisahihisha Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

513.

وَعَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{" تَصَدَّقُوا " فَقَالَ رَجُلٌ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ، عِنْدِي دِينَارٌ؟ قَالَ: " تَصَدَّقْ بِهِ عَلَى نَفْسِكَ " قَالَ: عِنْدِي آخَرُ، قَالَ: " تَصَدَّقْ بِهِ عَلَى وَلَدِكَ "‏ قَالَ: عِنْدِي آخَرُ، قَالَ: " تَصَدَّقْ بِهِ عَلَى خَادِمِكَ " قَالَ: عِنْدِي آخَرُ، قَالَ: " أَنْتَ أَبْصَرُ ".} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Toeni Swadaqah.” Mtu mmoja akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Ninayo dinari moja tu.” Akasema:  “Jitolee Swadaqah mwenyewe.” Yule mtu akasema: “Ninayo nyingine.” Akasema: “Mtolee Swadaqah mwanao.” Yule mtu akasema: “Ninayo nyingine.” Akasema: “Mtolee Swadaqah mkeo.” Yule mtu akasema tena: “Ninayo nyingine.” Akasema: “Mtolee Swadaqah mtumishi wako.” Yule mtu akasema: “Ninayo nyingine.” Akasema: “Wewe unajua zaidi uifanyie nini hiyo.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy, na wakaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

514.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{إِذَا أَنْفَقَتِ اَلْمَرْأَةُ مِنْ طَعَامِ بَيْتِهَا، غَيْرَ مُفْسِدَةٍ، كَانَ لَهَا أَجْرُهَا بِمَا أَنْفَقَتْ وَلِزَوْجِهَا أَجْرُهُ بِمَا اِكْتَسَبَ ‏ وَلِلْخَازِنِ مِثْلُ ذَلِكَ، وَلَا يَنْقُصُ بَعْضُهُمْ أَجْرَ بَعْضٍ شَيْئًا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwanamke akitoa Swaadaqah sehemu ya chakula cha nyumbani mwake bila ubadhirifu,[3] atapata thawabu kwa alichotoa, mumewe atapata thawabu kwa alichochuma, na aliyekihifadhi naye atapata sawa na hizo, wala hakuna atakayepunguziwa thawabu[4] zake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

515.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ‏ رضى الله عنه قَالَ: {جَاءَتْ زَيْنَبُ اِمْرَأَةُ اِبْنِ مَسْعُودٍ، فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ، إِنَّكَ أَمَرْتَ اَلْيَوْمَ بِالصَّدَقَةِ، وَكَانَ عِنْدِي حُلِيٌّ لِي، فَأَرَدْتُ أَنْ أَتَصَدَّقَ بِهِ، فَزَعَمَ اِبْنُ مَسْعُودٍ أَنَّهُ وَوَلَدُهُ أَحَقُّ مَنْ تَصَدَّقْتُ بِهِ عَلَيْهِمْ، فَقَالَ اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم "صَدَقَ اِبْنُ مَسْعُودٍ، زَوْجُكِ وَوَلَدُكِ أَحَقُّ مَنْ تَصَدَّقْتِ بِهِ عَلَيْهِمْ".} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Alikuja Zaynab[5] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) mke wa Ibn ‘Mas-‘uwd akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Leo umeamrisha Swadaqah, nami nilikuwa na vito vyangu, kwa hivyo ninataka nivitoe hivyo kama Swadaqah, lakini Ibn Mas-‘uwd alidai kuwa yeye na watoto wake wana haki zaidi niwatolee wao Swadaqah.”  Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Ibn Mas-‘uwd amesema kweli, kuwa mumeo na watoto wana haki zaidi ya kunufaishwa na Swadaqah[6] yako.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

516.

وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{مَا يَزَالُ اَلرَّجُلُ يَسْأَلُ اَلنَّاسَ حَتَّى يَأْتِيَ يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ لَيْسَ فِي وَجْهِهِ مُزْعَةُ لَحْمٍ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mtu hataacha kuomba hadi aje siku ya Qiyaamah hana usoni mwake nyama.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

517.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{مَنْ سَأَلَ اَلنَّاسَ أَمْوَالَهُمْ تَكَثُّرًا، فَإِنَّمَا يَسْأَلُ جَمْرًا، فَلْيَسْتَقِلَّ أَوْ لِيَسْتَكْثِرْ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Anayeomba watu mali zao ili aongezee mali yake mwenyewe, huyo anajipalilia makaa ya moto; kwa hivyo hebu aombe kidogo au kingi (na adhabu itamsubiri).”[7] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

518.

وَعَنِ اَلزُّبَيْرِ بْنِ اَلْعَوَّامِ رضى الله عنه‏ عَنِ اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {لَأَنْ يَأْخُذَ أَحَدُكُمْ حَبْلَهُ، فَيَأْتِي بِحُزْمَةِ اَلْحَطَبِ عَلَى ظَهْرِهِ، فَيَبِيعَهَا، فَيَكُفَّ اَللَّهُ بِهَا وَجْهَهُ، خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَسْأَلَ اَلنَّاسَ أَعْطَوهُ أَوْ مَنَعُوهُ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Az-Zubayr bin Al-‘Awwaam (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu kuchukua kamba yake, alete mzigo wa kuni mgongoni kwake, auuze, kwa huo, Allaah Ahifadhie heshima yake ni bora, kuliko kuombaomba watu, wawe wanakupa au wanakunyima.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

519.

وَعَنْ سَمُرَةَ بْنِ جُنْدُبٍ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{اَلْمَسْأَلَةُ كَدٌّ يَكُدُّ بِهَا اَلرَّجُلُ وَجْهَهُ، إِلَّا أَنْ يَسْأَلَ اَلرَّجُلُ سُلْطَانًا، أَوْ فِي أَمْرٍ لَا بُدَّ مِنْهُ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ

Kutoka kwa Samurah bin Jundub (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuomba ni mikwaruzo inayoharibu uso wa mtu isipokuwa akimuomba mtawala,[8] au katika hali ambayo hana budi nayo.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy ambaye pia aliisahihisha]

 

[1] Hicho ‘Kivuli’ kinamaanisha kuwa kila Swadaqah inayotolewa itageuka kuwa mwavuli kwa mtoaji Swadaqah ambao utamkinga dhidi ya jua lichomalo sana Siku ya Qiyaamah. Moja ya faida za Swadaqah ya khiari ni kuwa itakuwa kama dawa ya mapungufu katika Zakaah ya fardhi.

[2] Imekatazwa kuwapa Swadaqah watu baki kama watu wa familia yako wana shida kubwa. Kwa mujibu wa Muslim, imesimuliwa na Thawbaan kuwa, sehemu bora ya pesa ni ima ile iliyotomika kwa familia yako, au pesa zilizotumika kwa ajili ya farasi aliyetumika katika vita vya Jihaad (vita ya kidini) au pesa zilizotumika kwa marafiki.

[3] Inamaanisha kuwa, ilimradi mke huyo hana dhamiri ya siri ya kuidhuru nyumba ya mumewe, anaweza kutoa Swadaqah kama ilivyo desturi. Anaweza kumpa muombaji maskini mikate au unga. Ikiwa inahitajika Swadaqah zaidi, basi ni sharti apate idhini kutoka kwa mume wake.

[4] Inamaanisha kwamba, Allaah (سبحانه وتعالى)  Atampa kila mtu thawabu au zawadi kamili kwa Ukarimu Wake. Si kama Anayo zawadi moja tu anayoigawanya hiyo hiyo miongoni mwa watu wote. Hii inathibitisha kuwa mtu sharti umsaidie kila mtu kutenda matendo mema ili na yeye apate zawadi.

[5] Zaynab alikuwa anatoka kwa Banuw Thaqiyf, na babake aliitwa Mu’aawiyah, au ‘Abdullaah bin Mu’aawiyah, au Abuu Mu’aawiyah. Alisimulia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), mume wake, ‘Umar bin Al-Khatwaab, mwanawe, mpwa wake, na wengine walisimuliwa kutoka kwake.

[6] Hilo neno Swadaqah linawahusu watu wote, iwe ni tendo la khiari au la Swadaqah au tendo la lazima la kulipa Zakaah au Swadaqatul-Fitrw. Qur-aan tukufu imelitaja neno hili la Swadaqah pale tu ilipokuwa ikieleza mambo kuhusu kugawanya na kusambaza fedha za Zakaah. Inapokuwa hiyo Swadaqah ya khiari siyo kubwa sana, basi kwa kawaida huashiria tendo la wajibu la kutoa Swadaqah (Zakaah). Hapa inaelekea kuwa ni ulipaji wa lazima wa Swadaqah kwani mtu hana haja ya kuomba ruhusa ya mtu yeyote kuhusu Swadaqah ya khiari. Wengi wa Wanazuoni wanaafikiana kuwa mke anaweza kumpa mumewe. Halikadhalika kuna maafikiano ya maoni kuwa mwanaume hawezi kumpa Zakaah mkewe.

[7] Iwapo mtu asiyestahili anakusanya pesa kwa kuombaomba, atapata fedheha na aibu Siku ya Qiyaamah na atakabiliwa na mateso ya motoni. Kuna aina tatu za watu wanaostahili kupewa pesa ya Zakaah:

 

(a) Mtu ambaye mali yake inateketezwa ghafla na balaa lisilotazamiwa kiasi kwamba hana kitu hata cha kula. Mtu kama huyo anaweza kuomba pesa za Zakaah ili ziweze kumkimu.

(b) Mtu ambaye ameadhibiwa kimaonezi, au mtu aliyemkingia kifua au alisaini dhamana au mkataba fulani kwa ajili ya mtu mwingine na sasa analazimishwa alipe pesa kwa ajili ya huyo mtu mwingine ingawa hana pesa za kutosha kulipia hilo. Mtu kama huyo ana haki ya kupewa pesa za Zakaah ili awe na pesa za kutosha kulipia deni hilo.

(c) Mtu ambaye anafanya kazi au anataka kwa dhati kufanya kazi kwa uaminifu na bidii zote lakini haipati kazi, au mwenye pato dogo kuliko kiwango kinachotosheleza matumizi yake na kwa hivyo analazimika kukabiliwa na njaa.

[8] Hii inatujulisha kwamba kumuendea mfalme na kumuomba msaada wa kipesa inaruhusiwa. Mfalme anaruhusiwa ima kumpa mtu Swadaqah kutoka katika malipo ya Zakaah, au kutoka katika Khumus (moja ya tano ya mali iliyotokana na ngawira za vita na kupangiwa ihifadhiwe katika hazina). Iwapo muombaji ni maskini sana, anaweza kupewa kutoka kwenye Zakaah. Lakini akiwa ni tajiri, asipewe pesa kutoka katika Zakaah, bali apewe kutoka katika Khumus (fedha kutoka hazina ya serikali).

Share