01-Imaam Ibn Baaz: Kufunga Swiyaam Tarehe 13 Dhul-Hijjah Kwa Niyyah Ya Swiyaam Ayyaamul-Biydwh (Masiku Meupe)
Hukmu Ya Kufunga Swiyaam Tarehe 13 Dhul-Hijjah
Kwa Niyyah Ya Swiyaam Ayyaamul-Biydwh (Masiku Meupe)
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Mzazi wangu alikuwa na ada ya kufunga Swiyaam kila mwezi Masiku Meupe (Ayyamul-Biydhw). Na kwa kuwa masiku haya yatawafikiana na tarehe 13 Dhul-Hijjah ambayo ni siku miongoni mwa Ayyamut-Tashriyq (Masiku ya Tashriyq), je aifunge au itamtosheleza kufunga tarehe 14 na 15 Dhul-Hijjah pekee?
JIBU:
Haipasi kwa mzazi wako au mwengine kufunga tarehe 13 Dhul-Hijjah kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kufunga Ayyaamut-Tashriyq akasema kuwa hayo ni masiku ya kula na kunywa na kumdhukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) [Ahmad katika Musnad].
Isipokuwa kwa Haji asiyepata had-yu (mnyama wa kuchinja) ikiwa ni mwenye kutekeleza Hajj Tamattu’ au Qiraan, basi hana kosa kuzifunga Swawm siku hizo kama alivyopokea Al-Bukhaariy (Rahimahu-Allaah) katika Swahiyh yake kwamba ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wamehadithia kwamba: “Haikuruhusiwa kufunga katika Ayyaamut-Tashriyq isipokuwa kwa ambaye hakupata Al-Had-yu (mnyama wa kuchinja Hajj).
Hivyo anaweza (mtu) kufunga tarehe 14 na 15 na akipenda afunge tarehe 16 au siku nyingineyo katika mwezi wa Hajj hata akamilishe siku tatu (katika mwezi) na hivyo ni bora kufanya kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameusia kundi la Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kufunga Swiyaam siku tatu kila mwezi, ikiwa ni siku zinazoangukia Ayyamul-Biydhw au zisizoangukia.
Lakini akifunga Muislamu katika masiku meupe ni bora.
Na Allaah Ndiye Mwenye kuleta Tawfiyq.
[Fataawa Imaam Ibn Baaz, http://www.binbaz.org.sa/fatawa/591]