00-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Na Hakika Wewe Uko Juu Ya Kiwango Adhimu Cha Tabia Njema

 

 

 Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

00-Na Hakika Wewe Uko Juu Ya Kiwango Adhimu Cha Tabia Njema

 

www.alhidaaya.com

 

 

Hakuna sentensi itakayoweza kuelezea mazuri aliyokuja nayo Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); utukufu wake,  daraja yake, elimu na Risala aliyokuja nao pamoja na upana wa hikma zake,  na sifa na akhlaaq (tabia) zake.  

 

Jina lake pekee linatosha kuelezea tabia zake kwani Muhammad maana yake ni "Mwenye kusifiwa." Kwa hiyo bila shaka anamiliki sifa na tabia njema zilizokamilika ambazo hakuna mtu yeyote mwingine aliyemiliki;  ni cheo cha daraja ya juu kabisa hakuna atakayeweza kufikia!  Na si mwengine aliyemsifia kiumbe huyu bali ni Mwenyewe Allaah ('Azza wa Jalla) Anayesema:

 وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ﴿٤﴾

Na hakika wewe uko juu ya kiwango adhimu cha tabia njema. [Al-Qalam: 4]

 

Swahaba Sa'ad bin Hishaam (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipomuuliza Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  kuhusu tabia ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu:

كان خلقه القرآن. ألست تقرأ القرآن (( وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ )) أبو داود والنسائي   

Tabia yake ilikuwa ni Qur-aan, kwani husomi katika Qur-aan )) Na hakika wewe uko juu ya kiwango adhimu cha tabia njema. (( [Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayh wa aalihi wa sallam) akasema:

  ((إِنَّمَا بُعِثْتُ لِأُتَمِّمَ صَالِحَ الأَخْلاقِ‏))

 ((Hakika nimetumwa ili nikamilishe khulqa (tabia) njema)) [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ameipokea Imaam Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy Swahiyh Al-Jaami’ (2349), Swahiyh Al-Adab Al-Mufrad (207)]

 

Zitakazofuatia ni baadhi ya sifa na akhlaaq ambazo zinazompelekea Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuchukua nafasi adhimu na ya pekee katika ulimwengu huu, pamoja na kuacha athari zake ambazo zimewasisimua na kuwahamasisha watu wengi mno mpaka makafiri wakaingia Uislamu kwazo, na  hazitoweza kubadilika wala kufutika hadi Siku ya mwisho; Swalla Allaahu 'alayh wa aalihi wa sallam.

 

Wabillaahi At-Tawfiyq

 

 

Share