06-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Mu’aafaat, Nayo Ni Katika Du’aa Bora Kabisa
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
06-Kuomba Mu’aafaat, Nayo Ni Katika Du’aa Bora Kabisa
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((ما من دعوة يدعو بها العبد، أفضل من: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْمُعَافَاةَ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ))
((Hakuna du’aa yoyote anayoiomba mja iliyo bora zaidi kuliko: Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-Mu’aafaat duniani na Aakhirah)). [Ibn Maajah 3851]
Faida Na Sharh:
المعافاة Al-Mu’aafaat: Ni vile Allaah ('Azza wa Jalla) kukusalimisha na madhara na adha za watu, na kuwaepushia watu madhara na adha zitokazo kwako, Allaah ('Azza wa Jalla) kukutosheleza nao na kuwatosheleza wao nawe, na Allaah ('Azza wa Jalla) kukuondoshea adha zao, na kuwaondoshea wao adha zako. Na uhalisia wake ni Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa) kumhifadhi mja kutokana na kila analolichukia, linalomhuzunisha na linalomsumbua katika diyn yake, dunia yake na aakhirah yake.
Haya ni maombi ya barkah aliyotujulisha bwana wa mwanzo na wa mwisho. Kila Muislamu anatakiwa awe na pupa ya kuiomba du’aa hii wakati wowote anapokumbuka.
Imesimuliwa kuwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwahutubia watu juu ya mimbari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Rasuli wa Allaah alisimama hapa niliposimama mwaka wa kwanza. Kisha akalia na kusema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema:
((إِنَّ النَّاسَ لَمْ يُعْطَوْا فِي الدُّنْيَا خَيْرًا مِنَ الْيَقِينِ وَالْمُعَافَاةِ، فَسَلُوهُمَا اللَّهَ))
(( Hakika watu hawakupewa katika dunia kilicho bora zaidi kuliko yaqiyn na Al-Mu’aafaat. Basi mwombeni Allaah viwili hivyo)). [Imesimuliwa na Ahmad katika Al-Musnad 1/212 Hadiyth nambari 38 na Abu Ya’alaa 1/121].
Al-Mu’aafaat duniani ni kupata salama na amani kutokana na shari zote za kidhahiri na za zilofichika. Na jumla yake ni kusalimika na viumbe na kujitosha nao.
Na Al-Mu’aafat huko Aakhirah ni kusalimika na madhambi na athari zake mbaya na kutokuwa na haki yoyote ya mtu au dhulma yoyote kwa waja.