08-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Kutengenekewa Dini, Dunia, Aakhirah na Umri Kuwa Ziada Ya Kheri Zote Na Mauti Kuwa Mapumziko Na Shari Zote
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
08-Kuomba Kutengenekewa Dini, Dunia, Aakhirah na Umri Kuwa Ziada Ya Kheri Zote
Na Mauti Kuwa Mapumziko Na Shari Zote
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba na kusema:
اللَّهُمَّ أَصْلِحْ لِي دِينِي الَّذِي هُوَ عِصْمَةُ أَمْرِي، وَأَصْلِحْ لِي دُنْيَايَ الَّتِي فِيهَا مَعَاشِي، وَأَصْلِحْ لِي آخِرَتِي الَّتِي فِيهَا مَعَادِي، وَاجْعَلِ الْحَيَاةَ زِيَادَةً لِي فِي كُلِّ خَيْرٍ، وَاجْعَلِ الْمَوْتَ رَاحَةً لِي مِنْ كُلِّ شَرٍّ
((Ee Allaah! Nitengenezee Dini yangu ambayo ndiyo hifadhi ya jambo langu, na Nitengenezee dunia yangu ambayo ndipo yalipo maisha yangu, na Nitengenezee Aakhirah yangu ambayo ndiyo marejeo yangu, na Ufanye uhai kuwa ni nyongeza kwangu katika kila kheri, na Yafanye mauti ni pumziko kwangu na kila shari)). [Imekharijiwa na Muslim 2720]
Faida Na Sharh:
La kwanza kabisa aliloliomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika du’aa hii ni utengefu wa Dini, kwa kuwa Dini ndio makusudio makuu ya Muislamu. Mtu ambaye Dini yake imeharibika, basi kapita utupu na amekhasiri duniani na Aakhirah. Kumwomba Allaah utengenefu wa Dini ni kuomba tawfiyq ya kushikamana na Qur-aan na Sunnah bila kuzidisha au kupunguza. Na hili halitimu ila kwa masharti mawili:
1-Kumtakasia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee katika ‘ibaadah zote.
2-Kumfuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoamuru, na kama alivyofanya.
Mwenye kushikamana na haya, basi atahifadhika na shari zote, sababu zake, matokeo yake na hatima zake.
La pili aliloliomba ni kutengenekewa maisha katika nyumba hii fupi ya dunia isiyodumu. Kutengenekewa huku ni kama kula riziki ya halaal, kumwabudu Allaah ('Azza wa Jalla) kama inavyotakikana, kupata mke au mume mwema, watoto wema wenye kutuliza jicho, nyumba pana yenye utulivu na barkah, maisha matulivu ya usalama na utulivu wa kisaikolojia. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An Nahl (19:97)]
La tatu ni kutengenekewa na Aakhirah ambako ni marejeo ya watu wote kwa ajili ya hisabu itakayoamua hatima ya mtu; Jannah au Motoni. Kutengenekewa huko kunaanzia hapa hapa duniani kwa Muislamu kupewa tawfiyq na Allaah ('Azza wa Jalla) ya kufanya mema yanayomridhisha Allaah ('Azza wa Jalla) na kuishilia mwisho mwema kutakakokuwa daraja la kuokoka.
La nne aliloliomba ni kuwa kila sekunde ya maisha yake ni nyongeza ya kila la kheri. Anamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ampe Tawfiyq ya kuwa kila analolifanya liwe ni nyongeza ya kheri kwake na manufaa kwa wengineo. Ili kulifanikisha hili, Muislamu anatakiwa aliwekee nia njema kila analolifanya. Akilala, alale kwa nia ya kuupumzisha mwili ili apate nguvu ya kufanya matendo ya kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kadhalika. Akienda kazini, awe na nia ya kufanya kazi ili kuwakimu wanawe na mkewe. Hata akimwingilia mkewe, iwe kwa niyyah ya kushibisha matamanio yake halaal na kuwa ni kinga ya kufanya zinaa na kadhalika.
Hivyo umri bora zaidi wa Muislamu, ni umri mrefu uliosheheni kheri ndani yake kwake mwenyewe na kwa wengineo.
La mwisho ni kuomba mauti kuwa ni pumziko na kila shari. Pumziko hilo ni kutokana na humuum (wahka) na ghumuum (dhiki) za kidunia kutokana na fitnah na misukosuko, na mitihani mingineyo migumu ya kimaisha inayoweza kuteteresha iymaan ya Muislamu. Na hapa tunafahamu kuwa Muumini hupumzika mapumziko mazuri kabisa na anasalimika usalama kamili anapoondoka duniani. Imekuja katika Swahiyh mbili kuwa jeneza lilipita mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((مُسْتَرِيحٌ، وَمُ
سْتَرَاحٌ مِنْه))
((Amepumzika, na wamepumzika naye))
Wakauliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Nini "Al-Mustariyhu" na "Al-Mustaraahu minhu?" Akasema:
(الْعَبْدُ الْمُؤْمِنُ يَسْتَرِيحُ مِنْ نَصَبِ الدُّنْيَا وَأَذَاهَا إِلَى رَحْمَةِ اللهِ، وَالْعَبْدُ الْفَاجِرُ يَسْتَرِيحُ مِنْهُ الْعِبَادُ، وَالْبِلَادُ، وَالشَّجَرُ، وَالدَّوَابُّ))
((Mja Muumini hupumzika na taabu ya dunia na adha zake kwenda katika Rahmahh za Allaah. Na mja mwovu, waja hupumzika naye, nchi, miti na wanyama)). [Al Bukhaariy 6512]