42-Zawadi Kwa Wanandoa: Kukubali Kukosolewa Na Mke Kwa Moyo Mkunjufu

 

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

42-Kukubali Kukosolewa Na Mke Kwa Moyo Mkunjufu

 

الاستماع إلى نقد المرأة بصدر رح

 

 

Walikuwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  wakijibizana wakati mwingine, na alikuwa akiwahama mmoja wao hadi usiku.

 

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha)  anasema kuwa kulikuwa na maneno baina yake na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) , akaambiwa 'Aaishah na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) : “Ni nani utakaemridhia baina yangu na yako?” (kusuluhisha) Je, utamridhia 'Umar? akasema 'Aaishah: Simridhii 'Umar kabisa, 'Umar ni mkali. Akasema tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) : “Je, utamridhia baba yako baina yetu?” akasema 'Aaishah: ndio. Kisha akasema:” Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  akatuma mtu aitwe Abu Bakr”, kisha akasema: “Huyu ana jambo na jambo  lake ni kadhaa.’ Akasema 'Aaishah: kisha akasema tena: muogope Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) , na useme haki tupu, akasema: akanyanyua Abu Bakr mkono wake, akampiga pua yake hata damu ikatoka- kisha akasema: huna mama Ee mtoto wa Ummu Ruumaan, unasema haki na baba yako na haki hiyo asiiseme Mtume wa Allaah. Anasema 'Aaishah: pua yake ikasimama utafikiri Swalah wawili hali yakimwagiwa maji kutoka katika kifuko cha maji na mfano wake. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  kumwambia Abu Bakr: “Mimi sikukuitia hili.” Akasema 'Aaishah: kisha akasimama na kuchukua jarida lililokuwa nyumbani, kisha akaanza kumpiga nalo akageuka akamkimbia baba yake, akajificha nyuma ya mgongo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) . Akaendelea kusema 'Aaishah: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  akamwambia: “Nimekuapia ulipotoka, sisi hatukukuita kwa hilo (unalolifanya).” (Imefanyiwa takhrijy na Al-Haafidhw Ad-Dimashqiy)

 

'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) anahadithia kuwa kuna siku moja alikuwa ameghadhibika akamwambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) : “Wewe si unadai kuwa ni Mtume wa Allah! Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  akatabasamu, na akalivumilia hilo kwa huruma na ukarimu.” (Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ahmad)

 

Mwanamke anaweza kumshupalia mumewe na akateleza katika haki ya mumewe nasi tuna mfano mwema wa kuigwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  kwani yeye kwetu ni ruwaza njema na hakika ametufundisha jinsi gani ya kuamiliana. Katika misimamo na matukio kama haya, mwanamke ni sawa na mwanamme kwa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) : “Hakika wanawake ni ndugu wa wanaume.” (Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ahmad)

 

Ni bora zaidi kwa mwanamme awe ni mwenye kutumia akili zake vizuri kwa hekima na busara na haswa zaidi katika maeneo na matukio ambayo mwanamke atakuwa ameteleza na kupotea, ama akiyakabili makosa kwa makosa basi matokeo yake ni kuzidi na kupanuka tofauti hizi, na hili ni jambo lisilopendeza kabisa, na sio kwa maslahi ya wanandoa wawili.

 

 

 

 

 

Share