014-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Ni Vipi Mgonjwa Wa Kichocho Au Mfano Wake Anastanji?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
014-Ni Vipi Mgonjwa Wa Kichocho Au Mfano Wake Anastanji?
Mwenye kichocho, atastanji na kutawadha kwa kila Swalaah. Na vinavyomtoka vinakuwa havina madhara yoyote kwake madhali wakati wa Swalaah nyingine haujaingia. Na hii ndiyo kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa. Kauli hii imesemwa na Abuu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abuu Thawr na wengineo.
Mwenye ugonjwa huu, atakuwa na hukmu ya damu ya istihaadhwah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelizungumzia hilo aliposema:
((انما ذلك عرق، وليست بالحيضة، فاذا أقبلت الحيضة فدعي الصلاة، فاذا ذهب قدرها، فاغسلي عنك الدم وصلي))
((Hakika hiyo ni damu ya mshipa na si ya hedhi. Na hedhi ikija, basi acha Swalaah. Muda wake ukimalizika, oga ujitwaharishe damu, kisha swali)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (228), Muslim (333) na wengineo. An-Nasaaiy (1/185) ameisimulia kwa tamko la: “Basi oga ujitwaharishe na damu, utawadhe na uswali” kwa nyongeza ya “utawadhe”, nayo ni “Shaadha”. An-Nasaaiy na Al-Bayhaqiy ( 1/327) wameikosoa. Naye Muslim ameashiria kwamba ina walakini, na Al-Bukhaariy hakuifanyia “ikhraaj”. Angalia “Jaami’u Ahkaamin Nisaa” kilichotungwa na Sheikh wetu Mustwafa Al- ‘Adawy – Allaah Amnyanyulie hadhi yake – (1/223-226)].
Na kwa upande wa Al-Bukhaariy, amesema: Na akasema Ubayy: “Kisha tawadha kwa kila Swalaah mpaka uje wakati huo”. [Tamko hili linawezekanika kuwa ni Marfu’u toka kwa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kutoka kwa kauli ya ‘Urwa bin Az Zubayr msimulizi wa Hadiyth toka kwa ‘Aaishah. Aliwajibu kwa kauli hiyo akina mama waliomuuliza kuhusiana na hilo kama ilivyo kwa Ad-Daaramy (1/199). Al Haafidh katika “Al-Fat-h” (1/332), amepondokea kwenye uwezekaniko wa kwanza, na Al-Bayhaqiy kwenye “As-Sunan” (1/344), amepondokea kwenye uwezekaniko wa pili. Naye Sheikh letu – Allaah Amhifadhi – ameitilia nguvu katika “Jaami’u Ahkaamin Nisaa” (1/227)].
Ninasema (Abuu Maalik): "Hukmu hii bila shaka ni kwa mwenye udhuru kwa ajili ya kumwondoshea uzito. Na hakuna shaka kuwa sharia imekuja kwa ajili ya kuuondoshea umma uzito. Allaah Mtukufu Anasema:
(( يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ ))
(( Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito)).[Al-Baqarah: (2:185)]
Maalik na wengineo wanaona kwamba haimpasi mgonjwa huyo kustanji wala kutawadha ila tu kama atapata hadathi nyingine".
Ninasema (Abuu Maalik): "Ama kutokupasa kutawadha kwa kila Swalaah endapo kama hajapata hadathi, huenda hilo lina mwono kwa wale waliotia udhwa’iyf katika kuongezwa neno “na utawadhe kwa kila Swalaah” katika Hadiyth iliyotangulia. Na lenye nguvu hapa ni kutawadha kwa kila Swalaah kama itakavyokuja katika mlango wa hedhi. Ama kutopasa kustanji, basi hilo halina cha kuzungumziwa, kwani anaweza kutokwa na kinacholazimisha kustanji na akawa na wasaa wa kufanya hivyo kabla ya Swalaah bila ya uzito wowote. Anachosamehewa ni kile tu kinachomtoka wakati wa Swalaah kwa ajili ya kuepuka uzito. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".