016-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Inafaa Mtu Kukojoa Kwa Kusimama?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

016- Je, Inafaa Mtu Kukojoa Kwa Kusimama?

 

Alhidaaya.com

 

 

Katika mlango huu, kuna Hadiyth tano toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Tatu kati ya hizo ni Hadiyth Swahiyh. Katika Hadiyth ya kwanza, ‘Aaishah anakanusha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama. Na katika Hadiyth ya pili, inaelezwa kuwa alikojoa kwa kusimama, na ya tatu inaelezwa kuwa alikojoa kwa kukaa (kuchuchumaa).

Ama Hadiyth mbili Dhwa’iyf, moja inakataza kukojoa kwa kusimama na nyingine inakuelezea kukojoa kwa kusimama kama ni utovu wa hishma. Hadiyth zenyewe ndizo hizi:

 

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: “Atakayewaambieni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikojoa kwa kusimama, basi msimsadiki. Hakuwa akikojoa ila kwa kuchuchumaa”.[Hadiyth Swahiyh Lighayrih. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (12), An-Nasaaiy (1/26), Ibn Maajah (307) na Ahmad (6/36)].

 

 

2- Hadiyth ya Hudhayfah, anasema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda mwishoni mwa jalala la watu, akakojoa kwa kusimama. Mimi nilijivuta kando, lakini aliniambia nikurubie. Nilikurubia mpaka nikasimama nyuma yake, akatawadha na kupukusa juu ya khofu zake mbili.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (226), Muslim (273), na wengineo].

 

 

3- Ni Hadiyth ya ‘Abdur-Rahmaan bin Hasanah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akiwa ameshika mkononi mwake kitu kama ngao. Alikiweka kitu hicho, kisha akakaa nyuma yake na kukojoa akikielekea”.[Hadiyth Swahiyh Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (22), An-Nasaaiy (1/27), Ibn Maajah (346) na Ahmad (4/196)].  

 

4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, amesema: “Alisema ’Umar: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa kusimama akaniambia:

((يا عمر، لا تبل قائما))   

((Ee ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama)).

Akasema: “Sikukojoa tena kwa kusimama”. [Hadiyth Dhwaiyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (308), Al-Bayhaqiy (1/202) na Al-Haakim (1/185). At- Tirmidhiy amesema ni “Hadiyth Mu’allaq” na Dhwaiyf (1/67 – Ahwadhiy)].

 

 

5- Imepokelewa toka kwa Buraydah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

 (( ثلاث من الجفاء: أن يبول الرجل قائما، أو يمسح جبهته قبل أن يفرغ من صلاته، أو ينفخ في سجوده))

 

((Mambo matatu ni utovu wa adabu: Mtu kukojoa kwa kusimama, au kuupangusa uso wake kabla hajamaliza kuswali, au kupuliza wakati yuko katika sijdah)). [Hadiyth Munkari. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika kitabu cha “At-Taariykh” (496) na “Al-Bazzaaz” (1/547). Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy, wamesema ni Hadiyth Munkar, lakini imethibiti kutokana na kauli ya Ibn Mas-’oud].

 

 

Ninasema (Abuu Maalik): “Kutokana na Hadiyth hizi, Maulamaa wametofautiana juu ya hukmu ya kukojoa kwa kusimama katika kauli tatu”: [Al-Majmuu (2/98) na Al-Awswat (1/333)].

 

 

1- Ni karaha bila ya udhuru

 

Haya yamesemwa na ‘Aaishah, Ibn Masu’d na ‘Umar katika moja ya riwaya mbili. Pia Abuu Muusa, Ash-Sha’abiy, Ibn ‘Uyaynah, Hanafiy na Shaafi’iy.

 

2- Kunajuzu kwa hali yoyote

 

Haya yamesemwa na ‘Umar (katika riwaya ya mwisho), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar, Sahl bin Sa’ad, Anas, Abuu Hurayrah na Hudhayfah. Hii ndiyo kauli ya wafuasi wa madhehebu ya Hanbali.

 

3- Kama mtu yuko sehemu laini ambapo mkojo hauwezi kumrukia itajuzu, lakini kama si hivyo, basi ajizuie.

 

Haya ni madhehebu ya Maalik. Kauli hii imeungwa mkono na Ibn Al Mundhir.

Ninasema (Abuu Maalik): “Lenye nguvu ni kwamba hakuna ukaraha wowote wa kukojoa kwa kusimama madhali mtu ana uhakika kwamba mkojo hauwezi kumrukia. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

 

1- Ni kwamba hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyokataza hilo.

 

2- Ni kuwa yaliyopokelewa kuhusu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kukaa (kuchuchumaa), hayapingani na kujuzu kukojoa kwa kusimama, bali hilo linaashiria kujuzu kwa yote mawili.

 

3- Ni kwa kuthibitika kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama.

 

4- Ni kuwa ‘Aaishah kukanusha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama, kumejengewa juu ya kile anachokijua yeye kwa mujibu wa yale ambayo Rasuli anayafanya akiwa nyumbani. Kwa hiyo kukojoa kwake nje ya nyumba yake kwa kusimama, hakukanushiki. Na hakuna shaka kwamba kutojua jambo, hakumaanishi kwamba jambo hilo halipo. Na aliyejua kama vile Hudhayfah na wengineo, ni hoja kwa yule ambaye hakujua, na kwamba jambo yakinishi hutangulizwa kabla ya kanushi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share