018-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kutahiri
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
018-Kutahiri
Maana Na Hukmu Yake
Kutahiri (katika Lugha ya Kiarabu) ni kisoukomo (Maswdar) cha kitenzi ,(ختن)yaani amekata. Na kutahiriwa ni ima kukata ngozi inayofunika kichwa cha uume, au kukata ngozi iliyopo upande wa juu wa utupu wa mwanamke (ukeketaji). [Angalia Tuhfat Al-Mawduwd cha Ibn Al-Qayyim (uk 106, 132) na Al-Majmuu (1/301)].
Ama kwa upande wa hukmu yake, Maulamaa wana rai tatu:
1- Ni wajibu kwa mwanamume na mwanamke.
2- Ni jambo mustahabu kwao.
3- Ni wajibu kwa mwanamume, lakini kwa mwanamke ni mustahabu.
Ibn Qudaamah katika kitabu cha Al Mughny (1/85) anasema: “Ama kutahiriwa, hilo ni wajibu kwa wanaume na ni ukirimio kwa upande wa haki ya wanawake na wala si lazima kwao. Hii ndio kauli ya Maulamaa wengi….”
Naye An-Nawawy katika kitabu cha Al Majmu’i (1/301) anasema: “Na madhehebu sahihi kwa matni ya Ash-Shaafi’iy na yaliyokubaliwa kwa sauti moja na Jamhuri ya Maulamaa ni kuwa kutahiriwa ni wajibu kwa wanaume na wanawake…”
Ninasema (Abuu Maalik): “Ama kutahiriwa mwanamume, inavyoonekana ni kuwa jambo hilo ni la lazima kutokana na dalili zifuatazo:
1- Hilo ni mila ya Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Kwani imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((أختتن إبراهيم خليل الرحمن بعد ما أتت عليه ثمانون سنة))
((Kipenzi cha Ar-Rahmaan Ibraahiym alitahiriwa baada ya kufikisha miaka 80)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6298) na Muslim (370)].
Na Allaah Mtukufu Anamwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفاً وَمَا كَانَ مِنَ المُشْرِكِينَ))
((Kisha Tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibraahiym mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina)).[ An-Nahl (16:123].
2- Ni kwa yale yaliyopokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu mmoja aliyesilimu:
((ألق عنك شعر الكفر واختتن ))
((Jitakase na taka za ukafiri na utahiriwe)). [Al-Albaaniy ameifanya Hadiyth Hasan kwa
Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (356) na Al-Bayhaqiy (1/172). Katika Sanad yake kuna wapokezi wawili wasiojulikana pamoja na mkatiko. Lakini Al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth Hasan kwa Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine aliyoinasibishia katika Swahiyh ya Abuu Daawuud (383). Na katika “Al-Irwa’i” (79), “mimi sikuviona”. An-Nawawiy na Ash-Shawkaaniy wamesema kuwa ni Dhwa’iyf].
3- Kwamba kutahiriwa ni katika ‘ibaadah ya Waislamu, na ni sifa yao maalumu inayowatofautisha na Mayahudi na Wakristo. Na kwa ajili hiyo, imekuwa ni wajibu kama zilivyo ‘ibaadah nyinginezo.
4- Ni kwamba kutahiri ni kukata sehemu ya mwili, na hili ni haramu, na la haramu halihalalishwi ila kwa la wajibu.
Haya ndio madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Lakini Maalik amelichukulia msimamo mkali na kusema: “Mtu ambaye hakutahiriwa, basi hafai kuwa Imaam na ushahidi wake haukubaliwi”. Na Maulamaa wengi wamenukulu toka kwa Maalik akisema kuwa hilo ni Sunnah. Lakini kuacha Sunnah kwa mujibu wa Maalik, ni dhambi. [Tuhfat Al-Mawduwd (uk 113)].
Ama kwa mwanamke, bila shaka sharia ya kutahiriwa amewekewa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
(( إذا التقى الختانان وجب الغسل))
((Zinapokutana tupu mbili zilizotahiriwa, ni lazima kukoga)).[Hadiyth Swahiyh. Ibn Maajah ameitoa kwa tamko hili (611). Na katika Swahiyh Mbili, imekuja kwa tamko la: ((Na utupu kuugusa utupu, hakika imepasa kuoga))].
Na "Al-Khitaanaani" ni mahala pa kukatwa katika dhakari ya kijana na utupu wa msichana. Na hii yaonyesha kuwa wasichana walikuwa wakikeketwa.
Kuna Hadiyth zilizopokelewa juu ya wajibu wa kumkeketa mwanamke. Hadiyth zote hizo zimekosolewa. Kati ya Hadiyth hizo ni ile ya Ummu ‘Atwiyyah aliyesema kwamba kuna mwanamke fulani aliyekuwa akikeketa mjini Madiynah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((لا تنهكي، فإن ذلك أحظى للمرأة وأحب إلى البعل))
((Usikate sana, kwani hilo linampa hadhi zaidi mwanamke na linapendwa zaidi na mume)).[Hadiyth Dwa’iyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (5271), na amesema ni dhwa’iyf].
Na katika riwaya:
(( إذا خفضت فأشمي ولا تنهكي، فإنه أنضر للوجه، وأحظى عند الزوج))
((Unapokata, basi bakisha kidogo wala usikate chote, kwani hilo linapendeza zaidi usoni na linashabikiwa zaidi na mume)). [Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Khatiyb katika kitabu cha At-Taariykh (5/327). Tazama pia Jaami’ul Ahkaam An-Nisaa’i (1/19)].
Hadiyth hizi Sanad zake ni Dhwa’iyf ingawa Mwanachuoni Al-‘Allaamah Al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika As-Silsilat As-Swahiyhah (722).
Na kama mambo ni hivi, basi mwenye kusema anaweza kusema: “Kutahiri ni wajibu kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume ingawa Hadiyth hizi ni Dhwa’iyf. Kwani asili ni kuwa wote wawili wako sawa katika hukmu isipokuwa kama kuna dalili ya kuwapambanua, na dalili hiyo haipo”.
Na mwingine anaweza kusema: “Bali hilo ni jambo mustahabu, na ni takrima kwa mwanamke, lakini si wajibu. Na picha ya kupambanua hapa kati ya mwanamume na mwanamke ni kuwa kutahiriwa kwa upande wa mwanamume, kuna maslaha kwake yanayofungamana na utwahara ambao ni moja kati ya sharti za Swalaah. Kwani endapo kama govi hilo litabakia, basi mkojo hubaki na hujikusanya ndani”. [Muono huu ameuelezea Mwanachuoni Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kama ilivyo katika Al-Mumti’i (1/134)].
Ama kwa upande wa mwanamke, faida kubwa kwake ni kuwa kukeketa humpunguzia matamanio yake. Na hii ni kutafuta ukamilifu na wala si katika mlango wa kuondosha adha.
Ninasema (Abuu Maalik): “Kukeketa wanawake kunazungukia kati ya mustahabu na wajibu. Na imepokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
(( الختان سنة للرجال مكرمة للنساء))
((Kutahiriwa ni Sunnah kwa wanaume na ukirimio kwa wanawake)).[Hadiyth Dhwa’iyf].
Lakini Hadiyth hii ni dhwa’iyf. Na lau kama ingelikuwa ni Swahiyh, basi ingemaliza mzozo. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi."