022-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Twahara Za Kihukmu
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
022-Twahara Za Kihukmu
Aina Za Maji
Maji juu ya kutofautiana sampuli zake, hayatoki nje ya aina mbili:
1- Maji Mutwlaq (Maji Twahara)
Ni yale yenye kubakia kwenye asili ya maumbile yake. Na haya ni maji yoyote yaliyochimbuka toka ardhini au yaliyoteremka toka mbinguni. Allaah Mtukufu Anasema:
((وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُمْ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً لِيُطَهِّرَكُمْ به))
((Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili Akusafisheni kwayo)). [Al-Anfaal (8:11)].
Katika aina hii, yanaingia maji ya mito, theluji, mvua barafu, na visima, hata kama yatabadilika kwa kukaa sana au kwa kuchanganyika na kitu twahara ambacho ni vigumu kuepukana nacho. Vile vile maji ya bahari, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusu maji ya bahari alisema:
((هو الطهور ماؤه الحل ميتته))
((Maji yake ni twahara na mfu yake ni halali)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (83), At-Tirmidhy (69), An-Nasaaiy (1/176) na Ibn Maajah (386)].
Maji haya yote yanafaa kutawadhia na kuogea bila hitilafu yoyote kati ya Maulamaa, na hata kama yatachanganyika kidogo na kitu twahara yataendelea kubeba jina la maji. Katika Hadiyth ya Ummu Haani ni kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alioga yeye na Maymunah katika kijibeseni kimoja chenye athari ya kinyunya. [Imefanyiwa “ikhraaj” na An Nasaaiy (240) na Ibn Maajah (378)].
Na (ushahidi mwengine ni) kwa amri ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam kwa wanawake waliomwosha binti yake Zaynab alipowaambia:
((اغسلنها ثلاثا بماء وسدر واجعلن في الآخرة كافورا))
((Mwosheni mara tatu; kwa maji na mkunazi, na osho la mwisho fanyeni kwa kafuri)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (1253) na Muslim (939)].
Ama kama yatachanganyika na kitu twahara kikaondosha jina la maji na kuwa jina jingine kama chai kwa mfano, basi haijuzu kujitwaharisha nayo. Aidha, haijuzu kujitwaharisha hadathi kwa kutumia vimiminika vilivyokamuliwa toka vitu twahara kama maji ya waridi na mfano wake, kwani hayo si maji halisi.
Ibnu Al-Mundhir anasema: “Maulamaa wote tuliohifadhi kauli zao, wamekubaliana kwa kauli moja kuwa wudhuu haufai kwa maji ya waridi, maji ya miti na maji ya m-’asfara. Na haifai kujitwaharisha ila kwa maji “mutwlaq” yenye jina la maji..” [Al-Mughny (1/11) na Al-Muhallaa (1/199)].
2- Maji yaliyonajisika
Ni maji yaliyochanganyika na najsi ikaathiri moja kati ya sifa zake kwa kubadilisha harufu yake, au rangi yake au ladha yake, kwa namna ambayo mtu akiyatumia, ataona kwa yakini kwamba anatumia najsi (badala ya maji).
Haijuzu kutawadhia kwa maji haya kwa vile yenyewe ni najsi.