06-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Amechaguliwa Kutoka Kizazi Cha Nabiy Ismaa’iyl Kisha Katika Nasaba Na Kabila Bora Kabisa
Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
06-Amechaguliwa Kutoka Kizazi Cha Nabiy Ismaa’iyl
Kisha Katika Nasaba Na Kabila Bora Kabisa.
Nabiy Ismaa’iyl ('Alayhis-Salaam) pamoja na mama yake Haajar walikuwa ni watu wa mwanzo kabisa kuishi Makkah baada ya Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kuwaacha katika bonde la Makkah ambako hapakuwa na maisha yoyote. Kisha baada ya Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kujenga Al-Ka’bah, pamoja na mwanawe Nabiy Ismaa’iyl ('Alayhis-Salaam) akawaacha hapo Makkah na Nabiy Ismaa’iyl ('Alayhis-Salaam) akaoa na ndipo kizazi chake kikaendelea na kuendelea mpaka kufikia kuzaliwa Nabiy wa mwisho, naye ni Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Amethibitisha hayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:
عَنْ وَاثِلَةَ بْنِ الأَسْقَعِ، رضى الله عنه قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَى مِنْ وَلَدِ إِبْرَاهِيمَ إِسْمَاعِيلَ وَاصْطَفَى مِنْ وَلَدِ إِسْمَاعِيلَ بَنِي كِنَانَةَ وَاصْطَفَى مِنْ بَنِي كِنَانَةَ قُرَيْشًا وَاصْطَفَى مِنْ قُرَيْشٍ بَنِي هَاشِمٍ وَاصْطَفَانِي مِنْ بَنِي هَاشِمٍ)) قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ.
Imepokelewa kutoka kwa Waathilah bin Al-Asqa’ akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Amemteua Ismaa’iyl katika wana wa Ibraahiym, na Amemteua Kinaanah kutoka wana wa Ismaa’iyl, na Amemteua Quraysh kutokana na Kinaanah na Ameteua Baniy Haashim kutokana na Quraysh na Ameniteua mimi kutokana na Baniy Haashim)) [At-Tirmidhiy, ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3605)]
Na pia:
عَنْ الْمُطَّلِبِ بْنِ أَبِي وَدَاعَةَ قَالَ: جَاءَ الْعَبَّاسُ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَكَأَنَّهُ سَمِعَ شَيْئًا فَقَامَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى الْمِنْبَرِ فَقَالَ: ((مَنْ أَنَا؟)) فَقَالُوا: أَنْتَ رَسُولُ اللَّهِ عَلَيْكَ السَّلَامُ، قَالَ: ((أَنَا مُحَمَّدُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَبْدِ الْمُطَّلِبِ، إِنَّ اللَّهَ خَلَقَ الْخَلْقَ فَجَعَلَنِي فِي خَيْرِهِمْ فِرْقَةً، ثُمَّ جَعَلَهُمْ فِرْقَتَيْنِ فَجَعَلَنِي فِي خَيْرِهِمْ فِرْقَةً، ثُمَّ جَعَلَهُمْ قَبَائِلَ فَجَعَلَنِي فِي خَيْرِهِمْ قَبِيلَةً، ثُمَّ جَعَلَهُمْ بُيُوتًا فَجَعَلَنِي فِي خَيْرِهِمْ بَيْتًا وَخَيْرِهِمْ نَسَبًا)) قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ
Kutoka kwa ‘Al-Mutw-twalib bin Abiy Wadaa’ah amesema: Al-‘Abbaas alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama kwamba alisikia jambo, basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama katika minbari akasema: ((Je, mimi ni nani?)) Wakasema: “Wewe ni Rasuli wa Allaah ‘Alaykas-salaam.” Akasema: ((Mimi ni Muhammad bin ‘Abdillaah bin ‘Abdil-Mutw-twalib. Hakika Allaah Ameumba viumbe Akanijaalia kuwa katika kundi bora lao. Kisha Akawafanya kuwa katika makundi mawili, Akanijaalia kuwa katika kundi bora kati ya hayo (mawili). Kisha Akafanya makabila Akanijaalia kuwa katika kabila bora kati ya hayo. Kisha Akafanya nyumba Akanijaalia kuwa ni mbora wao katika hizo kwa kabila na unasaba)) [At-Tirmidhiy - Swahiyh Al-Jaami’ (1472)]
Nasaba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayomalizikia kwa ‘Adnaan inakubalika kuwa ni Swahiyh kwa ‘Ulamaa wote wa Siyrah na wale wanaodurusu nasaba za watu mashuhuri, nayo ni kama ifuatavyo:
Muhammad bin ‘Abdillaah bin ‘Abdil-Muttwalib bin Haashim bin ‘Abd-Manaaf bin Quswayy bin Kilaab bin Murrah bin Ka’ab bin Luayy bin Ghaalib bin Fihr bin Maalik bin Nadhwar bin Kinaanah bin Khuzaymah bin Mudrikah bin Ilyaas bin Madhwar bin Nizaar bin Ma’di bin ‘Adnaan.
Kisha inaendelea mpaka kufikia kwa Nabiy Ismaa’iyl ('Alayhis-Salaam).
Na katika Hadiyth ndefu ya ‘Abdullaah bin ‘Abbaas pindi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwandikia barua mfalme wa Roma kisha mfalme huyo akawa anamuuliza Abuu Sufyaan maswali kadhaa kuhusu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
ثُمَّ قَالَ لِتُرْجُمَانِهِ قُلْ لَهُ كَيْفَ نَسَبُ هَذَا الرَّجُلِ فِيكُمْ قُلْتُ هُوَ فِينَا ذُو نَسَبٍ.
…kisha (mfalme wa Roma akamuuliza mwenye kutarjumi. “Muulize, je, huyo mtu (yaani Nabiy Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatokana na nasaba gani?” Nikajibu: “Anatokana na nasaba bora kabisa kati yetu.” [Al-Bukhaariy]