07-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Miongoni Mwa Hayaa Zake: Alikuwa Akiwastahi Maswahaba Zake Kuwaambia Waondoke Nyumbani Kwake
Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
07-Miongoni Mwa Hayaa Zake:
Alikuwa Akiwastahi Maswahaba Zake Kuwaambia Waondoke Nyumbani Kwake
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye kustahi na kuona hayaa mno na amethibitisha hayo Swahaba wake mtukufu:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضى الله عنه قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم أَشَدَّ حَيَاءً مِنَ الْعَذْرَاءِ فِي خِدْرِهَا.
Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye kuona hayaa mno kuliko msichana asiyevunja ungo.” [Al-Bukhaariy, na Muslim]
Alisitahi na kuona hayaa kuwataka Maswahaba waondoke siku ya Nikaah yake na Mama wa Waumini Zaynab bint Jahsh, siku ambayo palikuwa na karamu nyumbani kwake. Maelezo kama yalivyokuja katika Hadiyth kwenye Al-Bukhaariy:
عَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه قَالَ: "بُنِيَ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم بِزَيْنَبَ ابْنَةِ جَحْشٍ بِخُبْزٍ وَلَحْمٍ فَأُرْسِلْتُ عَلَى الطَّعَامِ دَاعِيًا فَيَجِيءُ قَوْمٌ فَيَأْكُلُونَ وَيَخْرُجُونَ، ثُمَّ يَجِيءُ قَوْمٌ فَيَأْكُلُونَ وَيَخْرُجُونَ، فَدَعَوْتُ حَتَّى مَا أَجِدُ أَحَدًا أَدْعُو فَقُلْتُ: يَا نَبِيَّ اللَّهِ مَا أَجِدُ أَحَدًا أَدْعُوهُ، قَالَ: ((ارْفَعُوا طَعَامَكُمْ)) وَبَقِيَ ثَلاَثَةُ رَهْطٍ يَتَحَدَّثُونَ فِي الْبَيْتِ، فَخَرَجَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فَانْطَلَقَ إِلَى حُجْرَةِ عَائِشَةَ فَقَالَ: ((السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ وَرَحْمَةُ اللَّهِ)) فَقَالَتْ: وَعَلَيْكَ السَّلاَمُ وَرَحْمَةُ اللَّهِ، كَيْفَ وَجَدْتَ أَهْلَكَ بَارَكَ اللَّهُ لَكَ؟ فَتَقَرَّى حُجَرَ نِسَائِهِ كُلِّهِنَّ، يَقُولُ لَهُنَّ كَمَا يَقُولُ لِعَائِشَةَ، وَيَقُلْنَ لَهُ كَمَا قَالَتْ عَائِشَةُ، ثُمَّ رَجَعَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فَإِذَا ثَلاَثَةُ رَهْطٍ فِي الْبَيْتِ يَتَحَدَّثُونَ، وَكَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم شَدِيدَ الْحَيَاءِ، فَخَرَجَ مُنْطَلِقًا نَحْوَ حُجْرَةِ عَائِشَةَ فَمَا أَدْرِي آخْبَرْتُهُ أَوْ أُخْبِرَ أَنَّ الْقَوْمَ خَرَجُوا، فَرَجَعَ حَتَّى إِذَا وَضَعَ رِجْلَهُ فِي أُسْكُفَّةِ الْبَابِ دَاخِلَةً وَأُخْرَى خَارِجَةً أَرْخَى السِّتْرَ بَيْنِي وَبَيْنَهُ، وَأُنْزِلَتْ آيَةُ الْحِجَابِ" البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba iliandaliwa karamu ya mkate kwa nyama siku ya Nikaah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Zaynab bint Jahsh, nikatumwa kualika watu (wahudhurie karamu), basi watu wakaanza kuhudhuria (kwa makundi). Wakawa wanakula na kuondoka. Kundi lingine likawa linahudhuria kula na kuondoka. Nikaendelea kualika watu mpaka nikakosa tena watu wa kuwaalika. Nikasema: Ee Nabiy wa Allaah! Sipati tena watu wa kuwaalika! Akasema: ((Chukua chakula kilichobakia)). Kisha kundi la watu watatu wakawa wamebakia nyumbani kwake wakipiga gumzo. Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka kwenda chumbani kwa ‘Aaishah akasema: ((Assalaamu ‘Alaykum Ahlal-Bayt wa RahmatuLLaah)). Akajibu: “Wa ‘Alaykas-Salaam wa RahmatuLLaah. Je, umemkutaje mke wako Baaraka Allaahu Laka?” Kisha akaingia vyumbani mwa wake zake wote na akawaambia vile vile kama alivyomwambia ‘Aaishah nao wakasema vile vile kama alivyosema ‘Aaishah. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akarudi na kukuta kundi la wale watu watatu bado wangaliko wakiwa wanapiga gumzo. Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mtu mwenye kuona hayaa mno basi akatoka nje (kwa mara ya pili) kisha akaingia chumbani mwa ‘Aaishah. Sikumbuki kama nilimjulisha kuwa watu wameshaondoka. Akarudi na pindi alipofikia tu mlangoni, akavuta pazia baina yangu na yake, hapo Aayah ya hijaab ikateremshwa.” [Al-Bukhaariy]
Aayah hizo ziloteremshwa ni:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ ۖ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا ﴿٥٣﴾
Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy isipokuwa mkipewa idhini ya kwenda kula si kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni, na mkimaliza kula, tawanyikeni, na wala msikae kujiliwaza kwa mazungumzo. Hakika hiyo ilikuwa inamuudhi Nabiy, naye anakustahini, lakini Allaah Hasitahi (kubainisha) haki. Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Na haipasi kwenu kumuudhi Rasuli wa Allaah. Na wala kuwaoa wake zake baada yake abadani. Hakika jambo hilo mbele ya Allaah ni kubwa mno.
إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٥٤﴾
Mkidhihirisha kitu chochote au mkikificha, basi hakika Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu.
لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ ۗ وَاتَّقِينَ اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا ﴿٥٥﴾
Si dhambi juu yao wanawake kuonana na baba zao, na wala watoto wao wa kiume, na wala kaka zao, na wala watoto wa kiume wa kaka zao, na wala watoto wa kiume wa dada zao, na wala wanawake wenzao (wa Kiislamu), na wala iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah daima ni Mwenye kushuhudia kila kitu.
[Al-Ahzaab: 53-55]