039-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mkazi Akipukusa Kisha Akasafiri
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
039-Mkazi Akipukusa Kisha Akasafiri
Aliyepukusa khufu zake naye ni mkazi kwa muda wa chini ya siku na usiku wake kisha akasafiri, basi Maulamaa wana kauli mbili:
Ya kwanza:
Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa kujumlisha na ule muda aliopukusa kabla ya kusafiri. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake, na riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Ibn Hazm pia amesema hivyo. [Ikhtilaaf Al’ulamaa cha Al- Maruuziy (uk.31), Al-Mughniy (1/299) na Al-Muhalla (2/109)].
Ya pili:
Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku moja na usiku wake, kisha itampasa aoshe miguu yake anapotawadha. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-Haaq. [Al-Ummu (1/35), Ikhtilaaf Al’ulamaa (uk.31) na Al-Awsatw (1/446)].
Yenye nguvu ni kuwa ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa vile mtu huyu inapomalizika siku na usiku wake na yeye ni msafiri, basi ana haki ya kuutimiza muda kutokana na uwazi wa maana ya Hadiyth:
((يمسح المسافر ثلاثة أيام ولياليهن))
((Msafiri hupukusa siku tatu na masiku yake)).