041-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Masharti Ya Kupukusa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

041-Mlango Wa Twahara: Masharti Ya Kupukusa

 

Alhidaaya.com

 

 

Ili kupukusa juu ya khufu mbili kuweze kujuzu, ni sharti mtu azivae akiwa twahara. Imepokelewa toka kwa Al-Mughyrah bin Shu’ubah amesema: “Nilikuwa na Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari usiku mmoja. Nilimmiminia maji toka katika chombo, naye  akaosha uso wake na mikono yake, na akapaka kichwa chake. Kisha niliinama mzima mzima ili nizivue khufu zake naye akanambia:

((دعهما، فإني أدخلتهما طاهرتين))

((Ziwache, kwani mimi nimezivaa nailhali miguu ni twahara)).

Kisha akapukusa juu yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (206) na Muslim (232)].

 

Hadiyth hii imeufanya utwahara kuwa ni sharti ya kujuzu kupukusa kabla ya kuzivaa khufu mbili. Na jambo lenye kufungamanishwa na sharti, halijuzu ila kwa kuwepo sharti hilo. Na wudhuu ndio utwahara wa kisharia uliochukuliwa na Jamhuri ya Maulamaa. [Fat-h Al-Baariy (1/370)].

 

Faida

 

Mwenye kutawadha, kisha akaosha mguu wake mmoja halafu akauvisha khufu, kisha akauosha mguu wake mwingine halafu akauvika khufu, basi wudhuu wake unapotenguka, haitojuzu kwake kupukusa kwa sababu alivaa khufu moja kabla ya kukamilisha wudhuu wake. Lakini kama aliivua ya kwanza kisha akaivaa, basi itajuzu kupukusa. Haya yamesemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Muwattwa (1/46), Al-Ummu (1/33) na Al-Mughniy (1/282)].

 

Ama Abu Haniyfah na Ahmad (katika moja ya riwaya mbili), Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Shaykh wa Uislamu, wao wanaona kwamba inajuzu kwake kupukusa juu ya khufu hizo kwa mazingatio ya ukweli kuwa alizivaa katika miguu yake yote miwili hali ya kuwa ni twahara. [Al-Mabsuwtw (1/99), Al-Awsatw (1/442), Majmu’u Al-Fataawaa (21/209) na Al-Muhalla (1/100)].

 

Ninasema:

 

“Kusema kuwa inajuzu, hakuna tatizo lolote mpaka itakapoonyesha dalili kwamba utwahara haugawanyiki, na hivyo kupelekea kwenye kuzuia. Na kwa kiakiba tu na tahadhari, ni vizuri kuingiza miguu miwili katika khufu baada ya kumaliza kutawadha. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Share