045-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Uzindushi: Kubatilika Upukusaji Hakumaanishi Kutenguka Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

045-Uzindushi: Kubatilika Upukusaji Hakumaanishi Kutenguka Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

Mtu ambaye alikuwa anapukusa juu ya khufu zake mbili kisha akazivua bila ya kupata hadathi, Maulamaa wana kauli nne juu ya hukmu yake:

 

Ya kwanza:

 

Itampasa atawadhe upya. Haya ni madhehebu ya An-Nakh’iy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-haaq na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya zamani. [Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 31), Masaail Ahmad cha Ibn Haaniy (1/19) na Al-Majmu’u (1/557)].

 

Wanasema kuwa sababu ya hilo ni kuwa kupukusa panachukua mahala pa kuosha. Na kwa ajili hiyo, anapokiondosha kinachopukuswa, basi utwahara katika miguu miwili hubatilika, na matokeo yake ni kubatilika katika viungo vyote kwa sababu havigawanyiki.

 

Ya pili:

 

Itampasa aoshe miguu yake basi. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake na Abu Thawr. Pia ni kauli mpya ya Ash-Shaafi’iy. [Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 31), na Al-Awsatw (1/458)].

 

Ya tatu:

 

Ni lazima aoshe miguu yake miwili baada tu ya kuzivua khufu. Ikiwa atachelewa, basi atatawadha upya. Haya ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth. [Al-Mudawwanah (1/41)].

 Ya nne:

 

Hawajibiki kutawadha wala kuosha miguu. Hii ni riwaya iliyopokelewa toka kwa An-Nakh’iy. Haya haya yamesemwa na Al-Hasan Al-Baswriy, ‘Atwaa na Ibn Hazm. Aidha, yamekhitariwa na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah. [Al-Muhalla (1/105), Al-Awsatw (1/460), Al-Majmu’u (1/558) na Al-Ikhtiyaaraat (uk.15)].

 

Haya ndiyo madhehebu sahihi. Hii ni kwa vile, mtu huyu akiwa na khufu zake, kwa mujibu wa Hadiyth iliyothibiti, anakuwa na utwahara kamili. Na hilo haliwezi kutanguka anapozivua khufu zake isipokuwa kama kutapatikana dalili toka katika Hadiyth au Ijma’a. Na wanaosema kuwa itamlazimu kutawadha tena au kuosha miguu miwili, hao hawana hoja. Kauli hii inatiliwa nguvu na yale yaliyothibiti toka kwa Abu Dhwabyaan kwamba yeye alimwona ‘Aliy (Allaah Amridhie) akikojoa kwa kusimama, kisha akaomba aletewe maji, akatawadha na kupukusa juu ya viatu vyake. Halafu akaingia Msikitini, akavivua viatu vyake, kisha akaswali. [Isnad yake ni Swahiyh: Imetolewa na Al-Bayhaqiy (1/288) na At-Twahaawiy (1/58). Tazama Tamaam Al-Minnah (uk115)].

 

Kisha imefanyiwa kipimo kwa mtu aliyepaka maji kichwani kisha akazinyoa nywele. Bila shaka wao hawasemi kuwa itapasa kupaka maji tena kichwani au kutawadha tena!! Na hii ndiyo sawa hasa katika suala hili. Anapozivua khufu zake bila ya kupata hadathi, basi anaweza kuswali Swalaah zozote azitakazo mpaka pale wudhuu wake utakapotenguka. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Share