053-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Yaliyosuniwa Wakati Wa Kukoga (Picha Ya Josho Kamili)
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
053-Yaliyosuniwa Wakati Wa Kukoga (Picha Ya Josho Kamili)
Mhimili katika mlango huu ni Hadiyth mbili:
1- Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alipokuwa akikoga janaba:
“Alianza, akaiosha mikono yake miwili, kisha akatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, kisha huingiza vidole vyake katika maji, kisha hufikicha kwavyo mizizi ya nywele zake, halafu humimina [Na katika riwaya nyingine: mpaka anapopata uhakika kwamba ameshatotesha ngozi yake, humimina] juu ya kichwa chake mateko matatu kwa mikono yake, kisha humimina maji juu ya ngozi yake yote”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (330), Abuu Daawuud (251), An-Nasaaiy (1/131), At-Tirmidhiy (105) na Ibn Maajah (603)].
2- Hadiyth ya Maymuuna (Allaah Amridhie). Alisema:
“Nilimtengea Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) maji ya kukoga, akaosha mikono yake mara mbili au tatu, kisha akajimiminia maji kwenye mkono wake wa kushoto kwa kutumia mkono wake wa kulia akaosha utupu wake [Na katika riwaya nyingine: utupu wake pamoja na uchafu ulioipata], kisha alisugua mkono wake kwenye udongo au ukutani [kisha akauosha], kisha alisukutua na kupaliza, akauosha uso wake, mikono yake miwili na kichwa chake, kisha alijimiminia maji juu ya kiwiliwili chake, kisha alisimama kando, akaosha makanyagio yake mawili, nikampa kitambaa, kisha akaambatisha mkono wake hivi na wala hakukitaka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (266) na Muslim (317)].
Ninasema:
“Kutokana na Hadiyth hizi mbili na nyinginezo, tunahitimisha tukisema kuwa, linalopendeza ni kuwa kuoga janaba kunatakikana kuwe katika picha ifuatayo:
1- Kuosha mikono miwili mara tatu kabla ya kuiingiza katika chombo au kuanza kukoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah:
((Alianza, akaiosha mikono yake miwili….)).
Na katika tamko la Muslim (317) kwa Hadiyth ya Maymuuna:
((Akaosha viganja vyake viwili mara mbili au mara tatu, kisha akaingiza mkono wake katika chombo…)).
Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (1/429):
“Inawezekana kuwa aliviosha kwa ajili ya kuvisafisha uchafu. Pia yawezekana kuwa huo ni mwosho wa kisharia wakati wa kuamka usingizini”.
2- Kuosha uchafu wa utupu kwa mkono wa kushoto kutokana na maelezo ya Hadiyth ya Maymuunah. Ama kuukamata utupu kwa mkono wa kulia, hilo ni makruhu kutokana na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam):
((إذا بال أحدكم فلا يأخذن ذكره بيمينه، ولا يستنجى بيمينه، ولا يتنفس في الإناء))
((Anapokojoa mmoja wenu, basi asiikamate kabisa dhakari yake kwa mkono wake wa kulia, wala asistanji kwa mkono wake wa kulia, na wala asipumulie ndani ya chombo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (154) na Muslim (267)].
3- Kuosha mkono (baada ya kuosha utupu) na kuusafisha kwa sabuni au mfano wake kama mchanga. Maymuuna katika Hadiyth yake anasema:
((Kisha akaambatisha mkono wake ardhini akaupangusa kwa udongo, kisha akuosha….)).
Na katika tamko jingine:
((Kisha akapiga ardhi kwa mkono wake wa kushoto, akausugua msuguo wa nguvu)). [Hii ni kauli ya Muslim (317)].
An-Nawawiy katika Sharh Muslim (3/231) anasema:
“Ni kwamba inapendeza kwa anayestanji kwa maji anapomaliza, aoshe mkono wake kwa udongo (mchanga) au “ashnaan” (mada mfano wa sabuni) au ausugulie na mchanga au ukuta ili usafike vizuri kutokana na uchafu”.
4- Kutawadha wudhuu kamili kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah. Na hili limethibiti katika Hadiyth za ‘Aaishah na Maymuuna.
Al-Haafidh katika Al-Fat-h (1/429) anasema:
“Inawezekana kuwa kuanza kutawadha kabla ya kukoga, ni Sunnah ya kando, kwa kuwa ni lazima kuviosha viungo vya wudhuu pamoja na kiwiliwili chote wakati wa kukoga. Na inawezekana kuwa badala ya kuviosha tena wakati wa kukoga, itatosheleza kuoshwa kwake wakati wa kutawadha. Na yeye ametanguliza kuosha viungo vya wudhuu kwa ajili ya kuvipa hadhi yake, na ili mwenye kukoga apate picha ya twahara zote mbili; kubwa na ndogo”.
Ninasema:
“Kutawadha kabla ya kukoga ni Sunnah kwa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Thawr, Daawuud na Adh-Dhwaahiriy”. [Fat-h Al-Baariy (1/426), Al-Majmu’u (1/186) na Al-Istidhkaar (3/59)].
Faida Mbili
Faida Ya Kwanza
Hukmu Ya Kusukutua Na Kupaliza Maji Puani Wakati Wa Kukoga
Katika mlango wa wudhuu, tulieleza kwamba Maulamaa wamehitilafiana katika kauli nne kuhusu kusukutua na kupaliza maji puani wakati wa kutawadha. Nasi tulitilia nguvu kwamba ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani.
Ama kukoga, Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake pamoja na Ahmad, Atwaa na Ibn Al-Mubaarak ambao madhehebu yao ni mashuhuri, msimamo wao ni kuwa kusukutua na kupaliza maji puani ni lazima wakati wa kukoga janaba. [Angalia marejeo ya mas-ala katika Nguzo za Wudhuu].
Na kati ya dalili zao ni:
1- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:
((المضمضة والإستنشاق ثلاثا للجنب فريضة))
((Kusukutua na kupaliza maji puani ni mara tatu, kwa mwenye janaba ni fardhi)). [Hadiyth Mawdhu’u (ya kutungwa): Imefanyiwa "ikhraaj" na Ad-Daara Qutwniy (1/115). Pia imepokelewa Mursal. Tazama kitabu cha Naswb Ar-Raayat (1/87)].
2- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:
((من ترك موضع شعرة من جسده لم يغسلها فعل به كذا وكذا من النار))
((Mwenye kuacha sehemu ya unywele katika kiwiliwili chake asiuoshe, ataadhibiwa vibaya motoni)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (249), Ibn Maajah (599) na Ahmad (1/94). Angalia Adh Dha’iyfah (930)].
3- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:
((أداء الأمانة غسل الجنابة، وتحت كل شعرة جنابة))
((Kutekeleza amana ni kukoga janaba, na chini ya kila unywele kuna janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Maajah (598) kwa Sanad Dhwa’iyf. Tazama At-Talkhiysw (1/142)].
Hadiyth zote hizi ni Dhwa’iyf na hazifai kutolewa dalili.
4- Ni kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kilichoelezewa katika Hadiyth ya Maymuuna (kwa kiashirio wazi), na katika Hadiyth ya ‘Aaishah (iliyojumuisha wudhuu), hayo yanabainisha Kauli Yake Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa):
(( وإن كنتم جنبا فاطهروا ))
(( Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni)). [Al-Maaidah (5:6)].
5- Ni kwamba kuosha kiwiliwili chote ni wajibu, na uso ni sehemu ya kiwiliwili. Na kwa hivyo, imekuwa ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani, kwani mawili haya ni sehemu ya uso kama tulivyosema katika mlango wa wudhuu.
Ama waliosema kuwa hilo ni Sunnah, nao ni Maalik, Al-Layth na Al-Awzaa’iy ambao ni Jamhuri, dalili zao ni:
1- Kutawadha wakati wa kukoga si wajibu [kama ilivyotangulia], na kusukutua na kupaliza maji puani ni katika mambo yanayoambatana na wudhuu. Na kama wudhuu haupo, basi yanayoambatana nao pia hupomoka. [Fat-h Al-Baariy (1/443)].
2- Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kuyafanya mawili hayo, hakuonyeshi kuwa ni wajibu kwa kuwa tu amefanya, bali ni kwa kuonyesha kuwa hayo ni mazuri na yanapendeza kuyafanya. Nayo hayaonyeshi wajibu ila ikiwa ni ubainisho wa mjumuiko uliofungamana na wajibu. Na hapa mambo si hivyo. [Fat-h Al-Baariy (1/432)].
3- Ni kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kwa Abuu Dharri wakati alipomuuliza kuhusu janaba iliyompata akakosa maji:
(( الصعيد الطيب وضوء المسلم، وإن لم يجد الماء عشر حجج، فإذا وجد الماء فليمسه بشرته))
((Mchanga twahara ni kitwaharisho kwa Muislamu hata kama hakupata maji kwa miaka kumi. Na akiyapata maji, basi ayagusishe ngozi yake)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (124), Abuu Daawuud (233), An-Nasaaiy (1/171) na wengineo kwa njia tofauti. Yenye nguvu zaidi ni ya Abuu Qulaabah toka kwa ‘Amri bin Bijdaan toka kwa Abuu Dharri ikiwa Marfu’u kama ilivyo katika Al-‘Ilal ya Ad Daaraqutwniy (1113), Ibn Abiy Haatim (1/11) na ‘Amri ambaye hajulikani. Hadiyth hii ina ushahidi toka kwa Abuu Hurayrah, na pana mvutano wa yeye kuifanya Hasan. Lakini katika Al-Irwaa, Al-Al Baaniy amesema kuwa ni Swahiyh].
Wamesema: “Al-Basharah” ni ngozi ya nje, na kwa hivyo haihusiani na kusukutua na kupaliza maji.
4- Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-am. Amesema: “Tulielezana kuoga janaba mbele ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) naye akasema:
(( أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))
((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa karibuni].
Na katika tamko:
((أما أنا فأحثي على رأسي ثلاث حثيات من ماء فإذا أنا قد طهرت))
((Ama mimi, basi humwagia mateko matatu ya maji juu ya kichwa, na hapo nakuwa nimetwaharika)). [Ash-Shawkaaniy amenukuu toka kwa Al-Haafidh kauli yake: “Neno lake (Basi hapo ninakuwa nishatwaharika), halina asili yoyote sawasawa katika Hadiyth Swahiyh au Hadiyth Dhwa’iyf].
Na tamko hili halifai.
5- Ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kwa Ummu Salamah:
(( إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات من ماء، ثم تفيضين عليك الماء، فإذا أنت قد طهرت))
(( Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)).
Ninasema:
“Lau si Hadiyth ya mwisho ya Ummu Salamah, basi wajibu wa kusukutua na kupaliza maji puani ungelikuwa na sauti ya nguvu. Lakini Hadiyth ya Ummu Salamah, inaonyesha kwa kielelezo cha nguvu kwamba kiasi kitoshelezacho katika kukoga ni kile kilichotajwa, na hakukutajwa humo kusukutua wala kupaliza maji. Na wala haisemwi: “Mawili hayo yanaingia katika neno lake (kisha unajimiminia maji), kwani maana ya kumimina, haiyagusi mawili haya kama inavyoonekana wazi.
Hivyo basi, madhehebu ya Jamhuri inayosema kuwa kusukutua na kupaliza ni jambo mustahabb na wala si wajibu wakati wa kukoga, ndiyo yenye nguvu kwangu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
Faida Ya Pili
Ni Wakati Gani Miguu Miwili Huoshwa?
Lililo wazi kutokana na Hadiyth ya Maymuuna ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikawisha kuosha makanyagio yake mawili mpaka pale alipomaliza kukoga.
Al-Bukhaariy katika tamko lake anasema:
“Alipomaliza kukoga, aliosha miguu yake”.
Ama Hadiyth ya ‘Aaishah, hakuna kingine humo zaidi ya kuwa tu Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikuwa akitawadha kabla ya kukoga. [Katika riwaya ya Muslim (316) kutoka kwa ‘Aaishah, mwishoni mwa Hadiyth hii anasema: “..kisha akamimina juu ya kiwiliwili chake chote, kisha akaosha miguu yake miwili”. Ni ziada ambayo haikuhifadhiwa. Tizama ‘Ilal Muslim ya Hirawiy (69), Attamhiyd (22/93) na Fat-h Al-Baariy ya Ibn Rajab (1/234)]. Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wamekuwa na mielekeo minne kutokana na Hadiyth hizi mbili: [Fat-h Al-Baariy ya Ibn Hajar (1/362), Al-Mughniy (1/288), Sharh Al-‘Umdah (1/371) na Al-Khilaafiyaat cha Al-Bayhaqiy (2/425)].
1- Ni mustahabbu kukawisha kuosha miguu miwili wakati wa kukoga kutokana na Hadiyth ya Maymuuna. Haya ni madhehebu ya Jamhuri.
2- Ni kutawadha wudhuu kamili kabla ya kukoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah. Sababu ni kuwa Hadiyth hii inaelezea alivyokuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) akifanya aghalabu kinyume na Hadiyth ya Maymuuna ambaye ameelezea josho moja tu. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Maalik na Ahmad.
3- Mtu anakhiyarishwa, ima kuanza kuosha miguu miwili pamoja na wudhuu au kuiosha mwishoni. Hii ni riwaya ya Ahmad.
4- Kama mtu anaoga sehemu isiyo safi, basi ataiosha miguu yake mwishoni. Na kama si hivyo, basi ataiosha mwanzoni wakati akitawadha. Haya ni madhehebu ya Maalik.
Ninasema:
“Mwelekeo huu wa mwisho ndio wenye nguvu zaidi. Lakini pamoja na yote hayo, jambo hili lina wasaa na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
5- Ni kumimina maji juu ya kichwa mara tatu mpaka yafike katika mashina ya nywele.
6- Ni kuanzia upande wa kulia wa kichwa kisha upande wa kushoto.
7- Kufikicha (kusugua) nywele. Hadiyth ya ‘Aaishah inasema:
((Kisha hufikicha nywele zake kwa mkono wake mpaka anapohakikisha kuwa ameilowesha ngozi yake, hapo humiminia juu yake maji mara tatu..)).
Imepokelewa vile vile toka kwa ‘Aaishah akisema:
(( Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alipokuwa akikoga janaba, hutaka aletewe kitu kama “alhilaab”, huikamata kwa kiganja chake, kisha huanza kwa upande wake wa kulia wa kichwa, kisha upande wake wa kushoto….)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (258) na Muslim (318)].
“Alhilaab” ni chombo kinachojaa mkamuo mmoja wa maziwa ya ngamia (Ma’alim As-Sunan) cha Al-Khattwaabiy (1/69).
Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah vile vile akisema: (( Mmoja wetu alipokuwa akipatwa na janaba, huchukua kwa mkono wake mateko matatu juu ya kichwa chake, kisha huchukua maji kwa mkono wake juu ya upande wake wa kulia na kwa mkono wake mwingine juu ya upande wake wa kushoto. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (277)].
Faida
Je, Ndevu Huasuliwa Wakati Wa Kukoga Janaba?
Jamhuri ya Maulamaa ambao ni Maalik, Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm wamesema: “Haimlazimu kuziasulia, bali ni jambo mustahabbu”. [Al-Muhalla (2/33), Al-Awsatw (2/127) na At-Tamhiyd (22/95)].
Ninasema:
“Hili mahala pake ni pale yanapokuwa maji yanafika hadi kwenye ngozi, na kama si hivyo, basi ni lazima kuziasulia ili kuyafikisha maji ndani yake. Na la akiba zaidi kwa vyovyote, ni kuziasulia ndevu zake kutokana na ujumuishi wa neno la ‘Aaishah: ((basi huasulia kwayo mashina ya nywele zake”.
8,9- Kumimina na kuyaeneza maji katika kiwiliwili chote kwa kuanzia upande wa kulia kisha wa kushoto.
Kumimina na kueneza maji katika kiwiliwili kizima ni jambo lililothibiti katika Hadiyth zote zinazotoa picha ya josho lake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam).
Ama kuanzia kulia, ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema:
((Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kulikuwa kunampendeza kuanza kwa kulia akivaa viatu, akitembea, akijitwaharisha na katika mambo yake yote)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (168) na Muslim (268)].
Faida Mbili
Faida Ya Kwanza
Kujimiminia Maji Kiwiliwili Chote Kunakuwa Ni Mara Moja Tu.
Na hili liko wazi katika muktadha wa Hadiyth mbili za ‘Aaishah na Maymuuna. Ndani ya Hadiyth hizi, pametajwa kuoshwa mara tatu mikono miwili na kichwa. Ama kiwiliwili kizima, ‘Aaishah anasema:
((Kisha anamiminia juu ya kiwiliwili chake chote)).
Na Maymuuna anasema:
((Kisha alimiminia juu ya kiwiliwili chake)).
Na Ibn Batwaal amesema: [Fat-h Al-Baariy (1/439)].
“ Na kwa vile suala halikuainishwa kwa idadi, basi lichukuliwe chini ya ilivyotajwa, nayo ni mara moja, kwani asli ni kutozidisha juu yake”.
Ninasema:
“Na hili ni mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad na masahibu wa Maalik. Shaykh wa Uislamu amelikhitari hili. Na Jamhuri wamestahabbu kufanya mara tatu”.
Faida Ya Pili
Hukmu Ya Kusugua Viungo Vya Kukoga [Al-Muhalla (2/30), Al-Istidhkaar (3/63), Al-Mughniy (1/290), Bidaayat Al-Mujtahid (1/55) na As-Sayl Al-Jarraar (1/113)]
Maulamaa wamekhitalifiana:
Je, ni sharti kupitisha mkono katika kiwiliwili kizima wakati wa kukoga? Au yatosha kumimina maji tu katika kiwiliwili chote hata kama mtu hakupitisha mkono wake katika kiwiliwili chake?
Au kwa maana nyingine tunasema: Je, kukoga kunatimu kwa kujimiminia maji tu au ni lazima pia kusugua juu ya kitu?
Jamhuri ya Maulamaa (kinyume na Maalik na Al-Mazniy) wanaona kuwa hakuna ulazima kusugua, bali ni mustahabbu. Na lau kama mtu atajimwagia maji mwenyewe katika kiwiliwili chake, basi atakuwa ametekeleza aliyowajibishwa na Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa). Hali kadhalika, akipiga mbizi majini na maji yakaupata mwili wake wote.
Dalili za makundi mawili katika suala hili ni zile zile zilizokwishatangulia kuelezewa katika hukmu ya kusukutua na kupaliza maji puani.
Na lililo wazi ni kuwa kusugua ni jambo mustahabbu na wala si wajibu.
Na Hadiyth ya ‘Imraan ibn Haswiyn – pamoja na Hadiyth ya Ummu Salamah inayatilia nguvu madhehebu haya katika kisa cha “Al-Muzaadatayn”. Humo panaelezwa: ((… na mwisho wa hilo ulikuwa ni kumpa chombo chenye maji yule ambaye imempata janaba, akasema: Nenda, halafu ujimiminie”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (344)].
Na kwa haya, lau mtu akisimama chini ya bafu la manyunyu (bomba la kuogea), na maji yakafika katika kiwiliwili chake chote, basi kukoga kwake ni sahihi kukiambatana na niya.