057-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Masuala Yanayohusiana Na Kuoga
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
057-Masuala Yanayohusiana Na Kuoga
- Si lazima kutawadha baada ya kuoga
Aliyeoga josho la kisharia na akataka kuswali, basi si lazima atawadhe hata kama alikuwa hajatawadha wakati akioga, kwani twaharisho la janaba linaondosha vile vile twaharisho la hadathi ndogo. Hii ni kwa vile vizuizi vya janaba ni vingi zaidi kuliko vizuizi vya hadathi ndogo. Hivyo basi, kidogo humezwa na kingi.
Imepokelewa na ‘Aaishah akisema: ((Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa hatawadhi baada ya kuoga janaba)). [Hadiyth Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (107), An-Nasaaiy (1/137) na Ibn Maajah (579)].
Na katika riwaya nyingine: ((Anaoga na anaswali rakaa mbili, na wala simwoni akifanya wudhuu baada ya kuoga)). [Hadiyth Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (250) na Ahmad (6/119)].
Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) amesema: “Kama hukugusa utupu wako baada ya kumaliza kuoga, basi ni wudhuu gani ulio kamili zaidi ya kuoga?” [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdurraaziq katika Al-Muswannaf (1039)].
Ninasema:
“Juu ya haya, panazalikana nukta kwamba si lazima kwa mwenye kuoga janaba kunuwia kuondosha hadathi ndogo. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri na Ibn Taymiyah. [Al-Mabsuwtw (1/44), Ash-Sharh As-Swaghiyr (1/65), Al- Ummu (1/36), Majmu’u Al-Fataawaa (21/397) na Al-Muhalla (2/44)].
Ama Mahanbali, wao wanaona kwamba akinuwia twahara mbili, basi zote mbili zitamtosheleza. Lakini akinuwia kuoga janaba tu, basi hana ila hilo alilolinuwia tu. [Al-‘Uddat Sharh Al-‘Umdah (uk.48)].
- Yakikusanyika mawili yenye kuwajibisha kuoga kama hedhi na janaba, au janaba na ijumaa
Hapa josho moja tu litamtosheleza yote mawili kama atayanuwia yote mawili. Hii ni kauli ya Mafuqahaa wengi. [Al-Mughniy (1/292) bali imenukuliwa Ijma’a juu yake katika ((Rahmat Al- Umma Fiy Ikhtilaafi Al-Aimmah)) (uk 51). Na Ijma’a hii imetenguliwa kinyume na Ibn Hazm katika Al-Muhalla (uk.42-47). Mwanachuoni Arifu na Mweledi Al-Albaaniy amekubaliana naye katika Tamaam Al-Minnah (uk 126)].
- Mwanamke akiwa na janaba kisha akaingia hedhini kabla hajaoga
Kauli sahihi zaidi ya Maulamaa ni kuwa haimlazimu kuoga janaba, bali itamlazimu aoge janaba na hedhi kwa pamoja na ayanuwie yote mawili wakati damu ya hedhi inapokatika. Haya ni madhehebu ya Ahmad. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321)].
Maulamaa wengine wanaona kwamba itamlazimu kuoga janaba, kisha hedhi inapokatika, ataoga josho la hedhi. Haya ni madhehebu ya ‘Atwaa, An-Nakh’iy na Al-Hasan.
Nao wengine wamesema kuwa itamlazimu aoshe utupu wake, kisha damu inapokatika aoge.
Kauli zote hizi mbili hazina dalili yoyote, na lililo sahihi na sawa zaidi ni kauli ya kwanza.
Lakini hili halimkatazi kuwa akitaka kuoga janaba au kuuosha utupu wake, kisha aoge damu inapokatika, basi atafanya hivyo na hakuna kosa lolote kwake, lakini si lazima.
- Inajuzu kwa mwanamume kuogea mabaki ya maji ya mkewe
Hili limekwishaelezewa kiuchambuzi katika mlango wa (Hukmu za Maji).
- Inajuzu mume kuoga pamoja na mkewe
Inajuzu wote wawili kuangaliana tupu zao bila ya ukaraha wowote. Imepokelewa na ‘Aaishah akisema:
((Nilikuwa naoga mimi na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika chombo kimoja [yeye ananiwahi, nami namwambia: niachie mimi niachie] wote tukiwa na janaba)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321)].
- Haijuzu kuoga uchi hadharani
Kama akijisitiri watu wasimwone, basi hakuna ubaya. Tumekwishaitaja Hadiyth ya Maymuunah akisema: ((Nilimwekea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) maji ya kuoga [na pazia yake] akaosha mikono yake miwili…..)).
Na imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) kwamba Muusa Alayhi Ssalaam alioga uchi, hali kadhalika Ayyuub Alayhi Ssalaam. Lakini hili ni faraghani.
- Anayepatwa na hadathi wakati wa kuoga
Mwenye janaba akipatwa na hadathi kabla ya kumaliza kuoga, basi atakamilisha wala hatoanza upya, kwani hadathi haitengui josho, hivyo basi kuwepo kwake hakuathiri josho, bali ni juu yake kutawadha.
Na hii ni kauli ya Maulamaa wengi akiwemo ‘Atwaa na Ath-Thawry. Ibn Qudaamah na Ibn Al-Mundhir wamelikubali hilo.