015-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Niya

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

015-Niya

 

Alhidaaya.com

 

 

Niya maana yake ni kuazimia kufanya ‘ibaadah kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah Mtukufu. Swalaah haiswihi bila ya niya kwa hali yoyote, na niya haipomoki kwa hali yoyote ila kwa mtu kuondokewa na akili. Katika hali hiyo, taklifu nayo hupomoka, kwani akili ndiyo kitovu cha taklifu.

 

Ijma’a imefungika kuizingatia niya kuwa ni sharti ya kuswihi Swalaah. [Ad-Dusuwqiy (1/233), Mughnil Muhtaaj (1/148), Bidaayatul Mujtahid (1/167) na Kash-Shaaful Qinaa (1/313)]

 

Na asili ya hilo, ni Kauli Yake Allaah Mtukufu:

 

((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ))

((Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaat; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara)). [Al-Bayyinah (98:5)]

 

Na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( Hakika amali ni kwa niya, na hakika kila mtu ni kwa lile alilolinuwia)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mara nyingi, nayo imepasishwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

·       

Yasiyokuwa Na Mabishano:

 

1- Niya mahala pake ni moyoni na si kwa ulimi katika ‘ibaadah zote ikiwemo Swalaah.

 

2- Akitamka kwa ulimi kwa kusahau kinyume na yale aliyoyanuwia moyoni, yanayozingatiwa ni ya moyoni. Ni kama aliyekusudia moyoni kuswali Adhuhuri lakini ulimi ukateleza akataja Alasiri kwa kusahau.

 

3- Akitamka kwa ulimi bila kuweka niya moyoni, basi haitotosheleza.

 

4- Kutamka niya kwa sauti katika Swalaah ni katika bid-’a mbaya, na si katika bid-’a njema. Na haya yamekubaliwa na Waislamu wote. Hakuna yeyote aliyesema kwamba kuitamka niya kwa sauti ni Sunnah au bid-’a njema, na anayesema hivyo, basi amekhalifu Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Ijma’a ya Maimamu wanne na wengineo. Mwenye kusema hivi atatubishwa, na kama atatubu basi, kama atakataa ataadhibiwa adhabu stahiki. [Majmu’ul Fataawaa (22/233)]

 

Mbali na hilo kuwa bid-’a, pia huwakera wenye kuswali.

 

·       

Kuitamka Niya Hata Kwa Siri Ni Bid-’a

 

Sheikh wa Uislamu anasema: [Majmu’ul Fataawaa (22/237-238)]

 

“Hajanukuu Muislamu yeyote si kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wala kutoka kwa Swahaba yeyote kwamba Rasuli alitamka tamko la niya kabla ya kupiga takbiyr, si kwa siri wala kwa sauti, wala kwamba aliamuru hilo. Ni maarufu kwamba hima na shime za kunukuu hilo zipo tele lau kama hilo lingekuwepo, na juu ya uasili wa tawaatur kidesturi na kisharia, haiwezekani kufichwa unukuu wa hilo. Na kwa vile hakuna yeyote aliyenukuu, imejulikana kwa hakika isiyo na shaka kwamba hilo halikuweko. Kuzidisha hili na mfano wake katika sifa ya Swalaah, kunaingia ndani ya wigo wa mazidisho mengineyo yaliyozushwa kwenye ‘ibaadah nyinginezo kama mwenye kuzidisha adhana na iqaamah katika Swalaah ya ‘Iyd mbili, au mwenye kuswali rakaa mbili katika Jabal Marwa wakati wa kusai na mengineyo mfano wa hayo”.

 

Kisha niya ni nyepesi zaidi kuliko kuitamka. Mwenye kutawadha, kisha akatoka kuelekea Msikitini huku akiwa analijua lengo lake la kufanya hivyo, basi huyo kaipata niya. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu anasema: “Niya hufuata lijulikanalo. Mwenye kujua analotaka kulifanya, basi ashalinuwi kwa kuwa haiwezekani kutenda bila niya”. [Al-Ikhtibaaraat ukurasa wa 49]

 

·       

Kuainisha Swalaah

 

Katika niya, ni lazima mtu aiainishe Swalaah anayoiswali; kama ni ya Sunnah au ya Faradhi, Adhuhuri au Alasiri. Na makusudio ni kuhudhurisha haya katika moyo.

 

·       

Mahala Pa Niya

 

1- Hakuna mvutano wowote kati ya Maulamaa kwamba niya ikikutana na takbiyr (takbiyr ikaja baada yake moja kwa moja) basi itatosheleza, bali hili ndilo asili na bora zaidi.

 

2- Hakuna mvutano wowote kati yao kwamba niya baada ya takbiyr haitoshelezi.

 

3- Akinuwia Swalaah, kisha akashughulishwa, halafu akaja kuswali, Swalaah yake itaswihi  kwa kuwa niya yake inaambatana na hukmu madhali hakukusudia kuivunja Swalaah.  [Al-Inswaaf (1/23), na Al-Mubdi’u (1/417). Ibn ‘Uthaymiyn ameliunga mkono katika Al-Mumti’i (2/291)]

 

Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

·       

Kugeuza Na Kubadili Niya Wakati Wa Swalaah

 

[Al-Mumti’i (2/294-301) na Al-Ikliyl (1/348-355) cha Sheikh Wahiyd Baaliy Allaah Amhifadhi]

Kuna picha mbalimbali za kuhama kutoka niya moja kwenda nyingine katika Swalaah. Kati yake:

 

1- Kutoka Swalaah ya faradhi kwenda Swalaah yoyote ya Sunnah

 

Kwa mfano, haijuzu kwa mwenye kuswali Adhuhuri peke yake, kisha akaona watu wanaswali Jamaa, aigeuze Faradhi yake kuwa Sunnah, kisha aswali pamoja nao Jamaa.

 

2- Kutoka faradhi kwenda faradhi nyingine

 

Haijuzu, na faradhi zote mbili hubatilika. Faradhi ya kwanza kwa vile ameikata, na ya pili kwa kutoitilia niya kabla ya kuianza. Picha ya hii ni kama mtu aliyeanza kuswali Alasiri, kisha akakumbuka kwamba hakuswali Adhuhuri, hapo haitojuzu aigeuze kuwa Adhuhuri.

 

3- Kutoka Sunnah kwenda faradhi

 

Haijuzu vile vile kutokana na sababu iliyotangulia.

 

4- Kutoka Sunnah maalumu kwenda Sunnah yoyote

 

Haijuzu, kwa kuwa Sunnah maalumu inakusanya niya ya Sunnah yoyote. Mfano wake ni mtu aliyenuwia kuswali rakaa nne za Sunnah ya Adhuhuri, kisha akaona jamaa, halafu akaigeuza Sunnah hiyo rakaa mbili ili aiwahi jamaa.

 

5- Kutoka Sunnah maalumu kwenda Sunnah maalumu

 

Haijuzu, ni kama aliyenuwia Sunnah ya maamkizi ya Msikiti, kisha katikati yake akaigeuza Sunnah ya Alfajiri. Ya kwanza itabatilika kwa kuikata, na ya pili kwa kutoitilia niya mwanzoni.

 

6- Kutoka Sunnah yoyote kwenda Sunnah maalumu

 

Haijuzu kwa yaliyotangulia.

 

7- Kutoka niya ya imamu kuwa maamuma

 

Hii inajuzu kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusiana na kisa cha Abu Bakri kuwaswalisha watu. Anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia Msikitini, Abu Bakri alisikia mchakato wake na kuanza kurudi nyuma. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwashiria abaki alipo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaja mpaka akakaa kushotoni mwa Abu Bakri. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anawaswalisha watu kwa kukaa na Abu Bakri amesimama. Abu Bakri anafuata Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na watu wanaifuata Swalaah ya Abu Bakr”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (664) na Muslim (418].

 

8- Maamuma kutoka imamu kwenda imamu mwingine

 

Inajuzu, kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia. Watu walikuwa wakimfuata Abu Bakri, kisha wakamfuata Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na pia kisa cha kuuawa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) ambapo alimtanguliza ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf akakamilisha Swalaah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (664) na Muslim (418)].

 

9- Kutoka maamuma kuwa imamu

 

Inajuzu. Ni kama imamu kutokewa na udhuru katika Swalaah, na maamuma mmoja akakamata nafasi yake kutokana na Hadiyth ya ‘Umar iliyotangulia.

 

10- Kutoka anayeswali peke yake na kuwa imamu

 

Inajuzu. Ni kama mtu kuwa anaswali peke yake akaja mtu mwingine akamfuata. Hapo ataikamilisha Swalaah akiwa imamu kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Nililala kwa khalati yangu. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama usiku kuswali, nami nikasimama kuswali pamoja naye. Nilisimama kushotoni mwake, akanikamata kichwa changu na kunisimamisha kuliani mwake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (699) na Muslim (763)].

 

Katika hili hakuna tofauti kati ya Swalaah ya Sunnah au faradhi juu ya kauli Swahiyh.

 

11- Kutoka imamu na kuswali peke yake

 

Haijuzu ila kwa udhuru. Ni kama maamuma kupatikana na udhuru akamwacha imamu peke yake. Wakati huo itajuzu na Swalaah yake ni Swahiyh.

 

12- Kutoka maamuma na kuswali peke yake

 

Imesemwa: Inajuzu kutokana na udhuru wa kisharia kama imamu kurefusha Swalaah zaidi ya inavyotakikana kiSunnah, au maamuma kupata maumivu ya ghafla na mfano wake katika yanayomlazimisha kuswali peke yake, kufupisha na kuondoka. Waliosema hivi wametolea dalili kisa cha mtu aliyeswali nyuma ya Mu’aadh bin Jabal ambaye alirefusha kisomo. Mtu yule akatoka kwenye Swalaah, akaswali peke yake. Kisha akaenda kumlalamikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye hakumwamuru aswali tena. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (699) na Muslim (763)].

 

Imesemwa pia: Hapaswi kuswali peke yake, bali anatakikana aivunje Swalaah kama atatokewa na dharura yoyote, kisha aswali peke yake. Waliosema hivi wamejibu kwamba Hadiyth ya Mu’aadh inaonyesha kwamba mtu yule alitoka kwenye Swalaah, kisha akaswali peke yake kama ilivyo kwenye riwaya ya Muslim (465) isemayo: “Mtu akatoka kando, akatoa taslimu, kisha akaswali peke yake”.

 

Ninasema: [Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn ameliwafiki hili kinyume na alilowafiki Sheikh Wahiyd]

Rai ya kwanza ina nguvu zaidi hata kwa riwaya ya mwisho. Kitendo cha mtu yule hakionyeshi kwamba kuswali peke hakujuzu. Kisha ninalolipa nguvu mimi ni kuwa uimamu na umaamuma ni sifa ya ziada juu ya asili ya Swalaah. Niya ya wawili hawa, haina athari katika kuswihi kwa Swalaah ingawa inaweza kuathiri katika kuzipata thawabu za jamaa kama zinavyoonyesha juu ya hili Hadiyth kadhaa zilizotangulia kuhusiana na niya ya imamu na maamuma. Allaah Mtukufu Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

·       

Kutofautiana Niya Ya Imamu Na Maamuma

 

[Angalia Al-Manhiyyaat Ash-Shar-’iyyah Fiy Swifatis Swalaat cha Al Kamaaliy ukurasa wa 14 na zinazofuatia]

 

Hakuna mahitalifiano katika usharia wa maamuma kumfuata imamu na kuafikiana niya yao sawasawa ikiwa Swalaah ya faradhi au ya Sunnah. Kisha Maulamaa wametofautiana endapo kama niya ya imamu na maamuma itatofautiana. Lililo sahihi ni kuwa hakuna sharti ya kuwafikiana niya ya maamuma na niya ya imamu. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm. [Mughnil Muhtaaj (1/502), Al-Muhallaa (4/223) na Bidaayatul Mujtahid (1/167)] Na dalili ya hili ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( Hakika amali ni kwa niya, na hakika kila mtu ni kwa lile alilolinuwia)).

 

Ibn Hazm amesema: “Rasuli (Alayhis Salaam) ameeleza wazi hapa kwamba kila mmoja ni kwa lile alilolinuwia, na kwa hiyo, imekuwa sahihi kiyakini kwamba imamu ana niya yake na maamuma ana niya yake, na niya ya mmoja haifungamani na niya ya mwingine”.

 

Ama Hadiyth isemayo:

(( Hakika amefanywa imamu ili afuatwe, nanyi msikhitilafiane naye)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (689) na Muslim (411)].

 

Makusudio yake ni kuwa msikhitilafiane naye katika vitendo vya kidhahiri kwa dalili ya kauli yake katika Hadiyth hii hii:

(( Anaporukuu nanyi rukuuni, anaponyanyuka nanyi nyanyukeni, anaposujudu nanyi sujuduni, na anaposwali kwa kukaa, nanyi nyote swalini kwa kukaa)). Hadiyth hapa haifungamani na kutofautiana niya, na linaloonyesha hilo ni makubaliano ya Maulamaa wote kwamba mwenye kuswali Sunnah anaweza kumfuata mwenye kuswali faradhi pamoja na kuwa niya zao ni tofauti (kama itakavyokuja baadaye). Pia dalili nyinginezo zitakazokuja katika picha za kutofautiana niya mbili. Nazo ni:

 

1- Mwenye kuswali Sunnah kumfuata mwenye kuswali faradhi

Inajuzu kwa Maulamaa wote wakiwemo Maimamu wanne na wengineo kutokana na dalili zifuatazo:

 

(a) Hadiyth ya Abuu Dharri aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza: (( Utafanyaje ikiwa viongozi wako wanaichelewesha Swalaah na wakati wake, au wanaiua Swalaah na wakati wake?)) Nikamjibu: “Unaniamuru nini?” Akasema: ((Swali Swalaah katika wakati wake, na ikiwa utaiwahi pamoja nao basi swali, kwani hiyo itakuwa ni ziada kwako)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa katika mlango wa Nyakati zilizokatazwa kuswali].

 

(b) Hadiyth ya Yaziyd bin Al-Aswad aliyesema: “Nilikuwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hijjah yake. Nikaswali pamoja naye Swalaah ya Alfajiri katika Msikiti wa Al-Khayf. Alipomaliza Swalaah yake na kuondoka, mara walikuja watu wawili katika watu waliochelewa ambao hawakuwahi kuswali pamoja naye. Akasema: ((Nitawafuatia)). Wakaletwa huku vifua vyao vikitetema. Akawauliza: ((Kitu gani kimewazuia msiswali nasi?)) Wakasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Sisi tulikuwa tumeswali safarini. Akawaambia: ((Msifanye! Mkiswali safarini, kisha mkaja Msikiti wa jamaa, basi swalini pamoja nao, kwani hiyo inakuwa ni ziada kwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa katika mlango wa Nyakati zilizokatazwa].

 

2- Mwenye kuswali faradhi kumfuata mwenye kuswali Sunnah: Inajuzu kwa dalili zifuatazo:

 

(a) Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah isemayo: “Mu’aadh bin Jabal alikuwa akiswali na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Ishaa ya mwisho, kisha hurejea kwa watu wake na kuswali nao tena Swalaah hiyo”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (711) na Muslim (465) na tamko ni lake].

 Wengine wameongeza: Hiyo kwake ni Sunnah na kwao ni faradhi”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy katika Al-Umm (1/173, Atw-Twahaawiy (1/409) na Ad-Daara Qutwniy (1/274). Kuna “’an-‘ana” (fulani toka kwa fulani) ya Ibn Jariyj, naye ni mdanganyifu. Al-Haafidh kaipa daraja ya kuwa ni Swahiyh katika Al-Fat-h]

 

Al-Haafidh amesema: “Kwa Hadiyth hii, pametolewa dalili juu ya kuswihi mwenye kuswali faradhi kumfuata mwenye kuswali Sunnah, kwa msingi kwamba Mu’aadh alikuwa akinuwia faradhi kwa Swalaah ya kwanza, na Sunnah kwa Swalaah ya pili. Kisha ziada iliyoashiriwa, imetolewa dalili kadhalika”.

 

Ninasema: “Aliyoyaeleza Al-Haafidh yanaonyesha kwamba mimi nimepata katika riwaya ya Hadiyth nyingine – katika kisa cha mtu aliyemshitaki Mu’aadh – neno lake: “..na kwamba Mu’aadh aliswali pamoja nawe ‘Ishaa, kisha akaja akaanza kwa Suwrat Al-Baqarah…..Hadiyth. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa hivi karibuni]”. Ndani ya riwaya hii, kuna ishara kwamba Swalaah aliyoiswali Mu’aadh pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa faradhi ya ‘Ishaa.”

 

(b) Hadiyth ya Abu Bakrah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ya Adhuhuri ya vita. Baadhi yao walipanga safu nyuma yake na wengine mkabala na adui. Aliswali nao rakaa mbili, akatoa tasliym, kisha wakaondoka wale walioswali naye, wakasimama sehemu ya wenzao. Halafu wakaja wale (waliokuwa mkabala na adui) wakapanga swafu nyuma yake. Akaswali nao rakaa mbili, kisha akatoa tasliym. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa ameswali rakaa nne, na Maswahaba wake rakaa mbili mbili”. [Wapokezi wake wanaaminika:  Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1248). Al-Hasan kuisikia toka kwa Abu Bakrah kuna mvutano pamoja na kwamba Al-Bukhaariy amemfanyia “ikhraaj” Hadiyth nyingi, naye hatosheki kwa uwezekano wa kuwepo maonano tu!! Angalia Jaami’u At-Tahswiyl (1/163)]

 

Ash-Shaafi’iy anasema katika Al-Ummu (1/173):  “Ya mwisho katika mbili hizi ni Sunnah kwa Rasuli, na kwa wengineo ni faradhi”.

 

Na kwa picha hii yote, inajuzu kwa mtu aliyeikuta Jamaa ya watu wanaoswali tarawehe (ikiwa hakuwahi kuswali ‘Ishaa) kujumuika nao kwa niya ya ‘Ishaa. Imamu akitoa tasliym baada ya rakaa mbili, yeye atakamilisha peke yake, au atasimama kwa rakaa mbili zilizosalia. Imamu anaposimama kwa rakaa mbili nyinginezo, atamfuata, kisha atatoa tasliym pamoja naye. La kwanza ni bora zaidi. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Mwenye kuswali faradhi kumfuata mwenye kuswali faradhi nyingine:

 

Hii ina hali tatu:

 

(a) Kulingana idadi ya rakaa za faradhi mbili. Ni kama kuswali qadhwa ya Adhuhuri nyuma ya anayeswali Alasiri au ‘Ishaa. Hii inajuzu kutokana na ujumuishi wa yaliyotangulia.

 

(b) Idadi ya rakaa za maamuma za faradhi kuzidi rakaa za imamu. Ni kama anayeswali Adhuhuri nyuma ya anayeswali Alfajiri au Magharibi. Hii inajuzu kutokana na yaliyopita ya kutolazimu kuwa sawa niya mbili, na kwa kipimo  cha Swalaah ya aliyetanguliwa kwa rakaa, au mkazi kumfuata msafiri anayepunguza.

 

(c) Idadi ya rakaa za maamuma kuwa kidogo zaidi ya rakaa za imamu. Hii haijuzu. Ni kama anayeswali Alfajiri nyuma ya anayeswali Adhuhuri, au Magharibi nyuma ya ‘Ishaa. Sababu ya kutojuzu ni kuwa ni lazima maamuma akhilafiane na imamu wake katika vitendo vya dhahiri; ima kwa kufarikiana naye ili yeye atoe tasliym, au amsubiri aje atoe tasliym pamoja naye, au asimame naye kuthibitisha umaamuma wake na idadi ya rakaa za Swalaah yake zizidi kimakusudi, na hili litaitengua Swalaah yake.

 

Lakini je, maamuma anaweza kungoja mpaka imamu akabakisha idadi ya rakaa zilizo sawa na Swalaah yake, kisha akajiunga naye na kutoa tasliym kwa pamoja? Suala hili ni la kutafitiwa na kupekuliwa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

4- Mwenye kuswali kamili kumfuata mwenye kupunguza:

 

Hii inajuzu. Mwenye kuswali kamili ni lazima amalizie rakaa zilizobakia baada ya imamu wake kutoa tasliym. Hakuna mvutano wowote kati ya Maulamaa katika hili.

Imehadithiwa toka kwa ‘Imraan bin Haswiyn (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Nilishiriki vita pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na nilikuwa pamoja naye katika ukombozi wa Makkah. Alikaa Makkah masiku 18 haswali isipokuwa rakaa mbili. Alikuwa akisema: “Enyi wenyeji wa mji! Swalini rakaa nne, kwani sisi ni wasafiri”. [Hadiyth Dhwaíyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1229)].

 

Pamoja na  udhwa’íyf wake lakini kiuhalisia inatumika, kwani mkazi ni lazima aswali nne, na haijuzu aache rakaa yoyote.

 

·       

Faida

 

Haishurutishwi kutia niya ya kupunguza kwa anayetaka kupunguza Swalaah. [Majmu’u Al-Fataawaa (24/21, 104/105)]

 

Ndivyo walivyosema Masalaf wote. Hakuna yeyote aliyenukulu toka kwa Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliwaamuru Maswahaba wake; si kwa niya ya kupunguza wala niya ya kukusanya, na wala Makhalifa wake hawakuwa wakimwamuru kufanya hivyo aliyekuwa akiwafuata. Hii ni pamoja na kwamba waamuriwa au wengi wao, hawajui alifanyalo imamu. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotoka kwa Hijjah yake, aliswali pamoja nao Adhuhuri mjini Madiynah rakaa nne, na akaswali nao Dhul Hulayfah rakaa mbili nyuma yake ukiwa umma wa watu usiohesabika. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Hajji]

 

Wote hao walitoka kuhiji pamoja naye, na wengi wao walikuwa hawajui Swalaah ya safari; ima kwa ugeni wao katika Uislamu, au kuwa hawakuwahi kusafiri hususan akina mama.

 

Linaloonyesha kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali kwa kupunguza na Maswahaba wake na wala hawajulishi kabla ya kuingia kwenye Swalaah kwamba yeye anapunguza, ni Hadiyth ya Dhul Yadayn isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa tasliym baada ya rakaa mbili katika Swalaah ya Adhuhuri au Alasiri kwa kusahau, naye Dhul Yadayn akamuuliza: “Je, umepunguza Swalaah au umesahau?” Akajibu: “Sikusahau wala haikupunguzwa”. Akasema: “Naam, umesahau”. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Sijdah ya kusahau]. Rasuli hakumwambia: “Lau kama ningelipunguza, ningekujulisheni ili mtie niya ya kupunguza”.

 

Ninasema: “Faida ya hili ni kuwa msafiri anaposwali nyuma ya imamu katika mji fulani na akamwona amepunguza Swalaah, basi atatoa tasliym pamoja naye, na wala haishurutishwi kuwa alinuwia kupunguza kabla ya Swalaah”.

 

5- Mwenye kupunguza kumfuata mwenye kuswali kamili:

 

Hii inajuzu, lakini maamuma atalazimika wakati huo aswali rakaa nne hata kama alimfuata imamu kwa kitambo kifupi. Na hii ni kwa dalili zifuatazo:

 

- Imepokelewa toka kwa Muusa bin Salamah akisema: “Tulikuwa pamoja na Ibn ‘Abbaas Makkah. Nikamwambia: Sisi tukiwa nanyi, tunaswali rakaa nne, na tunaporejea kwenye msafara wetu, tunaswali rakaa mbili”. Akasema: “Hiyo ni Sunna ya Abul Qaasim Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/216), Ibn Khuzaymah (952) na Al-Bayhaqiy (3/153). Angalia Al-Irwaa (3/21)].

 

- Imepokelewa kwamba Ibn ‘Umar alipokuwa akiswali na imamu, huswali rakaa nne, na anaposwali peke yake, huswali rakaa mbili. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim].

 

- Imepokelewa toka kwa Abu Mujlaz akisema: “Nilimwambia Ibn ‘Umar: Msafiri huzipata rakaa mbili za wenyeji. Je, zitamtosha rakaa mbili, au aswali pamoja nao? Alicheka akasema: Ataswali pamoja nao”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/157). Angalia Al-Irwaa (3/22)].

 

Haijuzu kumfuata anayeswali Swalaah ambayo vitendo vyake ni tofauti na Swalaah yake. Ni kama anayeswali Adhuhuri kumfuata anayeswali Swalaah ya maiti, au Swalaah ya Kupatwa Jua na kadhalika. Hili litapelekea kwenda kinyume na vitendo vya dhahiri vya imamu, na hii haifai.

 

 

Share