027-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaat Adh-dhuhaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

027-Swalaat Adh-dhuhaa

 

Alhidaaya.com

 

 

Wakati wa Dhuhaa kwa mujibu wa Mafuqahaa, ni baina ya kunyanyuka jua na kupinduka. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyn (2/23) chapa ya Fikr]

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazozungumzia fadhila za Swalaah hii. Hadiyth hizo ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Dharri (Radhwiya Allaahu Anhu) asemaye: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( يصبح على كل سلامى من أحدكم صدقة، فكل تسبيحة صدقة، وكل تحميدة صدقة، وكل تهليلة صدقة، وأمر بالمعروف صدقة، ونهي عن المنكر صدقة، ويجزئ من ذلك ركعتان يركعهما من الضحى ))

((Kila kiungo cha mmoja wenu kinakuwa ni swadaqah. Kila tasbiyha moja ni swadaqah, kila tahmiydah moja ni swadaqah, kila tahliylah moja ni swadaqah, kuamrisha mema ni swadaqah, na kukataza munkari ni swadaqah. Rakaa mbili za Dhuhaa anazoziswali, zinamtosheleza na hayo yote)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (720), Abu Daawuud (1285), na Ahmad (5/167)].

 

2- Al Buraydah (Radhwiya Allaahu Anhu) anasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( في الانسان ستون وثلاثمائة مفصل، عليه أن يتصدق عن كل مفصل منها صدقة ))

((Kila mwanadamu ana viungo 360, ni juu yake akifanyie swadaqah kila kiungo katika hivyo)). Wakasema: “Nani atayaweza hayo ee Rasuli wa Allaah?”. Akasema:

(( النخامة في المسجد يدفنها، أو الشيئ ينحيه عن الطريق، فإن لم يقدر فركعتا الضحى تجزئ عنه ))

((Alifukie kohozi lililoko ndani ya Msikiti, au aondoshe kitu njiani, na kama hawezi, basi rakaa mbili za Dhuhaa zitamtosheleza)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (2/524) na Ahmad (5/354)].

 

Hadiyth hizi mbili zinaonyesha juu ya fadhila kubwa ya Swalaah ya Dhuhaa, hadhi yake adhimu na uthibitisho wa uhalali wake, na kwamba rakaa zake mbili zinatosheleza swadaqah ya viungo 360. Jambo lenye mambo haya, linastahiki kuendelea na kudumu nalo mtu daima…”.  [Naylul Awtwaar (3/78) chapa ya Al-Hadiyth]

 

3- Imepokelewa toka kwa Zayd bin Arqam akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatokea watu wa Qubaa wakiwa wanaswali Dhuhaa akawaambia:

(( صلاة الأوابين حين ترمض الفصال))

(( Swalaah ya watiifu warejelefu ni pale jua linaposhitadi na kuwataabisha ngamia wachanga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (748) na Ahmad (4/366)].

 

4- Imepokelewa toka kwa Jubayr bin Nafiyr toka  kwa Abud Dardaai na Abu Dharr toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Anasema:

(( ابن آدم، اركع لي ركعات من أول النهار، أكفك آخره))

((Ee mwanadamu! Rukuu kwa ajili Yangu rakaa kadhaa mwanzoni mwa mchana, Nitakutosheleza mwishoni mwake )).  [Swahiyh Bituruqihi (kwa Sanad tofauti): Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (475). Ina Hadiyth mwenza ya Nu’aym bin Hammaar iliyoko kwa Abu Daawuud (1289). Angalia Al-Irwaa (465)].

 

5- Imepokelewa na ´’Abdullaah bin ‘Amri akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituma kikosi cha vita, wakapata ngawira na wakarejea haraka. Watu wakazungumza kuhusu kushinda kwao vita haraka, wingi wa ngawira walizozipata na kurejea kwao haraka. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

(( ألا أدلكم على أقرب منهم مغزى وأكثر غنيمة وأوشك رجعة؟ من توضأ ثم غدا إلى المسجد لسبحة الضحى فهو أقرب منهم مغزى وأكثر غنيمة وأوشك رجعة ))

(( Je, nikuonyesheni lililo karibu zaidi kuliko vita vyao, lililo jingi zaidi kuliko ngawira zao na lililo haraka zaidi kuliko walivyorejea? Mwenye kutawadha, kisha akaenda Msikitini kwa ajili ya Sunnah ya Dhuhaa, basi yuko karibu zaidi kuliko vita walivyoshinda, ana ngawira nyingi zaidi kuliko walizopata na urejeaji wa haraka zaidi kuliko wao)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/175). Angalia Swahiyhut Targhiyb (663-664)].

 

· Hukmu Ya Swalaat Adh-Dhuhaa

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya Swalaah ya Dhuhaa kwa kauli sita. [Zaadul Ma’ad (1/341-360), Badai’ul Fawaaid, na Fat-hul Baariy (3/66)] Zilizo karibu zaidi ni tatu:

 

Ya kwanza:

 

Ni Sunnah na inapendeza kuendelea kuiswali bila kuacha. Hii ni kauli ya Jamhuri kinyume na Hanbali. [’Umdatul Qaarii (7/240), Mawaahibul Jaliyl (2/67) Rawdhwat At Twaalibiyna (1/337) na Al-Mughniy (2/132)]

 

Dalili yao ni:

 

1- Ujumuishi wa Hadiyth zilizotangulia zinazozungumzia fadhila ya Swalaah ya Dhuhaa na hususan Hadiyth isemayo:

((Kila kiungo cha mmoja wenu kinakuwa ni swadaqah..)).

 

2- Hadiyth ya Abu Hurayrah isemayo: “Kipenzi changu ameniusia mambo matatu: Kufunga siku tatu kila mwezi, rakaa mbili za Dhuhaa, na kuswali Witr kabla sijalala”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1178) na Muslim (721)]. Abud Dardaai na Abu Dharri wana Hadiyth kama hii.

 

3- Hadiyth ya Ma’adha Al-‘Adawiyya aliyesema: “Nilimwambia ‘Aaishah: Je, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhuhaa?” Akasema: “Naam, nne na anaongeza idadi aitakayo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1178) na Muslim (721)].

 

Ash-Shawkaaniy amesema katika An Nayl (3/76): “Haifichiki kwamba Hadiyth zenye kuithibitisha Dhuhaa, zimefikia upeo wa baadhi yake kutoishilia kwenye kusuniwa tu”.

 

Al Haafidh amesema katika Al Fat-h (3/66): “Al-Haakim amekusanya Hadiyth zilizokuja kuhusiana na Swalaat adh-dhuhaa katika mlango mmoja, na idadi ya wapokezi wa Hadiyth walioithibitisha imefikia kiasi cha Maswahaba ishirini”.

 

4- Ama kudumu bila kuiacha ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( أحب العمل إلى الله تعالى ما دام عليه صاحبه وإن قل ))

(( Amali inayopendeza zaidi kwa Allaah ni ile ambayo mtendaji wake hudumu nayo hata kama ni ndogo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (43) na Muslim (782) na tamko ni lake].

 

Ya pili:

 

Imesuniwa kuiswali wakati fulani na kuiacha wakati mwingine bila kudumu. Ni madhehebu ya Hanbali. [Al-Furu’u cha Ibn Muflih (1/567)]

 

Na dalili yao ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Sa’iyd aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali Dhuhaa mpaka tunasema hatoiacha, na huiacha mpaka tunasema hatoiswali tena”. [Hadiyth Dhwaíyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (477) na Ahmad (3/21-36). Angalia Al-Irwaa (460)].

 

2- Katika Hadiyth ya Anas kuhusiana na kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali Dhuhaa katika nyumba ya ‘Utbaan bin Maalik, na Fulaan Ibn Al-Jaaroud akamwambia Anas: “Je, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhuhaa? ”Akasema: “Sikumwona akiswali isipokuwa siku hiyo”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (670).

 

3- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Sikumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali Sunnah ya Dhuhaa, na mimi ninaiswali [ingawa yeye anaacha amali ambayo yeye ni wajibu kwake aifanye kwa kuchelea watu kuifanya ikaja kufaradhishwa kwao]”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1177/1128) na Muslim (718)].

 

Ya tatu:

 

Haiswaliwi ila kwa sababu fulani

 

Ni kama kupitwa na Qiyaamul Layl na mfano wake. Na hili ndilo alilolikhitari Ibn Al-Qayyim baada ya kuzichambua kauli kuhusiana na suala. [Zaadul Ma’ad (1/341-360) na Badaai’ul Fawaaid]

 

Hoja ya wenye kusema hivi ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuiswali isipokuwa kwa sababu fulani. Wamekubaliana kwamba iliswaliwa wakati wa dhuhaa kutokana na sababu mbalimbali:

 

1- Hadiyth ya Ummu Haani isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia nyumbani kwake Siku ya Ukombozi wa Makkah, akaoga na akaswali rakaa nane [Sunnah ya Dhuhaa]. Sikuiona Swalaah yoyote nyepesi kuliko hiyo isipokuwa yeye hutimiza rukuu na sijdah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1176), Muslim (719) na Abu Daawuud (1290)].

 

Ilikuwa ni kwa sababu ya Ukombozi. Wamesema: “Na Sunnah ya Ukombozi, ni kuswali rakaa nane”. At-Twabariy amelinukulu kutokana na alivyofanya Khaalid bin Al-Waliyd alipoikomboa Al-Hiyrah.

 

2- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposwali nyumbani kwa Utbaan bin Maalik alipomwomba aswali hapo katika sehemu ambayo yeye huswalia. Ikawa imewafikiana na wakati wa Dhuhaa. Msimulizi amekifupisha kisa kwa kusema: “Aliswali Dhuhaa katika nyumba yake”. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake tumeielezea karibuni].

 

3- ‘Abdullaah bin Shuqayq alimuuliza ‘Aaishah: “Je, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhuhaa?” Akasema: “Hapana, isipokuwa anaporudi toka safarini”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (717). Zimepokelewa toka kwa ‘Aaishah riwaya tofauti. Hapa ‘Aaishah ameifungamanisha Swalaah ya Dhuhaa ya Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam na safari. Na katika Hadiyth ya Muslim, ‘Aaishah amekanusha kabisa kumwona Rasuli akiswali, na katika riwaya nyingine amethibitisha hilo bila mpaka. Kundi la Maulamaa akiwemo ‘Abdul Barri wanayatilia nguvu yaliyopo katika Swahiyh Mbili pamoja na yale ambayo Muslim amebaki nayo peke yake. Wengine wameunganisha kati ya riwaya zote hizi. Angalia Fat-hul Baariy (3/67)]

 

Hii ni kwa vile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikataza kuingia usiku nyumbani toka safarini. Akawa anaingia mwanzoni mwa mchana, anaanza kwenda Msikitini na kuswali wakati wa Dhuhaa.

 

Wamesema: “Ama Hadiyth zinazoraghibisha na kubembelezea, hazionyeshi kwamba Swalaah hii ni ya kila siku kwa kila mtu. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kalihusisha hilo kwa Abu Dharri na Abu Hurayrah basi, na wala hakuwausia Maswahaba wakubwa!!

 

Ibn Al-Qayyim amesema: “Kwa kuzitaamuli Hadiyth Marfu’u na athar za Maswahaba peke yake, hatuoni kingine zaidi ya kauli hii”.

 

Sheikh wa Uislamu anaona kwamba mtu ambaye ni ada yake kuswali usiku, haisuniwi kwake kuswali Dhuhaa. Ama yule ambaye si ada yake, basi imesuniwa kwake aswali Dhuhaa kila siku katika hali zote.  [Al-Ikhtiyaaraat (uk. 64) na Al-Furu’u (1/567)]

 

Ninasema: “Ni wazi kabisa kwamba kauli ya kwanza ndiyo sahihi zaidi kutokana na ujumuishi wa uraghibisho kwa Swalaah ya Dhuhaa, na kuwa kwake inamtosheleza mtu kwa swadaqah ya viungo vyake 360. Ama pingamizi ya baadhi ya Maswahaba kama vile Ibn Mas-’oud, Ibn ‘Umar na wengineo, pingamizi hii haidhuru kitu, kwani wengineo wamethibitisha ruksa na uhalali wa Swalaah hii. Kila mmoja wao amesimulia aliyoyaona, na aliyejua ni hujja kwa ambaye hakujua.

 

Aidha, yaliyoelezewa kuhusiana na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na baadhi ya Maswahaba wake kuiacha baadhi ya nyakati, hakukanushi uhalali wake, kama ambavyo kuendelea nayo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si sharti ya ruksa hii, bali ni ruksa ya kuraghibisha kuiswali Swalaah hii kwa mujibu ya yaliyozungumzwa kuhusiana na fadhila zake. Na kwa ajili hiyo, ‘Aaishah amesema: “Sikumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali Sunnah ya Dhuhaa, na mimi ninaiswali [ingawa yeye anaacha amali ambayo yeye ni wajibu kwake aifanye kwa kuchelea watu kuifanya ikaja kufaradhishwa kwao]. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake tumeielezea karibuni].

 

· Wakati Wa Swalaah Ya Dhuhaa

 

Wakati wake unaanza tokea baada ya jua kunyanyuka na kumalizika wakati uliokirihishwa hadi kabla kidogo ya kupinduka jua madhali haujaingia wakati uliokatazwa kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa.  [Mawaahibul Jaliyl (2/68), Kash-Shaaful Qinaa (1/442), Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/332) na Asnal Matwaalib (1/203)]

 

Ninasema: “Kwa maelezo haya, wakati wake huanza baada ya takriban robo saa tokea kuchomoza jua”.

 

Wakati wake bora zaidi ni kucheleweshwa mpaka pale joto linaposhitadi kutokana na Hadiyth ya Zayd bin Arqam kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

(( صلاة الأوابين حين ترمض الفصال))

((Swalaah ya watiifu warejelefu ni pale jua linaposhitadi na kuwataabisha ngamia wachanga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (748) na Ahmad (4/366)].

 

Maana yake ni pale mchanga unapokuwa moto na kuzichoma kwato za ngamia wadogo, na hii inakuwa muda mfupi kabla ya jua kupinduka.

 

· Idadi Ya Rakaa Zake

 

Hakuna makhitilafiano yoyote ya kuwa uchache wa Swalaah ya Dhuhaa ni rakaa mbili kati ya waliosema kuwa ni Sunnah kutokana na Hadiyth tuliyoielezea isemayo:  ((Rakaa mbili za Dhuhaa anazoziswali, zinamtosheleza na hayo yote)), na Hadiyth ya Abu Hurayrah isemayo: “Kipenzi changu ameniusia mambo matatu…na rakaa mbili za Dhuhaa”. [Al-Fataawaa Al-Hin-diyyah (1/112), Ad-Dusuwqiy (1/313), Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/332) na Al-Inswaaf (2/190)]

 

Hakuna makhitilafiano yoyote ya kuwa uchache wa Swalaah ya Dhuhaa ni rakaa mbili kati ya waliosema kuwa ni Sunnah. Kisha wakakhitalifiana  kuhusu wingi wa rakaa zake kwa kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Wingi wake ni rakaa nane. Ni madhehebu ya Maalik, Shaafi’i na Hanbali. [Ad-Dusuwqiy (1/313), Al-Majmu’u (4/36), Ar-Rawdhwah (1/332), Al-Inswaaf (2/190) na Al-Mughniy (2/131)]

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Ummi Haani kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia nyumbani kwake Siku ya Ufunguzi wa Makkah, akaswali rakaa nane. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa karibuni].

 

Ya pili:

 

Wingi wake ni rakaa kumi na mbili. Ni madhehebu ya Hanafi kutokana na Hadiyth Marfu’u ya Anas: “Mwenye kuswali Dhuhaa rakaa kumi na mbili, Allaah Atamjengea kasri peponi”. [Hadiyth hii ni Dhwa’iyf].

 

Ya tatu:

 

Hakuna mpaka wa wingi wake. Hili limesimuliwa na baadhi ya Masalaf, nalo ndilo lenye uzito zaidi kwa sababu mbili:

 

1- Hadiyth ya Muaadhat isemayo: Nilimwambia ‘Aaishah: “ Je, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhuhaa? Akasema: “Naam, rakaa nne, na huzidisha idadi atakayo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (719)].

 

2- Kuishilia kwenye rakaa nane tu katika Hadiyth ya Ummu Haani kunajibiwa kwa mambo mawili:

 

La kwanza ni kwamba kuna Maulamaa waliosema kwamba hiyo ilikuwa ni Swalaah ya Ukombozi wa Makkah na si Swalaah ya Dhuhaa. La pili ni kuwa kuishilia kwenye rakaa nane, hakumaanishi kwamba hakuna ruksa ya kuongeza zaidi ya hapo, kwa kuwa suala hili linamhusu kila mtu binafsi. [Ash-Sharhul Mumti’i (4/120)]

 

 

Share