032-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Kupatwa Jua (Kusuwf)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

032-Swalaah Ya Kupatwa Jua (Kusuwf)

 

Alhidaaya.com

 

 

· Taarifu Yake

 

“Kusuwf” ni kupotea mwanga wa jua au mwezi au sehemu ya mwanga na kubadilika kuwa weusi, na “Khusuwf” ni kisawe chake. Wataalamu wengine wanasema kwamba “Kusuwf” ni kupatwa jua na “Khusuwf” ni kupatwa mwezi, na tafsiri hii ndiyo mashuhuri zaidi katika lugha. [Lisaan Al-‘Arab, Kash-Shaaf Al-Qinaa (2/60) na Asnaa Al-Matwaalib (1/385)]

Swalaah ya “Kusuwf” ni Swalaah inayoswaliwa kwa mtindo maalumu wakati jua au mwezi ukipatwa wote au sehemu. [Mawaahibul Jaliyl (2/199), Nihaayatul Muhtaaj (2/394) na Kash-Shaaful Qinaa (2/60)]

 

· Hukmu Ya Swalaah Ya Kupatwa Jua

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba Swalaah ya Kupatwa Jua ni Sunnah iliyokokotezwa. Lakini Abu ‘Awwaanah ameeleza kwamba ni wajibu kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa toka kwa Abu Haniyfah wakati ambapo Maalik ameichukulia kama ni Swalaah ya Ijumaa. Kauli hii ya kusema ni wajibu iliyopewa uzito na Ash-Shawkaaniy, Swiddiyq Khaan na kisha Al-Albaaniy, ina mwelekeo wa nguvu kutokana na kuthibiti maagizo ya kuiswali. [Fat-hul Baariy (2/612), As Saylul Jarraar (1/323), Ar-Rawdhwat An Nadiyyah (uk 156) na Tamaam Al-Minnah (uk.261)]

 

Ama hukmu ya Swalaah ya Kupatwa Mwezi, Maulamaa wamekhitalifiana juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni Sunnah iliyokokotezwa na huswaliwa jamaa kama Swalaah ya Kupatwa Jua. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Daawuud, Ibn Hazm, ‘Atwaa, Al-Hasan, An-Nakh’iy na Is-Haaq. Kauli hii imehadithiwa toka kwa Ibn ‘Abbaas. [Al-Ummu (1/214), Al-Mughniy (2/420), Al-Inswaaf (2/442), Bidaayatul Mujtahid (1/160) na Al-Muhalla (5/95)]

 

Na hoja yao ni haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Al-Mughiyrah ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Hakika jua na mwezi ni alama mbili kati ya Alama za Allaah. Havipatwi kwa kufa mtu wala kwa kuzaliwa, na mnapoona vimepatwa, basi mwombeni Allaah na mswali mpaka mwanga urudi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1060) na Muslim (904)].

Kuna Hadiyth kama hii ya ‘Aaishah, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abaas na Abu Bakrah.

 

2- Yaliyosimuliwa ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ya Kupatwa Mwezi.  [Angalia (Fat-h) (3/638)]

 

3- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba aliswali na wakazi wa Basrah Swalaah ya Kupatwa Mwezi rakaa mbili kisha akawaambia: “Nimeswali hivi kwa kuwa nimemwona Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: “Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/342). Pia Ash-Shaafi’iy kaifanyia “ikhraaj” mfano wake katika musnadi wake (484), na Al-Bayhaqiy kanukuu toka kwake (3/342) lakini Sanad yake haifai].

 

Ya pili:

 

Haiswaliwi kwa jamaa, nayo ni Sunnah kama Sunnah zinginezo bila kuzidisha katika rukuu. Ni kauli ya Abu Haniyfah na Maalik. [Ibn ‘Aabidiyn (2/183), Al-Badaai-’i (1/282), Mawaahibul Jaliyl (2/201), Bidaayatul Mujtahid (1/312), na Ad-Dusuwqiy (1/402)]

 

Wamesema: “Ni kutokana na uzito wakati wa usiku kinyume na mchana, na kutotaarifiwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliiswali kwa Jamaa pamoja na kwamba kupatwa mwezi kulikuwa zaidi kuliko kupatwa jua!!

 

Ninasema: “Kauli ya kwanza ina nguvu zaidi kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameagiza kuziswali Swalaah hizo mbili bila ya kufarakanisha”.

 

· Wakati Wake

 

Ni kuanzia pale jua linapoanza kupatwa mpaka linapoachiliwa kutokana na kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mnapoona vimepatwa, basi mwombeni Allaah na swalini mpaka mwanga urudi)). [Hadiyth Swahiyh:  Tushaitaja].

 

Kuachiliwa kumefanywa kuwa ndiyo lengo la Swalaah kwa ajili ya kumtaradhi Allaah Airejeshe neema ya mwanga. Na linapoachiliwa, basi lengo la Swalaah linakuwa lishapatikana. [Vitabu rejea vilivyotangulia]

 

· Kupita Kwake

 

Swalaah ya Kupatwa Jua inapita kwa moja ya mawili:

 

1- Kurejea mwanga kamili. Ikiwa mwanga utarejea kidogo, basi inajuzu kuswali kwa sehemu iliyobakia ya giza kana kwamba hiyo ndiyo bado inayopatwa.

 

2- Ni kuchwa jua likiwa bado limepatwa.

 

Na Swalaah ya Kupatwa Mwezi hupita kwa moja ya mawili:

 

1- Kurejea nuru kamili.

2- Kuchomoza jua au kutoweka mwezi ukiwa bado umepatwa. Na ikiwa mawingu yatazuia na mtu akashakia kama umeachiwa au la, basi ataswali kwa kuwa asili ni kubakia kusuwf. [Al-Mughniy (2/427), Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/87) na Al-Mawaahib (2/203)]

 

· Faida

 

Swalaah ya Kupatwa Jua huswaliwa wakati wowote hata katika nyakati zilizopigwa marufuku kuswali. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy.

 

· Yaliyosuniwa Kwa Mwenye Kushuhudia Kusuwf

 

1- Akithirishe dhikri, kuomba maghfirah, kupiga takbiyr, kutoa swadaqah na amali nyingine njema.

 

Aaishah anasema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Mtakapoona hilo, basi mwombeni Allaah, pigeni takbiyr, swalini na toeni swadaqah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1044) na Muslim ( 901)].

 

Na Asmaa anasema: “Hakika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamuru nimwache huru mtumwa jua lilipopatwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1056) na Muslim (903)].

 

2- Aende kuswali kwa Jamaa Msikitini

 

Hadiyth ya ‘Aaishah inaeleza: “Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda asubuhi kipando (mnyama), jua likapatwa, akarejea dhuhaa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapita baina ya vyumba, kisha akasimama na kuswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1056) na Muslim ( 903)].

 

‘Aaishah anasema tena kwenye tamshi lililopokelewa na Muslim: “Nikatoka na wanawake katikati ya vyumba. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja akiwa ameshuka toka juu ya kipando chake mpaka akafika sehemu yake aliyokuwa anaswalia”.

 

Al-Haafidh anasema kwenye Al Fat-h (3/633): “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ndani ya kipando hicho kutokana na kifo cha mwanawe Ibraahiym. Aliporejea, alikwenda Msikitini na hakuswali nje uwanjani. Na Sunnah katika Swalaah ya Kupatwa Jua ni kuswaliwa Msikitini, na lau si hivyo, kuswalia kwake jangwani kungelikuwa ni bora zaidi kwa kuwa ni wepesi kuona jua likiachiliwa. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

3- Wanawake watoke kwenda kuswali

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Asmaa binti Abiy Bakri aliyesema: “Nilimwendea ‘Aaishah mke wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jua lilipopatwa. Nikawakuta watu wamesimama wanaswali, naye pia kasimama anaswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1053) na Muslim ( 905)].

 

Tumeshalieleza tamko la ‘Aaishah aliposema: “Nikatoka pamoja na wanawake katikati ya vyumba Msikitini.”

Mwanamke mwenye kuchelea fitna husameheka kwenda Msikitini, na badala yake ataswalia nyumbani peke yake.

 

4- Ainadie Swalaah kwa kusema “As-Swalaatu Jaami’ah” bila adhana wala iqaamah

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema:”Jua lilipopatwa wakati wa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) palinadiwa: "As-Swalaatu Jaami’ah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1045)].

 

Swalaah hii haina adhana wala iqaamah kwa makubaliano ya Maulamaa wote.

 

5- Khutbah baada ya Swalaah

 

Katika Swalaah hii, imesuniwa kutolewa khutbah kama khutbah ya Swalaah ya ‘Iyd kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema kwamba baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumaliza Swalaah, alisimama na kuwakhutubia watu. Alimhimidi Allaah na kumsifu, kisha akasema: ((Hakika jua na mwezi ni alama mbili kati ya Alama za Allaah ‘Azza wa Jalla. Havipatwi kwa kufa mtu wala kwa kuzaliwa, na mnapoona vimepatwa, basi mwombeni Allaah, tamkeni takbiyr, swalini na toeni swadaqah)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Is-Haaq na Maulamaa wengi wa Hadiyth. [Al-Majmu’u (5/52), Asnaa Al-Matwaalib (1/286), Fat-hul Baariy (2/620) na Bidaayatul Mujtahid (1/311)]

 

Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad wamesema kwamba Swalaah ya Kusuwf haina khutbah!!  [Al-Badaai-’i (1/282), Mawaahibul Jaliyl (2/202), Al-Mughniy (2/425) na rejea zilizotangulia]

Wengine wamesema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukusudia khasa khutbah kwa vipengele vyake katika Swalaah hiyo, bali alikuwa anataka kuwabainishia watu jibu kwa wale wenye kuitakidi kwamba kupatwa jua kunatokana na kifo cha baadhi ya watu.

 

Haya yanajibiwa na yaliyomo kwenye Hadiyth Swahiyh zinazoelezea kwa uwazi kuhusu khutbah, masharti yake, himdi, kumsifu Allaah, mawaidha na mengineyo yanayobainishwa humo. Khutbah haihusiani na kuwajulisha tu watu sababu ya kusuwf, bali asili ya mambo ni kumfuata Nabiy, na mambo yanayomuhusu yeye pekee pasina wengine hayathibiti ila kwa dalili. [Fat-hul Baariy cha Ibn Hajar (2/620) chapa ya As-Salafiyyah]

 

· Namna Ya Kuswali Kusuwf

 

Swalaah ya Kusuwf ni rakaa mbili tu, hakuna mabishano kati ya Maulamaa kuhusu hili. Walilobishania ni utendaji wake kwa kauli tofauti. Zilizo mashuhuri zaidi ni mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni rakaa mbili. Kila rakaa ina visimamo viwili, visomo viwili, rukuu mbili na sijdah mbili. Wanaosema haya ni Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Ad-Dusuwqiy (1/405), Al-Ummu (1/215), Kash-Shaaful Qinaa (2/62) na Al-Mughniy (2/422)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Jua lilipatwa wakati wa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nabiy akaswali pamoja na watu. Akasimama kisimamo kirefu cha kiasi cha kusoma Suwrat Al-Baqarah. Kisha alirukuu rukuu ndefu, halafu akasimama kisimamo kirefu chini kidogo ya kisimamo cha kwanza. Kisha alirukuu rukuu ndefu chini kidogo ya rukuu ya kwanza”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1046) na Muslim (901)].

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali siku jua lilipopatwa. Alisimama akapiga takbiyr, akasoma kisomo kirefu, kisha alirukuu rukuu ndefu. Halafu alinyanyua kichwa chake akasema: Sami’a Allaahu liman hamidah, na akasimama tena kama alivyokuwa. Kisha alisoma kisomo kirefu chini ya kisomo cha mwanzo, halafu alirukuu rukuu ndefu chini ya rukuu ya kwanza, kisha akasujudu sijdah ndefu, halafu akafanya katika rakaa ya mwisho mfano wa hivyo, kisha akatoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1047) na Muslim (901)].

 

3- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku ya joto kali mno. Akawaswalisha Maswahaba wake na akakirefusha kisomo mpaka wakaanza kuanguka. Kisha alirukuu akarefusha, halafu akanyanyuka akarefusha, kisha akarukuu na kurefusha, halafu akasujudu sijdah mbili, kisha akasimama na kufanya mfano wa hayo. Zilikuwa ni rakaa nne na sijdah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (904), Abu Daawuud (1179), An-Nasaaiy (1/217) na Ahmad (3/374)].

 

 Ya pili:

 

Ni rakaa mbili. Kila rakaa ina kisimamo kimoja, rukuu moja na sijdah mbili kama Sunnah nyinginezo. Anayesema hivi ni Abu Haniyfah. Ibn Hazm amekhiyarisha kati ya namna zote. [Al-Badaai-’i (1/281), Tabyiynul Haqaaiq (1/228), Al-Muhalla (5/95) na Bidaayatul Mujtahid (1/307)]

 

Hoja za Abu Haniyfah na wenye kukubaliana naye ni:

 

Hadiyth ya Abu Bakrah aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akatoka akiliburura joho lake hadi akaishilia Msikitini. Watu wakamwendea haraka, akaswali nao rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1063), An-Nasaaiy (3/146) na At-Twayaalsaa (716)].

 

Wamesema: ”Swalaah yoyote, ni Swalaah iliyozoeleka”. Na katika riwaya ya An-Nasaaiy: “Akaswali rakaa mbili kama wanavyoswali”.

 

2- Hadiyth ya An Nu’umaan bin Bashiyr aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaanza kuswali rakaa mbili mbili huku akiomba mpaka likaachiliwa”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1193), Ahmad (4/267) na At-Twahaawiy. Angalia Al-Irwaa (3/131)].

 

Ibn Hazm kasema: “Tamshi hili (yaani kukariri rakaa mbili) linawajibisha tuliyoyaeleza”.

 

· Aina Nyinginezo Za Namna Ya Kuiswali

 

Imehadithiwa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliiswali kwa miundo mingineyo. Kati yake ni:

 

3- Kila rakaa rukuu tatu [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (901), Abu Daawuud (1177) na An-Nasaaiy (3/129) toka kwa ‘Aaishah].

 

4- Kila rakaa rukuu nne [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (908) na Abu Daawuud (1183)].

Ibn Al-Qayyim anasema: “Maimamu wakubwa hawalioni hilo kuwa ni sahihi, bali wanaliona ni kosa kama Al-Imaam Ahmad, Al-Bukhaariy na Ash-Shaafi’iy”.  [Zaadul Ma’ad (1/453) chapa ya Ar-Risaalah]

 

Ninasema: “Utendaji sahihi zaidi wa Swalaah hii ni kufanya rukuu mbili katika kila rakaa kama walivyosema Jamhuri kutokana na uwazi wa Hadiyth Swahiyh husika. Ama dalili za Abu Haniyfah na waliokubaliana naye, dalili hizi zimetaja rakaa mbili bila uainisho wakati Hadiyth za kundi la kwanza zimeainisha”.

 

Ama Hadiyth ya An-Nu’umaan bin Bashiyr kuhusu Swalaah ya rakaa mbili mbili, Al-Haafidh anasema katika mjalada wa tatu wa kitabu cha Al-Fat-h kwamba ikiwa Hadiyth hii imehifadhiwa, maana ya neno lake “rakaa mbili mbili” inaweza kuchukuliwa kama rukuu mbili. Ninasema: “Tushajua kwamba Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, hivyo hatuhitajii taawili yoyote”.

 

Ama riwaya zinazozungumzia kuhusu ziada ya rukuu mbili katika rakaa moja, Sheikh wa Uislamu (18/17-18) amesema kwamba hili limepewa udhaifu na Maulamaa weledi wanaosema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuswali Kusuwf isipokuwa mara moja tu siku alipofariki mwanaye Ibraahiym, na mwanaye huyu hakufa mara mbili, na wala hakuwa na Ibraahiym wawili. Isitoshe, imepokelewa kwa njia ya Tawaatur kwamba Nabiy aliswali Kusuwf siku hiyo kwa rukuu mbili katika kila rakaa.

 

Al-‘Allaamah Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (3/132) amesema: “Kauli ya mwisho kuhusiana na Swalaah ya Kusuwf ni kwamba lililo sahihi thabiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa Swalaah hii ni rakaa mbili, na kila rakaa ina rukuu mbili. Na haya yamethibiti toka kwa Maswahaba wengi yakielezewa kwenye vitabu vinavyoaminika, njia na riwaya mbalimbali.  Ama kinyume na hayo, basi yatakuwa ima Dhwa’iyf au Shaadh, na hayafai kwa hoja”.

 

· Picha Ya Swalaah Ya Kusuwf Kwa Muhtasari

 

1- Apige takbiyr, asome du’aa ya ufunguzi, asome isti’aadhah, asome Al-Faatihahh, na kisha asome kiasi cha Suwrat Al-Baqarah.

 

2- Arukuu rukuu ndefu.

 

3- Anyanyuke toka kwenye rukuu na aseme: “Sami’a Allaahu liman hamidahu, Rabbanaa walakal Hamdu”.

 

4- Asisujudu, bali asome Al-Faatihah na Suwrah fupi kidogo kuliko ile ya kwanza.

 

5- Arukuu tena rukuu ndefu na apunguze kidogo urefu kulinganisha na ile ya kwanza.

 

6- Anyanyuke toka kwenye rukuu na aseme: “Sami’a Allaahu liman hamidahu, Rabbanaa walakal Hamdu”.

 

7- Asujudu, kisha akae, halafu asujudu tena.

 

8- Anyanyuke kwenda rakaa ya pili, kisha afanye kama alivyofanya katika rakaa ya kwanza.

 

· Je, Husomwa Hwa Sauti Au Kimya Kimya?

 

Ahmad, Is-Haaq na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah wanasema kwamba ni Sunnah kusoma kwa sauti kinyume na Jamhuri. [Rejea zilizotangulia kuhusiana na namna ya kuswali]

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma kwa sauti katika Swalaah ya Khusuwf. Anapomaliza kusoma, hupiga takbiyr akarukuu, na anaponyanyuka toka kwenye rukuu husema: “Sami’a Allaahu liman hamidahu, Rabbanaa walakal Hamdu”. Kisha hufanya tena kisomo katika Swalaah ya Kusuwf rukuu nne katika rakaa mbili na sijdah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1065)].

 

2- Ni Naafilah iliyoruhusiwa kuswaliwa kwa jamaa. Hivyo basi, sehemu ya Sunnah yake ni kusomwa kwa sauti kama ilivyo kwa Swalaah za ‘Iyd, Tarawehe na Kuomba Mvua.

 

Jamhuri wamesema: “Husomwa kwa sauti katika Swalaah ya Kupatwa Mwezi tu, ama Kupatwa Jua haisomwi kwa sauti”. Hoja yao ni:

 

1- Yaliyomo kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia isemayo: “Akasimama kisimamo kirefu cha kiasi cha kusoma Suwrat Al-Baqarah”. Lakini hili haliwajibishi kuwa hakusoma kwa sauti bali inawezekana kuwa alisikia kutoka kwake Suwrah kadhaa alizozikadiria urefu wake na Al-Baqarah, au  alikuwepo sehemu ambayo sauti haikuwa ikimfikia.

 

2- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Nilikisia kisomo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).“ [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1187) na Al-Bayhaqiy (3/338)].

 

Wamesema: “Lau angelisoma kwa sauti, pasingehitajika dhana au makisio”. Nao wamejibiwa kwamba kauli hiyo haijathibiti kwa ‘Aaishah, kisha inapingana na kauli yake sahihi inayothibitisha Nabiy kusoma kwa sauti.

 

3- Hadiyth ya Samurah bin Jun-dub akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ya Kupatwa Jua, nami sikuisikia sauti yake”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (562), Abu Daawuud (1184), An-Nasaaiy (5/19) na Ibn Maajah (1264)]

 

Hili linajibiwa kwa Hadiyth iliyotangulia ya Ibn ‘Abbaas. Hadiyth Swahiyh haiwezi kurejeshwa kwa ajili ya Hadiyth hii. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Je, Mbali Na Swalaah Ya Kusuwf, Panaweza Kuswaliwa Pakitokea Matukio Ya Kuonyesha Nguvu Za Allaah Kama Matetemeko Na Mengineyo?

 

Maulamaa wana kauli nne kuhusiana na suala hili:

 

Ya kwanza:

 

Imesuniwa kuswali kwa kila janga au tukio la kuogofya kama tetemeko, upepo mkali, radi na mfano wa hayo. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Ibn Hazm na riwaya toka kwa Ahmad.

 

Ya pili:

 

Haiswaliwi Swalaah yoyote kutokana na matukio isipokuwa Kupatwa Jua na Mwezi tu. Hii ni kauli ya Maalik.

 

Ya tatu: Haiswaliwi Swalaah yoyote kutokana na matukio isipokuwa Kupatwa Jua na Mwezi na tetemeko la kudumu. Ni kauli ya Hanbali.

 

Ya nne: Haiswaliwi kwa jamaa isipokuwa Swalaah ya Kupatwa Jua na Mwezi, na kama kuna tukio jingine, basi mtu akae kwake nyumbani aswali na aombe. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy.

 

Ninasema: “Huenda kauli hii ndio iliyo karibu zaidi na usahihi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

 

Share