Kurudi Kulala Kabla Ya Alfajiri Baada Ya Tahajjud Inafaa?

Kurudi Kulala Kabla Ya Alfajiri Baada Ya Tahajjud Inafaa?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

A/alleykum.Napenda kufahamishwa ya kuwa baada ya kuswali swala za tahajud mfano umeswali na ukamaliza saa tisa na nusu yafaa kurudi kulala kisha baadae

kuamka na kuswali  swalat fajr saa kumi na moja?Au hairuhusiwi kulala tena mpka alfajr na zipi faida zake usipolala. Wassallam alleykum.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Kwanza tunapenda kukutanabahisha kosa la kufupisha Thanaa, Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na Maamkizi ya Kiislamu. Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate faida na mafunzo sahihi:

 

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Katika Maandishi

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”

 

Ama kuhusu swali lako ni kwamba, hakuna dhambi kurudi kulala baada ya Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha kuswali usiku), kwa sababu hukmu ya ‘ibaadah zote za Sunnah, huwa mtu anapata thawabu katika kuzitenda, na asipozitenda huwa hapati dhambi.

 

Hayo ni juu ya kuwa ziko baadhi yake ambazo zimesisitizwa kama mfano zile Swalaah za Rawaatib na pia mfano wa Swalaah ya Witr. Lakini  usipozitenda hutopata dhambi, na uikizitekeleza, utajichumia thawabu zake.

 

Na hivyo basi ukiweza kubakia mpaka Alfajiri kutekeleza ‘ibaadah khasa kuomba maghfirah wakati huo, kuna fadhila zake kuwa wamesifiwa wanaoomba maghfirah kabla ya Alfajiri kama Anvyosema Allaah ('Azza wa Jalla):

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾

Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. 

 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾

Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.

 

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾

Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. 

 

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾

Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾

Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]

 

Hata hivyo una khiari ya kubakia mpaka Alfajiri au kurudi kulala. Ila tahadhari mtu asikeshe usiku kwa 'ibaadah kisha akarudi kulala na kushindwa kuswali Swalaah ya Alfajiri.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share