039-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Jamaa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
039-Swalaah Ya Jamaa
- Taarifu Yake
Maana ya Swalaah Ya Jamaa ni kuiswali Swalaah pamoja na watu. [Jawaahir Al-Ikliyl (1/76)]
- Fadhla Yake, Umuhimu Wake Na Faida Zake
(a) Swalaah ya Jamaa ina fadhla kubwa kabisa, na kwa ajili hiyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameihimizia na kubainisha fadhla zake katika Hadiyth mbalimbali. Kati ya hizo ni:
1- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Swalaah ya Jamaa inaizidi Swalaah ya mtu peke yake kwa daraja ishirini na saba)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (645) na Muslim (650)].
2- Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Kuswali kwa Jamaa ni sawa na kuswali Swalaah ishirini na tano. Na anapoiswali kwenye ardhi mahame isokaliwa, akatimiza rukuu yake na sijdah yake, basi zinafikia Swalaah hamsini)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (560), Ibn Maajah (788) na Al-Haakim (1/208)].
3- Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kutawadha kwa ajili ya Swalaah na akautimiliza wudhuu, kisha akatembea kwenda kwenye Swalaah ya Faradhi, akaiswali pamoja na watu au pamoja na Jamaa au Msikitini, basi Allaah Humghufiria madhambi yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (232), An-Nasaaiy (2/111) na Ahmad (1/67)].
4- Na katika Hadiyth Marfu’u ya Abu Hurayrah:
((Na hiyo ni kuwa yeye akitawadha vizuri kama inavyotakiwa, kisha akatoka kwenda Msikitini na hakuna kimtoacho isipokuwa Swalaah tu, basi hatokanyaga hatua isipokuwa hunyanyuliwa kwayo daraja moja na hupomoshewa kwayo kosa moja. Na anaposwali, Malaika huendelea kumwombea rahma madhali ataendelea kubakia sehemu aliyoswalia (wakisema): “Ee Mola, Mpe rahma na baraka. Ee Mola, Mrehemu. Na mmoja wenu haachi kuwa ndani ya Swalaah madhali yu katika kuisubiri Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (647) na Muslim (649)].
5- Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Lau watu wangelijua yaliyomo ndani ya adhana na safu ya kwanza, kisha wasipate njia ya kulipata hilo ila kwa kura, basi wangelipiga kura. Na lau wangelijua yaliyomo ndani ya kuwahi mapema, basi wangelishindana. Na lau wangelijua yaliyomo ndani ya Swalaah ya ‘Ishaa na Alfajiri, basi wangeziendea japo kwa kutambaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (615) na Muslim (437)].
6- Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kuswali ‘Ishaa katika Jamaa, basi ni kama aliyesimama nusu ya usiku, na mwenye kuswali Alfajiri katika Jamaa basi ni kama aliyeswali usiku wote)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (656), Abu Daawuud (555), At-Tirmidhiy (221) na Ahmad (1/58)].
(b) Swalaah ya Jamaa ndiyo maana ya dini na nembo ya Uislamu kiasi ambacho ikiwa watu wa mjini wataiacha, basi watapigwa vita, na watu wa vitongojini watalazimishwa. [Al-Mughniy (2/176) na Al-Majmu’u (4/193)]
Swalaah Ya Jamaa Katika (Swalaah za) Faradhi
- Hukmu Ya Swalaah Ya Jamaa Kwa Wanaume
Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya Swalaah ya Jamaa kwa wanaume kwa kauli nyingi ambazo tunaweza kuzifupisha katika kauli mbili zifuatazo:
Ya kwanza:
Swalaah ya Jamaa ni faradhi kwa kila mtu binafsi isipokuwa kwa udhuru. Kauli hii imesimuliwa toka kwa Ibn Mas-’oud na Abu Muusa. Pia kaisema ‘Atwaa, Al-Awzaa’iy na Abu Thawr. Ni madhehebu ya Ibn Hazm na chaguo la Sheikh wa Uislamu ingawa wamekhitalifiana kati yao kama je Jamaa ni sharti ya kuswihi Swalaah au si sharti? [Al-Mughniy (2/176), Kash-shaaful Qina’a (1/454), Al-Badaai-’i (1/155), Al-Muhalla (4/188), na Majmu’u Al-Fataawaa (23/239)]
Dalili zao ni hizi:
1- Kauli Yake Ta’alaa:
((وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا فَلْيَكُونُوا مِن وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا))
((Na utapokuwa upo kati yao, ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Watakaposujudu basi wawe nyuma yenu (kuwalinda). Na lije kundi jingine ambalo halikuswali, liswali pamoja nawe, nao washike hadhari na silaha zao. Wale waliokufuru wanatamani kama mtaghafilika na silaha zenu na vifaa vyenu wakuvamieni mvamio mmoja. Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka (chini) silaha zenu. Na mshike hadhari zenu. Hakika Allaah Amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha)). [An Nisaa (4:102)]
Wanasema kwamba Allaah Ameamuru kuswaliwe Jamaa katika hali ya vita na khofu, hivyo katika hali ya usalama inakuwa na uzito na ulazima zaidi. Aidha, vitendo vingi vya Swalaah vimesamehewa katika Swalaah ya vita ili Jamaa ipatikane, na kama si kuwa kwake wajibu, basi visingesamehewa.
2- Kauli Yake Ta’alaa:
((وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ))
((Na simamisheni Swalaah na toeni Zakaat na rukuuni pamoja na wanaorukuu (katika utiifu))). [Al-Baqarah (2:43)]
Na hili linakuwa katika hali ya ushirika na wengine katika rukuu, na hivyo limekuwa agizo la kuswali Swalaah kwa Jamaa, nalo ni agizo wazi la wajibu.
3- Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake! Hakika mimi nilikusudia niamuru zikusanywe kuni ziwashwe moto, halafu niamuru Swalaah iadhiniwe, kisha nimwamuru mtu awaswalishe watu name nitoke niende kwa watu nikawachomee nyumba zao. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake! Lau kama mmoja wao anajua kwamba atapata kinofu kinono, au vijishale viwili vizuri vya kulengea shabaha, basi hakika angehudhuria ‘Ishaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (644) na Muslim (651)].
Wanasema kwamba Hadiyth yaonyesha kwamba Jamaa ni Fardhi ‘Ayni ( ya mtu mwenyewe binafsi), kwa kuwa lau kama ingekuwa ni Sunnah, basi anayeiacha asingetishiwa kuchomewa nyumba, na lau kama ingelikuwa ni Fardhi Kifaaya (ya kutoshelezana), basi ingetosha Rasuli kuiswali na watu alionao.
Kutoa dalili kwa Hadiyth hii kwamba Jamaa ni wajibu kwa kila mtu binafsi kumejibiwa kwa njia kadhaa. Kati yake ni kuwa:
- Wakusudiwa hapa ni wanafiki na si Waumini.
- Rasuli alikusudia lakini hakufanya, na kama ingelikuwa ni wajibu basi asingewaacha.
- Makusudio ni Swalaah ya Ijumaa kama ilivyo kwenye riwaya nyingine na kadhalika.
Wenye kusema ni wajibu wamezijibu njia hizi zote kwa majibu marefu ambayo hatuwezi kuyaeleza hapa. Unaweza kuyaangalia kwenye rejea husika. [Angalia Fat-hul Baariy (2/148-151), Ihkaamul Ahkaam cha Ibn Daqiyq Al-‘Iyd (1/166) na Al-Muhalla (4/191)]
4- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Mtu mmoja kipofu alimjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi sina mtu wa kuniongoza kunipeleka Msikitini. Akamtaka idhini Rasuli amruhusu aswalie nyumbani naye akamruhusu. Alipogeuka kuondoka alimwita na kumuuliza: Je unaisikia adhana? Akasema ndio. Akamwambia: Basi ijibu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (653), An-Nasaaiy (2/109) na wengineo]
5- Hadiyth ya Maalik bin Al-Huwayrith aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituambia nikiwa nimemjia na kundi la watu wangu:
((Wakati wa Swalaah ukiingia, basi mmoja wenu awaadhinie, na mkubwa wenu awaswalishe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (631) na Muslim (674)]
6- Hadiyth ya Abud Dardaai ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Hakuna watu watatu katika kijiji au jangwa ambao hawasimamishi Swalaah isipokuwa Shaytwaan huwatawala. Basi shikamana na Jamaa, kwani mbwa mwitu humla kondoo wa mbali)). [Tumeitaja katika mlango wa hukmu ya adhana]
7- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kusikia adhana kisha asiijibu, basi huyo hana Swalaah isipokuwa kwa udhuru)). [Imetiwa ila kuwa Mawquwf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (551), Ibn Maajah (794), Al-Haakim (1/245) na Al-Bayhaqiy (3/57, 174). Yeye katilia nguvu kuwa ni Mawquwf, na hili ndilo Swahiyh. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi]
La sahihi ni kuwa Hadiyth hii ni Mawquwf.
8- Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Mas-’oud akisema: “ Hakika hakukuwa na yeyote kati yetu anayebaki nyumbani asiende kuswali isipokuwa mnafiki ambaye unafiki wake ushajulikana au mtu mgonjwa. Ikiwa mtu mgonjwa, hutembea akishikiliwa na watu wawili mpaka akahudhuria Swalaah”. Anasema: “Hakika Rasuli wa Allaah ametufundisha Sunnah za uongofu, na kati ya Sunnah za uongofu ni kuswali kwenye Msikiti unaoadhiniwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (654), Abu Daawuud (550), An Nasaaiy (2/108) na Ibn Maajah (777) kwa konteksi ndefu zaidi]
Hili limejibiwa: Kwamba hii ni kauli ya Swahaba na haina zaidi ya kuelezea udumifu katika Swalaah ya Jamaa na kutoiacha. Na kauli kama hii haitolewi hoja ya ulazima wa jambo. Isitoshe, kuna dalili katika Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kuwa wanaohusishwa na makamio ya kuchomewa nyumba ni wanafiki.
Ya pili: Swalaah ya Jamaa si wajibu kwa kila mtu binafsi. Ni kauli ya Jamhuri; Abu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy ingawa wamekhitalifiana kati yao kama je Jamaa ni Sunnah tu, au Sunnah Iliyokokotezwa, au ni Fardhi Kifaayah? [Al-Badaai-’i (1/155), Ibn ‘Aabidiyn (1/371), Al-Qawaaniyna (69), Al-Khurashiy (2/16), Al-Majmu’u (4/184) na Mughnil Muhtaaj (1/229)]
Hoja zao ni:
1- Neno la Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:
((Swalaah ya Jamaa inaishinda Swalaah ya mtu peke yake kwa daraja ishirini na saba)) na zingine zenye maana kama hii. Wanasema kwamba uzidiano unaonyesha kwamba Swalaah mbili zinashirikiana katika asili ya ubora na hii inaonyesha kwamba si wajibu kwa kila mtu binafsi. Haisemwi: “Kulifanya la wajibu ni bora kuliko kuliacha”, wala haisemwi: “Tamshi lake “af-‘alu” laweza kuja kuthibitisha sifa ya upande mmoja wa kitu na kuikanusha ya upande mwingine, na “afdwalu” yenye kudhifiwa kwenye Swalaah ya mtu pweke hivyo hivyo. Kwa kuwa hili linaswihi katika “af-‘alu” moja kwa moja bila kukutanishwa na “min”. Na hata baadhi ya matamshi yaliyopo kwa Muslim yanasema: ((Huizidi Swalaah ya kuswali peke yake)), na hili latueleza wazi kwamba inasihi mtu kuswali peke yake. [Twarhu At-Tathriyb cha Al-‘Iraaqiy]
Wa mwanzo wamejibu wakisema kwamba uzidiano ni kwa Swalaah ya mwenye udhuru – kwa kukusanya baina ya dalili -, nayo inakuwa chini ya Swalaah ya Jamaa kwa ubora.
2- Hadiyth ya Yazid bin Al-Aswad kuhusu kisa cha watu wawili walioswali nyumbani walikofikia, wakaenda Msikitini na hawakuswali. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Msifanye, mkiswali nyumbani kwenu mlikofikia, kisha mkaja kwenye Msikiti wa Jamaa, basi swalini pamoja nao, kwani Jamaa inakuwa ni Sunnah kwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa nyakati marufuku kuswali]
Wanasema: “Rasuli hakuwakanushia kuswali nyumbani kwao walikofikia”.
Limejibiwa: “Hili ni tukio la kibinafsi ambapo inawezekana wakawa na udhuru wa kuacha kuswali Jamaa.
3- Hadiyth ya Abu Muusa aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Watu wenye malipo makubwa zaidi katika Swalaah ni wale wenye kutembea toka mbali kisha wa mbali zaidi. Na yule anayengojea Swalaah mpaka akaswali na imamu ana malipo makubwa zaidi kuliko yule anayeswali kisha akalala)) [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (651) na Muslim (662)]
Na katika tamko la Muslim: “Mpaka aiswali katika Jamaa na imamu”.
Hadiyth iko wazi kwamba anayeswali peke yake na anayeswali Jamaa wanashirikiana katika asili ya malipo.
Ninasema: “Hii ndiyo hoja yao yenye nguvu zaidi kwa mujibu wa mwono wangu”.
4- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema katika vita vya Khaybar:
((Mwenye kula mti huu –yaani kitunguu saumu- basi asikurubie kabisa Msikiti wetu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (853) na Muslim (561)]….na Hadiyth nyingine zenye maana sawa na hii.
Wamesema: “Hadiyth hii inalazimisha moja ya mawili: Ima iwe kula vitu hivi inaruhusika na Swalaah ya Jamaa iwe si wajibu kwa mtu binafsi yake, au Swalaah ya Jamaa iwe ni wajibu kwa mtu binafsi yake, na mtu asiruhusiwe kula vitu hivi. [Ihkaamul Ahkaami Sharhi ‘Umdatil Ahkaam cha Ibn Daqiyq Al-‘Iyd (1/119)]
Jamhuri wanasema kwamba mtu anaruhusiwa kula vitu hivi na Jamaa inakuwa si wajibu kwake kwa kuwa inajuzu kuiacha kutokana na kula vitu hivi. Lakini wamejibiwa kwamba Jamaa ni wajibu na haitimu ila kwa kuacha kula kitunguu saumu, hivyo ni lazima kuacha kukila wakati wa Swalaah.
5- Inawezekana kutolea dalili kwa Hadiyth ya mtu aliyeswali nyuma ya Mu’aadh aliyerefusha sana kisomo. Mtu yule akajitoa kwenye Swalaah, akaswali peke yake, kisha akaenda kumshtakia kwa Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam, na Rasuli hakukipinga kitendo chake cha kuacha Jamaa. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa “kukhitalifiana nia ya imamu na maamuma” katika sharti za kuswihi Swalaah]
Hili linajibiwa kwamba kurefusha imamu ni udhuru wa kuacha Jamaa.
- Lenye nguvu katika hoja hizi
Hakuna shaka kwamba kukusanya kati ya Hadiyth zilizotangulia kiasi inavyowezekana ni jambo la lazima. Nukta ambayo Hadiyth hizi zinakutania bila kukiacha chochote –kwa mwono wangu- ni kusema kwamba Swalaah ya Jamaa ni fardhi ya kutoshelezana kama alivyosema Ash-Shaafi’iy Rahimahul Laahu. Hii ndio kauli sahihi yenye uwiano mzuri zaidi. Lakini inatakikana ijulikane kwamba haipotezi Jamaa na kuiatilisha bila ya udhuru, isipokuwa mnyimwa kheri na mkosa bahati.
- Hukmu ya Swalaah ya Jamaa kwa wanawake
[Nimeitoa kwenye kitabu changu cha Fiqhu As-Sunna Lin-Nisaai ukurasa wa 146-149 kwa mabadilisho kidogo. Angalia Al-Badaai-’i (1/155), Ash-Sharhu As-Swaghiyr (1/156), Mughnil Muhtaaj (1/229) na Al-Mughniy (2/202)]
Kwa mujibu wa Ijma’a ya Maulamaa, Swalaah ya Jamaa si wajibu kwa wanawake lakini sheria inawaruhusu kuswali Jamaa kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri.
Swalaah ya mwanamke katika Jamaa inakuwa kwa aina mbili:
1- Mwanamke aswalishwe na mwanamke mwenzake. Hili linaruhusika kutokana na mambo matatu:
(a) Ujumuishi wa Hadiyth zilizotangulia kuhusiana na fadhila za Swalaah ya Jamaa. Na asili ni kuwa ((Wanawake ni ndugu moja na wanaume)). [Hasan kwa Sanad tofauti. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (236), At-Tirmidhiy (113) na Ahmad (6/256)]
(b) Hakuna katazo lolote la wanawake kuswalishana wenye.
(c) Kutendwa hilo na baadhi ya Maswahaba wanawake kama Ummu Salamah na ‘Aaishah. Imepokelewa toka kwa Rabtwah Al-Hanafiyyah kwamba ‘Aaishah aliwaswalisha na akasimama kati yao katika Swalaah ya faradhi. [Swahiyh kwa Hadiyth wenza: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (3/141), Ad-daaraqutwniy (1/404) na Al-Bayhaqiy (3/131)]
Na imepokelewa toka kwa ‘Ammaar Ad-Dahniy toka kwa mwanamke katika watu wake aitwaye Hujayrat toka kwa Ummu Salamah kwamba aliwaswalisha akasimama katikati yao. [Swahiyh kwa Hadiyth wenza: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (3/140), Ad-daaraqutwniy (1/405) na Al-Bayhaqiy (3/131)]
Kutokuwepo mpingaji wa kitendo hiki cha Maswahaba hawa akina mama, kunaonyesha kwamba inajuzu kisheria mwanamke kuwa imamu wa wenzake. Imepokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru Ummu Waraqah aweke mwadhini wa kumwadhinia, na akamwamuru awaswalishe watu wa nyumbani kwake. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (592), Ibn Khuzaymah (3/89), Al-Bayhaqiy (3/130) na Ad-daaraqutwniy (1/403)]
Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, na haya ndiyo waliyoyasema Mashafii na Mahanbali.
2- Mwanamke aswalishwe na mwanamume. Ni sawa akiswalishwa peke yake, au pamoja na wanawake wenzake, au nyuma ya Jamaa ya wanaume. Haya yanajuzu kutokana na Hadiyth nyingi. Kati ya hizo ni:
- Hadiyth ya Anas aliyesema: “Niliswali mimi pamoja na yatima katika nyumba yetu nyuma ya Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam, na mama yangu –Ummu Salamah- akiwa nyuma yetu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (727) na Muslim (658)]
- Hadiyth ya Ummu Salamah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotoa tasliym, wanawake husimama anapomaliza tasliym yake, naye hukaa kidogo mahala pake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (870), Abu Daawuud (1040), An-Nasaaiy (2/66) na Ibn Maajah (932)]
- Maangalizo
1- Mtu anaweza kuswali Jamaa yeye na mke tu faraghani au na yeyote katika maharimu zake, kwa kuwa inajuzu kukaa naye faraghani kwingineko kokote.
2- Haijuzu mwanamume kumswalisha mwanamke ajnabiya peke yake kutokana na ujumuishi wa kauli yake Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Asikae kabisa mwanamume na mwanamke faraghani, kwani watatu wao ni shaytwaan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1171) na Ahmad (172)]
3- Mwanamume anaweza kuliswalisha kundi la akina mama, kwa kuwa wingi wao huondosha ufaragha, hakuna katazo lililoripotiwa, na baadhi ya Masalaf wameripotiwa kulitenda hilo. Lakini hili litafanyika ikiwa patasalimika na fitna, na kama fitna ipo, basi haijuzu, kwani Allaah Hapendi ufisadi.
Hukumu zaidi kuhusiana na Swalaah ya Jamaa ya akina mama zitakuja kuelezewa mbeleni Insha-Allaah.
- Idadi inayotakikana ya kupatikana Jamaa
Mafuqahaa wamekubaliana kwamba uchache wa idadi ya kufanyika Jamaa ni watu wawili, yaani imamu na maamuma. Kwa hawa wawili, fadhila ya Jamaa hupatikana. Na hii ni kwa Hadiyth zifuatazo:
1- Hadiyth ya Maalik bin Al-Huwayrath aliyesema: “Watu wawili walimjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakitaka kusafiri. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Ikiwa mmeshatoka, basi adhinini, kisha kimuni Swalaah, halafu awaswalisheni mkubwa wenu zaidi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (630) na Muslim (674)]
2- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusiana na kisa cha kulala kwake pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa khalati yake Maymounah isemayo: “Akasimama kuswali, nami nikatawadha kiasi alivyotawadha yeye, kisha nikaja na kusimama kushotoni kwake, akanigeuza na kunileta kuliani kwake. Halafu aliswali rakaa nyingi, kisha akalala kwa ubavu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (138) na Muslim (763)]
3- Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy kwamba mtu mmoja alikuja baada ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumaliza kuswali. Rasuli akasema: ((Nani atamtolea swadaqah huyu?)) Mtu mmoja akasimama na kuswali naye. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (574), At-Tirmidhiy (220), Ad-daaramiy (1368) na Ahmad (10980)]
4-Tumeeleza kwenye mlango wa Swalaah ya usiku namna Ibn Mas-’oud na Hudhayfah walivyoswali na Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam.
Kisha Maulamaa wamekhitalifiana kama Jamaa inapatikana katika Swalaah ya faradhi ikiwa kuna imamu na kijana mdogo mpambanuzi. La sahihi ni kwamba Jamaa inapatikana kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas. Isitoshe, hakuna dalili ya kufarikisha kati ya Swalaah ya Sunnah na ya faradhi katika hilo, na mtoto mdogo mpambanuzi anaweza kuwa imamu ikiwa anaswali Sunnah kama itakavyokuja. Hivyo inajuzu mtoto kuwa maamuma wa mswaliji faradhi aliyebaleghe. Haya ni madhehebu ya Hanafi na Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Badaai-’i (1/156), Mughnil Muhtaaj (1/229) na Al-Mughniy (2/178). Angalia Haashiyat Ad-Dusuwqiy (1/319) na Jawaahir Al-Ikliyl (1/76). Wamaalik wametofautisha kati ya faradhi na Sunnah!! Na Hadiyth iliyotangulia ya Abu Sa’iyd ni hoja dhidi yao]
- Wapi huswaliwa Swalaah ya Jamaa?
Swalaah ya Jamaa inaweza kuswaliwa mahala popote palipo twahara; nyumbani, jangwani au Msikitini. Ni kwa neno lake Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:
((Ardhi imefanywa kwangu ni sehemu ya kuswalia na kujitwaharishia. Na mtu yeyote katika umma wangu ambaye Swalaah imemwadilia, basi aswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (335) na Muslim (521) kutoka Hadiyth ya Jaabir]
Na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaambia watu wawili: ((Mkiswali nyumbani kwenu mlikofikia, kisha mkaja kwenye Msikiti wa Jamaa, basi swalini pamoja nao, kwani Jamaa inakuwa ni Sunnah kwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake imeshatajwa]
Isipokuwa kuswali Swalaah za faradhi kwa Jamaa Msikitini inakuwa ni bora zaidi kuliko sehemu nyingine. Ni kwa Hadiyth ya Zayd bin Thaabit ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Swalini enyi watu majumbani mwenu, kwani bora ya Swalaah ni mtu kuswali nyumbani kwake isipokuwa Swalaah ya faradhi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (731) na Muslim (781)]
Kuongezea na hilo ni kuwa kuswaliwa Msikitini huiongezea nguvu nembo ya Swalaah, hudhihirisha wingi wa Waislamu, na mtu hupata thawabu za kukanyaga hatua kwenda Msikitini.
- Nyudhuru zinazoruhusu kutohudhuria Jamaa
Kuna nyudhuru jumuiya na nyudhuru binafsi zinazoruhusu kutohudhuria Jamaa Msikitini. Ubainisho wa hili ni kama ifuatavyo:
(a) Nyudhuru jumuiya
1,2- Mvua na tope zinazomletea mtu uzito wa kutoka kwenda Msikitini
Imepokelewa toka kwa Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar aliadhini kwa ajili ya Swalaah katika usiku wenye baridi na upepo kisha akasema: “Swalini majumbani”. Kisha akasema: “Ikiwa usiku ni wa baridi na mvua, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwamuru mwadhini aseme: “ Swalini majumbani”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (666) na Muslim (697)]
Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari, mvua ikatunyeshea na akasema: ((Aswali atakaye kati yenu kwenye hema yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (698), Abu Daawuud (1065) na At-Tirmidhiy (409)]
Lakini kama atatoka kwenda kwenye Jamaa, basi itakuwa ni bora zaidi kutokana na Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy aliyesema: “Lilikuja wingu na mvua ikanyesha mpaka dari likavuja (lilikuwa ni la majani ya mtende). Swalaah ikaqimiwa, nami nikamwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisujudu kwenye maji na tope na nikaona athari ya tope kwenye paji lake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (669) na Muslim (1167)]
Hakika Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihudhuria Jamaa ingawa mvua ilikuwepo na tope na akasujudu juu yake.
3- Baridi kali
Ni ile inayopita kiwango kilichozoeleka kwa watu. Hadiyth ya Ibn ‘Umar inayogusia hili tushaielezea nyuma takriban.
Imepokelewa toka kwa Na’iym An-Nahhaam kwamba iliadhiniwa Alfajiri katika siku ya baridi naye akiwa katika guo la mke akasema: “Laiti mwadhini angelinadi: Na mwenye kukaa, basi hana makosa”. Na hapo mwadhini wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanadi mwishoni mwa adhana yake: Na mwenye kukaa, basi hana makosa”. Na hii ni katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika adhana za mwisho mwisho. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/220), ‘Abdul Razzaaq (1927) na Al-Bayhaqiy (1/398)]
Zaidi ya nyudhuru hizi, Maulamaa wameongezea udhuru wa kiza kinene ambapo mtu anakuwa hawezi kuiona njia yake kuelekea Msikitini.
- Faida
An-Nawawiy kasema: “Masahibu zetu wamesema: Jamaa hupomoka kwa nyudhuru sawasawa tukisema kwamba ni Sunnah, au Fardhi Kifaayah, au Fardhi ‘Ayn. Kwa kuwa, hata sisi tukisema kwamba ni Sunnah, basi inakuwa ni kokotezwa na ni karaha kuiacha kama ilivyobainika nyuma. Na kama ataiacha kwa udhuru, basi ukaraha utaondoka, na hii haimaanishi kwamba kama ataiacha Jamaa kwa udhuru atazipata fadhila zake, bali bila shaka fadhila hizo hazipati. Maana yake inakuwa ni kupomoka madhambi na ukaraha”. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy]
(b) Nyudhuru binafsi
4- Ugonjwa
Ni ule wenye kumpa mtu uzito wa kuweza kwenda Msikitini kwa ajili ya Jamaa. Ibn Al-Mundhir kasema: “Siyajui makhitalifiano yoyote kati ya Maulamaa kuhusu kutokwenda mgonjwa kwenye Jamaa kutokana na ugonjwa, na kwa vile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipougua, hakwenda Msikitini na akasema: ((Mwamrisheni Abu Bakri aswalishe watu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (664) na Muslim (418)]
Na ikiwa ugonjwa ni mdogo usioleta tabu kama kuuma gego, maumivu kidogo ya kichwa au homa ya mbali, basi huo si udhuru. Kidhibiti ni uzito unaompata mgonjwa mithili ya uzito wa kutembea kwenye mvua”. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (4/205)]
Na kama atapiga moyo konde, akaenda Msikitini na ugonjwa wake kama ataweza, basi ni bora zaidi. Imepokelewa toka kwa Ibn Mas-’oud akisema: “Hakika hakukuwa na yeyote kati yetu anayebaki nyumbani asiende kuswali isipokuwa mnafiki ambaye unafiki wake ushathibiti au mtu mgonjwa. Ikiwa mtu mgonjwa, hutembea akishikiliwa na watu wawili mpaka akahudhuria Swalaah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (654) na wengineo, nasi tushaitaja]
5- Ila kama upofu na mfano wake
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu Thawbaan bin Maalik aswalie nyumbani kwake wakati alipomwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Macho yangu hayaoni, na mimi ninawaswalisha watu wangu. Mvua inaponyesha, bonde linalotenganisha kati yangu na wao hufurika nami nashindwa kwenda Msikiti wao, nikabaki kuwaswalisha watu wangu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (425) na Muslim (33)]
Huyu, ana nyudhuru mbili kwa pamoja; upofu na mvua. Na katika tamshi la Hadiyth ya Anas: “Mtu mmoja katika Answar aliniambia: Mimi siwezi kuswali nawe. Alikuwa ni pandikizi la mtu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (670) na Abu Daawuud (657)]
Baadhi ya Maulamaa wanauchukulia upandikizi wa mtu na utipwatipwa kama ni udhuru. Na hata kipofu, kama hakupata wa kumwongoza kwenda naye Msikitini, huo unakuwa ni udhuru kwake wa kutohudhuria Jamaa kwa mujibu wa Jamhuri. Lakini Mahanafi wanampa udhuru kwa hali yoyote hata kama ana mtu wa kumpeleka Msikitini. [Ibn ‘Aabidiyn (1/373), Ad-Dusuwqiy (1/391) na Kash-Shaaful Qina’a (1/497)]
6- Khofu
Ni kama mtu kujikhofia kutokana na mtawala, dhalimu, adui, mwizi na kadhalika. Au hata kuyaogopea mali yake, au mke wake, au wale alio na jukumu la kuwalinda. Hili ni katika udhuru wa kutohudhuria Jamaa kwa Maulamaa ingawa wamekhitalifiana katika baadhi ya vipengele. [Ibn ‘Aabidiyn (1/374), Mughnil Muhtaaj (1/235) na Al-Mughniy (1/631)]
Na mhimili wa haya ni Hadiyth Marfu’u toka kwa Ibn ‘Abbaas isemayo:
((Mwenye kusikia adhana, kisha asizuiliwe na udhuru wowote kuiendea –Wakauliza: Ni upi udhuru Ee Rasuli wa Allaah? Akasema: Ni khofu au ugonjwa- basi Swalaah yake aliyoiswali haitokubaliwa)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Takhriyj yake imeshatangulia katika mlango wa hukmu ya Swalaah ya Jamaa]
Tumeshaeleza kwamba Hadiyth hii si Swahiyh.
7- Kutengwa chakula kwa mwenye njaa
Imepokelewa toka kwa Naafi’i toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Akitengewa mmoja wenu mlo wa usiku na Swalaah ikaqimiwa, basi anzeni na chakula. Asiharakie mpaka amalize kula)). Ibn ‘Umar alikuwa akitengewa chakula na Swalaah inaqimiwa. Haendi kuswali mpaka amalize kula huku akikisikia kisomo cha imamu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (673) na Muslim (559)]
Jamhuri ya Maulamaa wamelichukulia neno lake: “basi anzeni na chakula” kama ni Sunnah, kisha wakakhitalifiana. Kuna wanaolihusisha hilo na aliyebanwa na njaa, na hili ni mashuhuri kwa Ash-Shaafi’iy. Wengine kama Ath-Thawriy, Ahmad na Is-Haaq hawalihusishi na njaa bali wanalijengea juu ya kitendo cha Ibn ‘Umar. Ibn Hazm kapetuka hayo akisema kwamba akiswali kisha akaja kula, basi Swalaah yake ni batili!! Wengine wanaona ni bora kuanza na Swalaah kwa yule ambaye hana hamu sana ya kula, na hili limenukuliwa toka kwa Maalik na Maswahibu zake wakisema: “Kama ataharakia kula kisha akaswali, basi ni Sunnah kuiswali tena!!” [Fat-hul Baariy (2/188) kwa mabadilisho kidogo]
Ninasema: “Ama kusuniwa kuiswali tena, hili halina dalili. Ama kutanguliza kula kabla ya Swalaah kuwa ni Sunnah na si wajibu, dalili yake ni Hadiyth ya ‘Amri bin ‘Umayyah aliyesema: “ Nilimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akila paja la mbuzi kwa kukata vinofu, akaitwa kwenye Swalaah, akasimama na kukitupa kisu. Akaswali na wala hakutawadha”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (675) na Muslim (355)]
8- Kubanwa na haja ndogo au kubwa
Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Msiswali chakula kikiwa tayari, au mtu akibanwa na haja ndogo au kubwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (560), Abu Daawuud (89) na Ahmad (6/43)]
Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Al-Arqam ya kwamba alitoka kwenda kuhiji au kufanya ‘Umrah akiwa pamoja na watu, na alikuwa akiwaswalisha. Na siku moja, aliqimu Swalaah –Swalaah ya Alfajiri- kisha akasema: “Mmoja wenu atangulie –naye akaenda msalani- kwani nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “
((Akitaka mmoja wenu kwenda msalani na Swalaah ikaqimiwa, basi aende kwanza msalani)). [Swahiyh kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (88), An-Nasaaiy (2/110), At-Tirmidhiy (142), Ibn Maajah (616) na wengineo]
Kubanwa na haja ndogo au kubwa ni nyudhuru mbili ambazo kila moja hupomosha Jamaa kwa makubaliano ya Maulamaa wote kutokana na dalili zilizotangulia. Kwa kuwa mtu akiswali huku amebanwa na moja kati ya haja mbili, basi anakuwa mbali na khushuu ya Swalaah, na anakuwa haizingatii tena Swalaah yake.
9- Kula kitunguu maji, kitunguu saumu, “shallots” na mfano wake kama harufu yake itabakia
Huu ni udhuru wa kutokwenda kwenye Jamaa ili watu na Malaika wasiudhike. Imepokelewa toka kwa Jaabir kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kula kitunguu saumu hichi))-, Akasema mara nyingine: ((Mwenye kula kitunguu maji, kitunguu saumu na “shallots”- basi asiukaribie kabisa Msikiti wetu, kwani Malaika wanaudhika na yale yanayowaudhi wanadamu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (854) na Muslim (564) na tamko ni lake]
Makusudio hapa ni kuvila vitu hivi vikiwa vibichi. Kama vikipikwa akavila, basi hakuna ubaya kwani sababu ya kukerwa na harufu inakuwa haipo. Imepokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema juu ya mimbar: “ Kisha nyinyi enyi watu mnakula mimea miwili, siioni isipokuwa ni mibaya; kitunguu hiki na kitunguu saumu. Mimi nimemwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapomkuta mtu ana harufu yake Msikitini, humwamuru atoke kwenda Al-Baqiy’i. Mwenye kuvila, basi avile vikiwa vimepikwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (567) na An-Nasaaiy (2/43) kwa ufupi]
Maulamaa wamemjumuisha kwenye udhuru huu mtu mwenye kufanya kazi yenye harufu mbaya kama mchinjaji na muuza nyama, muuza mafuta na kadhalika. Pia mtu mwenye maradhi ya kuwakera watu kama ukoma na mbalanga. [Ad-Dusuwqiy (1/389), Mughnil Muhtaaj (1/236) na Kash-Shaaful Qina’a (1/497)]
Ninasema: “Wenye kustahiki zaidi kuingizwa kwenye orodha hii ni wavutaji sigara ambao wamekuwa wengi hivi leo. Watu hukerwa nao zaidi kuliko wanavyokereka na mlaji kitunguu na kitunguu saumu. Hii ni pamoja na kwamba asili ya kitunguu na kitunguu saumu ni halali kinyume na uvutaji sigara. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.
- Faida
Jingine waliloliongezea Maulamaa katika nyudhuru za kutokwenda kwenye Jamaa ni kutopata nguo ya kujisitiri uchi, bali Ash-Shaafi’iy na baadhi ya Mahanafi wanasema kwamba ikiwa ana nguo yenye hadhi sawa na wenzake atakwenda kwenye Jamaa, na kama hana basi asitoke. [[Ad-Dusuwqiy (1/380), Mughnil Muhtaaj (1/236) na Kash-Shaaful Qina’a (1/496)]
- Angalizo: Je, bwana harusi anasameheka asitoke kwenye Jamaa kwa ajili ya harusi yake?
Mafuqahaa wa Kishafii na Kihanbali wanaona kwamba bi harusi kupelekwa kwa mume ni udhuru unaomruhusu mume kubakia awe na mke, na asitoke kwenda Jamaa kwa muda wa siku saba ikiwa mke ni bikra, na siku tatu ikiwa mke mkuu!! Mashafii wamelihusisha hili la kutokwenda Jamaa na Swalaah za usiku tu!! [Mughnil Muhtaaj (1/236) na Kash-Shaaful Qina’a (1/497)]
Ninasema: “Hili ni kosa, alilolielezea Ash-Shaafi’iy ni ukaraha. Na kiini cha kosa hili ni kutoifahamu vizuri Hadiyth ya Anas. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Ni Sunnah ikiwa mtu atamwolea mke mkuu bikra, akae kwa bikra siku saba, kisha agawe siku. Na akimwolea bikra mke mkuu, akae kwa mke mkuu siku tatu, kisha agawe siku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5214) na Muslim (1461)]
Maana ya Hadiyth hii ni wazi kwamba kama mtu ana mke mkuu akaoa bikra, basi atalala kwa bikra siku saba, kisha atazigawa siku kwa wakeze kwa usawa, na hakuna hapa kinachopinga kwamba asitoke kwenda kuswali. Pia, kama ana mke bikra akao mke mkuu, atakaa kwa mke mkuu siku tatu.
Linalobainisha kwa uwazi zaidi kwamba haya ndiyo makusudio ya kukaa ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa Ummu Salamah, alikaa kwake siku tatu na akasema:
((Watu wako hawatapata madhaliliko kwa sababu yako, ukitaka nitalala kwako siku saba, na nikilala kwako siku saba, nitalala pia siku saba kwa wake zangu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1460), Abu Daawuud (2122), Ibn Maajah (1917) na Maalik (1123)]
- Adabu za kwenda Msikitini na yafanywayo kabla ya Swalaah
1- Kuacha kazi wakati wa Swalaah unapoingia
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye kuwahudumia wakeze, na wakati wa Swalaah unapoingia hutoka kwenda kuswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (676), At-Tirmidhiy (2489) na Ahmad (6/49)]
2,3- Kutawadha nyumbani, kwenda kwa miguu Msikitini, na kukithirisha hatua na kuzihesabu
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kujitwaharisha nyumbani kwake, kisha akatembea kwa miguu kwenda katika nyumba kati ya Nyumba za Allaah ili kutekeleza faradhi kati ya Faradhi za Allaah, basi hatua zake mbili zinakuwa; moja yao inapomosha dhambi na nyingine inanyanyua daraja)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (666)]
Na imepokelewa toka kwa Abu Musa Al-Ash’ariyy ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mtu mwenye malipo makubwa zaidi katika Swalaah, ni yule anayetembea toka mbali, kisha wa mbali zaidi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (651) na Muslim (662)]
Na imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Banu Salamah walitaka wahamie kwenye Msikiti wa karibu zaidi, na Rasuli wa Allaah hakupenda mji kubaki mahame bila watu akasema:
((Enyi Banu Salamah! Je, hamzihesabu hatua zenu?)). Wakabakia [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1887), Ibn Maajah (784) na Ahmad (3/106)]
Na katika tamshi la Hadiyth ya Jaabir: “Akatukataza akisema:
((Hakika nyinyi mnapata kila hatua daraja)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (664) na Ahmad (3/336)]
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Je, niwaonyesheni jambo ambalo Allaah Hufuta kwalo makosa na Hunyanyua kwalo daraja?)) Wakasema: “Tuonyeshe Ee Rasuli wa Allaah. Akasema: ((Kuutimiliza wudhuu pamoja na ukali wa baridi na maumivu ya viungo, kukithirisha hatua kwenda Msikitini, na kusubiri Swalaah baada ya Swalaah, basi hayo ndiyo ya kuazimiwa kweli)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (251), At-Tirmidhiy (51), An-Nasaaiy (1/89) na Ahmad (2/235)]
Imepokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kwenda Msikitini mwanzo wa mchana au mwisho wa usiku, Allaah Humwandalia mashukio Peponi kila anapokwenda mwanzo wa mchana au mwisho wa usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (662) na Muslim (669)]
4- Kuharakia kwenda Msikitini na kuiwahi Swalaah
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Na lau wangelijua yaliyomo katika kuiwahi Swalaah, basi wangelishindana. Na lau wangelijua yaliyomo kwenye Swalaah ya ‘Ishaa na Alfajiri, basi wangeziendea japo kwa kutambaa. Na lau wangelijua yaliyomo kwenye safu ya kwanza, basi wangelipiga kura)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (720) na Muslim (437)]
Na imepokelewa kutoka kwake vile vile akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Na anapoingia Msikitini, anakuwa ndani ya Swalaah madhali Swalaah ndiyo inayomzuia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (477) na Muslim (649) kwa ufupi]
5- Kwenda Msikitini kwa miguu na kwa utulivu bila haraka
Imepokelewa toka kwa Abu Qataadah akisema: “Tulipokuwa tukiswali pamoja na Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam, mara ghafla alisikia zogo la watu. Alipomaliza kuswali aliuliza: Mna nini? Wakasema: Tumekimbilia Swalaah. Akawaambia: ((Msifanye. Mnapokuja kwenye Swalaah kuweni watulivu, mnachokipata kiswalini, na mnachokikosa kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (635) na Muslim (603)]
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayra kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mnapoisikia adhana, basi nendeni kwa miguu katika Swalaah. Jipambeni kwa utulivu na umakini, na wala msifanye haraka. Mnachokipata kiswalini, na mnachokikosa kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (636) na Muslim (602)]
6- Kusoma adhkaar zilizothibiti wakati wa kutoka na kuingia Msikitini
Atasema anapotoka: “Ee Mola! Nijaalie nuru katika moyo wangu, na nuru katika ulimi wangu, na Ujaalie nuru katika masikio yangu, na Unijaalie nuru katika macho yangu, na Unijaalie nuru nyuma yangu na nuru mbele yangu, na Ujaalie nuru juu yangu na nuru chini yangu. Ee Mola Nipe nuru”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6316) na Muslim (763)]
Na atasema wakati anapoingia kwa mguu wake wa kulia: “Bismillaah. Ee Allaah Mrehemu Muhammad”. [Hadiyth Hasan Lighayrih: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abus Sunniy (88). Ina Hadiyth wenza na angalia Swahiyh Al-Kalim At-Twayyib (63)]
Na “Ee Allaah! Nifungulie milango ya Rehma Yako”.
7- Kutoshikanisha vidole akiwa Msikitini isipokuwa kwa haja
Kwa kuwa mtu anakuwa ndani ya hukmu ya Swalaah madhali amekaa akiisubiri Swalaah, na mwenye kuswali haijuzu kwake kushikanisha vidole kama ilivyotangulia katika mlango wa mambo yaliyokirihishwa katika Swalaah. Maana ya hili tunaipata katika Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Akitawadha mmoja wenu nyumbani kwake kisha akaenda Msikitini, basi anakuwa ndani ya Swalaah mpaka arejee. Basi na asifanye hivi, na akashikanisha baina ya vidole vyake)). [Hadiyth Hasan kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/206). Ina Hadiyth wenza kwa Ahmad (3/42), Ad-daaramiy (1406) Ibn Khuzaymah (439) na wengineo]
Hadiyth hii ina mvutano, na kuifanya Hasan kuna nguvu zaidi.
Ama Hadiyth ya ‘Abdullah bin ‘Amri iliyoelezewa na Al-Bukhaariy kwa anwani isemayo: “Kushikanisha vidole Msikitini na kwingineko” isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ee ‘Abdullah bin ‘Amri! Utafanya nini ukibakia baina ya watu wasio na kheri, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akashikanisha kati ya vidole vyake)) [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (466), Abu Daawuud (4342) na Ibn Maajah (3957)]…. na mfano wake, ni kuwa uhakiki unasema kwamba hakuna mgongano kati ya Hadiyth mbili, kwa kuwa linalokatazwa ni kufanya hilo kwa njia ya mchezo. Makusudio ya yaliyomo ndani ya Hadiyth ni kuiga na kutoa taswira ya maana katika nafsi kwa picha ya hisia. Au yawezekana kusema: “Katazo limehusishwa tu na mtu anapokuwa ndani ya Swalaah, au anapokuwa anaisubiri kwa kuwa hapo anahukumiwa kuwa yuko kwenye Swalaah. Na Hadiyth ya Ibn ‘Amri na mfano wake hazina hayo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Angalia Fat-hul Baariy (1/566) chapa ya Al-Ma-’arifah]
8- Kuswali rakaa mbili za maamkizi ya Msikiti
Hili lishazungumzwa kirefu katika mlango wa Swalaah za Sunnah.
9- Kutoswali Sunnah Swalaah inapoqimiwa
Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Swalaah inapoqimiwa, hapana Swalaah ila ya faradhi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (710), Abu Daawuud (1266), An-Nasaiy (2/116), At-Tirmidhiy (421) na Ibn Maajah (1151)]
Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Bahiynah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu anaswali rakaa mbili baada ya Swalaah kuqimiwa. Rasuli alipomaliza Swalaah, watu walimzonga mtu yule, na Rasuli akamwambia: ((Je, Asubuhi ni rakaa nne? Je, Asubuhi ni rakaa nne?)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (663-711), An-Nasaaiy (2/117) na Ibn Maajah (1153)]
Katika tamshi jingine: ((Mmoja wenu anakurubia kuswali Alfajiri rakaa nne)).
Na kama atahirimia Swalaah ya Sunnah kabla ya iqaama, kisha ikaqimiwa naye yuko ndani ya Swalaah, basi kauli adilifu zaidi ni kusema: Akijua kuwa ataimaliza Swalaah kabla imamu hajahirimia, basi ataikamilisha, na kama si hivyo, basi ataivunja kutokana na Hadiyth hii. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Angalia madhehebu ya Maulamaa: Ibn ‘Aabidiyn (1/479), Jawaahir Al-Ikliyl (1/77), Mughnil Muhtaaj (1/252) na Al-Mughniy (1/456)]
(10) Kutotoka Msikitini baada ya kuadhiniwa na kabla ya Swalaah ya faradhi isipokuwa kwa dharura
Imepokelewa toka kwa Abu Ash-Sha’athai akisema: “Tulikuwa tumekaa Msikitini pamoja na Abu Hurayrah. Mwadhini akaadhini, na mtu mmoja akasimama akaanza kutoka Msikitini. Abu Hurayrah akamwandama kwa jicho mpaka akatoka nje, kisha akasema: “Ama huyu, bila shaka amemwasi Abal Qaasim Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (655), Abu Daawuud (536), An-Nasaaiy (2/29), At-Tirmidhiy (204) na Ibn Maajah (733)]
Kama kuna dharura inayoshurutisha mtu kutoka, basi hakuna ubaya. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka baada ya Swalaah kuqimiwa na watu kunyoosha safu. Alikuwa ashasimama sehemu yake ya kuswalia, na tulipokuwa tunasubiri apige takbiyr, aliondoka na kutuambia: Bakini kama mlivyo. Tukabakia kama tulivyo mpaka akatutokea tena huku kichwa chake kikitona maji. Alikuwa kaoga”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (639) na Muslim (605)]
11-Asisimame mtu -Swalaah inapoqimiwa- ila baada ya kumwona imamu
Imepokelewa toka kwa Abu Qatadah akisema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Inapoqimiwa Swalaah msisimame mpaka mnione)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (637) na Muslim (604)]
Fiqh ya suala hili ishaelezwa kwenye mlango wa adhana.
- Adabu zinazohusiana na wanawake
12- Kumwomba ruksa mume ya kwenda Msikitini na mume asimkatalie
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Mke akimwomba ruksa mmoja wenu ya kwenda Msikitini, basi asimzuie)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5238) na Muslim (442)]
Kasema tena Ibn ‘Umar: “Mke wa ‘Umar alikuwa anahudhuria Jamaa ya Swalaah ya Alfajiri na ‘Ishaa Msikitini. Akaulizwa: Kwa nini unatoka nawe wajua kwamba ‘Umar anachukia hilo na analifanyia wivu? Akasema: Kipi kinamzuia anikataze? Akasema: Kinachomzuia asinikataze ni Kauli ya Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Msiwazuie vijakazi wa Allaah na Misikiti ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (900), Muslim (442) kwa ufupi na wengineo]
Ruksa hii wanayopewa wake na waume zao ya kwenda Msikitini ni wajibu kwa wanaume kuitoa kutokana na katazo la wazi la kuwazuia, ikiwa hakuna visababisho vya fitna kama kujishaua, kujitia manukato na kujipodoa. Kama lipo lolote katika hivyo, si lazima kuwapa ruksa na inakuwa ni haramu kutoka. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu (1/279)]
Inaweza kusemwa: Ruksa iliyotajwa si ya wajibu, kwa kuwa lau ingelikuwa ni wajibu, basi maana ya kuomba ruksa isingelikuwepo kwa kuwa ruksa haipatikani ila atakapokuwa mwenye kuombwa ruksa ni mwenye kuchaguzwa katika kukubali au kukataa. [Fat-hul Baariy (2/404) chapa ya As-Salafiyyah] Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
13- Wajiweke mbali na manukato, kujipamba na mambo yote ya kufitinisha
Imepokelewa toka kwa Zaynab mke wa ‘Abdullah bin Mas-’oud akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituambia:
((Akienda mmoja wenu Msikitini, basi asiguse manukato)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (443) na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (9425)]
Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Msiwazuie vijakazi wa Allaah na Misikiti ya Allaah. Na watoke bila kujitia chochote)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrih: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/438) na Abu Daawuud (565)]
14- Wasichanganyike na wanaume wakati wa kuingia au kutoka Msikitini
Kwa ajili ya sababu hii, wanawake katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakiharakia kutoka baada ya kumalizika Swalaah. Ummu Salamah amesema: “Rasuli wa Allaah alipokuwa anatoa tasliym, wanawake husimama wakati anapoimalizia tasliym yake, na yeye hukaa sehemu yake kidogo kabla hajasimama. Tunaona -na Allaah Anajua zaidi- kwamba kufanya hivyo ni ili wanawake wapate nafasi ya kutoka kabla mwanamume yeyote hajawakuta”.
[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (870)]