043-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Masuala Yanayohusiana Na Sifa Ya Swalaah Ya Jamaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

043-Masuala Yanayohusiana Na Sifa Ya Swalaah Ya Jamaa 

 

Alhidaaya.com

 

 

· Sutrah Ya Imamu Ni Sutrah Kwa Maamuma

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba sutrah ya imamu ni sutrah kwa walio nyuma yake. Maana ya kusema hivi ni mambo mawili:

 

1- Kwamba kama hakikuingia kati ya imamu na sutrah kitu cha kuikatizia Swalaah, basi Swalaah ya maamuma ni sahihi na haiathiriwi na chochote chenye kupita katika baadhi ya safu zao wala kati yao na imamu. Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas inasema: “Nilielekea nikiwa nimepanda punda jike na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaswali na watu Mina bila kuwepo ukuta. Nikapita mbele ya baadhi ya safu, nikashuka na kumwachilia punda aende zake kujilia. Nikaingia kwenye safu na hakuna yeyote aliyenilalamikia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (76) na Muslim (504)].

 

2- Kwamba kikipita chenye kukatizia Swalaah kati ya imamu na sutrah yake, basi kitakata Swalaah yake na Swalaah yao. Imepokelewa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake akisema: “Tulishuka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) toka pande za Adhakhar. Swalaah ikawadia, naye akaswali akielekea ukuta kama Qiblah chake. Sisi tulisimama nyuma yake, na mara akatokeza mnyama akipita mbele yake. Rasuli akawa anamzuia mpaka tumbo lake likaambata ukuta, na mnyama ikabidi apite nyuma yake”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (708), Ibn Maajah (3603) na Ahmad (2/196)].

 

Na lau kwamba sutrah yake si sutrah yao, basi kusingelikuweko tofauti kati ya kupita mnyama huyo mbele yake na nyuma yake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

· Hukmu Ya Imamu Kusoma Basmalah "بسم الله " Kwa Sauti Katika Swalaah Ya Kusoma Kwa Sauti

 

Suala hili ni moja kati ya masuala yajulikanayo zaidi, yenye mikwamo ya kifiqhi, yenye kuzungumzwa zaidi kwenye midahalo na yenye kuandikwa sana kwenye vitabu. [Nasbu ar Raayah (1/336)].

 

Na kwa ajili hiyo, kundi la Maulamaa wameliandikia kiainishi na kipambanuzi suala hili. Kiufupi, Maulamaa wana kauli mbili katika suala hili:

 

Ya kwanza: Ni Sunnah kuisoma kimya. Ni kauli ya Hanbali na Aswhaabu Ar Ra’ay, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. At-Tirmidhiy kasema: “Maulamaa wengi katika Maswahaba wakiwemo Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy walikuwa wakilifanya hili pamoja na Taabi’iyna waliokuja baada yao. Ibn Al-Mundhir kalitaja toka kwa Ibn Mas-’oud, Ibn Az Zubayr na ‘Ammaar (Radhi za Allaah ziwe juu yao wote). Aidha, wamelisema hili akina Al-Awzaaiy, Ath-Thawriy na Ibn Al-Mubaarak. [Al-Mabsuutw (1/15), Al-Mughniy (1/345) na Kash-Shaaful Qinaa (1/335). Ninasema: “Ama imamu Maalik, yeye hasomi basmalah mwanzoni mwa Swalaah. Angalia Al-Mudawwanah (1/64)”].

 

Hoja yao ni:

 

1- Hadiyth ya Anas: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr na ‘Umar, walikuwa wanafungua Swalaah kwa Al-Hamdu lil-Laahi Rabbi Al-‘Aalamiyna”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (743) na Muslim (399)].

 

Na katika riwaya ya Muslim toka kwake: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan, nami sikumsikia yeyote kati yao akisoma Bismil-Laahi Ar Rahmaan Ar Rahiym”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (399)].

 

Riwaya ya kwanza imehojiwa kwa kusemwa kuwa maana ya neno lake “wanafungua Swalaah kwa Al-Hamdu lil-Laahi Rabbi Al-‘Aalamiyna” ni Suwrat Al-Faatihah kabla ya Suwrah nyingine. Hapa basmalah haikanushwi wala haithibitishwi.

 

Ama riwaya ya pili, hii hata kama isnadi yake ni Swahiyh, lakini baadhi ya Maulamaa wameizungumzia kwa upande wa kwamba msimulizi kaichukulia riwaya ya kwanza hivyo, akakosea. Iliyohifadhiwa ni riwaya ya kwanza.  [Angalia Fat-hul Baariy (2/266-267)].

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifungua Swalaah kwa takbiyr na kusoma “Al-Hamdu Lil-Laahi Rabbi Al-‘Aalamiyna”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498)].

 

Wamesema: “Iko wazi kwamba basmalah haisomwi kwa sauti, na inaiunga mkono Hadiyth ya Anas”.

 

3-Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abdillaah bin Al-Mughaffal aliyesema: “Baba yangu alinisikia nikisema: Bismil Laahi Ar Rahmaan Ar Rahiym akaniambia: Uzushi, tahadhari na uzushi. Mimi sikumwona Swahaba yeyote wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ila alikuwa anachukia sana uzushi katika Uislamu. Mimi niliswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan na sikumsikia yeyote kati yao akiitamka, basi nawe usiitamke. Ukiswali basi sema: “Al-Hamdu Lil-Laahi Rabbi Al ’Aalamiyna”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (244) na An-Nasaaiy (2/135)].

 

Imejibiwa kwamba ni Dhwa’iyf, haifai kutolewa dalili.

 

4- Ni Neno Lake Allaah ‘Azza wa Jalla katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:

((Nimeigawanya Swalaah kati Yangu na kati ya Mja Wangu nusu mbili, na Mja Wangu atapata ayaombayo. Akisema mja: Al-Hamdu Lil-Laahi Rabbi Al ’Aalamiyna, Allaah Ta’alaa Husema: Mja Wangu amenihimidi…)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (395), Abu Daawuud (821), At-Tirmidhiy (2953), An-Nasaaiy (2/135) na Ibn Maajah (838)]..

 

Imetolewa hoja na yule aliyesema kwamba basmalah haisomwi kabisa kwenye Swalaah.

 

5- Hapana shaka kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akiisoma kabisa kwa sauti, usiku au mchana, mara tano kila siku, akiwa safarini au mjini kwake. Haiwezekani akafanya hivyo kisha hilo likafichika kwa Makhalifa Waongofu au Maswahaba wengineo, au watu wa mji wake katika enzi hizo bora. [Zaadul Ma’ad (1/206-207)].

 

Ya pili: Ni Sunnah isomwe kwa sauti. Hili ni mashuhuri kwa Ash-Shaafi’iy. Hoja yake ni:

 

1- Aliyoyasimulia Na’iym Al-Mujmir akisema: “Niliswali nyuma ya Abu Hurayrah akasoma: Bismil Laahi Ar Rahmaan Ar Rahiym. Halafu akasoma Al-Faatihahh hadi  ((غير المغضوب عليهم ولا الضالين ))  akasema: Aamiyn, na watu wakaitikia Aamiyn. Na anasema kila anaposujudu: Allaahu Akbar. Na anaposimama toka kikao cha rakaa mbili husema: Allaahu Akbar. Na anapotoa tasliym husema: Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi yangu iko Mkononi Mwake! Hakika mimi nawafananishieni Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/134), Ahmad (2/497), Ibn Khuzaymah (499) na Ibn Hibaan (1797)]

 

Hili limejibiwa kwa kusemwa kuwa kuna uwezekano wa kuwa Abu Hurayrah amewafananishia Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika sehemu kubwa ya Swalaah na si katika sehemu zote, pakizingatiwa kwamba kuna wengineo waliopokea toka kwa Na’iym toka kwa Abu Hurayrah bila kutaja basmalah. Hivyo Hadiyth haiko wazi ya kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma basmalah kwa sauti.

 

2- Hadiyth ya Qataadah aliyesema: “Anas aliulizwa: Vipi kilikuwa kisomo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Akasema: Kilikuwa ni “madda”, kisha akasoma بسم الله الرحمن الرحيم  na anavuta الرحمن na anavuta الرحيم . [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5046)].

 

Hili limejibiwa kwamba haliko wazi kama Anas alilisikia hili toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah, bali lililothibiti toka kwake ni kuwa hakuwa akiisoma kwa sauti kama ilivyotangulia.

 

3- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifungua Swalaah yake kwa بسم الله الرحمن الرحيم . [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (245) na wengineo. Angalia Hadiyth nyinginezo katika mlango wake ambazo hazikosi maneno katika Nasbu Ar Raayah (1/328)].

 

Imejibiwa, kwa kuwa ni Dhwa’iyf, haifai kwa hoja. Kisha upo uwezekano ndani yake wa kusomwa kwa siri au kwa sauti.

 

· Lenye Nguvu Zaidi

 

Kutokana na hoja zilizotangulia, tunaona kwamba hakuna katika kuisoma basmalah kwa sauti katika Swalaah, Hadiyth Swahiyh bayana yenye uzito sawa wa kidalili na Hadiyth ya Anas ya kutosomwa kwa sauti. Hivyo basi, ni bora kuisoma kimya kimya. Lakini pamoja na hivyo, la sawa zaidi ni kuwa kinachosomwa kimya kimya, kinaweza kuruhusiwa kusomwa kwa sauti kwa ajili ya maslaha muhimu kama vile imamu kuwafundisha maamuma. Pia mtu anaweza kuacha lililo bora zaidi kwa ajili ya kuziunganisha nyoyo na kuliunganisha neno kwa ajili ya kuchelea watu kulikimbia lenye maslaha kwao. [Majmuu Al-Fataawaa (22/436). Angalia Nasbu Ar Raayah (1/328)].

 

Angalizo:

 

Ni vyema ijulikane kwamba makhitalifiano katika suala hili si makubwa sana. Haitakikani kwa watu kuwa na ukereketwa wa kupita kiasi chake. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema: “Ama kuwa na kasumba na suala hili na mengineyo, hilo ni katika nembo za mifarakano na makhitilafiano ambayo tumekatazwa. Mwenye kulipigia debe hilo, basi huyo anazidi kuzisimika bendera za kuufarikisha umma kwa suala hili ambalo ni moja kati ya masuala yenye makhitilafiano madogo mno. Ni kazi tu ya Shaytwaan anayechochea watu wabebe bendera za mifarakano”. [Majmuu Al-Fataawaa (22/405)].

 

· Maamuma Kusoma Al-Faatihahh Nyuma Ya Imamu

 

Hili lina kauli tatu za Maulamaa:

 

Ya kwanza: Maamuma hasomi si katika Swalaah ya kusoma kimya kimya wala Swalaah ya kusoma kwa sauti. Ni kauli ya Abu Haniyfah na masahibu zake. [Al-Mabsuutw (1/200) na Al-Badaai-’i (1/103)]. Dalili yao ni:

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mwenye imamu, basi kisomo cha imamu ni kisomo kwake)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (850) na Ahmad (14166). Fat-hul Qadiyr (1/339)].

 

Kwa kuwa ni Dhwa’iyf kwa pande zake zote, haifai kwa dalili.

 

2- Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Adhuhuri, kisha mtu mmoja akawa anasoma nyuma yake: سبح اسم ربك الأعلى. Alipomaliza aliuliza: Nani aliyesoma? Au: Msomaji ni nani kati yenu? Mtu yule akasema: ((Hakika nilidhani kwamba baadhi yenu ni wenye kunipokonya Suwrah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (398), An-Nasaaiy (917) na Abu Daawuud (828)].

 

Lengo la kusema hivi ni kukataza kunyanyua sauti wakati maamuma anaposoma Suwarah nyuma ya imamu katika Swalaah ya kusoma kwa sauti ya chini kama inavyoonekana!!.

 

3- Kusoma Al-Faatihahh si wajibu kimsingi – kwa upande wao - hivyo kwa maamuma ndio kabisa!! Hili linapingwa kabisa kama ilivyo wazi.

 

Ya pili:

 

Ataisoma katika Swalaah ya kimya kimya na si katika Swalaah ya kusoma kwa sauti. Ni kauli ya Jamhuri na chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Mughniy (1/330), Kash-Shaaful Qinaa (1/464), Mawaahibul Jaliyl (1/537) na Majmu’u Al-Fataawaa].

 

Hoja ya kauli hii ni:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

((وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ))

((Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa)).  [Al-A’araaf (7:204)].

 

2- Hadiyth: ((Hakika amefanywa imamu ili afuatwe. Anapopiga takbiyr basi nanyi pigeni takbiyr [Na anaposoma, basi nyamazeni] )).  [Wahafidhi wakuu wa Hadiyth wameitia doa ziada hii: Muslim kaifanyia “ikhraaj” (404), Abu Daawuud (603), na An-Nasaaiy (931)].

 

3- Hadiyth ya Ibn Shihaab toka kwa Ibn Ukaymah toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimaliza Swalaah ambayo alisoma kwa sauti kisha akauliza: ((Je, mmoja wenu kasoma nami hivi punde?)) Akasema mtu mmoja: Ndio, ee Rasuli wa Allaah. Akasema: ((Mimi nasema, kwa nini napokonywa kisomo?)). Akasema: Watu wakaacha kusoma pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah ambazo Rasuli anasoma kwa sauti wakati walipolisikia hilo toka kwake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (826), At-Tirmidhiy (312), An-Nasaaiy (2/140) na Ibn Maajah (848)].

 

Baadhi yao wamesema: Hadiyth hii ni yenye kunasikhi kisomo nyuma ya imamu katika Swalaah za kusoma kwa sauti!!

 

4- Hadiyth: ((Mwenye imamu, basi kisomo cha imamu ni kisomo kwake)). [Hadiyth Dhwa’iyf:Tumeitaja nyuma kidogo].

 

Wamesema: Muradi ni kwa Swalaah za kusoma kwa sauti.

 

Ya tatu:

 

Ni lazima aisome katika Swalaah ya kimya kimya na katika Swalaah ya kusoma kwa sauti. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy – katika madhehebu mapya - na wafuasi wake na Ibn Hazm. Imekhitariwa na Ash-Shawkaaniy na Ibn ‘Uthaymiyn. [Al-Ummu (1/93), Al-Majmu’u (3/322), Al-Muhalla (3/236), Al-Furu’u (1/428), Naylul Awtwaar (2/250) na Al-Mumti’i (4/247)].

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya ‘Ubaadah bin Swaamit ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hana Swalaah asiyesoma Faatihahtul Kitaab)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (756) na Muslim (394)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba kasema: ((Mwenye kuswali Swalaah yoyote bila kusoma Ummul Qur-aan, basi Swalaah hiyo ni pungufu, -mara tatu- haikutimu)). Abu Hurayrah akaulizwa: Hata tukiwa nyuma ya imamu? Akasema: Isome katika nafsi yako”.   [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (395), Abu Daawuud (821), At-Tirmidhiy (2953), An-Nasaaiy (2/135) na Ibn Maajah (838)].

 

Hadiyth hizi mbili zinauweka ujumuishi wa Aayah Tukufu na Hadiyth: ((Na anaposoma, basi nyamazeni)) katika umahususi isipokuwa maamuma kusoma Al-Faatihahh. Hii ni pamoja na kuwa ziada ya ((Na anaposoma, basi nyamazeni)), ni katika ziada ambayo wahafidhi wakubwa wa Hadiyth wamekhitalifiana kwa upande wa usahihi wake. Abu Daawuud kasema: “Haikuhifadhiwa”. Hivyo hivyo kasema Ibn Mu’iyn, Abu Haatim Ar-Raaziy, Ad-daaraqutwniy na Abu ‘Aliy An-Niysaabuuriy. Kukubaliana wahafidhi wote hawa juu ya udhwa’iyf wake, kunatangulizwa juu ya uSwahiyh wake na hususan panapozingatiwa kwamba hakuna Sanad Swahiyh iliyosimuliwa. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (4/123). Chapa ya Ihyaau At-Turaath Al’Arabiy].

 

Kinachotilia nguvu uainisho na ubainisho huu ni:

 

3- Hadiyth ya ‘Ubaadah bin As-Swaamit akisema: “Tulikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah ya Alfajiri. Rasuli wa Allaah akasoma, na kisomo kikawa kizito kwake. Alipomaliza alisema: ((Je, nyinyi mnasoma nyuma ya imamu wenu?)). Tukasema: Na’am, lakini haraka haraka  ee Rasuli wa Allaah. Akasema: ((Msifanye isipokuwa Faatihahtul Kitaab, kwani hana Swalaah asiyeisoma)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (823), Al-Bukhaariy katika mlango wa “Sehemu ya kisomo” (63,64), At-Tirmidhiy (311) na wengineo].

 

4- Imepokelewa toka kwa mtu mmoja katika Maswahaba wa Rasuli akisema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Huenda nyinyi mnasoma nyuma ya imamu, na imamu anasoma?)) Wakasema: Ni kweli tunafanya hivyo. Akasema: ((Basi msifanye isipokuwa kama mmoja wenu anasoma Ummul Kitaab)). Au alisema: ((Faatihahtul Kitaab)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/60), Al-Bukhaariy (63) katika mlango wa “Sehemu ya kisomo” na Al-Bayhaqiy (2/166)].

 

5- Ama yale waliyodai ya kwamba Hadiyth ya Abu Hurayrah imezinasikhi Hadiyth zenye kuamuru kusoma, basi Al-Haazimiy naye katika kitabu cha “Al-I’itibaar” kurasa za 72-75, amedai kinyume chake kwa kuzifanya Hadiyth wajibishi ni zenye kuzinasikhi Hadiyth katazishi. Na kiukweli ni kuwa hakuna dalili yoyote kuhusiana na hili au lile, bali lililo wajibu ni kurejea kwenye qaaidah  za kukusanya (Al-Jam’u) au umilishi (At-Tarjiyh). Hii ni juu ya kwamba kauli yake: “Watu wakaacha kusoma katika pale aliposoma kwa sauti” imedarijiwa toka kauli ya Az-Zuhriy kama ilivyo katika riwaya ya Ahmad (2/240) na wengineo. Al-Bukhaariy amekubaliana na hili katika kitabu chake cha Taarikhuhu pamoja na Abu Daawuud, Ya’aquub bin Yuusuf, Adh-Dhahliy, Al-Khattwaabiy na wengineo. An-Nawawiy kasema: “Hili halina khilafu kabisa kati yao”.

 

Ninasema: “Ikiwa ni hivyo, basi hakuna hoja tena, na mapingamizi yote yameanguka. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Ni Wakati Gani Maamuma Anasoma Al-Faatihahh Nyuma Ya Imamu Wake?

 

[Naylul Awtwaar (2/251) chapa ya Al-Hadiyth kwa mabadilisho kidogo].

 

Tushajua kwamba kusoma Al-Faatihahh ni nguzo ya lazima katika kila rakaa sawasawa kwa imamu, kwa anayeswali peke yake na kwa maamuma. Hivyo basi, ni wakati gani maamuma ataisoma katika Swalaah ya kisomo cha sauti? Baadhi wamesema ni pale anaponyamaza imamu kati ya Al-Faatihahh na Suwrah. Wengine wamesema ataisoma nyuma ya imamu Aayah baada ya Aayah, na hili ni bora zaidi kwa kuwa isti’aadhah  (أعوذ بالله من الشيطان الرجيم) ambayo mahala pake ni baada ya takbiyr ya kuhirimia Swalaah haitocheleweshwa, na pia haitorudiwa tena wakati mtu anapotaka kusoma Al-Faatihahh ikiwa aliileta isti’aadhah mahala pake mwanzoni, na akaichelewesha Al-Faatihahh mpaka pale imamu atakaposoma Suwrah. Isitoshe, itamtosheleza “Aamiyn” moja tu wakati yeye na imamu wanapomaliza kusoma Al-Faatihahh.

 

· Kuitikia “Aamiyn” Kwa Sauti Kwa Imamu Na Maamuma Katika Swalaah Ya Kisomo Cha Sauti

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayra kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Imamu akisema “Aamiyn” basi nanyi semeni “Aamiyn”, kwani yeyote ambaye “Aamiyn” yake itawafikiana na “Aamiyn” ya Malaika, ataghufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (870) na Muslim (410)].

 

Imepokelewa toka kwa Waael bin Hujar akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma: غير المغضوب عليهم ولا الضالين akasema: Aamiyn, na akaivuta kwayo sauti yake”. [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (248), Abu Daawuud (932), Ahmad (4/315) na wengineo, nayo ina Sanad tofauti].

 

At-Tirmidhiy kasema: “Hivi ndivyo walivyosema Maulamaa wengi katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Taabi’iyna na waliofuata baada yao. Wanaona mwanamume anyanyue sauti yake kwa “Aamiyn” na asiifiche. Haya pia ndiyo wayasemayo akina Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-Haaq”.

 

Na imepokelewa toka kwa Ibn Jariyj toka kwa ‘Atwaa akisema: “Nilimwambia: Je, Ibn Az-Zubayr alikuwa akiitikia “Aamiyn” baada ya Al-Faatihahh? Akasema: Na’am, na walio nyuma yake pia mpaka Msikiti hurindima”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (2640) na Ash-Shaafi’iy kama ilivyo kwenye Musnadi wake (230)].

 

· Je, Maamuma Ataitikia “Aamiyn” Sambamba Na Imamu Au Baada Yake?

 

Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba maamuma asiitikie ila baada ya kuitikia imamu wake kutokana na mwonekano wa Hadiyth isemayo: ((Hakika si jinginelo, imamu amefanywa kuwa imamu ili afuatwe)). Na Hadiyth isemayo: ((Imamu akiitikia “Aamiyn”, nanyi itikieni “Aamiyn”)).

 

Lakini kauli yenye nguvu ni kuitikia maamuma baada ya imamu kusema ولا الضالين kwa kuwa hili limekuja wazi. Katika Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash’ariy, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akipiga takbiyr, nanyi pigeni takbiyr, na akisema غير المغضوب عليهم ولا الضالين basi semeni: “Aamiyn, Allaah Atakupendeni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (404), Abu Daawuud (972), An-Nasaaiy (2/196) na Ibn Maajah (901)].

 

Na hii pia ni kwa ajili ya kwenda pamoja kwa “Aamiyn” ya imamu, maamuma na Malaika, na hapo wakapata maghfirah kwa Idhni ya Allaah Mtukufu.

 

· Ni Karaha Imamu Kurefusha Swalaah Kama Itakuwa Ni Uzito Kwa Baadhi Ya Maamuma

 

Imepokelewa toka kwa Abu Mas-’oud akisema: “Mtu mmoja alisema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi ninajichelewesha sana na Swalaah ya Alfajiri kwa kuwa fulani huirefusha sana. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakasirika, sikumwona akiwa ameghadhibika sehemu yoyote kama alivyokuwa ameghadhibika siku hiyo. Kisha akasema: ((Enyi watu! Hakika miongoni mwenu wapo wenye kuwakimbiza watu. Basi yeyote atakayeswalisha watu, basi afupishe Swalaah, kwani nyuma yake yuko mdhoofu, mzee na mwenye jambo linalomsubiri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (704) na Muslim (466)].

 

Na mtu yule aliposwali nyuma ya Mu’aadh na Mu’aadh akasoma Al-Baqarah au An-Nisaai, alikwenda kulalamika kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Rasuli akasema: ((Ee Mu’aadh! Je, unawakimbiza watu wewe? –mara tatu- Kwa nini usiswalishe kwa سبح اسم ربك na والشمس وضحاها na والليل إذا يغشى )). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (705) na Muslim (465)].

 

Ninasema: “Na hii ni kama inakuwa ni uzito kwa baadhi ya maamuma. Ikiwa imamu atajua kwamba wameridhika na urefushaji, basi hakuna ukaraha. Makusudio kiujumla, ni imamu kuchunga hali ya maamuma wake. Katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar ni kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamuru kukhafifisha Swalaah, naye hutuswalisha kwa kusoma As-Swaaffaat.” [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/95), Ahmad (2/26) na wengineo].

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samura akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah kama mnavyoswali Swalaah zenu hivi leo, lakini yeye alikuwa akikhafifisha. Swalaah yake ilikuwa ni nyepesi zaidi kuliko Swalaah yenu. Alikuwa anasoma katika Swalaah ya Alfajiri Al-Waaqiah au Suwrah nyinginezo mfano wake”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/104), Ibn Khuzaymah (531), ‘Abdul Razzaaaq (2720) na wengineo].

 

Ibn Mas-’oud amezitaja Suwrah ishirini za Al-Mufasswal. Anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakutanisha kati yake Suwrah mbili katika kila rakaa”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (775) na Muslim (722)].

 

Hivyo basi, kidhibiti cha kurefusha au kufupisha Swalaah ni hali ya maamuma na ridhaa yao, pamoja na kuitimiliza Swalaah bila ya kupunguza nguzo yake yoyote. Anas amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifupisha Swalaah na kuitimiliza”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (706) na Muslim (469)].

 

Na anasema tena: “Sikuswali kamwe nyuma ya imamu yeyote mwenye kukhafifisha zaidi na mwenye kuitimiliza Swalaah zaidi kuliko Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hakika alikuwa anaposikia mtoto analia, hukhafifisha kuchelea mama yake kubabaika”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (708) na Muslim (469)].

 

· Kumkumbusha Imamu Kama Kisomo Kitamkanganya

 

Kama kisomo kitamkanganya imamu, basi maamuma ana wajibu wa kumkumbusha. Jamhuri imelipendelea hilo kutokana na Hadiyth ya Al-Masuur bin Yaziyd Al-Asadiy Al-Maalikiy aliyesema: “Nilimshuhudia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma kwenye Swalaah, kisha akaacha kitu hakukisoma. Mtu  mmoja akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Umeacha Aayah kadha wa kadha. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Mbona usinikumbushe?!)). [Hadiyth Hasan kwa mwega wa  nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (907), Al-Bukhaariy katika “Sehemu ya Kisomo” (194) na Ibn Khuzaymah (1648). Ina Hadiyth mwenza].

 

Hili pia linatolewa ushahidi na Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ambapo alisoma na kutatizikiwa. Alipomaliza alimuuliza Ubayya: ((Umeswali nasi?)) Akajibu: Na’am. Akamwambia: ((Nini kilikuzuia?)). [Hadiyth Hasan kwa mwega wa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (907), Ibn Hibaan (1/316-Ihsaan) kwa Sanad Hasan. Abu Haatim ameiweka sawa irsali yake (1/77), na inatolewa ushahidi na iliyo kabla yake].

 

· Angalizo

 

Imamu akikosea katika usomaji, haitakikani kumrekebisha isipokuwa kama kosa litakuwa ni lenye kubadili maana. Imepokelewa toka kwa Ubayya bin Ka’ab ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Mimi nimesomeshwa Qur-aan kwa lahaja saba, hakuna kati yake isipokuwa ni bainifu na toshelezi. Nikisema: Ghafuwran Rahiyman, au nikasema: Samiy-’an ‘Aliyman, au nikasema: ‘Aliyman Samiy-’an, basi Allaah Yuko hivyo, madhali Aayah ya adhabu haikumaliziwa kwa rahma, au Aayah ya rahma kwa adhabu)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/41, 51), Abu Daawuud (1477) na Adh-dwiyaau katika Al-Mukhtaarah (1173)].

 

· Ni Karaha Kwa Maamuma Kufanyiana Tashwishi Kwa Kisomo Na Takbiyr

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaaa ‘itikaaf Msikitini akawasikia wakisoma kwa sauti. Akafunua pazia na kuwaambia: ((Jueni kwamba kila mmoja wenu ni mwenye kumnong’oneza Mola wake, basi msiudhiane nyinyi kwa nyinyi, wala baadhi yenu wasisome kwa sauti za juu zaidi kuliko wenzao.)) Au akasema: ((Katika Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh Bitwuruqihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1332), Ahmad (3/94) na wengineo. Angalia As-Swahiyhah (1597, 1603)].

 

Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn imeelezwa katika milango iliyopita kuhusiana na mtu aliyesoma nyuma yake سبح اسم ربك الاعلى , na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Hakika nilidhani baadhi yenu watanipokonya Suwrah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (398) na wengineo. Imeelezwa nyuma kidogo].

 

· Wajibu Wa Kumfuata Imamu Na Uharamu Wa Kumtangulia

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: ((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe. Akipiga takbiyr, basi  nanyi pigeni takbiyr, akirukuu nanyi rukuuni, na akisema: Sami’a Allaahu liman hamidah, basi semeni: Rabbaanaa walakal hamdu, akisujudu nanyi sujuduni. Na akiswali kwa kukaa, nanyi nyote swalini kwa kukaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (734) na Muslim (414, 416)].

 

Na katika tamshi la Muslim: ((Msimtangulie imamu, akipiga takbiyr basi pigeni takbiyr…)). Hadiyth

 

Na imepokelewa vile vile toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hivi haogopi mmoja wenu akinyanyua kichwa chake kabla ya imamu, Allaah kukigeuza kichwa chake kuwa cha punda, au Allaah kuifanya sura yake sura ya punda?!)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (691) na Muslim (427)].

 

Hadiyth hizi zinaonyesha kwamba ni haramu kumtangulia imamu katika Swalaah. Jamhuri wanasema kwamba Swalaah ya mwenye kumtangulia imamu ni sahihi lakini anakuwa ni mwenye kupata madhambi. Ahmad na Ahlu Adh-Dhwaahir wamesema kwamba Swalaah yake itabatilika. Pia Ibn ‘Umar kasema hivyo hivyo. [Fat-hul Baariy (2/215)].

 

· Pia Haijuzu Kwenda Naye Sambamba

 

Imepokelewa na Al-Barraai akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposema: Sami’a Allaahu liman hamidah, hainamishi yeyote kati yetu mgongo wake mpaka Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awe ameteremka na kusujudu, kisha tunaporomoka kusujudu baada yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (690) na Muslim (474)].

 

Ama kuachwa nyuma na imamu, ikiwa itakuwa kwa udhuru kama ugonjwa na mfano wake, basi hakuna ubaya. Na kama mtu atafanya makusudi kujichelewesha, basi inakuwa ni makruhu. Baadhi ya Maulamaa wamesema kuwa ikiwa ataachwa na imamu kwa zaidi ya nguzo moja, basi Swalaah yake ni batili kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe)). Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

· Je, Imamu Atafuatwa Kama Kazidisha Katika Swalaah?

 

Ni kama imamu kusahau akaenda rakaa ya tano na maamuma wakampigia tasbiyh asiwajali akiwa na uhakika kwamba hakusahau. Kwa hili, Sheikh wa Uislamu amesema: “Ikiwa watasimama pamoja naye bila kujua, basi Swalaah zao hazitabatilika. Lakini ikiwa watajua, basi haitakikani kumfuata, bali watamsubiri mpaka atakapokuja kutoa tasliym pamoja nao, au watatoa tasliym kabla yake, lakini kumsubiri ni bora zaidi.”

 

Ninasema:

 

“Mtu anaweza kusema: Watamfuata kutokana na ujumuishi wa dalili zenye kuamuru kumfuata, na kwa vile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliponyanyuka kwenda rakaa ya tano, Maswahaba walisimama na Rasuli hakuwaamuru wakae kama imamu atasimama kwenda rakaa ya tano. Suala hapa ni ijtihaad tu, basi nawe tafiti. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

Imamu Akiswali Kwa Kukaa Kutokana Na Udhuru

 

Tumeshaeleza nyuma kwamba inaswihi mtu mzima wa afya kumfuata mgonjwa. Ikiwa watu wenye kuweza kusimama wataswalishwa na imamu aliyekaa kutokana na udhuru, je watasimama au watakaa? Maulamaa wana kauli mbili katika suala hili:

 

Ya kwanza:

 

Ni lazima na wao pia waswali kwa kukaa. Ni kauli ya Ahmad, Is-Haaq, Al-Awzaa’iy, Ibn Al-Mundhir, Daawuud na Ibn Hazm. Ni kauli iliyosimuliwa toka kwa Jaabir, Abu Hurayrah, Usayd bin Khudhayr na Qays bin Fahd. Kwa upande wao, hakuna Swahaba yeyote aliyejulikana kwenda kinyume na hilo. [Al-Mughniy (2/162), Al-Furu’u (2/578), Al-Awsatw (4/205), Al-Muhalla na Naylul Awtwaar (3/203)].

 

Wametoa dalili kwa haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali nyumbani kwake akishtakia kuumwa, akaswali kwa kukaa, na watu nyuma yake wakaswali kwa kukaa. Aliwaashiria wakae, na alipomaliza alisema: ((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe. Akirukuu nanyi rukuuni, na akinyanyuka, nanyi nyanyukeni. Na akiswali kwa kukaa, basi nanyi swalini kwa kukaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (688) na Muslim (412)].Kuna Hadiyth ya Anas na Abu Hurayrah kama hii.

 

2- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Rasuli wa Allaah alishtakia kuumwa tukaswali nyuma yake akiwa amekaa huku Abu Bakr akiwasikilizisha watu takbiyr yake. Akatugeukia akatuona tumesimama, akatuashiria, tukakaa na tukaswali nyuma yake kwa kukaa. Alipotoa tasliym alisema: ((Mmekurubia hivi punde kufanya kitendo cha Wafursi na Warumi. Wanawasimamia wafalme wao wakiwa wamekaa, basi msifanye. Wafateni maimamu wenu. Akiswali kwa kusimama, basi swalini kwa kusimama, na akiswali kwa kukaa basi nanyi swalini kwa kukaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (413), Abu Daawuud (606), An-Nasaaiy (3/9) na Ibn Maajah (1240)].

 

Ya pili:

 

Haijuzu wao kuswali kwa kukaa, bali wataswali kwa kusimama. Kauli hii imeungwa mkono na wengi akiwemo Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy. [Fat-hul Qadiyr (1/261), Al-Mabsuutw (1/218), Sharhul Ma’aaniy (1/406), Al-Ummu (1/151), Al-Majmu’u (4/164), Al-Ihkaam cha Ibn Daqiyq Al-’Abdu (1/225) na Twarhu At-Tathriyb (2/334)].

 

Dalili zao ni:

 

1- Kujibu dalili za wa kauli ya kwanza. Hapa wao wana njia tatu:

 

(a) Dai la kuwa Hadiyth hizo ni mansukh. Iliyozinasikhi ni Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusu Abu Bakr kuwaswalisha watu wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa mgonjwa. Hadiyth inasema: “Kisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijihisi kidogo nafuu, akatoka kwa ajili ya Swalaah ya Adhuhuri akiwa kati ya watu wawili, mmoja wao akiwa ‘Abbaas. Abu Bakr alikuwa anawaswalisha watu, na Abu Bakr alipomwona, alianza kurudi nyuma, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwashiria kwamba asirudi na kusema: Niketisheni pembeni yake, nao wakamkalisha pembeni ya Abu Bakr. Abu Bakr akaanza kuswali akimfuata Rasuli (akiwa amesimama), na watu wakimfuata Abu Bakr, huku Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amekaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (687) na Muslim (418)].

 

Wamesema: “Na hili lilikuwa katika maradhi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyofia. Na Abu Bakr aliswali nyuma yake na watu wakiwa wamesimama, na hii inaonyesha kwamba hukmu ya mwanzo imenasikhiwa”.

 

Hili limejibiwa kwa njia hizi zifuatazo:

 

1- Ni kwamba Abu Bakr alikuwa ndiye imamu na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefungamanishwa naye kama ilivyo kwenye baadhi ya riwaya. Hili limeandamizwa kwa kusemwa kwamba riwaya hizi lau kama zingelikuwa ni sahihi, basi lingechukuliwa kwa Swalaah nyingi, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliugua kwa muda wa siku kumi na mbili zenye jumla ya Swalaah 60.

 

2- Imamu Ahmad kasema: “Hakuna ndani yake hoja, kwa kuwa Abu Bakr alikuwa ameianza Swalaah akiwa amesimama. Na kama aliianza kwa kusimama, basi nao waliswali kwa kusimama. Akaashiria kuoanisha kati ya Hadiyth mbili kwa kuichukulia Hadiyth ya kwanza kwamba aliianza Swalaah kwa kukaa, na kuichukulia Hadiyth ya pili kwamba aliianza Swalaah kwa kusimama, halafu akaishiwa nguvu za kusimama akakaa. Anasema: Pale itakapowezekana kuoanisha kati ya Hadiyth, basi itakuwa ni wajibu, na naskh haitokuwepo.

 

Hili limeandamiziwa kwa kusemwa kwamba linajibiwa na yaliyoko kwenye Hadiyth ya Jaabir na ya ‘Aaishah ambapo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaashiria Maswahaba wake wakae baada ya kuwa wameanza Swalaah kwa kusimama. Uandamizi huu umejibiwa kwa kusemwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameianza Swalaah kwa kukaa, na wao iliwalazimu wakae kwa kukaa kwake kinyume na kumfuata kwao Abu Bakr, kwani imamu wao huyu, aliianza Swalaah kwa kusimama, hivyo iliwalazimu kusimama, na wakaendelea kusimama.

 

3- Ni kwamba hamna ndani ya Hadiyth linaloashiria kwamba watu walikuwa wamesimama na Abu Bakr amekaa. Pengine wao ndio walikuwa wamekaa. Linaloonyesha hilo ni kwamba watu walikuwa wakiifuata Swalaah ya Abu Bakr, na kama wangekuwa wamesimama, basi wasingeliifuata Swalaah yake isipokuwa safu ya kwanza, kwa kuwa safu hii itakuwa imezikinga safu nyingine zisimwone. Haya kayasema Ibn Hazm.

 

Al-‘Iraaqiy kaliandamiza hili kwa njia kadhaa. Kati yake ni kwamba Maswahaba waliianza Swalaah kwa kusimama nyuma ya Abu Bakr. Na mwenye kudai kwamba waliibadili hali hii, basi na alete dalili. Na kama hilo lingefanyika, basi lingenukuliwa bila shaka. Kasema pia kwamba muradi wa wao kumfuata Abu Bakr, ni kuifuata sauti yake na si kwa kumwona.

 

4- Tukichukulia kwa nadharia tete kwamba imethibiti kuwa Maswahaba waliswali kwa kusimama nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku yeye akiwa amekaa, basi hilo haliarifu naskh, bali linaarifu kuruhusika hilo tu na kubainisha kwamba agizo la kuwaamuru wakae, ni agizo la Sunnah na si agizo la wajibu.

 

Hili limejibiwa kwa kusemwa: Hili linakataliwa. Amri haiwi ya Sunnah ikiwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameisisitizia kwa kuiashiria akiwa kwenye Swalaah, pia akaizungumzia kwa maneno ya wazi baada ya tasliym, na kisha akakifananisha kitendo chao na kitendo cha makafiri wa kimajusi. Vielelezo vyote hivi vinaonyesha kwamba katazo ni la uharamishaji.

 

(b) Dai la kuwa hilo linamhusu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake. Na hili ndilo mashuhuri katika kauli ya Maalik na kundi la Maswahibu zake. [Kwa ajili ya hili, madhehebu ya Maalik yanasema kwamba Swalaah ya mwenye kuweza kusimama haiswihi asilani akiswalishwa na imamu aliyekaa. Angalia Al-Mudawwanah (1/81) na Mawaahibul Jaliyl (2/97)].

 

Wameitilia nguvu kwa yaliyosimuliwa kwa njia Marfu’u katika Hadiyth iliyofanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaraqutwniy ambayo isnadi yake ni mbovu: ((Asiswalishe tena yeyote baada yangu kwa kukaa)), na kwamba hakuna Khalifa yeyote aliyeswalisha watu kwa kukaa!!

 

Limejibiwa hili kwamba asili ni kuwa umahususi unakuwa haupo mpaka iwepo dalili ya kuuthibitisha, na Hadiyth iliyosimuliwa ni Dhwa’iyf, haifai. Ama kutoa dalili ya Makhalifa kutoswalisha kwa kukaa, dalili hiyo ni dhwa’iyf zaidi, kwani kuacha kitu hakuonyeshi kwamba ni haramu, na huenda wao walitosheka kuwatanguliza watu wenye kuweza kusimama kuswalisha.

 

(c) Kuliawilisha neno lake: ((Basi swalini kwa kukaa)) wakisema: “Linachukuliwa kwa maana ya: Akikaa kwa tashah-hudi, basi nanyi kaeni kwa tashah-hudi!!

 

Limejibiwa kwamba huku ni kuipindisha habari na kuitoa nje ya ujumuishi wake bila dalili, na konteksi ya Hadiyth inamzuia aliyekwishafahamu kukimbilia kwenye taawiyl hii. Kati ya vyenye kuzuia, ni Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwapa ishara ya kukaa, na pia kuwaelezea sababu ya kujifananisha na hilo na makafiri wa kimajusi.

 

2- (Kati ya dalili za wenye kupinga maamuma kuswali kwa kukaa) ni kwamba kusimama ni nguzo kwa maamuma mwenye kuiweza. Haijuzu kuiacha kama zilivyo nguzo nyinginezo.

 

3- Kila mmoja miongoni mwao ana faradhi yake. Faradhi ya imamu ni kukaa, na faradhi ya maamuma ni kusimama.

 

· Hoja Yenye Nguvu Katika Suala Hili

 

Hakuna shaka yoyote kwamba kauli zote mbili zina uzito wa kuzingatika ingawa kauli ya kwanza ndiyo yenye uzito zaidi pamoja na kuzingatiwa hali ya imamu wakati anapoanza Swalaah. Kama ataianza kwa kukaa, basi ni lazima maamuma wakae, na kama ameianza kwa kusimama, itawalazimu kusimama. Lakini kama atalazimika kukaa kutokana na udhuru, je watakaa au watasimama? Hapa ni mahala pa ijtihaad, ingawa sababu ya kujifananisha na Wafursi na Warumi inatilia nguvu kukaa kwao.

 

Ama kukimbilia kwenye naskh, mimi hili silioni kama ni lenye nguvu kutokana na baadhi ya miono iliyotangulia, na kwa kuwa kulisema hilo kunahitajia naskh mara mbili. Ni kuwa asili katika hukmu ya mwenye kuweza kusimama ni kuwa asiswali kwa kukaa, na kusimama kumenasikhiwa kwenda kwenye kukaa kwa yule ambaye imamu wake ameswali kwa kukaa. Hivyo dai la naskh ya kukaa baada ya hapo linahukumia kufanyika naskh mara mbili, na hili liko mbali, bali linakwenda kinyume na qaaidah ya hukmu.

 

Na dai la naskh linajibiwa vile vile ya kwamba Maswahaba wanne walilifanya hilo – inasemekana sita - na hakuna yeyote aliyelikataa kwa mujibu wa inavyojulikana kwao mpaka Ibn Hibaan akasema: “Kwangu mimi ni aina ya Ijma’a ambayo wote wamekubaliana juu ya kujuzu kwake”.

 

· Kuibalighisha Takbiyr Ya Imamu Kama Itahitajika

 

Inajuzu mtu kuibalighisha takbiyr ya imamu ikiwa hilo litahitajika. Ni kama Msikiti kuwa mkubwa na sauti ya imamu kushindwa kufika kwenye safu za mwisho. Asili ya uhalali wa hili kama litahitajika, ni kitendo cha Abu Bakr wakati alipowaswalisha watu wakati wa maradhi ya kifo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo kwenye Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Abu Bakr (Radhwiya Allaahu Anhu) akarudi nyuma, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakaa pembeni mwake, na Abu Bakr akiwabalighishia watu takbiyrah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (712) na Muslim (418)].

 

Ama kubalighisha nyuma ya imamu bila haja, hilo ni bid-’a isiyopendeza kwa makubaliano ya maimamu. [Majmu’u Al-Fataawaa cha Sheikh wa Uislamu (23/403)]. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

· Imamu Kumweka Mtu Mwingine Badali yake

 

Imamu akitokewa na udhuru ndani ya Swalaah kama kutengukwa na wudhuu au akakumbuka kwamba ana hadathi au mfano wa hilo, hapo itambidi amtangulize mtu kati ya maamuma atakayekamilisha Swalaah badala yake. Asili ya hili ni:

 

1- Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad kuhusu kisa cha kwenda Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukoo wa ‘Amri bin ‘Awf ili kusuluhisha kati yao, na Abu Bakr alipowaswalisha watu. Hadiyth inasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja na watu wanaswali. Kisha Abu Bakr akarudi nyuma mpaka akaingia sawa kwenye safu, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangulia akaswalisha…..”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (684) na Muslim (431)].

 

2- Hadiyth ya ‘Amr bin Maymoun kuhusiana na kisa cha kudungwa kisu ‘Umar akiwa ndani ya Swalaah. Hadiyth inasema: “ Na hakuchelewa ila alipiga takbiyr. Nikamsikia akisema: Ameniuwa – au amenila mbwa -, wakati alipomchoma. ’Umar akaukamata mkono wa ‘Abdul Rahman bin ‘Auf akamtanguliza. Na ‘Abdul Rahmaan akawaswalisha Swalaah khafifu..” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3700)].

 

Tukio hili lilikuwa mbele ya Maswahaba, nao waliridhia ‘Umar kumtanguliza ‘Abdul Rahmaan badala yake ili akamilishe nao Swalaah. Hakuna yeyote aliyelipinga hilo, na hivyo limekuwa ni Ijma’a.

 

3- Imepokelewa toka kwa Khalid bin Al-Lajlaaj ya kwamba siku moja ‘Umar bin Al-Khattwaab aliwaswalisha watu. Na alipokaa kwenye rakaa mbili za mwanzo, alirefusha kikao. Na alipoanza kunyanyuka, alirejea nyuma, akaukamata mkono wa mtu mmoja kati ya maamuma na kumtanguliza mahala pake. [Isnadi yake ni laini: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Al-Mundhir katika Al-Awsatw (4/241) na Al-Bayhaqiy (3/114)].

 

Akaeleza kwamba alimpitia mmoja wa wakeze, kisha akauhisi umajimaji ndani ya Swalaah.

 

4- Imepokelewa toka kwa Abu Raziyn akisema: “ ‘Aliy alituswalisha kisha damu ya pua ikamtoka. Akamkamata mtu akamtanguliza, naye akarudi nyuma”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (3670), Ibn Al-Mundhir (4/242) na Al-Bayhaqiy (3/114)].

 

· Hapa Kuna Mas-ala Mawili:

 

(a) 

Aliyekamata mahala pa imamu, je ataitimiza Swalaah yake yeye au Swalaah ya imamu wake aliyemtanguliza?  [Angalia Al-Muhalla cha Ibn Hazm (4/220)].

 

Faida ya mas-ala haya inadhihiri pale mwenye kuchukua mahala pa imamu atakapokuwa ametanguliwa kwa rakaa moja kwa mfano kisha akakamata nafasi ya imamu katika rakaa ya pili. Linaloonekana kuwa na nguvu zaidi ni kuwa ataikamilisha rakaa hiyo ya pili pamoja nao, kisha anapomaliza kusujudu sijdah mbili, atawaashiria wakae, halafu yeye atasimama kwenda rakaa yake ya pili. Anapoitimiza, atakaa na kusoma tashah-hudi, halafu atasimama, na maamuma watasimama pamoja naye ili kukamilisha rakaa mbili zilizosalia, au rakaa moja kama Swalaah ni ya Magharibi. Na ikiwa Swalaah ni ya Alfajiri, atafanya hivyo hivyo kwa kutoa tasliym pamoja nao.

 

Abu Haniyfah na Maalik wamesema: “ Bali atawaswalisha Swalaah ya imamu wa kwanza. Kuweka wazi hili ni kuwa ataswali nao rakaa yake ya kwanza (ambayo ni ya pili kwao), kisha atakaa tashah-hudi juu ya hukmu ya Swalaah ya imamu wa kwanza!! Kisha atakamilisha nao Swalaah.

 

Na hapa kuna angalizo. Ni kuwa imamu wa kwanza aliyetoka, uimamu wake ushabatilika na maamuma watakuwa wanamfuata imamu mpya, na imamu huyu haswali isipokuwa Swalaah yake mwenyewe. Hivyo watamfuata katika lile linalowalazimu, na hawatamfuata katika lile lisilowalazimu, na watasimama pale walipofikia na watamngoja mpaka afikie pale walipofikia wao, halafu hapo watamfuata. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

(b)

Imamu akiwaswalisha watu kisha akakumbuka kwamba alikuwa na hadathi baada ya kumaliza Swalaah

 

Jamhuri akiwemo Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Abu Thawr, Al-Mazniy na wengineo wamesema kwamba yeye ataswali tena lakini maamuma hawataswali. Lakini kundi jingine akiwemo Abu Haniyfah na Maswahibu zake, Ath-Thawriy na wengineo wamesema kwamba wote wataswali tena upya.

 

Kauli ya kwanza ya Jamhuri ndiyo yenye nguvu zaidi, nayo imesimuliwa toka kwa ‘Umar, mwanawe ‘Abdullah, ‘Uthmaan na ‘Aliy. [Al-Awswat cha Ibn Al-Mundhir (4/212)]

 

 

Share