050-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Adhana Ya Ijumaa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
050-Adhana Ya Ijumaa
· Adhana Khatibu Anapokaa Juu Ya Mimbari
Imepokewa toka kwa As-Saaib bin Yazid akisema: “Mwanzo wa adhana ya Siku ya Ijumaa ulikuwa wakati imamu anapokaa juu ya mimbari Siku ya Ijumaa wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakri na ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhum). Ulipokuwa ukhalifa wa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu Anhu) – na watu wakaongezeka – ‘Uthmaan aliamuru adhana ya tatu Siku ya Ijumaa, nayo ikaadhiniwa hapo Az Zawraa, na jambo likathibiti hivyo. Watu hawakumkosoa kwa hilo, lakini walimkosoa aliposwali Swalaah kamili Mina”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (916), Abu Daawuud (1087), At-Tirmidhiy (516), An-Nasaaiy (3/101) na Ibn Maajah (1135)].
Katika Hadiyth hii kuna faida mbili:
Ya kwanza: Kwamba adhana Siku ya Ijumaa inakuwa baada ya imamu kukaa juu ya mimbari.
Ya pili: Kwamba Sunnah ni adhana moja tu kwa Ijumaa wakati imamu anapokaa. Ama kitendo cha ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu Anhu), si vizuri kukifuata katika wakati wetu wa sasa. Yeye aliongeza adhana ya kwanza kwa sababu ya kimantiki, nayo ni kuongezeka watu na nyumba zao kuwa mbali na Msikiti wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alitaka kuwajulisha kuingia wakati wa Swalaah kama ilivyo kwa Swalaah nyingine za Faradhi. Akaijumuisha adhana hiyo na Ijumaa na akaubakisha umahususi wake na adhana baada ya khatibu kukaa. Basi yeyote ambaye hakuitizama sababu hii na akashikamana na adhana ya ‘Uthmaan kibubusa, basi hawi ni mwenye kumfuata Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali anakuwa ni mwenye kumkhalifu, kwa kuwa hakutizama kwa jicho la mazingatio sababu hiyo ambayo lau kama isingelikuweko, basi ‘Uthmaan asingeiongezea juu ya Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake wawili.
Na ni jambo lililo wazi kabisa kwamba ujulisho wa kuingia wakati wa Swalaah katika zama yetu ya sasa unapatikana bila kuongeza adhana hii, kwani mtu anaweza kusikia adhana ya Ijumaa baada ya kila mita chache anazotembea zikitokea Misikiti mbalimbali yenye vipaza sauti, pamoja na watu wengi kuwa na saa za kutegesha wakati na mfano wake.[Angalia Al-Ajwibat An-Naafi’at cha Al-Albaaniy Allaah Amrehemu uk. 28].
Pamoja na yote haya, Ibn ‘Umar alikuwa akimkosoa ‘Uthmaan kwa adhana ya kwanza akisema: “Hakika Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anapanda mimbari, Bilaal huadhini, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapomaliza khutba huqimu Swalaah. Na adhana ya kwanza ni bid-’a”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/48)].
Kiufupi, kama itapatikana sababu ya kuwepo adhana ya ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu Anhu), basi itafanywa kwa haja na maslaha. Lakini kama hakuna, basi Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake wawili isipetukwe. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
· Adhana Ya Ijumaa Ina Nyakati Mbili:
(a) Baada ya kupinduka jua na imamu kukaa juu ya mimbari
Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba wakati wa Ijumaa na wakati wa Adhuhuri, ni baada ya jua kupinduka kwa kuwa Ijumaa ni badala ya Adhuhuri!!. Iispokuwa tu wao wamependelea iwahishwe mwanzo wa wakati wake baada ya kupinduka jua. Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya Salamah bin Al-Akwa’a aliyesema: “Tulikuwa tunaswali Ijumaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jua linapopinduka, kisha tunarejea kukifuatilia kivuli”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4168) na Muslim (860)].
2- Hadiyth ya Anas: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali Ijumaa wakati jua linapopinduka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (903), Abu Daawuud (1084), At-Tirmidhiy (503) na Ahmad (3/128)].
(b) Kabla ya kupinduka jua anapokaa imamu juu ya mimbari
Imaam Ahmad ameujuzisha wakati huu na ameutolea dalili kwa Hadiyth mbili zilizotangulia. Udhahiri wake ni kuwa Swalaah ndiyo iliyokuwa ikiswaliwa wakati jua linapopinduka, na adhana ilikuwa ni kabla yake. Hadiyth hizo mbili zimewekwa wazi na..
3- Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullaah aliyesema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali Ijumaa, kisha tunakwenda kwa ngamia wetu, tunawapumzisha wakati jua linapopinduka, yaani kuwanyunyizia maji”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (858), An-Nasaaiy (3/100) na Ahmad (3/331)].
Kuna athari nyingi Swahiyh toka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaahu Anhum) zinazotaarifu kujuzu adhana kabla ya jua kupinduka. Kati ya athari hizo ni:
4- Imepokelewa toka kwa Abu Raziyn amesema: “Tulikuwa tunaswali Ijumaa pamoja na ‘Aliy. Wakati mwingine tunakikuta kivuli cha kupinduka jua, na wakati mwingine hatukikuti”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/18)].
5- Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Salamah akisema: “‘Abdullaah (yaani: Ibn Mas-’oud) alituswalisha Ijumaa wakati wa Dhuhaa na akatuambia: Nimewaogopeeni joto”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/17). Kuna maneno kuhusu huyu ‘Abdullah bin Salamah, lakini riwaya yake haifanyiwi hofu kwa matukio aliyoyahudhuria na kuyashuhudia].
6- Imepokelewa toka kwa Bilaal Al-‘Absiy: “Kwamba ‘Ammaar aliwaswalisha watu Ijumaa na watu wako makundi mawili. Baadhi wanasema jua limepinduka, na wengine wanasema halijapinduka”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/18)].
7- Imepokelewa toka kwa Sammak bin Harb akisema: “ An-Nu’umaan bin Bashiyr alikuwa akituswalisha Ijumaa baada ya jua kupinduka”. [Isnadi yake ni Hasan: Al-Bukhaariy ameitaja ishara (2/449), na Ibn Abu Shaybah ameiunga (2/18)].
· Ni Marufuku Kuuza Baada Ya Adhana Ya Ijumaa
Ni kwa Neno Lake Ta’alaa:
(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))
(( Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah Siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua)). [Al-Jum-‘ah (62:9)]
Na katazo kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa, linajumuisha kuuza, kufunga ndoa na mikataba mingineyo. Mahanbali wamesema na kuungwa mkono na Ibn Hazm kwamba mengine yote hayakatazwi isipokuwa kuuza tu.
Na je inafaa kuuza baada ya adhana? Kuna kauli mbili za Maulamaa zilizojengewa juu ya msingi wa kwamba je katazo linahukumia kutohalalika mauzo au kuhalalika? Jamhuri wanasema kwamba mauzo ni halali, kwa kuwa katazo halimo ndani ya mauzo yenyewe, bali nje yake, kwa kuwa yakifanyika yatamzuia mtu asiende Ijumaa. Hivyo mauzo kiasili ni halali lakini yanakuwa na ukaraha wa tahriym.
Ni mashuhuri kwa Maalik na Hanbali kwamba mauzo hayafai na hayakubaliki.