052-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Wanayotakiwa Kuyafanya Maamuma Wakati Wa Khutbah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
052-Wanayotakiwa Kuyafanya Maamuma Wakati Wa Khutbah
1- Wajisogeze karibu na khatibu
Imepokelewa toka kwa Samrah bin Jun-dub ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hudhurieni khutbah, na mkurubieni khatibu, kwani hakika mtu hatoacha kujiweka mbali mpaka awekwe nyuma peponi hata kama ataingia)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1108) na wengineo].
Na imepokewa toka kwa Aws bin Aws toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuoga Siku ya Ijumaa na akasafisha kichwa chake, akatoka mwanzo wa wakati na akawahi mwanzo wa khutbah, na akatembea kwa miguu asipande kipando, na akawa karibu na imamu, na akasikiliza na kunyamaza, basi anapata kwa kila hatua amali ya mwaka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (345), At-Tirmidhiy (496), An-Nasaaiy (3/95) na Ibn Maajah (1087)].
2- Wamwelekee khatibu kwa nyuso zao wakati anapotoa khutbah
Imesuniwa maamuma wamwelekee khatibu wakati anapokhutubu kwa nyuso zao. Hili halina uthibitisho wowote sahihi uliorufaishwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini imethibiti toka kwa Ibn ‘Umar ya kwamba imamu alikuwa hakai isipokuwa yeye humwelekea. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5391), na kwa njia ya Ibn Al-Mundhir (4/74) na Al-Bayhaqiy (3/199)].
Na imepokelewa toka kwa Anas ya kwamba yeye alikuja Siku ya Ijumaa, akaegemea ukutani, na akamwelekea imamu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/118), na Ibn Al-Mundhir toka kwake (4/74)].
At-Tirmidhiy kasema (2/283): “ Hili walilifanya Maulamaa katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengineo; walikuwa wakipendelea kumwelekea imamu wakati anakhutubu”.
3- Waisikilize khutbah na wasizungumze wakati inaendelea
Tumeeleza katika Hadiyth ya Salmaan kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haogi mtu Siku ya Ijumaa, kisha akanyamaza wakati imamu anakhutubu, isipokuwa hughufiriwa yaliyo kati yake na Ijumaa nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa nyuma kidogo].
Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukimwambia mwenzako nyamaza Siku ya Ijumaa na imamu anakhutubu, basi umejiharibia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (934) na Muslim (851)].
Na katika Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake ikiwa Marfu’u: (( Na aliyejiharibia, na akaziruka shingo za watu, basi thawabu zake ni nakisi)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (347) na Ibn Khuzaymah (1810)].
Jamhuri ya Maulamaa wameharamisha watu waliohudhuria khutbah kuzungumzishana.
Faida Mbili:
Ya kwanza:
Ikiwa baadhi ya hadhira wataongea, basi inajuzu kuwanyamazisha kwa ishara. Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama anakhutubu siku moja juu ya mimbari, mtu mmoja alisimama na kusema: Lini kitasimama Qiyaamah ee Nabii wa Allaah? Rasuli hakumjibu, na watu wakamwashiria akae, naye akakataa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6167), Ibn Al-Mundhir (1807) na Ibn Khuzaymah (1796)].
Ninasema: “Kumjibu aliyetoa salaam hujumuishwa na hili pia, hakuwi ila kwa kuashiria”.
La pili:
Inajuzu kuzungumza na khatibu wakati anakhutubu kwa haja, sawasawa kwa kuanza kumsemesha au kumjibu kama atamsemesha mtu. Anas amesema katika Hadiyth: “Bedui mmoja wa majangwani alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anakhutubu Siku ya Ijumaa na kusema: Ee Rasuli wa Allaah! Mifugo imeangamia”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa Swalaah ya kuomba mvua].
Na katika kisa cha Sulayk Al-Ghatwafaaniy, alipoingia Msikitini akakaa – na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakhutubu -, Rasuli alimuuliza: ((Je, umeswali rakaa mbili?)). Akasema: Hapana. Akamwambia: ((Simama uswali rakaa mbili)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishaelezwa].
4- Mtu asiziruke shingo za watu wala asitenganishe kati ya watu wawili
Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Bisr akisema: “Alikuja mtu mmoja akiziruka shingo za watu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Kaa. Hakika umewaudhi watu na umechelewa)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1118), An-Nasaaiy (3/103) na Ahmad (4/188)].
Na pia Hadiyth ya ‘Abdullah bin ‘Amri tuliyoielezea: (( Na aliyejiharibia, na akaziruka shingo za watu, basi thawabu zake ni nakisi)). [Hadiyth Hasan: Imetajwa nyuma kidogo].
Makamio haya hayatamgusa mtu aliyekuta mwanya kati ya watu wawili, kwa kuwa uzembe umefanywa na wao, na mrukaji hatakuwa na makosa. Pia kwa aliyepatikana na haja ikabidi atoke, kisha akataka kurudi kwenye nafasi yake.
Katika Hadiyth Marfu’u ya Salmaan: “ Kisha akaenda na asiingie kati ya watu wawili, halafu akaswali aliyoandikiwa, kisha imamu anapotoka akasikiliza, basi hughufiriwa yaliyo kati yake na Ijumaa nyingine”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma kidogo].
Kutenganisha kati ya wawili inakuwa ni pamoja na kukaa kati yao, au kumtoa mmoja wao na kukaa mahala pake. Pia kunaweza kuwa kwa kuwaruka tu, na ziada iliyopo katika urukaji huu, ni kunyanyua miguu juu ya vichwa vyao na mabega yao.
5- Mtu asimsimamishe mtu na kukaa mahala pake
Imepokelewa toka kwa Jaabir toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Kamwe asimsimamishe mmoja wenu mtu Siku ya Ijumaa, kisha aende yeye akakae mahala pake, lakini aseme: Fungueni nafasi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2177), Ahmad (3/295), na kama hii hii katika Swahiyh Mbili toka kwa Ibn ‘Umar].
Kusema: “Fungueni nafasi”, ni pale wakati khatibu bado hajaanza kuzungumza, na kama ameanza basi ni kwa ishara.
6- Akisinzia basi akakae sehemu nyingine
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Akisinzia mmoja wenu [katika majilisi yake Siku ya Ijumaa], basi ahame toka majilisi yake [kwenda kwingine])). [Hadiyth Hasan kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1119), At-Tirmidhiy (526), Ahmad (2/22) na wengineo].
Hikma ya kubadilisha sehemu ni kwamba msogeo huondosha usingizi. Pia yawezekana hikma ikawa ni kuihama tu sehemu ambayo mghafala umempata kwa kulala, ingawa mlalaji hana makosa. [Naylul Awtwaar (3/298)].
7- Je, inajuzu “Al-Ihtibaa” wakati wa khutbah?
“Al-Ihtibaa” ni kuisimamisha miundi miwili na kuizungushia nguo, au kuifumbata mikono miwili juu ya magoti na kuyafanya mhimili wa kujiegemezea. Ibn Al-Athiyr amesema: “Hilo limekatazwa kwa kuwa kikao hiki huleta usingizi na kumfanya mtu asiisikie khutbah mbali na kuhatarisha uvunjifu wa wudhuu wake”.
Imesimuliwa toka kwa Mu’aadh bin Anas toka kwa baba yake: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza “Al-Ihtibaa” Siku ya Ijumaa na imamu anakhutubu”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1110), At-Tirmidhiy (514) na Ahmad (3/439)].
Hadiyth hii ina mvutano, na kauli yenye nguvu inasema kuwa ni Dhwa’iyf”. Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wengi wameruhusu “Al-Ihtibaa”.
Ninasema: “Ikiwa ni hivyo, basi kuacha ni bora hata kama Hadiyth ni Dhwa’iyf. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
8- Akikumbuka Swalaah ya Faradhi aliyoisahau au alilala ikampita..
Atasimama na kuilipa hata kama imamu anakhutubu. Ni kwa Hadiyth ya Anas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kusahau Swalaah [au akalala ikampita], basi aiswali anapoikumbuka, haina kafara isipokuwa hilo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (597) na Muslim (684)].