19-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Swahaba Walitahadharishwa Kuporomoka ‘Amali Zao Kwa Kumwita Kwa Sauti Ya Juu
Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
19-Swahaba Walitahadharishwa Kuporomoka ‘Amali Zao Kwa Kumwita Kwa Sauti Ya Juu
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliwafunza adabu Swahaba wasimwite Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sauti ya juu. Na Akawawekea tahadharisho la kuporomoka ‘amali zao pindi wakifanya hivyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٢﴾
Enyi walioamini! Msipandishe sauti zenu juu ya sauti ya Nabiy, na wala msiseme naye kwa sauti ya juu, kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu; zisije zikaporomoka ‘amali zenu nanyi hamhisi.
Wakajaribiwa, na wao wakatii amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakawa wana khofu kuongea na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sauti ya juu hadi wengine wakawa wanaweka kijiwe mdomoni ili kiwazuie kumwita kwa sauti ya juu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ يَغُضُّونَ أَصْوَاتَهُمْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ امْتَحَنَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ لِلتَّقْوَىٰ ۚ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٣﴾
Hakika wale wanaoteremsha sauti zao mbele ya Rasuli wa Allaah, hao ndio ambao Allaah Amejaribu nyoyo zao kwa ajili ya taqwa. Watapata maghfirah na ujira adhimu.
Na mabedui nao ambao hakuwa na ustaarabu wakafunzwa adabu pia kutokumwita ovyo ovyo: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ يُنَادُونَكَ مِن وَرَاءِ الْحُجُرَاتِ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ﴿٤﴾
Hakika wale wanaokuita (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) nyuma ya vyumba, wengi wao hawatii akilini.
وَلَوْ أَنَّهُمْ صَبَرُوا حَتَّىٰ تَخْرُجَ إِلَيْهِمْ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٥﴾
Na lau kwamba wao wangelisubiri mpaka ukawatokea, bila shaka ingelikuwa ni khayr kwao. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.
[Al-Hujuraat: 1-4]