13-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Nikaah: Mlango Wa Matumizi
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلنِّكَاحِ
Kitabu cha Nikaah (Ndoa)
بَابُ اَلنَّفَقَاتِ
13-Mlango Wa Matumizi
974.
عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {دَخَلَتْ هِنْدُ بِنْتُ عُتْبَةَ اِمْرَأَةُ أَبِي سُفْيَانَ عَلَى رَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ . فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! إِنَّ أَبَا سُفْيَانَ رَجُلٌ شَحِيحٌ لَا يُعْطِينِي مِنْ اَلنَّفَقَةِ مَا يَكْفِينِي وَيَكْفِي بَنِيَّ، إِلَّا مَا أَخَذْتُ مِنْ مَالِهِ بِغَيْرِ عِلْمِهِ، فَهَلْ عَلِيَّ فِي ذَلِكَ مِنْ جُنَاحٍ ؟ فَقَالَ: "خُذِي مِنْ مَالِهِ بِالْمَعْرُوفِ مَا يَكْفِيكِ، وَيَكْفِي بَنِيكِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Siku moja Hind bint ‘Utbah[1] mke wa Abuu Sufyaan[2] aliingia kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Kwa hakika Abuu Sufyaan ni mtu bakhili mwenye tamaa, wala hanipi kinachonitosha mimi na wanangu ila ninachokichukua katika mali yake ilhali hajui, je nikifanya hivyo nina dhambi? Akasema: “Chukua kwa wema katika mali yake kinachokutosha wewe na wanao.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim]
975.
وَعَنْ طَارِقِ الْمُحَارِبِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {قَدِمْنَا اَلْمَدِينَةَ، فَإِذَا رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَائِمٌ يَخْطُبُ وَيَقُولُ: "يَدُ اَلْمُعْطِي اَلْعُلْيَا، وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ: أُمَّكَ وَأَبَاكَ، وَأُخْتَكَ وَأَخَاكَ، ثُمَّ أَدْنَاكَ أَدْنَاكَ"} رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ
Kutoka kwa Twaariq Al-Muhaaribiyy[4] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tulienda Madiynah tukamkuta Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) yuko juu ya mimbari amesimama anawahutubia watu: “Mkono wa mtoaji ni wa juu,[5] anza kwa unayemlisha: mama yako, baba yako, dada yako na ndugu yako, halafu aliye karibu nawe zaidi.” [Imetolewa na An-Nasaaiy, na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Ad-Daaraqutwniy]
976.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {لِلْمَمْلُوكِ طَعَامُهُ وَكِسْوَتُهُ، وَلَا يُكَلَّفُ مِنْ اَلْعَمَلِ إِلَّا مَا يُطِيقُ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mtumwa ana haki kwa bwana wake kupata chakula chake na nguo zake[6] wala halazimishwi kufanya kazi ila anayoiweza.” [Imetolewa na Muslim]
977.
وَعَنْ حَكِيمِ بْنِ مُعَاوِيَةَ اَلْقُشَيْرِيِّ، عَنْ أَبِيهِ قَالَ: {قُلْتُ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! مَا حَقُّ زَوْجَةِ أَحَدِنَا عَلَيْهِ ؟ قَالَ: "أَنْ تُطْعِمَهَا إِذَا طَعِمْتَ، وَتَكْسُوَهَا إِذَا اِكْتَسَيْتَ، وَلَا تَضْرِبِ اَلْوَجْهَ، وَلَا تُقَبِّحْ…"} اَلْحَدِيثُ. وتَقَدَّمَ فِي عِشْرَةِ اَلنِّسَاءِ.
Kutoka kwa Hakiym bin Mu’aawiyah Al-Qushayriyy amepokea kutoka kwa baba yake amesema: “Nilisema Ee Rasuli wa Allaah! Ni ipi haki ya mke wa mmoja wetu juu ya mumewe? Akasema: ‘Ni kumlisha unapokula na kumvisha unapovaa’.” Hadiyth imetangulia katika mlango wa matengamano ya waume kwa wake zao.
978.
وَعَنْ جَابِر بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنْ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ فِي حَدِيثِ اَلْحَجِّ بِطُولِهِ قَالَ فِي ذِكْرِ اَلنِّسَاءِ: {وَلَهُنَّ عَلَيْكُمْ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema kutoka katika Hadiyth ya Hajj iliyotajwa kwa urefu alisema alipowataja wanawake: “Wao (wanawake) wana haki inayowapasa nyinyi chakula chao na nguo zao kwa wema.”[7] [Imetolewa na Muslim]
979.
وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرٍو رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {كَفَى بِالْمَرْءِ إِثْمًا أَنْ يُضَيِّعَ مَنْ يَقُوتُ} رَوَاهُ النَّسَائِيُّ
وَهُوَ عِنْدَ مُسْلِمٍ بِلَفْظِ: "أَنْ يَحْبِسَ عَمَّنْ يَمْلِكُ قُوتَهُ"
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Yatosha mtu kuwa ana dhambi kwa kumtelekeza anayemlisha.”[8] [Imetolewa na An-Nasaaiy].
Nayo iko kwa Muslim kwa tamshi: “Kuzuia chakula kwa yule anayekimiliki.”
980.
وَعَنْ جَابِرٍ يَرْفَعُهُ، فِي اَلْحَامِلِ اَلْمُتَوَفَّى عَنْهَا قَالَ: {لَا نَفَقَةَ لَهَا} أَخْرَجَهُ اَلْبَيْهَقِيُّ، وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ، لَكِنْ قَالَ: اَلْمَحْفُوظُ وَقْفُهُ
وَثَبَتَ نَفْيُ اَلنَّفَقَةِ فِي حَدِيثِ فَاطِمَةَ بِنْتِ قَيْسٍ كَمَا تَقَدَّمَ. رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Jaabir amesema kuhusu mwanamke mjamzito aliyefiwa na mumewe, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hana matumizi.”[9] [Imetolewa na Al-Bayhaqiyy na wapokezi wake ni madhubuti lakini amesema: Ilivyohifadhiwa ni kuwa Hadiyth hii ni Mawquwf]
Na imethibiti mwanamke huyo kutopewa matumizi katika Hadiyth ya Faatwimah bint Qays kama iliyotangulia. [Imetolewa na Muslim]
981.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {اَلْيَدِ اَلْعُلْيَا خَيْرٌ مِنْ اَلْيَدِ اَلسُّفْلَى، وَيَبْدَأُ أَحَدُكُمْ بِمَنْ يَعُولُ. تَقُولُ اَلْمَرْأَةُ: أَطْعِمْنِي، أَوْ طَلِّقْنِي} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَإِسْنَادُهُ حَسَنٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini, mmoja wenu aanze na anayemlisha. Mwanamke husema[10]: “Nilishe au nipe talaka.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniy na Isnaad yake ni hasan]
982.
وَعَنْ سَعِيدِ بْنِ اَلْمُسَيَّبِ فِي اَلرَّجُلِ لَا يَجِدُ مَا يُنْفِقُ عَلَى أَهْلِهِ قَالَ: {يُفَرَّقُ بَيْنَهُمَا} أَخْرَجَهُ سَعِيدُ بْنُ مَنْصُورٍ: عَنْ سُفْيَانَ، عَنْ أَبِي اَلزِّنَادِ، عَنْهُ. قَالَ: {فَقُلْتُ لِسَعِيدِ بْنِ اَلْمُسَيَّبِ: سُنَّةٌ ؟ فَقَالَ: سُنَّةٌ} وَهَذَا مُرْسَلٌ قَوِيَ
Kutoka kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib amesema kuhusu mtu aliyekuwa hapati matumizi ya mkewe: “Watatenganishwa.” [Imetolewa na Sa’iyd bin Manswuwr kutoka kwa Sufyaan[11] naye kutoka kwa Abuu Az-Zinaad[12]]
Kutoka kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib amesema: “Nilisema kumuambia Sa’iyd bin Al-Musayyib je hii ni Sunnah? Akasema: ndiyo ni sunnah.” [Hadiyth hii ni Mursal yenye nguvu]
983.
وَعَنْ عُمَرَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ {أَنَّهُ كَتَبَ إِلَى أُمَرَاءِ اَلْأَجْنَادِ فِي رِجَالٍ غَابُوا عَنْ نِسَائِهِمْ: أَنْ يَأْخُذُوهُمْ بِأَنَّ يُنْفِقُوا أَوْ يُطَلِّقُوا، فَإِنْ طَلَّقُوا بَعَثُوا بِنَفَقَةِ مَا حَبَسُوا} أَخْرَجَهُ اَلشَّافِعِيُّ. ثُمَّ اَلْبَيْهَقِيّ بِإِسْنَادِ حَسَنٌ
Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Aliwaandikia viongozi wa majeshi kuhusu watu walio mbali na wake zao muda mrefu, kuwa watoe matumizi au wawataliki wake zao, ikiwa watawataliki watume gharama[13] za zile siku walizozuwia kutoa.” [Imetolewa na Ash-Shaafi’iyy na Al-Bayhaqiyy kwa Isnaad hasan]
984.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {جَاءَ رَجُلٌ إِلَى اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! عِنْدِي دِينَارٌ ؟ قَالَ: "أَنْفِقْهُ عَلَى نَفْسِكَ". قَالَ: عِنْدِي آخَرُ ؟ قَالَ: "أَنْفِقْهُ عَلَى وَلَدِكَ". قَالَ: عِنْدِي آخَرُ ؟ قَالَ: "أَنْفِقْهُ عَلَى أَهْلِكَ". قَالَ: عِنْدِي آخَرُ، قَالَ: "أَنْفِقُهُ عَلَى خَادِمِكَ". قَالَ عِنْدِي آخَرُ، قَالَ: "أَنْتَ أَعْلَمَ"} أَخْرَجَهُ اَلشَّافِعِيُّ وَاللَّفْظُ لَهُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَأَخْرَجَهُ النَّسَائِيُّ وَالْحَاكِمُ بِتَقْدِيمِ اَلزَّوْجَةِ عَلَى اَلْوَلَدِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Alikuja mtu kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nina dinari moja (niifanyeje?) akasema: Jitolee mwenyewe. Akasema: Ninayo nyingine. Akasema: Mpe mwanao. Akasema: Ninayo nyingine. Akasema: Mpe mkeo. Akasema: Ninayo nyingine. Akasema: Mpe mtumishi wako. Akasema: Ninayo nyingine. Akasema: Wewe ndiye unaejua zaidi (cha kuifanyia).” [Imetolewa na Ash-Shaafi’iyy na Abuu Daawuwd. Matini ya Hadiyth ni ya Abuu Daawuwd, vile vile An-Nasaaiy na Al-Haakim wameipokea kwa kumtanguliza mke mbele ya mtoto]
985.
وَعَنْ بَهْزِ بْنِ حَكِيمٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ جَدِّهِ قَالَ: {قُلْتُ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! مَنْ أَبَرُّ ؟ قَالَ: "أُمَّكَ". قُلْتُ: ثُمَّ مِنْ ؟ قَالَ: "أُمَّكَ". قُلْتُ: ثُمَّ مِنْ " ؟ قَالَ: "أُمَّكَ". قُلْتُ: ثُمَّ مِنْ ؟ قَالَ: "أَبَاكَ، ثُمَّ اَلْأَقْرَبَ فَالْأَقْرَبَ"} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَحُسَّنَهُ
Kutoka kwa Bahz bin Hakiym kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake amesema: Nilisema Ee Rasuli wa Allaah! Nimfanyie nani wema? Akasema: “Mama yako.” Nikasema: Kisha nani? Akasema: “Mama yako.” Nikasema kisha nani? Akasema “Mama yako.” Nikasema kisha nani? Akasema: “Baba yako, kisha jamaa wa karibu zaidi.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy amesema ni sahihi]
[1] Hind bint ‘Utbah bint Rabiy’a bin ‘Abd Shams alisilimu mwaka wa Fat-h Makkah baada ya mume wake kusilimu katika mwaka huo huo wa Fat-h Makkah. Kifo cha baba yake ‘Utbah, mjomba wake Shaiba na kaka yake Al-Waliyd huko Badr vilimshtua sana na alifurahi sana pindi Hamza alipouwawa katika vita vya Uhud.
[2] Jina lake ni Sakhr bin Harb bin Umaiyyah bin ‘Abd Shams ambaye alibeba bendera ya ukafiri na alikuwa kiongozi aliyepigana na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Alisilimu katika Fat-h Makkah pindi Al-‘Abbaas alipomchukuwa kwa Nabiy kabla ya kuingia Makkah. Aliishi akiwa ni Muislamu mzuri.
[3] Lengo la Hadiyth hii kuwekwa hapa ni kuonesha majukumu aliyokuwa nayo mtu katika kusimamia mahitaji ya mkewe au wakeze na watoto wake. Inaonyesha hali kadhalika kuwa ikiwa mtu atakataa kutoa haki anayotakiwa kutoa, basi Shariy’ah itaruhusu haki hiyo itolewe kwa njia nyingine. Kwa maneno mengine, ikiwa mtu amedhulumiwa anaweza kutafuta haki yake kupitia njia nyingine.
[4] Twaariq bin ‘Abdillaah Al-Muhaaribiyy alikuwa ni Swahaba ambaye alipokea baadhi ya Hadiyth. Alikuwa Muhaaribiyy bin Khasfa, katika kabila la Banu Ghatafan.
[5] Mkono unaotoa ni bora kuliko mkono unaopokea. Ni vizuri mtu kutokopa fedha. Hadiyth hii haikutaja mke na watoto kwani wao wameshaingizwa katika matumizi ya familia. Maelezo ya ziada ni kuwa familia ya mtu tajiri inajumuisha jamaa zake wa karibu kama kaka na dada zake walio masikini ili nao waishi maisha mazuri.
[6] Kilichokuwa kizuri katika muamala wa mtu na watumwa au wafanyakazi ni pale anapokula amlishe anachokula na amvishe anachovaa. Kadhalika asizidishiwe kazi ila anachoweza kufanya kama kuna uzito basi asaidiwe.
[7] Lengo la kuwekwa kwa Hadiyth hii ni matumizi yatachukuliwa kulingana na kipato cha mtu. Ikiwa mtu ni tajiri mkewe anaweza kuomba ziada ya matumizi, inayolingana na uwezo wa mumewe. Ikiwa hali yake ni ya umasikini atapata kile kinacholingana na uwezo wa mumewe.
[8] Maelezo ya Hadiyth hii yanasisitiza kuwa ni dhambi kuwatekeleza wale ambao umeamrishwa kuwahudumia. Watu ambao ni lazima kishariy’ah kuwahudumia kwa daraja la mwanzo kabisa ni mke, watoto, wafanyakazi wake na wazazi wake.
[9] Mwanamke asiyekuwa na mimba na aliyeachika talaka tatu, kwa makubaliano ya ‘Ulamaa, hana haki ya kupewa nyumba na gharama zake. Mjamzito, aliyeachika talaka tatu anayo haki ya kupewa chakula lakini siyo nyumba. Mjane asiye na mimba anapewa nyumba lakini siyo chakula. Mjane mwenye mimba ana haki ya nyumba, kuna tofauti ya rai kutokana na ‘Ulamaa ikiwa ana haki ya kupewa chakula na gharama zingine za maisha. Mjadala upo katika huduma za nyumba na maisha kwa mwanamke aliyekuwa katika eda. Pindi eda yake inapomalizilka, hana haki ya chochote katika yaliyotangulia.
[10] Hadiythi hii inatupambanulia kwamba ikiwa mwanamme hawezi gharama za mke wake, wataachanishwa ikiwa mwanamke ametaka hivyo. Hata hivyo, ikiwa mwanamke atapendelea asubiri kwa matamu ya maisha na machungu yake, atakuwa ni mwenye kupata ujira.
[11] Huyu ni Sufyaan bin Sa’iyd bin Masruq Ath-Thawriy Abuu ‘Abdillaah Al-Kufi. Alikuwa ni Imaam maarufu na makini, Hafidhi na mwenye elimu kubwa ya Hadiyth, alikuwa ni mwenye taqwa. Alizaliwa mwaka 77H na alikufa katika mji wa Basra mwaka 161H.
[12] Jina lake halisi ni ‘Abdullaah bin Dhakwaan, ni katika ukoo wa Al-Amawi wa Madiynah. Alikuwa ni miongoni mwa maimaam wakubwa, Ahmad anamuelezea kwa kusema: “Alikuwa ni mtu madhubuti na kamanda wa Waumini.” Al-Bukhaariy naye anamuelezea kwa kusema: “Isnaad iliyokuwa bora zaidi ni kutoka kwa Abuu Az-Zinaad naye kutoka kwa Al-A’raaj kutoka kwa Abuu Hurayrah (ambaye amepokea kutoka kwa Nabiy).” Alifariki mwaka 130 Hijriya au 131.
[13] Katika Hadiyth nyingine inasisitiza kuwa fedha inayotumiwa na mtu kwa ajili ya mke wake na watoto wake ndiyo yenye ujira mkubwa na ni bora kuliko ile inayotumika katika kuwapa maskini wa mbali (wasiokuwa ndugu).