26-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Alifikishwa Mbingu Ya Saba Katika Safari Ya Usiku Mmoja Ya Israa Wal-Mi’raaj
Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
26-Alifikishwa Mbingu Ya Saba Katika Safari Ya Usiku Mmoja Ya Israa Wal-Mi’raaj
Tukio la miujiza ya Allaah (‘Azza wa Jalla) la Al-Israa wal Mi’raaj ambalo amemjaalia Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asafiri usiku mmoja tu na kumfikisha mbingu ya saba. Dalili ya safari hiyo ya mijuzia ni katika Quraan ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾
Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake; ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Al-Israa: 1]
Na pia Kauli Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala):
ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ ﴿٨﴾
Kisha akakurubia na akashuka.
فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ ﴿٩﴾
Kisha akawa kiasi cha umbali wa mipinde miwili au karibu zaidi.
فَأَوْحَىٰ إِلَىٰ عَبْدِهِ مَا أَوْحَىٰ ﴿١٠﴾
(Allaah) Akamfunulia Wahy mja Wake yale Aliyomfunulia Wahy.
مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ ﴿١١﴾
Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.
أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ ﴿١٢﴾
Je, mnambishia kuhusu yale aliyoyaona?
وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ ﴿١٣﴾
Na kwa yakini amemuona (Jibriyl) katika uteremko mwingine.
عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ ﴿١٤﴾
Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa.
عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ ﴿١٥﴾
Karibu yake kuna Jannah ya Al-Ma-waa.
إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ ﴿١٦﴾
Ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika
مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ ﴿١٧﴾
Jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka.
لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ ﴿١٨﴾
Kwa yakini aliona miongoni mwa Aayaat (ishara, dalili) za Rabb wake kubwa kabisa. [An-Najm: 8-18]
Na Hadiyth kadhaa ziloelezea kuhusu safari hiyo; miongoni mwazo ni zifuatazo ambazo alipofika mbingu ya saba ndipo ilipofaridhishwa Swalaah tano kwa Waislamu:
‘Abdullaah bin Mas’uwd alisema, “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa vitu vitatu: alipewa Swalaah tano, alipewa Aayah mbili za kumalizia Suwrah ya Al-Baqarah na kusamehewa kwa madhambi ya wale watu ambao hawamshirikishi Allaah miongoni mwa ummah wake.” [Muslim Namba 329].
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Allaah Alinipa ufunuo na Akasema kuwa Ummah wangu wanawajibika kuswali Swalaah khamsini (50) kila siku; usiku na mchana. Nilishuka kwenda kwenye mbingu ya Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) akaniluza: “Lipi Rabb wako Amekupatia kwa ajili ya ummah wako?” Nikasema: “Swalaah Khamsini.” Akasema: “Rejea kwa Rabb wako na omba Akupunguzie katika idadi hiyo ya Swalaah, maana watu wako hawawezi kubeba mzigo huo mzito. Kama vile nilivyotiwa katika mtihani na wana wa Israaiyl na nikawajaribu nikawaona kuwa walikuwa dhaifu sana na hawawezi kubeba mzigo kama huo.” Hivyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimgeukia Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) kama vile akitaka kupata ushauri wake juu ya hilo. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema: “Ndiyo, sawa, kama unataka hivyo.” Na wakarejea tena juu kwa Allaah.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608].
Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nilirejea kwa Rabb wangu na kusema, “Ee Rabb wangu, Fanya vitu viwe vyepesi kwa ajili ya Ummah wangu. Allaah Alipunguza idadi ya Swalaah khamsini na kuwa tano kwa ajili yangu. Nilishuka chini nikaenda kwa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) ambaye alisema: “Hakika watu wako hawataweza kubeba mzigo huu mzito. Rejea kwa Rabb wako umwombe afanye wepesi wa hilo, Ee Muhammad! Mimi nilijaribu kuwalingania Ummah wangu wana Israaiyl ili wafanye kidogo zaidi ya hayo, lakini hawakuweza kuyafanya hayo bali waliishia kukata tamaa.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608].
Basi nikawa natangatanga kati ya mbingu ya Muwsaa na kwa Rabb wangu mwisho Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema: “Kuna Swalaah tano kila siku, usiku na mchana Ee Muhammad. Kila Swalaah imebeba uzito wa Swalaah kumi, na hivyo hizo ni khamsini vile vile. Mtu yeyote anayetia niyyah ya kufanya jambo zuri na asipolifanya basi atapata thawabu kwa hilo, na kama atalifanya hilo tendo, basi itaandikwa thawabu kumi kwa hilo. Wakati ambapo mtu aliyenuia kufanya uovu na akaacha kuufanya haitasajiliwa hiyo na kama atafanya uovu huo basi utasajiliwa uovu mmoja tu. Hapo nikashuka kwa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) na kumwambia hayo, Muwsaa akasema: “Nenda kwa Rabb wako ili afanye mambo yawe mepesi zaidi.” Juu ya kauli hiyo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nimekuwa nikienda kwa Rabb wangu mara kwa mara hadi naona aibu kusimama mbele yake. [Muslim].
Juu ya hilo Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema: ”Kwa jina la Allaah! Shuka sasa!” Kisha Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaamka akiwa ndani ya Masjid Al-Haraam (Msikiti Mtukufu wa Makkah)” [Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608]
Na pia ndani ya maelezo ya Al-Bukhaariy kuna maelezo zaidi kuwa: “…nilipoondoka nilisikia sauti: “Nimetoa amri Yangu na kisha nimewapunguzia uzito Waja Wangu.”