08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Dhahabu Na Fedha (Silver)
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Zakaah
08-Zakaah Ya Dhahabu Na Fedha (Silver)
Ikiwa masharti tuliyoyataja yatakamilika katika dhahabu na fedha pamoja na mmiliki wake, zikafikia kiwango, zikapitiwa na mwaka mmoja na mfano wa hivyo, basi hapo itabidi zitolewe Zakaah, na itakuwa mara moja tu kila mwaka.
Kiwango cha dhahabu na fedha na kiasi cha Zakaah ya kila kimoja
Imekuja katika Hadiyth ya ‘Aliyy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema:
((إذا كانت لك مائتا درهم وحال عليها الحول، ففيها خمسة دراهم، وليس عليك شيء - يعني في الذهب- يكون لك عشرون دينارا، فإذا كانت لك عشرون دينارا، وحال عليها الحول ففيها نصف دينار))
((Ikiwa una dirham 200 na zikapitiwa na mwaka, basi kuna dirham 5 ndani yake, na hupaswi na chochote – yaani katika dhahabu – mpaka uwe na dinari 20. Kama una dinari 20 na zikapitiwa na mwaka, basi kuna nusu dinari ndani yake)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1558), At-Tirmidhiy (616), An-Nasaaiy (5/37), Ibn Maajah (1790) na Ahmad (1/121). Al-Bukhaariy kasema ni Swahiyh – kama alivyonukuu toka kwake At-Tirmidhiy – na Al-Haafidh ameifanya ni Hasan katika Al Fat-h. Na katika Swahiyh Abiy Daawuud (1391), Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:
((ليس فيما دون خمس أواق من الورق صدقة))
((Hakuna Zakaah chini ya wakia (ounce) tano ya fedha [silver])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1484) na Muslim (979)]
أواق ni wingi (plural) wa أوقية (singular) . Na wakia moja ni sawa na dirham 40 kwa makubaliano ya wataalamu. Hivyo wakia 5 zitakuwa sawa na dirham 200 (5×40)]
Tunajifunza kutokana na viwili hivi mambo kadhaa:
Kwanza: Ni kwamba:
- Kiwango cha fedha ya wakia (5) ambayo ni sawa na dirham 200 ya fedha safi, ni sawa na gram 595 za fedha.
- Kiwango cha dinari 20 za dhahabu ni sawa na mithqali 20, na mithqali 20 ni sawa na gram 85 za dhahabu krati 24, gramu 97 za dhahabu krati 21, na gramu 113 za dhahabu krati 18.
Pili: Ni lazima mwaka kamili wa Hijria ukipitie kiwango na zaidi ili Zakaah ipate uwajibu wa kutolewa.
Tatu: Kiasi cha Zakaah kwa dhahabu na fedha (silva) ni 2.5%= 1/40 (moja ya arobaini)
Mfano bainishi:
Mtu anamiliki nusu kilo ya dhahabu ya krati 24. Ni kiasi gani cha Zakaah atatoa ikipitiwa na mwaka?
Tunasema: Kwa kuwa kiasi cha dhahabu inayomilikiwa ni zaidi ya kiwango (gramu 85), hapa itabidi itolewe 2.5% (asilimia mbili na nusu). Kipimo cha wajibu kutolewa kitakuwa ni 500 gr X 1/40 = 12.5 gr
Itatolewa gramu 12.5 katika gramu 500 (ya dhahabu).
Je, dhahabu inaweza kuchanganywa na fedha ili kukamilisha kiwango?
Mtu akiwa na dhahabu isiyotimiza kiwango, na kiasi kingine cha fedha isiyotimiza kiwango, hapa ‘Ulamaa wana kauli mbili:
Ya kwanza:
Ataichanganya dhahabu na fedha ili kiwango kitimie halafu atatoa Zakaah. Ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa (Abu Haniyfah na Maalik, na ni riwaya toka kwa Ahmad, na kauli ya Ath-Thawriy na Al-Awzaa’iy).
Dalili yao wanasema kuwa manufaa ya viwili hivyo ni mamoja, ni vitu vya thamani, na hukusudiwa kwavyo biashara. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/267)]
Ya pili:
Hachanganyi kimoja na kingine. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, riwaya toka kwa Ahmad, kauli ya Abiy ‘Ubayd, Ibn Abiy Laylaa, Abiy Thawr na Ibn Hazm. Kauli hii imekhitariwa na Al-Albaaniy na Ibn ‘Uthaymiyn, nayo ndiyo yenye nguvu In Shaa Allaah. [Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (6/82), Al-Albaaniy katika Tamaam Al-Minnah (uk 360) na Ibn ‘Uthaymiyn katika Ash-Sharhu Al-Mumtií (6/107)]
Dalili zao:
1- Ujumuishi wa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):
((ليس فيما دون خمس أواق من الورق صدقة))
((Hakuna Zakaah chini ya wakia tano ya fedha)). [Takhriyj yake imetajwa nyuma kidogo]
Na kauli yake:
((ليس عليك شيء –يعنني في الذهب- حنى يكون لك عشرون دينارا))
((Huwajibikiwi na chochote –yaani katika dhahabu – mpaka uwe na dinari 20)). [Takhriyj yake imetajwa nyuma kidogo]
Hadiyth hizi mbili zinadulisha kuwa mwenye kuchanganya dhahabu na fedha, anakuwa amewajibisha Zakaah ya kila kimoja ya viwili hivi chini ya kiwango chake.
2- Kuchukulia kipimo kwa ngómbe, mbuzi na kondoo, –uchambuzi wake utakuja– hawa kiwango cha mmoja hakikamilishwi kwa mwingine pamoja na kuwa lengo la kuwa nao ni moja, nalo ni kuwazalisha. Aidha, shayiri haichanganywi na ngano hata kwa wenye kusema dhahabu huchanganywa na fedha (silver). Aina moja haichanganywi na aina nyingine. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
Faida
Mali ya wabadilishaji pesa (sarafu) hutolewa ndani ya duara hili. Hawa dhahabu na fedha huchanganywa ndani ya mali yao, na sio kuchanganya aina moja na nyingine. Na kwa vile lengo la viwili hivi ni biashara, basi vinakuwa ni mali ya biashara. [Ash-Sharhu Al-Mumtií (6/109). Angalia Al-Mughniy (3/2-3)]
Tukikubaliana na kauli ya kuchanganya, je huchanganywa sehemu au thamani?
Wenye kujuzisha kuchanganya dhahabu na fedha wamekhitalifiana juu ya kauli mbili:
1- Maalik, Abu Yuwsuf, Muhammad na Ahmad katika riwaya yake, wanasema uchanganyaji unakuwa ni kwa sehemu. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (23/267)]
Maana ya hii ni kuwa mwenye nusu ya kiwango cha dhahabu na nusu ya kiwango cha fedha, Zakaah itamwajibikia. Vile vile, kama ana robo ya kiwango cha kimojawapo, na robo tatu ya kingine, au mfano wa hivyo. Kisha atatoa 2.5% kwa kila kimoja.
2- Ama Abu Haniyfah, yeye anaona kimoja kichanganywe na kingine kwa kutiwa thamani ya kimoja kwa kingine kwa namna ya kuwanufaisha zaidi masikini. Kwa maana nyingine, kingi kichanganywe kwenye kichache. [Angalia iliyotangulia]
Kwa mfano, ikiwa ana nusu ya kiwango cha fedha na robo ya kiwango cha dhahabu, na robo ya kiwango cha dhahabu ikawa thamani yake sawa na nusu ya kiwango cha fedha, hapo Zakaah itakuwa lazima kwake.