046-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Ahqaaf Aayah 10 قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كَانَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ وَكَفَرْتُمْ بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
046-Asbaabun-Nuzuwl Al-Ahqaaf Aayah 10
Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَكَفَرْتُم بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴿١٠﴾
Sema: Mnaonaje ikiwa (hii Qur-aan) ni kutoka kwa Allaah, na mkaikanusha; na akashuhudia shahidi miongoni mwa wana wa Israaiyl juu ya mfano wa haya, na akaamini nanyi mkatabari? Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Ahqaaf (46:10)]
Sababun-Nuzuwl:
حَدَّثَنَا أَبُو الْمُغِيرَةِ عبد القدوس بن حجاج قَالَ : حَدَّثَنَا صَفْوَانُ قَالَ : حَدَّثَنَا عَبْدُ الرَّحْمَنِ بْنُ جُبَيْرِ بْنِ نُفَيْرٍ ، عَنْ أَبِيهِ ، عَنْ عَوْفِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ : انْطَلَقَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمًا وَأَنَا مَعَهُ حَتَّى دَخَلْنَا كَنِيسَةَ الْيَهُودِ بِالْمَدِينَةِ ، يَوْمَ عِيدٍ لَهُمْ ، فَكَرِهُوا دُخُولَنَا عَلَيْهِمْ ، فَقَالَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : يَا مَعْشَرَ الْيَهُودِ أَرُونِي اثْنَيْ عَشَرَ رَجُلًا يَشْهَدُونَ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ ، يُحْبِطِ اللَّهُ عَنْ كُلِّ يَهُودِيٍّ تَحْتَ أَدِيمِ السَّمَاءِ الْغَضَبَ ، الَّذِي غَضِبَ عَلَيْهِ قَالَ : فَأَسْكَتُوا مَا أَجَابَهُ مِنْهُمْ أَحَدٌ ، ثُمَّ رَدَّ عَلَيْهِمْ فَلَمْ يُجِبْهُ أَحَدٌ ، ثُمَّ ثَلَّثَ فَلَمْ يُجِبْهُ أَحَدٌ ، فَقَالَ : أَبَيْتُمْ فَوَاللَّهِ إِنِّي لَأَنَا الْحَاشِرُ ، وَأَنَا الْعَاقِبُ ، وَأَنَا النَّبِيُّ الْمُصْطَفَى ، آمَنْتُمْ أَوْ كَذَّبْتُمْ . ثُمَّ انْصَرَفَ وَأَنَا مَعَهُ حَتَّى إِذَا كِدْنَا أَنْ نَخْرُجَ نَادَى رَجُلٌ مِنْ خَلْفِنَا : كَمَا أَنْتَ يَا مُحَمَّدُ . قَالَ : فَأَقْبَلَ . فَقَالَ ذَلِكَ الرَّجُلُ : أَيَّ رَجُلٍ تَعْلَمُونَي فِيكُمْ يَا مَعْشَرَ الْيَهُودِ ؟ قَالُوا : وَاللَّهِ مَا نَعْلَمُ أَنَّهُ كَانَ فِينَا رَجُلٌ أَعْلَمُ بِكِتَابِ اللَّهِ مِنْكَ ، وَلَا أَفْقَهُ مِنْكَ ، وَلَا مِنْ أَبِيكَ قَبْلَكَ ، وَلَا مِنْ جَدِّكَ قَبْلَ أَبِيكَ . قَالَ : فَإِنِّي أَشْهَدُ لَهُ بِاللَّهِ أَنَّهُ نَبِيُّ اللَّهِ ، الَّذِي تَجِدُونَهُ فِي التَّوْرَاةِ ، قَالُوا : كَذَبْتَ ، ثُمَّ رَدُّوا عَلَيْهِ قَوْلَهُ ، وَقَالُوا فِيهِ شَرًّا ، قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : كَذَبْتُمْ لَنْ يُقْبَلَ قَوْلُكُمْ ، أَمَّا آنِفًا فَتُثْنُونَ عَلَيْهِ مِنَ الْخَيْرِ مَا أَثْنَيْتُمْ ، وَلَمَّا آمَنَ أَكْذَبْتُمُوهُ ، وَقُلْتُمْ فِيهِ مَا قُلْتُمْ ، فَلَنْ يُقْبَلَ قَوْلُكُمْ . قَالَ : فَخَرَجْنَا وَنَحْنُ ثَلَاثَةٌ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، وَأَنَا وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَلَامٍ ، وَأَنْزَلَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ فِيهِ : قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كَانَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ وَكَفَرْتُمْ بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَى مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ
Ametuhadithia Abul Mughiyrah ‘Abdul-Qudduws bin Hajjaaj amesema: Ametuhadithia Swafwaan bin ‘Amri amesema: Ametuhadithia ‘Abdur-Rahmaan bin Jubayr bin Nafiyr toka kwa baba yake, toka kwa ‘Awf bin Maalik aliyesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa pamoja nami, aliondoka siku moja mpaka tukaingia kwenye Sinagogu la Mayahudi mjini Madiynah. Ilikuwa ni siku ya sikukuu yao, nao walichukia sisi kuingia (kwa kuwa walijua kuingia kwa Rasuli wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم ni kwa ajili ya kufichua uongo wao na kuwalingania haki wasioitaka). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaambia: “Enyi jamii ya Mayahudi! Nionyesheni [katika “Al-Musnad” maneno hayafahamiki, ndio tukayaandika toka kwenye “Majma’u Az Zawaaid”] watu 12 miongoni mwenu ambao kila mmoja kati yao atashahadia kwamba
لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ
hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) (mkifanya hilo) Allaah Atamwondoshea kila Myahudi aliye chini ya paa la mbingu ghadhabu ambayo Amemghadhibikia.” (kutokana na ukafiri wao, dhulma zao, na kuwaua Manabii pasina haki). Wakanyamaza tulii, na hakuna yeyote aliyemjibu kati yao [imeandikwa hivi hivi katika “Al-Majma’u”]. Halafu akawauliza mara ya pili, na hakuna aliyemjibu, kisha mara ya tatu na hakuna aliyemjibu. Akawaambia: “Mmekataa! Basi Wa Allaah, hakika mimi, pasi na shaka yoyote, ndiye Al-Haashir (Mkusanyaji; watu watakusanywa kufuata athari ya nyayo zangu Siku ya Qiyaamah, kwani mimi ndiye wa mwanzo kufufuliwa), na mimi ni Al-‘Aaqib (Nabiy wa Mwisho, hakuna baada yangu Nabiy), na mimi ndiye Nabiy Mteule, ni sawa mmeamini au mmekadhibisha.” (hizi ndizo sifa zangu na haya ndio majina yangu). Kisha akaanza kuondoka nikiandamana naye, na tulipokaribia kutoka, mtu mmoja aliita toka nyuma na kusema: Simama hapo hapo: Ee Muhammad. (Mtu huyu ni ‘Abdullaah bin Salaam ambaye alikuwa ni mwanazuoni mkubwa wa Kiyahudi, na alikuwa amesilimu bila wao kuwa na taarifa). [Rasuli wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم] akageuka, na mtu yule (‘Abdullaah bin Salaam]) akawauliza: Enyi Jamii ya Mayahudi! Mimi mnanitambua kama nani kati yenu? (imeandikwa hivi katika “Al-Majma’u”). Wakasema (kabla hawajajua kuwa amemwamini Rasuli wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم): Wa Allaah, hatujui kuwepo mtu mjuzi zaidi ndani yetu wa Kitabu cha Allaah kuliko wewe, wala mwenye ufahamu zaidi wa Diyn kuliko wewe, wala kuliko baba yako, wala kuliko babu yako kabla ya baba yako (Mwanazuoni, mtoto wa Mwanazuoni na mjukuu wa Mwanazuoni). Akasema: Kwa hivyo basi, mimi ninamshuhudilia kuwa yeye ni Nabiy wa Allaah ambaye mnamkuta ametajwa ndani ya Tawraat. Wakasema: Umeongopa. Wakaipinga kauli yake, na wakamsema vibaya sana (baada ya kujua kasilimu). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaambia: “Mmeongopa, kauli yenu haikubaliwi. Hivi punde tu mmemsifia kwa sifa njema ukomo wa kumsifu, lakini alipoeleza Iymaan yake, mmemkadhibisha, na kumsema vibaya, hivyo maneno yenu kuhusu yeye hayatokubaliwa.” Tukatoka tukiwa watatu; Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) mimi na ‘Abdullaah bin Salaam. Na Allaah (عز وجل) Akateremsha kumzungumzia (‘Abdullaah bin Salaam):
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَكَفَرْتُم بِهِ وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ مِثْلِهِ فَآمَنَ وَاسْتَكْبَرْتُمْ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴿١٠﴾
Sema: Mnaonaje ikiwa (hii Qur-aan) ni kutoka kwa Allaah, na mkaikanusha; na akashuhudia shahidi miongoni mwa wana wa Israaiyl juu ya mfano wa haya, na akaamini nanyi mkatabari? Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.” [Al-Ahqaaf (46): 10]
[Ahmad katika Mujallad wa 6 ukurasa wa 25]
Al-Haythamiy katika “Majma’u Az-Zawaaid” Mujallad wa 7 ukurasa wa 106 amesema: Hadiyth hii imesimuliwa na At-Twabaraaniy, na Wapokezi wake ni Wapokezi wa As-Swahiyh. Walioikhariji ni Ibn Hibaan katika “Mawaarid Adh-Dhwam-aan” ukurasa wa 518, At-Twabaraaniy katika Mujallad wa 26 ukurasa wa 12, na Al-Haakim katika “Al-Mustadrak” Mujallad wa 3 ukurasa wa 416 na kusema kuwa ni Swahiyh juu ya sharti ya Masheikh Wawili. Adh-Dhahabiy ameikubali.
Nami (Muqbil Al-Waadi’iyy) nasema: Hadiyth iko juu ya sharti ya Muslim, kwa kuwa Al-Bukhaariy hakukhariji kwa ‘AbdurRahmaan bin Jubayr wala kwa baba yake. Pia hakumkharijia Swafwaan bin ‘Amri ila ikiwa Mu’allaq kama ilivyo katika Wasifu wake katika “Tahdhiyb At-Tahdhiyb”.