003-Aal-'Imraan: Utangulizi Wa Suwrah

 

003-Aal-Imraan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 200

 

Jina La Suwrah:

 

Imeitwa Aal-‘Imraan (Familia Ya ‘Imraan), na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila za Suwrah, na pia kutajwa kwake katika Aayah namba (35).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Uthibitisho kwamba Dini ya Kiislamu ndio ya Dini ya haki. Radd (kujibu kwa kukanusha) kwa shubuhaat (tuhuma) za Watu wa Kitabu (Mayahudi na Naswara). Kuwathibitisha Waumini. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya kwamba Allaah ni Mmoja, na kusimamisha dalili na hoja juu ya hilo

 

3-Kubainisha ‘Al-Walaa na Al-Baraa (kupendana na kuchukiana kwa ajili ya Allaah), na tahadhari juu ya kumtawalisha asiye kuwa Muumini.

 

4-Kuchambua hali za Ahlul-Kitaab na baadhi ya itikadi zao na maasi yao.

 

5-Kuupa umuhimu upande wa malezi, na maelekezo kwa Waumini.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa kwamba Allaah ni Mmoja, na imeithibitishwa aina tatu za Tawhiyd: (i) Tawhiyd Al-Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah katika ibaada). (ii) Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah (Kumpwekesha Allaah katika Uola Wake). (iii) Tawhiyd Asmaa Wasw-Swifaat (Kumpwekesha Allaah katika Majina Yake Mazuri Na Sifa Zake Kamilifu)

 

2-Imebainishwa watu walivyogawanyika kuhusu kuzifahamu Aayah zenye maana za wazi, na zisizokuwa wazi maana zake.

 

3-Wametahadharishwa makafiri wanaompinga Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba: Ufalme, nguvu, vyeo, watoto, mali, havitawasaidia mbele ya Adhabu ya Allaah, na kwamba mwisho wao ni khasara ya wazi Duniani na Aakhiirah. Na Allaah Akawapigia mifano ya Makafiri waliotangulia na wataokuja baada yao, na jinsi utavyokuwa mwisho wao.

 

4-Kumetajwa kutokea kwa Vita vitukufu vya Badr na Uhud. Na katika vita vya Uhud, kuna maelezo ya matukio ya vita hivi na mafunzo waliyopata Waumini walipoenda kinyume na matakwa ya Rasuli wao (صلى الله عليه وآله وسلم) katika mbinu za kupigana kwenye vita hivyo vya Uhud ikasababisha kushindwa kwa Waislamu. Vita hivyo vilibainisha na kuwafichua wazi   Waumini wakweli na wanafiki.

 

5-Vimetajwa vitu vinavyopendwa zaidi na nafsi ya mwanaadam, na kutanabahishwa kwamba hivyo vyote ni vitu vya starehe fupi ya kilimwengu na pambo lake lenye kutoweka. Lakini kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kuna marejeo mazuri na thawabu adhimu ambazo Allaah Amewaandalia wenye taqwa, nayo ni Jannah yenye uhai wa starehe na neema za kudumu milele.  

 

6-Imethibitishwa umuhimu wa Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na ndani yake imetaja mara nne Kalimah ya Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى):

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ

Na imeeleza pia Amri ya Allaah kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) awalinganie kwenye neno la sawasawa, ambalo ni neno la Tawhiyd.

 

7-Suwrah inaongoza katika hidaaya, kwani inawalingania watu wote kwenye Dini moja ya Uislamu na inawaambia kuhusu malipo watakayopewa watu wema na adhabu watakazopewa makafiri na kwamba Allaah (عزّ وجلّ) Haridhii dini yeyote ile isipokuwa Dini ya Kiislamu.

 

8-Suwrah imetaja kuhusu mke wa ‘Imraan, Bi Hannah na kumzaa kwake Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام). Imeelezewa kisha cha Nabiy Zakariyyaa (عليه السّلام) na kuzaliwa kwa Yahyaa. Pia kuzaliwa kwa ‘Iysaa (عليهم السّلام).  Rejea Aayah (36).  

 

9-Kuna uchambuzi wa hali za Ahlul-Kitaab (Watu wa Kitabu; Mayahudi na Manaswaara), na kuufedhehesha uovu na upotevu wao, ukiwemo kumpinga Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) na yaliyowatokea ambayo ni kutofautiana katika Dini zao, na maovu waliyoyafanya, ya kuzikadhibisha Aayaat za Allaah, na kuwauwa Manabii Wake, na wale wanaolingania haki. Na pia kule kugoma kwao kuhukumiwa na Kitabu cha Allaah.

 

10-Suwrah inawajadili Watu wa Kitabu kwa dalili, ushahidi na hoja za waziwazi kabisa za kuthibitisha kuwa Dini ya Kiislamu ndio Dini ya haki iliyokuja kukhitimisha Dini za Manabii wote waliotangulia. Basi Suwrah  inakanusha upinzani wao dhidi ya Tawhiyd ya Allaah na ukanushaji wao wa Dini ya mwisho ya Kiislamu.

 

11-Suwrah imeeleza majadiliano yao juu ya Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) na kuwabainishia haki kwenye jambo lake (Ibraahiym), na kutaja sifa zao nyingi ambazo walikuwa nazo (Ahlul-Kitaab), kama vile walivyokuwa wakitaka kuwapoteza Waislam, na kule kuzipinga kwao Aayaat za Allaah, na kule kuchanganya kwao haki na baatwil, na kuingiza maneno yao kwenye Kitabu chao, kwa lengo la kuwarubuni na kuwadanganya Waumini, na yasiyokuwa hayo.

 

12-Imebainishwa kuwa Ahlul-Kitaab wa awali waliomwamini Allaah na kumwamini Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) hawako sawa, na kwamba wako kati yao wanasoma Aayaat za Allaah (سبحانه وتعالى) usiku na mchana, na wanaamini Siku ya mwisho, wanaamrisha mema na kukataza mabaya.

 

13-Suwrah imetoa tanbihi juu ya ‘Aqiydah ya Al-Walaa Wal-Baraa (kupendana na kuchukiana kwa ajili ya Allaah), na kulisisitiza hilo, na tahadhari juu ya kuwapenda wasiokuwa Waumini.

 

14-Imebainishwa kuwa mapenzi ya Allaah yana alama na dalili zake, ikiwemo kumfuata Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumpenda Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumtii.

 

15-Imeeleza pia khabari za Manabii na kwamba daraja zao ni za juu, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwachagua. 

 

16-Imetajwa pia adabu nyingi za malezi, wasia wa kumcha Allaah (سبحانه وتعالى), kushikamana na Dini ya Allaah, kuacha kutengana na kukhtalifiana, na kuwaamrisha Waumini walinganie kheri, na kuwahimiza kutoa mali zao kwa njia ya Allaah.

 

17-Imetajwa baadhi ya Hukmu za Kisharia kama vile Jihaad, kuzuia watu kula riba, na adhabu za wanaozuia Zakaah.
 

18-Waumini wamefunzwa subra na wameshajiishwa kuhusu subra katika hali za neema na hali za misiba ya nafsi na mali na dhiki nyenginezo.

 

19-Imetajwa kuhusu Shuhadaa na fadhila zao. Hali kadhaalika imetajwa malipo watakayopata Waumini nayo ni Jannah na mapokezi mazuri humo kutoka kwa Rabb wao.  

 

20-Imetajwa ukosefu wa adabu wa Mayahudi na dhulma yao kubwa iliyovuka mipaka kwa kumsingizia na kumpachika Allaah (سبحانه وتعالى) sifa ya ufakiri, ilhali Yeye Ni Al-Ghaniyy (Tajiri na Mkwasi Hahitaji lolote), na Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaradd kwa hilo na kuwaadhidi adhabu waonje adhabu kali. 

 

21-Wamesifiwa Waumini wenye kutafakari Uumbaji wa Allaah na wenye kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kila nyakati na katika kila hali, na Kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) katika kumuomba duaa, na zikatajwa fadhila zao na malipo yao mazuri kabisa ya kuingizwa Jannah.

 

22-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwataka Waumini wavute subira na ribaatw (wabakie imara) na wamche Allaah ili wapate kufaulu. Rejea katika faida ya Aayah ya mwisho kupata fadhila za ribaatw.

 

Fadhila za Suwrah: 

 

1-Ni Taa Mbili Zitakazokuja Siku Ya Qiyaamah Kuwa Ni Shafaa’ah (Kiombezi) Kwa Wanaoisoma Na Kutekeleza Amri Zake:

 

عن أبي أُمامةَ الباهليِّ رضِي اللهُ عنه، قال: سمعتُ رسولَ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّمَ يقول : اقْرَؤوا القُرْآنَ؛ فإنَّه يأتي يَومَ القيامةِ شفيعًا لأصحابه، اقرَؤوا الزَّهْرَاوَيْنِ: البقرةَ وسورةَ آلِ عِمْرانَ.

Amesimulia Abuu Umaamah Al-Baahiliy (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Someni Qur-aan kwani itakuja Siku ya Qiyaamah ikiwa ni shafaa’ah (kiombezi) kwa watu wake wanaoisoma na kutekeleza (amri zake). Someni taa mbili: Al-Baqarah na Aal-‘Imraan. [Muslim]

 

1-Itakuwa Kama Mawingu Mawili Na Itawatetea Wanaoisoma Na Kutekeleza Amri Zake:

 

Amesimulia An-Nawwaas bin Sam-‘aan (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Siku ya kufufuliwa, Qur-aan na watu waliokuwa wakiisoma na kutekeleza mafunzo yake, wataletwa mbele wakitangulizwa na Suwratul-Baqarah na Aal-‘Imraan.” Akasema An-Nawwaas: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akatoa mifano mitatu kwa Suwrah mbili hizi na sikusahau mifano hiyo tokea wakati huo. Alisema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): “Zitakuja kama mawingu mawili au vivuli viwili vyeusi kati yake kuna nuru, au makundi mawili ya ndege waliotandaza mbawa zao wakiruka, zitawatetea watu wake (wanaoshikamana nazo).” [Muslim]

 

Rejea pia Al-Baqarah kupata fadhila inayohusiana na Suwrah hii ya Aal-‘Imraan.

 

Faida:

 

Aal-‘Imraan ni baba yake Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام).  Rejea Aayah (35-37). Mama yake ni ndugu wa Nabiy Zakariyyah (عليه السّلام): Familia ya ‘Imraan ni miongoni mwa familia Alizozifadhilisha Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya walimwengu. Rejea Aayah namba (33-34). Na kisa chao kimetajwa kwenye Aayah namba (35-37).

 

Aayah za mwisho wa Suwrah hii [Aal-‘Imraan: (190-200]) ni Aayah ambazo ameteremshiwa Nabiy Allaah (سبحانه وتعالى) usiku mmoja zikamliza mno. Nazo ni Sunnah za kuzisoma pindi mtu anapoamka kwa ajili ya Tahajjud (kuamka usiku kuswali).  

 

 

 

Share