010-Yuwnus: Utangulizi Wa Suwrah
010-Yuwnus: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 109
Jina La Suwrah: Yuwnus
Suwrah imeitwa Yuwnus, na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (98) kuhusu kaumu ya Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) kwamba ni kaumu pekee ambao waliamini na wakatubia kabla ya kuteremshiwa adhabu.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuuthibitisha Unabii (na Risala ya) Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa dalili, na kuwalingania wanaopinga ili waamini, pamoja na kuwatishia (uwepo wa) adhabu. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuiweka misingi ya ‘Aqiydah, na kuithibitisha Tawhiyd na Risalah pamoja na kuwakumbusha watu walioghafilika na Aayaat (Ishara, Dalili) za Allaah, kwamba marejeo yao kwa Rabb wao kwa kufufuliwa, kuhesabiwa matendo na malipo yake.
3-Kuwakumbusha viumbe watafakari Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uumbaji wa viumbe, Uendeshaji ulimwengu, Utoaji rizki, Uumbaji wa mbingu na ardhi na yaliyomo ndani yake), na hikma Zake.
4-Kulengea katika kuusalimisha moyo kutokana na uthibitisho kwamba Qur-aan ni mawaidha, shifaa (poza, tiba), hidaaya na rehma.
5-Kuradd shubha za washirikina kwa dalili na hoja za wazi.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa Risalah ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Allaah.
2-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah ya Al-Uluwhiyyah kwamba Yeye Ni Mmoja Pekee na Ndiye Anayepasa kuabudiwa.
3-Imethibitishwa kukusanywa viumbe vyote Siku ya Qiyaamah na jazaa (malipo), na kuna ukumbusho wa kwamba marejeo ya mwisho ya viumbe ni kwake Allaah (سبحانه وتعالى). Na pia wanaadam wamegawanyika makundi mawili; Waumini na makafiri.
4-Imetajwa wazi itikadi za washirikina, na ile misimamo yao kuhusu Qur-aan, pamoja na kutajwa shubha zao na kuziraddi, na kuthibitishwa kuwa Qur-aan ni Kitabu cha Allaah.
5-Zimetajwa baadhi ya adhabu na maangmizi za watu wa nyumati zilizopita, baada ya kumshirikisha Allaah na kuwapinga Rusuli.
6-Imetajwa mazingatio juu ya uwezo Aliouweka Allaaah kwa wanaadam wa kuweza kutembea bara na baharini.
7-Imetolewa mifano ya wazi ya mapambo na starehe za dunia, na kukumbushwa kwamba dunia itaondoka haraka sana.
8-Imetajwa utofauti ya hali za Waumini na makafiri kesho Aakhirah, na kubatwilika kwa viabudiwa vya washirikina.
9-Imethibitishwa kwamba Qur-aan imeteremshwa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na dalili ya kuwa madai ya wanayoipinga ni uzushi wa wazi, na washirikina wameshindwa kuleta japo Suwrah moja mfano wake.
10-Imethibitishwa kuwa Ilimu ya Allaah imeenea kote na kwa viumbe wote, na kutaja athari za Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) uliokuwa wazi.
11-Imewabashiria Vipenzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) hapa duniani na Aakhirah.
12-Kuna maamrisho ya kutakiwa kudhihirisha furaha kwa Uislamu na Qur-aan.
13-Kumliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kutajwa kisa cha Nabiy Nuwh na Nabiy Muwsaa (عليهما السّلام) na kisa cha Bani Israaiyl na watu wa Firawni.
14-Imetajwa kuokoka kwa watu wa Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) kwa kuamini kwao, na kutubia kwao, na kwamba kaumu ya Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) ni kaumu pekee iliyoamini kabla ya kuteremshiwa adhabu.
15-Ameamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aelekee katika Dini ya haki ya Allaah, na onyo la kutokumshirikisha Allaah.
15-Imethibitshwa kwamba dhara yoyote ile inayomsibu mtu, hakuna wa kuiondosha isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Na kwamba Allaah Akimtakia mtu kheri, basi hakuna wa kuizuia.
16-Suwrah imekhitimishwa kwa kumliwaza Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) avute subira mpaka Allaah (سبحانه وتعالى) Ateremshe Hukmu Yake.