016-An-Nahl: Utangulizi Wa Suwrah

 

016-An-Nahl: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 128

 

Jina La Suwrah: An-Nahl

 

Suwrah imeitwa An-Nahl (Nyuki), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (68).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ukumbusho juu ya neema unaoonyesha (Uadhimu wa) Mwenye kuneemesha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwaraddi washirikina, kuwakemea shirki zao na kuwaonya.

 

3-Kusimamisha dalili juu ya Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba Sharia ya Uislamu inatokana na asili ya Dini ya Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام).   

 

4-Kuthibitisha ukweli wa Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na ukweli wa yale aliyokuja nayo.

 

5-Kubainisha Neema mbali mbali za Allaah kwa Waja Wake.

 

6-Kubainisha sifa za Waumini na washirikina na kuthibitisha kufufuliwa Siku ya Qiyaamah na jazaa za Waumini duniani na Aakhirah, na adhabu za washirikina duniani na Aakhirah kutokana na shirki na kufru zao,.

 

7-Kusisitiza wema na ihsaan kwa watu, kutimiza ahadi hata ikiwa lengo ni kuwalingania katika Dini ya Allaah kuwafahamisha ukafiri wao na ushirikina wao. Pia matahadharisho ya kutenda machafu na munkari na dhulma.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitisha kwamba Siku ya Qiyaamah ni kweli na kwamba haina shaka kutokea kwake. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Ametakasika na Ametukuka kwa Uluwa kutokana na wanayomshirikisha.

 

2-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Al-Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah katika ibaada) kwamba hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye Allaah (سبحانه وتعالى). Na uthibitisho wa Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji na kadhaalika) kwa kubainisha Qudra ya Allaah katika kuumba mbingu, ardhi, wanaadam, na wanyama. Pia  kulidhalilisha jua na mwezi, usiku na mchana, na vinginevyo.

 

3-Zimetajwa Neema nyingi na mbalimbali za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa wanaadam. Miongoni mwazo ni wanyama na vinavyopatikana kwao ambavyo ni vipando vya watu, na kubebeshwa mizigo safarini, kupatikana ngozi zao, maziwa na pambo. Pia neema ya maji yatokayo mbinguni yanayootesha mazao mbalimbali. Neema ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuitisha usiku na mchana, kuitisha bahari na faida zinazopatikana humo za mapambo, nyama safi, na meli zinazopita humo kuwapatia watu rizki zao. Kujaalia milima thabiti ardhini. Kujaalia nyota za kuwaongoza watu njia na mengineyo. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anamalizia kuhusu Neema Zake kuwa haiwezekani kuziorodhesha hesabuni. Na hayo yote Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja kuwa ni Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa watu wenye kutafakari, wenye kutia akilini, wenye kukumbuka na wenye kushukuru.

 

4-Kuna matahadharisho kwa washirikina, ya yale yaliyowapata waliomshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwapinga Rusuli wa Allaah (عليهم السلام), ambayo ni maangamizi na adhabu za dunia na zinazowangojea Aakhirah.

 

5-Suwrah imebainisha tofauti ya kutolewa roho kwa kafiri na Muumin: Kafiri hutolewa kwa adhabu na kubashiriwa kuingizwa motoni huko Aakhirah. Ama Muumin, yeye hutolewa roho yake huku Malaika wakimtolea Salaam na bishara ya kuingizwa Jannah.  

 

6-Imebainishwa jinsi washirikina na waabudiwa wao watakavyokanushana ibaada zao Siku ya Qiyaamah. 

 

7-Imetajwa baadhi ya mila na desturi za kijaahiliyyah, za dhulma ya hali ya juu, kuwachukia watoto wa kike na kuwazika wakiwa hai.

 

8-Zimetajwa neema nyenginezo za Allaah (سبحانه وتعالى) nazo ni maziwa masafi yanayotoka matumboni mwa wanyama. Pia mazao mbalimbali. Na neema ya kupata asali kutokana na nyuki, ambayo ni shifaa ya magonjwa mbalimbali. Na Aayah (80-81) za zimeendelea kutaja Neema Zake Allaah (سبحانه وتعالى) za sufi, ngozi, vivuli na kadhaalika.  

 

9-Kuna mifano ya wazi baina ya Muumini na kafiri. Muumini ni mwenye kushukuru. Ama kafiri ni aliyekosa shukurani na mwenye kukufuru. Na mifano ya tofauti ya Mwabudiwa wa haki ambaye ni Allaah (سبحانه وتعالى) na waabudiwa wasiokuwa wa haki.

 

10-Imetajwa baadhi ya tabia njema, ikiwemo uadilifu, ihsaan, kujitolea, kukemea uovu, kuhimiza watu kutekeleza ahadi, na kuwakemea watu juu ya kuvunja ahadi.

 

11-Ukumbusho wa Muumini kutenda mema ili apate maisha mazuri duniani na Aakhirah.

 

12-Kuna amri ya kuomba kinga dhidi ya shaytwaan katika kusoma Qur-aan, jambo ambalo ni miongoni mwa adabu za kuisoma Qur-aan.  

 

13-Imetajwa baadhi ya shubha ambazo walizizusha washirikina dhidi ya Qur-aan, pamoja na kuzifanyia raddi.

 

14-Imetajwa hukmu ya mtu anayekufuru baada ya kuwa Muumini (mwenye kurtadd), na anayelazimishwa kukufuru, ilihali moyo wake umethibitika katika imaan.

 

15-Imetajwa amrisho la kula vizuri vya halali na haramisho la kula vya haramu kama nyama ya nguruwe. Na kubainisha kwamba kuhalalisha na kuharamisha ni kazi ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

16-Ametajwa Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) na baadhi ya sifa na fadhila zake, na ukumbusho kwa watu kuwa alikuwa haniyfah (mwenye kuelemea haki) wala hakuwa mshirikina, na sifa yake ya kuwa mwenye kushukuru. Rejea Aayah (120) kwenye uchambuzi wa fadhila na sifa za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام).

 

17-Imetajwa njia muhimu za kufanya daawah ya Allaah, na jinsi ya kuamiliana na watu, ambako ni kuwalingania kwa hekima, na mawaidha mazuri.

 

18-Suwrah imekhitimishwa kwa amri ya kuvuta subira katika mitihani na kwamba subra inatokana na tawfiyq ya Allaah (سبحانه وتعالى) baada kumuomba Yeye Amjaalie mja Wake kuvumilia.

 

Faida:

 

Suwrah ya An-Nahl ni Suwrah inayobainisha kwa wingi Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) ambazo haiwezekani kuziorodhesha hesabuni kama Anavyosema Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayah namba (18). Na mojawapo ya neema ni Kuumba An-Nahl (Nyuki) wanaotoa asali matumboni mwao ambayo ni shifaa, tiba na kinga ya magonjwa. Rejea Aayah namba (68-69).

 

 

 

 

Share