030-Ar-Ruwm: Utangulizi Wa Suwrah

 

030-Ar-Ruwm: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 60

 

Jina La Suwrah: Ar-Ruwm

 

Suwrah imeitwa Ar-Ruwm (Nchi ya Roma), na inayodalilisha ni kutajwa Warumi katika Aayah namba (2).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Msisitizo kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mfanyaji wa kila jambo Peke Yake, na kubainisha Desturi ya Allaah kwa Viumbe Wake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwabashiria Waja Wake kwamba watawashinda Wamajusi wa Waajemi, na kuthibitisha kwamba ushindi hauji kwa idadi au vifaa, bali ni kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee, Humsaidia Amtakaye, na Humshinda Amtakaye.

 

3-Kuweka wazi dalili za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kubatilisha ushirikina.

 

4-Kuthibitisha uwepo wa kufufuliwa na malipo ya Aakhirah.

 

 Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetoa khabari kuhusu vita vya Ruwm na Fursi, na Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya kumalizika vita kwa kushinda Wafursi, na kwamba, Warumi watawashinda Wafursi baada ya miaka michache. Na hii bila ya shaka ilihakiki.   

 

2-Imewataka makafiri juu ya kufikiria vile Alivyoviumba Allaah; mbingu na ardhi na vilivyomo, na watembee ili wajionee jinsi watu wa mwanzo walivyoangamizwa.

 

3-Imetajwa baadhi ya yatakayojiri Siku ya Qiyaamah, na mafikio ya Waumini na makafiri.

 

4-Zimekariri Aayah za Allaah zinazobainisha Ishara na Dalili za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Uumbaji Wake na Ishara nyenginezo

 

5-Imetajwa Uwezo wa Allaah wa kuumba viumbe na kuwafufua nayo ni mepesi mno kwa Allaah (سبحانه وتعالى).  

 

6-Imetajwa mahimizo ya kushikamana na Dini Haniyfah (iliyoelemea katika haki) na kuifata, na makatazo ya kufata njia ya washirikina.

 

7-Imebainisha hali ya washirikina wanapofikwa na shida humuomba Allaah kwa kurudi Kwake kisha wanapoondoshewa shida zao, wanarudi kumshirikisha Allaah.

 

8-Imetaja kuwa ufisadi unaodhihirika ardhini ni kutokana na makosa wanayoyachuma watu wenyewe na itawafuatilia adhabu.

 

9-Imebainishwa Rehma na Neema za Allaah (سبحانه وتعالى); miongoni mwazo ni Kuwaruzuku waja na Kuwapelekea pepo za rehma zenye kuteremsha mvua katika ardhi iliyokufa, kisha ikarudi kufufuka, basi hii ni Ishara na Dalili ya wazi ya Uwezo wa Allaah kuwafufua viumbe.   

 

10-Imebainishwa ukaidi wa makafiri na kwamba Allaah Amewapigia mifano kila aina lakini bado wamekufuru.

 

11-Suwrah imekhitimishwa kwa Amri ya Allaah kumuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuvuta subira na kuthibitika katika Dini.

 

 

 

Share