032-As-Sajdah: Utangulizi Wa Suwrah
032-As-Sajdah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 30
Jina La Suwrah: As-Sajdah
Suwrah imeitwa As-Sajdah (Sijda), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Ubainisho wa uhakika wa viumbe, na hali za watu duniani na Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kubainisha Utukufu wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake Kamilifu, na Uwezo Wake katika Kuumba, Kudabiri mambo, Kufufua na malipo.
3-Kuinua utajo wa Qur-aan, kwani hiyo ndio iliyokusanya kila aina ya uongofu.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan kwamba haina shaka ndani yake, na kwamba imeteremshwa na Rabb wa ulimwengu, na kuwapinga washirikina wanaodai kuwa imetungwa.
2-Imetajwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi na kubainisha baadhi ya mambo yanayoonyesha Uwezo Wake.
3-Imeweka wazi baadhi ya hoja za makafiri katika kupinga kwao kufufuliwa pamoja na kuwaraddi kwenye hilo.
4-Imetajwa baadhi ya mambo ya Siku ya Qiyaamah hasa kwa watu waovu wakiwa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) .
5-Imetajwa baadhi ya sifa za Waumini, na waliyoahidiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Peponi katika Neema Zake.
6-Imetajwa kuwa Waumini hawako sawa na mafasiki na ikatajwa malipo yao; Waumini watapata Jannaat na makazi mazuri na takrima humo. Mafasiki makazi yao yatakuwa ni motoni.
7-Imetajwa kuhusu Nabiy Muwsaa (عليه السلام), na Neema aliyopewa na Allaah (سبحانه وتعالى) ya kupewa Tawraat.
8-Da’wah kwa washirikina kutakiwa waizingatie na kutafakari Qur-aan.
9-Simulizi za baadhi ya ujinga wa washirikina.
10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwapuuza washirikina na kujitenga nao.
Fadhila Za Suwrah:
Ni Sunnah kuisoma Suwrah As-Sajdha katika Swalaah ya Alfajiri siku ya Ijumaa:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ الم * تَنْزِيلُ السَّجْدَةَ وَ هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Alfsjiri siku ya Ijumaa:
الم ﴿١﴾ تَنزِيلُ
As-Sajdah (32) na
هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ
Suwrah Al-Insaan (76). [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]