040-Ghaafir: Utangulizi Wa Suwrah
040-Ghaafir: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 85
Jina La Suwrah: Ghaafir
Suwrah imeitwa Ghaafir (Mwenye Kughufuria), na inayodalilisha ni kutajwa Sifa hii ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayah namba (2).
Na Suwrah imeitwa pia Al-Muumin kwa kutajwa katika Hadiyth:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ السَّائِبِ، قَالَ صَلَّى لَنَا النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم الصُّبْحَ بِمَكَّةَ فَاسْتَفْتَحَ سُورَةَ الْمُؤْمِنِينَ حَتَّى جَاءَ ذِكْرُ مُوسَى وَهَارُونَ أَوْ ذِكْرُ عِيسَى - مُحَمَّدُ بْنُ عَبَّادٍ يَشُكُّ أَوِ اخْتَلَفُوا عَلَيْهِ - أَخَذَتِ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم سَعْلَةٌ فَرَكَعَ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ السَّائِبِ حَاضِرٌ ذَلِكَ . وَفِي حَدِيثِ عَبْدِ الرَّزَّاقِ فَحَذَفَ فَرَكَعَ . وَفِي حَدِيثِهِ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ عَمْرٍو . وَلَمْ يَقُلِ ابْنِ الْعَاصِ .
Amesimulia ‘Abdullaah Bin As-Saaib (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha Swalaah ya Asubuhi Makkah, akafungua (Swalaah) kwa Suwrah Al-Muumin (akasoma) mpaka alipofikia kutajwa Muwsaa na Haaruwn au kutajwa ‘Iysaa (عليهم السّلام), kikohozi kikamshika akarukuu. ‘Abdullaah bin As-Saaib alikuwepo hapo. Na katika Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Abdur-Razzaaq (maneno yalikuwa): Alikata (kisomo) akarukuu. [Muslim]
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha hali ya wanaobishana Aayah za Allaah (ili wazipinge na wazibatilishe), na kuwaradd juu ya madai yao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kubainisha haqq (haki) na baatwil na kubatilisha mijadala ya wale waliokuwa wakijadili juu ya Aayah za Allaah ili wazipinge na wazibatilishe.
3-Hali za makafiri wa nyumati zilotangulia, waliokadhibisha Rusuli wao na maangamizi yao.
4-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo Wake wa Kuumba kwa dalili kadhaa, na Uwezo wa Kufufua.
5-Kutaja baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah na hali za watu, na Hukmu ya uadilifu ya Allaah Siku hiyo ya malipo ya kheri na shari.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa kuwa Qur-aan ni Uteremsho kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na kumsifu Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Sifa Zake za wingi wa Kughufuria na Kupokea tawbah za Waja Wake, kisha kuthibitishwa Tawhiyd Yake, na kwamba marejeo yatakuwa Kwake Siku ya Qiyaamah.
2-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameliwazwa kutokana na yaliyomsibu kutoka kwa watu wake; washirikina wa Makkah, kwamba Rusuli wa kabla yake pia walikadhibishwa na kaumu zao, lakini Allaah Aliwaadhibu.
3-Daawah kwa wanaadam juu ya kufanya ibaada kwa ikhlas, na kuwakumbusha vitisho vya siku ya Qiyaamah.
4-Imewasifu Malaika wanaobeba ‘Arsh ya Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba miongoni mwa kazi zao, ni kuwaombea maghfirah Waumini, na kuwaombea duaa.
5-Imetajwa kwamba kuna mauti mawili na uhai miwili. Rejea Faida ya Aayah (namba 11).
6-Imetajwa Siku ya Qiyaamah ambayo hakuna kitakachofichika, wala hakutakuwa na dhulma, na hakutakuwa na mfalme, wala mwenye kutakabari, wala mwenye kujifanya jabari, bali Ufalme Utabakia wa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee. Na Siku hiyo, nyoyo zitafika kooni kwa kiwewe, huzuni na majuto, na hata rafiki wa dhati hataweza kumsaidia mwenziwe.
7-Imeelezewa sehemu ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), na Akatajwa Muumin mmoja kutoka watu wa Firawni aliyewaonya watu wake wasimuue Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), na akawalingania waikubali Risala ya Allaah, na akawaonya Siku ya Qiyaamah ambayo ni Siku ya kuitana. Pia akawalingania Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na akawaonya kuingizwa motoni. Na pia ikatajwa jeuri na kibri cha Firawni kutaka kupanda mbinguni ili amuone Allaah (سبحانه وتعالى), na kumkadhibisha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Na imethibitishwa adhabu za maisha ya Barzakh kaburini, kwamba Firawni anaendelea kuadhibiwa asubuhi na jioni na atatendelea hivyo mpaka ifike Siku ya Qiyaamah.
8-Imetajwa mazungumzo kati ya watu walio wadhaifu na walio na nguvu uwezo na waliotakabari. Watu wadhaifu wanaomba msaada kwa waliotakabari lakini hakuna kusaidiana Siku hiyo, bali watakanushana. Na ikatajwa watu wa motoni wanavyowaomba Walinzi wa moto wawaombee kwa Allaah (سبحانه وتعالى) takhfifu ya adhabu lakini duaa yao haikubaliwi!
9-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameliwazwa kwa kutakwa avute subira na aombe maghfirah na Kumsabbih Rabb wake asubuhi na jioni.
10-Imehimizwa kumuomba duaa Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba kutokumuomba, ni aina ya kibri. Na imetanabahishwa Kumpwekesha Allaah katika ibaada na kubatilisha viabudiwa vyote kinyume na Allaah.
11-Imetajwa aina kadhaa za Neema za Allaah kwa watu, ili waweze kushukuru.
12-Wameonywa makafiri waliokadhibisha Risala ya Allaah kwa baadhi ya vitisho na adhabu za Siku ya Qiyaamah.
13-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwaonya washirikina wa Makkah ya kwamba watakuja kutaka kuamini baada ya kuiona adhabu, lakini kuamini kwao hakutawafaa, na kwamba Desturi ya Allaah itahakiki kama walivyoadhibiwa nyumati za nyuma, na hivyo watakuwa katika khasara.
Faida:
Suwrah hii ya Ghaafir (40) ni Suwrah ya mwanzo katika mfululizo wa Suwrah zinazoanzia na herufi za حم. Ya mwisho wake ni Suwrah Al-Ahqaaf (46).