048-Al-Fat-h: Utangulizi Wa Suwrah

 

048-Al-Fat-h: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 29

 

Jina La Suwrah: Al-Fat-h

 

Suwrah imeitwa Al-Fat-h (Ushindi) yaani Ushindi wa Makkah, na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila na Faida na kwa kutajwa neno hili katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kupewa bishara Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waumini juu ya Al-Fat-h (Ushindi wa Makkah) na kumakinishwa (kuwa imara) katika ardhi. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumbashiria Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba wake (رضي الله عنهم) kwa aina mbali mbali za bishara.

 

3-Kuwatambulisha wanafiki na makafiri, na kubainisha uhalisia wao.

 

4-Kubainisha mengi katika Fadhila na Rehma za Allaah kwa Waumini.  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kumbashiria Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba wake (رضي الله عنهم) Al-Fat-h  (Ushindi wa Makkah), na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amemghufuria Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) madhambi yake yaliyotangulia na yanayofuatia, na Amemtimizia Neema Zake, na kwamba Atamuongoza katika njia iliyonyooka, na Atamjaalia nusra ya nguvu.

 

2-Kisha Waumini wakabashiriwa kwa kuteremshiwa utulivu, na kuingizwa Jannaat, na kufutiwa maovu yao. Na wanafiki na washirikina wakaahidiwa ghadhabu za Allaah na Laana Yake juu yao, na mwishowe kuingizwa moto wa Jahannam.

 

3-Imetajwa bay’ah (fungamano la ahadi ya utiifu) baina ya Swahaba na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaunga mkono kwa Kuwa pamoja nao kwa Ujuzi Wake, Anawasikia na Anawaona na Anajua niya zao. Na hiyo ilikuwa chini ya mti. Na hiyo ni bay’ah inayojulikana Bay’atur-Ridhwaan (fungamano la ahadi liloridhiwa na Allaah) kama ilivyotajwa katika Aayah namba (18), kuwa Allaah Amewaridhia Waumini waliofungamana ahadi ya utiifu chini ya mti, Akawateremshia utulivu na Akawaahidi ushindi, na kuwajaalia ghanima za vita nyingi.   

 

4-Imebainishwa hali halisi ya wanafiki na washirikina kama vile kubakia nyuma wasiende kupigana Jihaad, kisha watake kuombewa maghfira. Kisha pindi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba wake (رضي الله عنهم) walipoondoka kwenda Khaybar, wanafiki wakataka kwenda nao ili wapate kupewa ghanima (ngawira za vita).

 

5-Imebainishwa fadhila za Allaah na Rehma Zake kwa Waja Wake Waumini kama, kuwazuia wasiingie Makkah kwanza kupigana vita na washirikina, juu ya kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwajaalia ushindi, na washirikina wakawa chini ya udhibiti wa Waumini. Basi Kuwazuia Kwake, ni kutokana na Hikma Zake (سبحانه وتعالى) kwamba, wasije kuwakanyaga na kuwaua Waumini waliolazimika kubakia Makkah. Na pia, kwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mjuzi wa ghaibu, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Alijua kuwa watakuweko washirikina watakaokuja kuingia Uislamu  baada ya Fat-h Makkah (Ushindi wa Makkah), kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Anamhidi Amtakaye kwa Rehma Zake. Na washirikina wengi wakaja kuingia Uislamu baada ya Fat-h Makkah.     

 

6-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsadikisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ndoto Aliyomuotesha, kwamba wataingia Al-Masjidul-Haraam kwa amani, hali ya kuwa wamenyoa vichwa vyao na wengine wamepunguza nywele. Na Akajaalia kabla ya kuingia Makkah ushindi, na ufunguzi wa Khaybar.

 

7-Imethibitishwa kwa dalili za wazi, kwamba Dini ya Kiislamu itakuja kushinda dini zote ulimwenguni.

 

8-Suwrah imekhitimishwa kwa kuelezwa sifa za Waumini juu ya makafiri, kuwa Waumini ni wakali zaidi dhidi ya makafiri, lakini wanahurumiana baina yao. Na ni wenye kusimamisha Swalaah na kutafuta Fadhila na Radhi za Allaah. Na kwamba alama zao zinadhihirika katika nyuso zao kutokana na athari za kusujudu, basi Allaah Amewaahidi Waumini watendao mema, maghfira na ujira adhimu ambao ni kuwaingiza Peponi.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Suwrah Al-Fat-h ni Suwrah kipenzi kabisa kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ زَيْدِ بْنِ أَسْلَمَ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَسِيرُ فِي بَعْضِ أَسْفَارِهِ وَعُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ يَسِيرُ مَعَهُ لَيْلاً، فَسَأَلَهُ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ عَنْ شَىْءٍ، فَلَمْ يُجِبْهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ثُمَّ سَأَلَهُ فَلَمْ يُجِبْهُ، ثُمَّ سَأَلَهُ فُلَمْ يُجِبْهُ، فَقَالَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ ثَكِلَتْ أُمُّ عُمَرَ، نَزَرْتَ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ثَلاَثَ مَرَّاتٍ، كُلَّ ذَلِكَ لاَ يُجِيبُكَ‏.‏ قَالَ عُمَرُ فَحَرَّكْتُ بَعِيرِي، ثُمَّ تَقَدَّمْتُ أَمَامَ النَّاسِ، وَخَشِيتُ أَنْ يُنْزَلَ فِيَّ الْقُرْآنُ، فَمَا نَشِبْتُ أَنْ سَمِعْتُ صَارِخًا يَصْرُخُ بِي فَقُلْتُ لَقَدْ خَشِيتُ أَنْ يَكُونَ نَزَلَ فِيَّ قُرْآنٌ‏.‏ فَجِئْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَسَلَّمْتُ عَلَيْهِ فَقَالَ ‏"‏ لَقَدْ أُنْزِلَتْ عَلَىَّ اللَّيْلَةَ سُورَةٌ لَهِيَ أَحَبُّ إِلَىَّ مِمَّا طَلَعَتْ عَلَيْهِ الشَّمْسُ ‏"‏‏.‏ ثُمَّ قَرَأَ ‏"‏‏  إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُبِينًا

Amesimulia Zayd Bin Aslam (رضي الله عنه): Baba yangu amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikua akitembea katika baadhi ya safari zake, na ‘Umar Bin Al-Khatw-twaab (رضي الله عنه) akitembea pamoja nae wakati wa usiku. ‘Umar akamuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kitu, ikawa hakumjibu. Kisha akamuuliza tena lakini hakumjibu. Kisha akamuuliza tena lakini hakumjibu. ‘Umar akasema: Amekukosa mama yako ee ‘Umar! Umemsisitiza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) mara tatu na mara zote hakujibu! ‘Umar (رضي الله عنه) akasema: Nikamuondoa mnyama wangu, kisha nikatangulia mbele ya Waislamu. Nikaogopa isijeteremka kwangu mimi Qur-aan, basi sikuingia katika jambo jengine. Haujapita muda hata kidogo mara nikasikia mpiga ukelele akiniita. Nikasema: Niliogopa isijekua imeteremka Qur-aan kunihusu mimi! Nikaenda kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikamsalimia, akasema: “Nimeteremshiwa usiku huu, Suwrah  ambayo ni kipenzi zaidi kwangu kuliko chochote kilicho chomozewa na jua (ulimwenguni).” Kisha akasoma:

 إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا﴿١﴾

“Hakika Tumekupa ushindi (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), ushindi bayana.” [Al-Fat-h (48:1) – Al-Bukhaariy]

 

Faida:

 

حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ مُحَمَّدٍ، حَدَّثَنَا يَحْيَى بْنُ آدَمَ، حَدَّثَنَا يَزِيدُ بْنُ عَبْدِ الْعَزِيزِ، عَنْ أَبِيهِ، حَدَّثَنَا حَبِيبُ بْنُ أَبِي ثَابِتٍ، قَالَ حَدَّثَنِي أَبُو عَنْ وَائِلٍ، قَالَ كُنَّا بِصِفِّينَ فَقَامَ سَهْلُ بْنُ حُنَيْفٍ فَقَالَ أَيُّهَا النَّاسُ اتَّهِمُوا أَنْفُسَكُمْ فَإِنَّا كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَوْمَ الْحُدَيْبِيَةِ، وَلَوْ نَرَى قِتَالاً لَقَاتَلْنَا، فَجَاءَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ فَقَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَلَسْنَا عَلَى الْحَقِّ وَهُمْ عَلَى الْبَاطِلِ فَقَالَ ‏"‏ بَلَى ‏"‏‏.‏ فَقَالَ أَلَيْسَ قَتْلاَنَا فِي الْجَنَّةِ وَقَتْلاَهُمْ فِي النَّارِ قَالَ ‏"‏ بَلَى ‏"‏‏.‏ قَالَ فَعَلَى مَا نُعْطِي الدَّنِيَّةَ فِي دِينِنَا أَنَرْجِعُ وَلَمَّا يَحْكُمِ اللَّهُ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ فَقَالَ ‏"‏ ابْنَ الْخَطَّابِ، إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ، وَلَنْ يُضَيِّعَنِي اللَّهُ أَبَدًا ‏"‏‏.‏ فَانْطَلَقَ عُمَرُ إِلَى أَبِي بَكْرٍ فَقَالَ لَهُ مِثْلَ مَا قَالَ لِلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ إِنَّهُ رَسُولُ اللَّهِ، وَلَنْ يُضَيِّعَهُ اللَّهُ أَبَدًا‏.‏ فَنَزَلَتْ سُورَةُ الْفَتْحِ، فَقَرَأَهَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَلَى عُمَرَ إِلَى آخِرِهَا‏.‏ فَقَالَ عُمَرُ يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَوَفَتْحٌ هُوَ قَالَ ‏"‏ نَعَمْ ‏"‏‏.‏

Amesimulia Abuu Waail (رضي الله عنه): Tulikuwa Swiffiyn, Sahl bin Hunayf (رضي الله عنه) akasimama na kusema: Enyi watu! Tuhumuni nafsi zenu, kwani sisi tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) siku ya Hudaybiyah na lau kama tungeambiwa tupigane tungelipigana. ‘Umar Bin Al-Khatw-twaab (رضي الله عنه) akaja na akasema: Ee Rasuli wa Allaah!  Hivi hatukuwa katika haki na wao katika baatwil? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ndiyo (tuko katika haki).”  Akasema: Hivi hawatakuwa Peponi waliouawa miongoni mwetu na watu wao waliouawa wao kuwa motoni? Akasema: “Ndiyo.” ‘Umar akasema: Je, ni kwa misingi ipi basi tunaitia udhalili Dini yetu? Hivi turudi kabla Allaah Hajahukumu kati yetu na wao? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ibn Al-Khatw-twaab! Mimi ni Rasuli wa Allaah, na Allaah Hanitupi abadani!” ‘Umar akaenda kwa Abubakar, akamwambia kama alivyomuambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Yule ni Rasuli wa Allaah, na Allaah Hampotezi abadani!” Basi ikateremka Suwrah Al-Fat-h (48), Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamsomea ‘Umar mpaka mwisho wa Suwrah. ‘Umar akasema: Ushindi ndio huo? Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Naam.”  [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share