038-Swaad: Utangulizi Wa Suwrah

 

038-Swaad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 88

 

Jina La Suwrah: Swaad

 

Suwrah imeitwa Swaad, na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1), na ambayo ni katika herufi zinazojulikana kuwa ni Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah zinazotokea katika mwanzo wa baadhi ya Suwrah.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Mapambano dhidi ya baatwil na mwisho wake (kwa aliyejipamba na ubatilifu). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kusimamisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo Wake.

 

3-Kuthibitisha ukweli wa Unabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

4-Kuthibitisha kufufuliwa na kuziradd hoja za washirikina.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzuwa Qur-aan na kusifiwa kwamba ni yenye ukumbusho. Kisha imebainishwa misimamo ya washirikina na ada zao za kutokumuamini Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), na kumfanyia istihzai na dhihaka, na kumpachika sifa ovu. Hivyo basi ni kuikanusha Risala ya Allaah.

 

2-Imetajwa kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa yaliyomsibu kutoka kwa watu wake, kwa kuwataja baadhi ya Manabii waliokadhibishwa na watu wao pia.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtaja na kumsifia Mja Wake Daawuwd (عليه السّلام) na Neema Zake Alizomjaalia, zikiwemo kumtunukia mwanawe ambaye ni Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام). Kisha ikatajwa kisa cha watu wawili walioingia kwa Nabiy Daawuwd (عليه السّلام) kumtaka awahukumu kuhusu kondoo wao, naye akatoa hukumu, lakini akahisi kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtia mtihanini, akaporomoka kumuomba Rabb wake maghfirah. 

 

4-Na pia Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtaja na kumsifu Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام) na Neema kadhaa Alizojaaliwa; miongoni mwazo ni kupewa ufalme ambao hatoupata tena mtu baada yake, na kutiishiwa (kudhalilishwa) upepo aweze kusafiri safari ndefu kwa muda mfupi tu, na pia kutiishiwa (kudhalilishiwa) majini.     

 

5-Na pia Allaah (سبحانه وتعالى) Amemtaja na kumsifu Nabiy Ayyuwb (عليه السّلام) na kisa chake cha mitihani aliyopewa ya maradhi, na jinsi alivyovuta subira hadi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuondeshea maradhi na kumbadilishia kila lilobaya kwa zuri.

 

6-Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amewataja na kuwasifu Nabii Wake wengineo nao ni Ibraahiym, Is-haaq, Ya’quwb, Ismaa’iyl, Al-Yasaa na Dhul-Kifl (عليهم السّلام).

 

7-Imetajwa baadhi ya neema na raha za kudumu milele, Alizoziandaa (سبحانه وتعالى) huko Jannah kwa wamchao Yeye ambayo ni neema za kudumu.

 

8-Ikafuatilia kutajwa yaliyoandaliwa motoni kwa watu waovu, na hali zao huko za kulaumiana na kuombeana adhabu humo.

 

9-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Aadam (عليه السّلام) na Ibliys aliyefanya kiburi akakataa amri ya Rabb wake, Akalaaniwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na kuepushwa na Rehma Zake. Ibliys akaahidi kuwapotosha watu isipokuwa waliokhitariwa kwa ikhlaas zao. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akaapa kumuingiza katika moto wa Jahannam na kuijaza kwa watakaomfuata.  

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Kumuunga mkono Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuthibitisha kuwa Qur-aan ni ukumbusho kwa walimwengu, na wanaoipinga watakuja kujua khabari za ukweli wa Qur-aan. Rejea Aayah (88) kupata faida.

 

 

 

 

 

Share