051-Adh-Dhaariyaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

051-Adh-Dhaariyaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 60

 

Jina La Suwrah: Adh-Dhaariyaat

 

Suwrah imeitwa Adh-Dhaariyaat (Pepo zinazopeperusha vumbi kuzitawanya), na inayodalilisha ni kutajwa mwanzo kabisa katika Aayah namba (1)

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwafahamisha majini na wanaadam kuwa rizki yao inatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee ili watekeleze ibaada kwa ikhlaasw. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kusimamisha dalili ya kwamba ibaada haiwi isipokua kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee na kwamba kufufuliwa ni kweli.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) kuapia baadhi ya vitu Alivyoviumba kama vile Adh-Dhaariyaat (pepo zinazopeperusha vumbi kuzitawanya), mawingu, na vinginevyo. Kisha ikafuatilia jibu la kiapo ambalo, kuthibitisha kuwa kufufuliwa na kulipwa yote ni kweli.

 

2-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaendelea kuapia kwa mbingu zilizojaa njia madhubuti na kwa kufuatilia madai ya wenye kukadhibisha, na Kuwaahidi adhabu ya moto.

 

3-Imetajwa Aliyoyaanda Allaah (سبحانه وتعالى) Peponi kwa wenye kumcha Yeye Allaah (عزّ وجلّ), na zikatajwa sifa zao kuwa ni wenye kuamka usiku kwa ajili ya ibaadah, na wenye kuomba maghfira kabla ya Alfajiri, na wenye kutoa baadhi ya mali zao kwa wahitaji.

 

4-Imetajwa baadhi ya Ishara na Dalili za Allaah ambazo wenye yaqini wanaziamini.

 

5-Imethibitishwa kuwa rizki za wanaadam zinatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee na ikaapiwa jambo hili kwa Rabb wa mbingu na ardhi ya kwamba ni haqq (kweli)!

 

6-Imetajwa baadhi ya visa vya Manabii akianziwa Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) pindi Malaika walimwendea kwake na ikabainishwa ukarimu wake kwa wageni. Kisha akabashiriwa yeye na mkewe kujaaliwa mwana ambaye ni Is-haaq, juu ya kuwa wamefikia umri wa uzee.

 

7-Kisha Malaika hao wakaelezea kusudio lao la kutumwa kuwa waelekee kwa kaumu ya Nabiy Luutw (عليه السّلام) kuwaangamiza kwa kufru na uasi wao wa matendo yao machafu yanayokwenda kinyume na maadili sahihi.

 

8-Ikatajwa pia Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) alipotumwa kwa Firawni na miujiza bayana, lakini Firawni akafanya kibri na kumpachika Nabiy Muwsaa kwa sifa ovu ya uchawi au majnuni. Basi akaangamizwa kwa gharka pamoja na jeshi lake.

 

9-Kisha kaumu nyenginezo; kaumu ya ‘Aad na maangamizo yao ya upepo mkali wa dhoruba ulioangamiza kila kitu. Kisha kaumu ya Thamuwd na maangamizi yao ya radi na umeme. Kisha kaumu ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام).

 

10-Yametajwa yanadalilisha Uwezo na Ukamilifu wa Allaah (سبحانه وتعالى), Muumbaji  wa mbingu na ardhi na kwamba Ameumba kila kitu kwa jozi mbili.

 

11-Imetajwa onyo la kutokuabudu asiyekuwa Allaah.

 

12-Ameamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ajitenge mbali na washirikina  aepukane na maudhi yao.

 

13-Imebainishwa lengo na sababu ya kuwaumba majini na wanaadam kwa ajili ya kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee.

 

14-Imetajwa kuwa umuhimu wa daawah na kwamba ukumbusho na mawaidha yananufaisha Waumini.

 

16-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwatishia washirikina ya kuwa itawapata sehemu katika adhabu kama ile itakayowapata wale wanaofanana nao miongoni mwa wenye kukadhibisha, na kuwatishia makafiri kutokana na Siku watakayorejeshwa kwa Allaah kuhesabiwa na kuadhibiwa.

 

 

 

Share